- Spishi 28 za wanyamapori wakubwa na wa kati zathibitishwa.
- Tanzania yaongoza Afrika kwa idadi kubwa ya tembo na simba wa porini.
- Faru waendelea kuwa miongoni mwa wanyama walio hatarini zaidi kutoweka.
- Sasa tishio kwa wanyamapori si ujangili, bali uvamizi wa hifadhi na migogoro.
Sensa ya Taifa ya Wanyamapori ya mwaka 2024/2025 imetoa ripoti yake ambayo inatoa picha mchanganyiko: upande mmoja kuna mafanikio makubwa katika kudhibiti ujangili na kuongeza idadi ya baadhi ya wanyama muhimu. Upande mwingine kuna tishio jipya la uvamizi wa maeneo ya hifadhi, na hivyo kuibua migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Zoezi hilo lilifanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kubaini idadi, mtawanyiko, mwenendo na hali ya ustawi wa wanyamapori nchini.

Ripoti ya sensa hiyo iliyofanyika kuanzia Septemba 2024 hadi Oktoba 2025, ilikabidhiwa kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika hafla iliyofanyika ikulu jijini Dar es Salaam.
Matokeo ya sensa hiyo yalitangazwa jijini Arusha na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Dkt Eblate Mjingo, katika hafla iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wa uhifadhi. Mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Ashatu Kijaji, aliyemwakilisha Rais Suluhu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, spishi nyingi zimeongezeka kwa idadi, huku nyingine zikibaki katika viwango vinavyoonyesha uthabiti.
Spishi 28 zathibitishwa
Matokeo yanaonyesha kuwa Tanzania kwa sasa ina spishi 28 za wanyamapori wakubwa na wa kati, ambazo zimethibitishwa katika mifumo yote mikubwa ya ikolojia iliyofanyiwa utafiti.
Hata hivyo, ripoti hiyo, inaonyesha mafanikio hayo hayajasambaa kwa kiwango kinachofanana katika maeneo yote ya nchi. Baadhi ya spishi zimeongezeka kwa kasi, nyingine zimeongezeka kwa kiwango kidogo, huku nyingine zikionyesha dalili za kupungua kutokana na sababu mbalimbali zinazohusishwa zaidi na shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya mazingira.
Tembo waongezeka
Miongoni mwa wanyamapori waliopata ufuatiliaji wa karibu zaidi katika sensa hii ni tembo wa Afrika.
Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2014 Tanzania ilikuwa na tembo 46,408, lakini kufikia mwaka 2025, idadi hiyo iliongezeka hadi tembo 66,714.
Kwa mujibu wa Dkt Mjingo, ongezeko hilo linaonyesha wazi kuwa mikakati ya Serikali ya kuimarisha ulinzi wa maeneo ya hifadhi, kuwekeza katika doria, matumizi ya teknolojia na ushirikiano na wananchi vimeanza kuzaa matunda.

Pamoja na mafanikio hayo, anasema tofauti na miaka ya nyumba ambapo changamoto dhidi ya wanyamapori ilikuwa ujangili, hivi sasa tatizo kubwa ni kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na tembo kutokana na kuendelea kupungua kwa maeneo ya asili ya wanyama hao, kunakosababishwa na uvavimizi .
Dkt Mjingo anasema jambo la kushangaza ni kwamba wakati mwanzoni mwa miaka ya 2000 Tanzania ilikuwa na zaidi ya tembo 130,000, migogoro kati ya binadamu na tembo haikuwa mikubwa kama ilivyo sasa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nyati pia wameendelea kuonyesha ongezeko kubwa la idadi. Takwimu katika ripoti hiyo zinaonyesha kuwa mwaka 2014 Tanzania ilikuwa na nyati 242,945, lakini kufikia mwaka 2025 idadi hiyo imefikia 328,437. Ongezeko hilo linaifanya Tanzania kuendelea kushika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa idadi ya nyati wanaoishi katika mazingira ya asili.
“Mafanikio hayo yanaonyesha uwezo wa mifumo ya ikolojia ya Tanzania kuendelea kuzalisha na kuhifadhi wanyamapori licha ya changamoto zinazoongezeka kutokana na shughuli za kibinadamu,” alisema Dkt Mjingo.
Katika kundi la wanyama wanaohamahama kwa idadi kubwa, nyumbu wameendelea kuonyesha uimara wa kiikolojia. Takwimu zinaonyesha kuwa idadi yao imeongezeka kutoka 1,501,108 mwaka 2014 hadi kufikia 1,598,290 mwaka 2025. Wanyamapori wengine walioongezeka ni pundamilia ambao idadi imeongezeka kutoka 306,620 mwaka 2014 hadi 340,111.
Twiga waongezeka kwa kiwango kidogo
Ripoti inaonyesha, Twiga pia wameendelea kuongezeka, ingawa kwa kiwango kidogo. Wameongeza kutoka 27,478 hadi 29,185 katika kipindi hicho cha miaka 10.
Kwa upande wa simba, matokeo ya sensa yanaonyesha kuwa mwaka 2014 Tanzania ilikuwa na simba 16,800, huku mwaka 2025 idadi hiyo ikifikia simba 17,200.
Kwa mtazamo wa kawaida, ongezeko la simba 400 linaweza kuonekana kuwa dogo. Hata hivyo, mtaalamu wa uhifadhi John Shaga anasema ongezeko hilo lina umuhimu mkubwa kwa sababu simba ni mnyama anayezaliana polepole na anayehitaji eneo kubwa la kuishi. Hivyo, hata ongezeko dogo linaashiria kuwa mazingira yanaendelea kuwa salama kwa ustawi wa spishi hiyo.
Takwimu hizo pia zinaifanya Tanzania kuendelea kushika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa idadi ya simba wanaoishi porini. Kwa mujibu wa taarifa ya sensa, Tanzania ina simba 17,200, ikifuatiwa na Afrika Kusini yenye simba 3,284, Botswana 3,064, Kenya 2,515 na Zambia 2,349.
Mbali na spishi maarufu, sensa imeonyesha mafanikio makubwa kwa wanyama wengine ambao mara nyingi hawapatiwi uzito mkubwa katika mijadala ya umma, lakini wana mchango mkubwa katika afya ya mifumo ya ikolojia.
Kwa mfano, tandala wameongezeka kutoka 3,877 mwaka 2014 hadi kufikia 6,417 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 65. Palahala nao wameongezeka kutoka 12,586 hadi 20,983.
Kwa upande wa pofu, matokeo yanaonyesha ongezeko kubwa zaidi. Idadi yao imeongezeka kutoka 52,558 hadi kufikia 102,591 mwaka 2025. Wanyama wengine walioongezeka ni korongo ambao idadi yao imeongezeka kutoka 3,488 hadi kufikia 6,904.

Aidha, choroa wameongezeka kutoka 1,079 hadi 1,320, huku spishi nyingi nyingine zikiendelea kubaki katika viwango vinavyoonyesha uthabiti wa mazingira wanamoishi.
Uwindaji haramu watishia faru
Kwa upande wa faru, mwaka 2014 Tanzania ilikuwa na faru 142 lakini mwaka 2025 idadi hiyo imeongezeka hadi 285. Ingawa idadi hiyo imeongezeka maradufu, Dkt Mjingo anasema bado kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na historia ya spishi hiyo.
Faru wameendelea kuwa miongoni mwa wanyama walio katika hatari kubwa zaidi ya kutoweka kutokana na uwindaji haramu unaochochewa na biashara ya pembe zao katika masoko ya kimataifa. Hata hivyo, si kila spishi imeonyesha ongezeko. Sensa imebaini kuwa sheshe wamepungua kutoka 4,540 hadi 4,247.

Ingawa kupungua huko si kwa kiwango kikubwa lakini Dkt Mjingo anasema ufuatiliaji unatakiwa ili kubaini kama ni mabadiliko ya kawaida ya kiikolojia au kuna sababu nyingine zinazohitaji hatua za haraka.
Chanzo cha mafanikio
Kwa mujibu wa Dkt Mjingo mafanikio haya yamechochewa na mkakati wa muda mrefu wa kuimarisha ulinzi wa hifadhi, matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na ushirikiano kati ya taasisi za ndani na nje ya nchi.
“Matumizi ya droni, mifumo ya ufuatiliaji wa kielektroniki na doria za pamoja, yamekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza matukio ya ujangili yaliyokuwa yakisababisha upotevu wa wanyamapori muhimu,’’ anasema Dkt Mjingo.
Akizungumza wakati akipokea ripoti ya sensa, Rais Suluhu aliitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali za asili ili Watanzania waone thamani ya urithi huo na kushiriki kikamilifu katika kuutunza kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Rais Suluhu alisema matokeo ya sensa hiyo yanaonesha mafanikio makubwa ya juhudi za uhifadhi nchini na kuthibitisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa mataifa yenye utajiri mkubwa wa wanyamapori duniani.
“Naagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuongeza juhudi za utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali za asili ili Watanzania waone thamani ya urithi huo wa taifa na kushiriki kikamilifu katika kuutunza kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” Rais Suluhu alinukuliwa akisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mzava, akizungumza kwenye uzinduzi wa sensa hiyo jijini Arusha, aliimpongeza Serikali kwa kugharimia sensa hiyo kwa asilimia 100. Shilingi bilioni 4 zimetumika kwenye kazi hiyo.
“Kihiostoria ni mara ya kwanza kwa kutoa fedha zote kutoka kwa serikali yenyewe. Tuwapongeze TAWIRI kwa kazi hii kubwa na nzuri. Bunge tunaahidi tutaendelea kushirikiana na serikali/wizara kuhakikisha kwamba majukumu mliyokabidhiwa myatekeleze, mnatekeleza vizuri. Pili, pamoja na kwamba sisi ni viongozi wa kisiasa, tunaheshimu sayansi, tunaheshimu tafiti. Tunawaahidi, tutaheshimu matokeo ya sensa hii na tuko tayari kushirikiana pamoja kufanya yalete ustawi mzuri wa taifa letu,” alisema.
Dkt Kijaji alisema: “Tunayo maelekezo sasa kuhakikisha takwimu hizi zinawafikia Watanzania wote.”
Aliwataka watalamu na wahifadhi kwa ujumla wake watumie matokeo ya sensa hii kuona mambo gani yafanywe ili kurekebisha dosari zinazohatarisha ustawi wa wanyamapori na ikolojia kwa jumla. Sensa ya wanyamapori nchini Tanzania hufanywa kila baada ya miaka 10.
Kuhusu sensa 2024/2025
Tofauti na sensa ya kwanza iliyofanyika mwaka 2014/2015, sensa ya mwaka 2024/2025 imefanyika kwa kutumia mbinu za kisasa zaidi zinazowezesha kupata takwimu sahihi na pana kuliko ilivyowahi kutokea hapo awali.

Aidha, sensa iliyopita ilihusisha eneo la takribani kilomita za mraba 297,224, ilhali sensa ya mwaka 2024/2025 imeongeza eneo la utafiti hadi kufikia kilomita za mraba 340,748. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 18, hatua inayowezesha kupata picha halisi zaidi ya mwenendo wa wanyamapori katika mifumo mbalimbali ya ikolojia nchini.
Kwa mujibu wa Dkt Mjingo, sensa ya mwaka huu imeleta hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia za kisasa. Mbinu zilizotumika ni pamoja na upigaji picha wa anga, pamoja na matumizi ya kamera maalumu zinazofungwa. Aidha, utafiti wa ardhini ulifanyika sambamba na teknolojia hizo ili kuongeza usahihi wa takwimu zilizokusanywa.
Anasema matumizi ya teknolojia hizo yameongeza uwezo wa kubaini maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa wanyamapori, kufuatilia mienendo yao na kutathmini hali ya mifumo ya ikolojia kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko ilivyowezekana katika sensa zilizopita.
Picha ya bango: Sensa ya Taifa ya Wanyamapori ya mwaka 2024/2025 katika ripoti yake inaonyesha kuna mafanikio makubwa katika kudhibiti ujangili na kuongeza idadi ya baadhi ya wanyama muhimu. Upande mwingine kuna tishio jipya la uvamizi wa maeneo ya hifadhi, na hivyo kuibua migogoro kati ya binadamu na wanyamapori. Picha kwa hisani Wizara ya Maliasili na Utalii.