- Jamii za Pate na Kwale zinarejesha nyasi bahari kupitia upandaji na ulinzi wa maeneo ya tengefu, hatua inayolenga kurejesha makazi na chakula cha nguva pamoja na kuimarisha afya ya bahari.
- Juhudi hizo zimeanza kuleta matokeo, huku jamii zikishuhudia ongezeko la samaki na viumbe wengine wa baharini, pamoja na dalili za nguva kurejea katika maeneo yenye nyasi bahari.
- Wataalamu wanaonya kuwa upandaji pekee hautoshi, wakitaka ulinzi wa maeneo ya nyasi bahari, udhibiti wa uvuvi haramu na kuruhusu maeneo yaliyoharibiwa kujirejesha yenyewe pale inapowezekana.
- Utafiti na teknolojia vinaweza kusaidia kujua walipo nguva waliosalia, huku matumizi ya eDNA yakitoa dalili kwamba nguva huenda bado wanazunguka katika baadhi ya maeneo ya pwani ya Kenya.
KWALE, Kenya – Zaidi ya miaka 20 imepita tangu Amiri Juma, mvuvi kutoka Kibuyuni, Kaunti ya Kwale, alipomwona nguva (Dugong dugon) katika eneo la Mipwa, kijiji jirani cha Wasini.
Hii leo, akiwa na umri wa miaka 63, Juma bado anakumbuka vizuri siku ambayo wavuvi walimnasa mnyama huyo anayejulikana kama ng’ombe wa baharini na kumchinja.
“Namjua nguva; aliwahi kushikwa na jarife. Aliyemshika wakati huo sasa ni marehemu. Siku hiyo watu walipika na kuila nyama yake. Mimi sikuweza kuila kwa sababu niliposhika nyama yake, mwili wangu ulianza kuwasha,” alisema Juma.

Kwa mujibu wa Juma, hilo lilikuwa tukio la kawaida, kwani hakukuwa na uelewa kuhusu umuhimu wa kumhifadhi nguva. Anasema ilikuwa rahisi sana kuwaona nguva, na hii pia ilikuwa ishara nzuri kwa wavuvi kuwa bahari ilikuwa na samaki wengi.
Juma anaamini kutoweka kwa mnyama huyo baharini kumechochewa na shughuli nyingi za uvuvi. “Bahari imeingiliwa sana. Zamani kulikuwa na mitego tu. Sasa watu wanaingia kila sehemu, usiku na mchana. Wanyama wengi wamepotea. Hata samaki wamepungua,” anasema.
Hapo zamani nguva alikuwa kitoweo kitamu sana kwa familia nyingi eneo la pwani, kabla ya kuwekwa kwa sheria inayopiga marufuku kumkamata.
Faki Kassim, mvuvi kutoka kijiji cha Bodo, Kaunti ya Kwale, anasema takriban miaka 30 iliyopita, yeye na wavuvi wenzake walikuwa wakishika nguva, kumchinja na kuuza nyama yake. “Nguva ana ngozi ngumu sana. Nyama yake ni nyekundu na yenye mafuta mengi. Miaka mingi iliyopita tulikuwa tukiuza kipande kimoja cha nyama yake kwa shilingi moja,” anasema.
Anaeleza kuwa kabla ya kumchinja nguva, walilazimika kutekeleza itikadi zao zilizoambatana na mnyama huyo. Mvuvi yeyote aliyemshika nguva alilazimika kuapishwa kabla ya kumchinja.

“Nguva ana maumbile ya binadamu. Ana matiti, uchi wake ni kama mwanamke, na yeye pia hupata hedhi. Kwa mujibu wa imani hiyo ya jadi, nguva anapokuwa katika siku zake za hedhi, huchukua jani la mkoko na kujifunika nalo. Anapomaliza, jani hilo huganduka. Ilikuwa lazima mvuvi aape kwamba hakumdhulumu mnyama huyo kabla ya kumchinja,” anasema Kassim.
Omar anasema ingawa sababu kamili ya kutoweka kwa nguva haijathibitishwa kisayansi, uharibifu wa makazi na vyanzo vya chakula chake umeonekana kuwa miongoni mwa vitisho vikubwa na umehusishwa moja kwa moja na kupungua kwake.
“Nguva hukaa karibu na ufuo wa bahari kwa sababu chakula chake ni nyasi bahari. Lakini hizo pia ndizo sehemu ambazo binadamu wanafanya shughuli nyingi. Hilo ndilo suala ambalo linaleta changamoto kubwa,” anasema.

Katika Kisiwa cha Pate, Kaunti ya Lamu, kikundi cha wanawake kinachojulikana kama Shanga Itifaq kinaendeleza juhudi za uhifadhi wa ikolojia ya bahari kwa kupanda nyasi bahari na mwani, lengo lake likiwa kuzuia kutoweka zaidi kwa nguva baharini.
Kikundi hicho cha wanawake 13 na wanaume sita, kikiongozwa na Amina Bakari, maarufu kama Mama Nyasi Bahari, kilianzishwa mwaka 2018.
Wao hutenga siku moja kwa wiki kupanda angalau gunia 17 za kilo 50 za nyasi bahari katika eneo lao la tengefu lililoko Pate Marine Community Conservancy (<PMCC), lenye ukubwa wa jumla ya ekari 9,290. Kwa sasa wamepanda ekari 9 za nyasi bahari aina ya Kambani (Thalassodendron ciliatum, na mtimbi mrefu (Enhalus acoroides).
Baada ya wiki moja, nyasi hizo huwa zimeota na samaki huanza kuonekana maeneo hayo. Amina anasema asilimia 100 ya nyasi hizo hustawi.
Amina anaeleza Mongabay kuwa walipoanza kazi hiyo, hawakulenga kumsaidia nguva pekee, bali walitaka kurejesha afya ya bahari iliyokuwa imeanza kupoteza samaki na viumbe wengine.
“Tuliona samaki na viumbe wengine baharini wamepungua, ndipo tukaanza kujifunza umuhimu wa nyasi bahari. Leo tunazihifadhi, kuzipanda na kuzitunza kwa sababu tumeona ndizo msingi wa maisha ya bahari,” anasema Amina.

Kikundi hicho kilipata mafunzo ya jinsi ya kuhifadhi na kupanda nyasi bahari kutoka kwa mashirika kama vile Fauna & Flora International na Northern Rangelands Trust. Sasa wameanza kuona mafanikio, kwani kila wanapoenda kukagua eneo lao la tengefu, huona alama zinazoonyesha kuwa nguva amepita na kula nyasi bahari.
Nguva huacha njia za malisho zenye mistari. Kulingana na Amina, ni vigumu sana kwao kujua idadi ya nguva wanaopita na kula katika tengefu lao, lakini kila wanapoenda kupanda nyasi, wao huona mistari iliyoachwa na nguva.
“Nguva hula nyasi bahari na kuacha mistari. Kwa kawaida huwa hang’oi nyasi yote, huzibakisha na kisha nyasi hiyo baadaye huchipuza tena,” anasema Amina. Mbali na nguva, jamii hiyo pia imeshuhudia kuongezeka kwa kaa, kasa, samaki na viumbe wengine wanaotegemea nyasi bahari kama makazi na maeneo ya kuzaliana.
“Kwa kawaida, wavuvi wanapotoka baharini hufika bandarini, ambapo Kitengo cha Usimamizi wa Pwani (BMU) hurekodi kiasi cha samaki walioshika. Kitambo, kwa wiki tulikuwa tunaweza kuandikisha tani mbili za samaki kutoka kwa wavuvi. Kwa sasa tunaona samaki wameongezeka, na kwa wiki tunarekodi tani 5 hadi 7 za samaki kutoka kwa wavuvi,” anasema Amina.
Hata hivyo, Amina anasema changamoto kubwa wanayopitia katika kutekeleza shughuli zao ni ukosefu wa elimu kwa baadhi ya jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi bahari. Tatizo lingine ni ukosefu wa boti za kufikia maeneo ya mbali ya nyasi bahari, na gharama kubwa za shughuli za ufuatiliaji.
Ripoti iliyochapishwa mwaka 2021 na American Journal of environmental studies inaonyesha kuwa bahari ya Kenya, kwa wakati huo, ilikuwa na nguva 20 pekee.
Nguva ni mnyama anayeishi kwenye kina kifupi karibu na ufuo baharini. Ana mchango mkubwa katika mfumo mzima wa ikolojia ya bahari, kwani husaidia kumea kwa nyasi bahari, ambayo ni muhimu kwa chakula cha samaki. Mnyama huyo ni miongoni mwa wale walioorodheshwa na shirika la IUCN kama aliye katika hatari ya kutoweka.
Utafiti unaonyesha kuwa kati ya mwaka 2000 na 2016, eneo la nyasi bahari nchini Kenya lilikuwa likipungua. Kwa wastani, kila eneo la kilomita za mraba 25 lilipoteza kilomita za mraba 1.9 za nyasi bahari.
Ripoti iliyochapishwa na Western Indian Ocean Journal of Marine Science mwaka wa 2024, kuangalia uwezekano wa mifumo ya ikolojia ya nyasi bahari kusaidia urejeshaji wa nguva nchini Kenya kwa kutumia uchunguzi wa angani (aerial survey), ilibaini uwepo wa nguva Lamu.
Ripoti hiyo inasema eneo la Lamu linakadiriwa kuwa na nguva 14, huku idadi kubwa zaidi ikipatikana Kiunga. Wengine wanapatikana katika maeneo ya Doa, Kisiwa cha Sii, Mwarembo, Mbayai, Funzi na Kiwayuu, Kiunga – Pezali, Konani, Ndia-mbili, Mlango-wa-huseni na Kui.
Hii inahusishwa na uharibifu mdogo wa nyasi bahari ambazo ni chakula cha nguva, pamoja na uwepo wa maeneo ya tengefu ya kuhifadhi bahari humo.
Utafiti wa angani uliofanywa mwaka 2023 katika ukanda wa pwani wa Kenya wenye urefu wa kilomita 600 ulibaini kuwepo kwa nguva wawili pekee. Shirika la Kimataifa la Ustawi wa Wanyama (IFAW) lilisema hali hiyo inatofautiana sana na ripoti za miaka ya 1960, wakati makundi ya nguva hadi 500 yalionekana katika pwani ya Kenya.
Utafiti huo ulibaini kuwa kukamatwa kwa nguva kwa bahati mbaya katika zana za uvuvi, uwindaji wa makusudi na uharibifu wa maeneo yenye nyasi bahari ni miongoni mwa vitisho vikuu kwa wanyama hao. Pia ulitaka kuimarishwa kwa utekelezaji wa sheria dhidi ya nyavu za kuvulia samaki aina ya gill nets, ambazo zinaweza kuwaua nguva, pamoja na kuimarishwa kwa ulinzi wa maeneo yenye nyasi bahari.
Shakue Bausi ni mkaazi wa kijiji cha Shangashakani, na ni mmoja wa wanachama wa kikundi cha Shanga Itifaq na anahudumu kama mshauri mkuu. Pia amekuwa mvuvi kwa zaidi ya miaka 15. Anasema akianza shughuli za uvuvi, ilikuwa jambo la kawaida kuona alama za nguva na hata wanyama hao wenyewe, hasa katika maeneo yaliyojaa nyasi bahari.
“Nguva chakula chake ni nyasi bahari. Lakini kwa sababu ya uvuvi mbaya ambao unaendelea baharini, malisho yake yaliharibiwa na wakaanza kupotea. Hiyo ndiyo sababu kuu ambayo ilinifanya nijiunge na kikundi hiki ili tupande nyasi bahari kama njia mojawapo ya kumrudisha na kumhifadhi,” alisema Bausi.
Anasema shughuli nyingi za upanzi wa nyasi bahari hufanywa na kina mama. “Lakini kuna nyingine huwa hawawezi, hivyo basi sisi wanaume huingilia kati. Sisi huwa mstari wa mbele kuingia kwa maji mengi kuangalia mahali ambapo upanzi unafanyika, halafu wao wanatufuata nyuma,” anaeleza.
Licha ya kwamba kuna msimu ambapo samaki huwa vigumu kupatikana baharini, hasa miezi ya Juni, Julai na Agosti, jamii ya eneo hilo imeanza kuona mabadiliko yanayoletwa na mradi huo, ikiwepo ongezeko la samaki wanaovuliwa kila siku, na kuongezeka kwa ajira.
“Huwa tunatumia zile pesa tunakusanya kila wiki au mwezi, pamoja na fedha za kufadhili miradi, kama zile tulizopata kutoka Kenya Marine Fisheries Socio-economic Development (KEMFSeD) kuajiri wanajamii ambao sio wanachama wa kikundi kutusaidia na kazi za kutayarisha upanzi wa nyasi bahari na pia mwani,” anasema Bausi. “Mradi huu umenisaidia kupata pesa za kusomesha watoto wangu. Zaidi, ile nyumba ninayoishi sasa sio kama zamani. Nimejenga nyumba ya matofali. Ile ya zamani ilikuwa ya udongo”.

Bausi, hata hivyo, anafafanua kuwa eneo ambalo mradi huo unafanyika ni mbali na makwao, na wao hutumia mashua ndogondogo, ambayo mara nyingi haitoshi kuwabeba wanachama wote.
“Boti ambayo tunatumia ni ndogo, na wanachama ni zaidi ya kumi. Kwa hivyo, hatuwezi kuwachukua watu wote kwa pamoja. Boti inapoenda na kurudi huwa ni gharama kwetu kununua mafuta. Pia hatuna vifaa vya kutusaidia katika kuendeleza mradi, kwa mfano gumboots. Unakuta kina mama wanavaa dera kwenda baharini, na kawaida dera likishika maji hushikana na mwili. Mwanamke anafaa kujistiri,” anasema Bausi.
Kikundi hicho kina malengo ya kupanua mradi huo hadi zaidi ya ekari tisa. Zaidi, uwe mradi unaotambulika kimataifa na watu wafike eneo hilo na kujifunza jinsi ya kuhifadhi mazingira ya bahari.
Charles Muthama, mwanasayansi mtafiti kuhusu nyasi bahari kutoka Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Samaki (KMFRI), na mzamiaji kwa zaidi ya miaka 30 katika taaluma hiyo, anasema hajawahi kuona nguva, lakini anapozama, huona sehemu ambazo nguva amepitia.

Muthama anasema kupanda nyasi bahari pekee hakutoshi. “Mazingira ya bahari yakiacha kuathiriwa, huwa yanajirekebisha. Hiyo ndiyo njia nafuu na yenye matokeo bora kuliko kupanda nyasi kila mahali,” anafafanua.
Kwa mujibu wake, wanasayansi wa KMFRI, pamoja na watafiti kutoka Msumbiji, Madagaska na visiwa vya Western Indian Ocean, wamekuwa wakitengeneza ramani ya nyasi bahari chini ya mpango wa Large Scale Seagrass Mapping and Management Initiative (LaSMMI) ili kufahamu maeneo yanayonawiri vyema na kutofautisha maeneo yanayostawi na yale yaliyoathiriwa.
“Tunaangalia kiwango cha uharibifu. Kama eneo limeharibika kwa zaidi ya asilimia 50, tunaweza kuingilia kulirejesha. Kama halijaharibika sana, tunaacha mazingira yajirekebishe yenyewe. Tunataka nyasi zinazoangamia zipate nyasi changa mbadala zinazoota upya ili mfumo mzima wa bahari uwe na mapato endelevu. Samaki na viumbe wengine baharini wanapoendelea kuzaana katika sehemu hizi, wavuvi wataendelea kuvua bila kufikia kiwango cha samaki kuadimika,” anasema Muthama.
Juhudi mbadala za tengefu
Takriban kilomita 460 kutoka Kaunti ya Lamu, wakazi wa Jimbo, Kaunti ya Kwale, chini ya uongozi wa Jimbo BMU, hutumia mbinu ya kuhifadhi eneo la bahari, maarufu kama tengefu.
Mohammed Bakari, afisa wa miradi wa Jimbo BMU, anasema mradi huo ulianza mwaka 2024 baada ya kubaini kuwa uvuvi haramu, hasa matumizi ya nyavu haramu, ulikuwa umeharibu nyasi bahari.
“Tuliona nyasi bahari zimeharibika, na samaki na viumbe wengine baharini wameanza kupotea, tukakubaliana na wanajamii kuanzisha eneo la uhifadhi ili bahari ijiregeshe katika hali nzuri,” anasema Bakari.
Anaeleza kuwa eneo hilo la uhifadhi hufungwa kwa miezi 10 kila mwaka kuanzia Aprili hadi Januari, na kufunguliwa kwa uvuvi halali pekee katika miezi ya Februari na Machi, ili kuruhusu samaki kuzaliana na kurejesha mfumo wa ikolojia.
Doria za mara kwa mara zinazotekelezwa na wanajamii zimechangia kupunguza visa vya uvuvi haramu kutoka takribani visa 16 hadi kimoja au sufuri kwa mwezi, jambo ambalo limewezesha nyasi bahari kujirejesha.
Bakari alisema tayari wameanza kushuhudia kurejea kwa aina mbalimbali za samaki, wakiwemo, wayo (Pseudorhombus arsius), ishara kuwa makazi ya baharini yanaendelea kuimarika.
Bakari anasema jamii yao ina imani kuwa juhudi zao za kuendelea kuhifadhi nyasi bahari zitamsaidia mnyama huyo kurudi maeneo hayo. “Mahali penye chakula ndipo atakaporudi. Tukihifadhi nyasi bahari, atarejea,” anasema Bakari.
Baadhi ya nyasi bahari ambazo wanazihifadhi katika tengefu lao ya hekari 56.7 ni pamoja na mshipi (Enhalus acoroides), Thalassia hemprichii, noodle seagrass (Syringodium isoetifolium), Halodule wrightii na Halodule uninervis.
Mradi huo wa uhifadhi wa nyasi bahari umeleta manufaa ya kiuchumi kwa jamii kupitia ajira za kupiga doria za baharini, ukodishaji wa boti, mafunzo ya ufuatiliaji wa rasilimali, na usimamizi wa taka. Bidhaa zinazotumika kwenye shughuli za doria pia hununuliwa katika maduka ya wenyeji.
“Bahari ikiwa nzuri, samaki wanaongezeka, jamii inanufaika na hata viumbe waliopotea kama nguva wana nafasi ya kurudi,” anasema Bakari.
Nchini Kenya, sheria ya kupiga marufuku kushika mnyama aliye kwenye hatari ya kuangamia inatekelezwa na Huduma ya Wanyamapori ya Kenya (KWS), chini ya Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori ya mwaka 2013.
Dkt Mohammed Omar, Mwanasayansi Mkuu Mwandamizi na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa Bahari na Pwani katika Taasisi ya Utafiti na Mafunzo ya Wanyama (WRTI), anasisitiza umuhimu wa kulinda maeneo ambayo nguva bado anaonekana kwa njia ya usimamizi maalum kupitia mpango wa matumizi ya bahari (Marine Spatial Planning). Anasema hili litasaidia kuzuia shughuli za kibinadamu kuathiri makazi yake.

“Kila kiumbe baharini kina kazi yake. Nguva anapokula nyasi bahari, husaidia kuchochea ukuaji na uzalishaji wa nyasi hizo. Pia huchangia kurutubisha mazingira. Kutoweka kwake kunaweza kuathiri ukuaji wa nyasi hizo,” anasema Omar. “Tunataka kuhakikisha sehemu ambazo nguva anapatikana zimetambuliwa, na shughuli zitakazoruhusiwa huko ziendane na mahitaji ya mazingira yake. Bila kufanya hivyo, hata maeneo ambayo nguva wamebaki, kama Lamu, yanaweza kumpoteza kabisa”.
Nguva ana uwezo wa kuishi kwa miaka 70 ama zaidi. Ana kiwango cha chini cha uzazi, na huwekeza nguvu nyingi katika kulea mtoto wake. Nguva wa kike huanza kuzaa anapofikisha umri wa angalau miaka kumi au hata 17. Kipindi cha ujauzito wake huchukua miezi 13 hadi 15, na kwa kawaida, huzaa mtoto mmoja. Mtoto hunyonya kwa muda wa miezi 14 hadi 18. Muda kati ya kuzaliwa kwa mtoto mmoja na mwingine hutofautiana kati ya miaka miwili na saba, kulingana na eneo wanapoishi, na upatikanaji wa chakula. Vipindi kati ya uzazi vinaweza kurefuka kutokana na uhaba wa chakula.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2021 iliyochapishwa na American Journal of Environment Studies, katika miaka ya 1940-1960 kulikuwa na nguva wengi sana pwani ya Kenya. “Hapa Mombasa kulikuwa na nguva wengi baharini… hata mia moja, kwa sababu nguva huishi kama familia,” anasema Omar.
Katika zoezi la kuhesabu nguva mwaka wa 2017 kutoka eneo la Kwale hadi Lamu, ukanda wa Pwani wenye urefu wa zaidi ya kilomita 600, Omar anasdema waliona nguva wawili Lamu, karibu na sehemu za Ndau kwenda juu mpaka Kiwayu. “Mwingine tulimpata katika eneo la Msambweni,” anasema.
Mwaka 2023, Omar anasema walirudi tena kuhesabu wanyama hao. “Tuliona nguva wawili sehemu hiyo hiyo ya Ndau mpaka Kiwayu. Lakini Kwale hatukuona. Hatuna hakika kama wametoweka ama bado wako. Lakini pia tumegundua kuwa hizi nyasi bahari kila siku zinaenda zikiathirika na kupungua. Zikipungua inamaanisha chakula chao pia kinapungua. Ndiyo sababu wanazidi kutoweka,” anasema Omar.
Anaeleza kuwa barani Afrika, Msumbiji ndiyo ina idadi kubwa ya nguva. “Tunafanya utafiti ili tujaribu kuelewa ikiwa nguva wanaopatikana kule Mozambique (Msumbiji) wanapatikana pengine, tuseme Tanzania, na hata Uarabuni, na ikiwa ni hawa hawa wanakuja mpaka Kenya, ama ni tofauti,” anasema.
Ikumbukwe kwamba nchini China, tayari nguva wameshaangamia, ilhali Australia inaendelea kuwa na idadi kubwa ya nguva, ambao husaidia mfumo wa ikolojia ya miamba ya matumbawe na kuchangia ukuaji endelevu wa nyasi bahari, hasa wanapozila.
Teknolojia ya kisasa
Watafiti wana mbinu mbalimbali za kutumia teknolojia ya kisasa kufuatilia ikolojia ya nyasi bahari na jinsi nguva anaweza kuhifadhiwa. KMFRI inaeleza kuwa matumizi ya teknolojia ya kisasa ya Environmental DNA (eDNA) yanaweza kuwa suluhisho muhimu katika kubaini uwepo wa nguva na kuimarisha juhudi za kuhifadhi nyasi bahari, ambayo ni makazi yake muhimu.
Lilian Daudi, mwanasayansi mtafiti kutoka KMFRI, anasema kupungua kwa nguva pia ni tatizo katika eneo lote la Western Indian Ocean (WIO). Anasema watafiti wanaelekeza nguvu katika teknolojia ya eDNA. “Ukichukua sampuli ya maji na kufanya uchambuzi wa DNA, unaweza kubaini kama nguva, kasa au samaki wamewahi kupita katika eneo hilo bila kuwaona moja kwa moja”.

Anafafanua kuwa utafiti wa awali karibu na eneo la Gazi, Kaunti ya Kwale, ulionyesha mabaki ya vinasaba ya nguva, ishara kwamba viumbe hao huenda bado wanazunguka katika baadhi ya maeneo ya pwani ya Kenya, ingawa hawaonekani mara kwa mara.
Alisema eDNA inaweza kutoa ushahidi wa kisayansi wenye uhakika zaidi kuhusu maeneo wanayopita viumbe hao.
Kenya ni miongoni mwa nchi zilizotia saini Mkataba wa Makubaliano kuhusu Uhifadhi wa Nguva (Dugong Memorandum of Understanding – MOU), mfumo wa kimataifa wa uhifadhi chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Spishi Zinazohamahama (CMS).
Mkataba huo unazitaka nchi kuchukua hatua za kukabiliana na vitisho kwa nguva, ikiwemo kulinda makazi yao, kufuatilia idadi yao na kupunguza vifo vinavyosababishwa na shughuli za binadamu. Pia unahimiza nchi kuimarisha sheria dhidi ya ukamataji na uuwaji wa nguva pamoja na biashara ya wanyama hao au sehemu zao.
Picha ya bango: Nguva akiwa baharini. Picha kwa hisani ya Jamii Forums, Tanzania.
Katika Mkondo wa Mida nchini Kenya, wavuvi sasa wanakabiliana na mabadiliko ya bahari kwa matumaini