- Walinzi wa jamii nchini Kenya wanabeba jukumu kubwa la kulinda wanyamapori, lakini wengi wanakabiliwa na uhaba wa vifaa, mafunzo na mishahara isiyolipwa kwa wakati, hali inayotishia juhudi za uhifadhi.
- Kupunguzwa kwa ufadhili wa wafadhili wa kimataifa, ikiwemo USAID na AFD, kumeacha baadhi ya hifadhi za jamii zikishindwa kulipa mishahara ya walinzi kwa miezi sita hadi saba huku shughuli za doria zikidorora.
- Mabadiliko ya tabianchi yanaongeza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, huku ukame wa muda mrefu ukichochea ujangili, uvamizi wa wanyamapori na changamoto mpya kwa walinzi wa hifadhi.
- Katika maadhimisho ya Siku ya Walinzi wa Wanyamapori Duniani, wataalamu na walinzi wanatoa wito kwa serikali na wadau kuwekeza zaidi katika ustawi wa walinzi ili kulinda mafanikio yaliyopatikana katika uhifadhi wa wanyamapori nchini Kenya.
KAJIADO, Kenya — Purity Lakara hajutii chaguo lake la kuwa askari wa wanyamapori. Katika miaka saba ya kuhudumu katika Team Lioness, kikosi cha askari wanawake nchini Kenya, amepanda vyeo vitatu, kutoka constable hadi senior sergeant wa sasa.
Mwaka 2021, Lakara alikuwa miongoni mwa askari wawili waliosafiri Madrid kupokea Tuzo ya Kimataifa ya Ustawi wa Wanyama kutoka kwa Serikali ya Uhispania, tuzo iliyotambua mchango wa kikosi hicho katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira.
Katika Hifadhi ya Jamii ya Olgulului/Ololarashi, iliyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Amboseli, siku yake ya kawaida inajumuisha kuratibu askari kutoka kambi tatu katika shughuli za doria, ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia, ufuatiliaji wa wanyamapori, na usuluhishi wa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
“Nililelewa karibu na Amboseli na maeneo yaliyolindwa, na nikapata shauku ya uhifadhi wa wanyamapori tangu utotoni. Niliangalia jamii ya eneo hili ikiishi pamoja na wanyamapori, na wakati mwingine wakikabiliwa na changamoto katika kufanya hivyo. Ninafurahi kuwa na kazi inayonipa fursa ya kuhifadhi wanyamapori na kusaidia jamii yangu,” Lakara aliiambia Mongabay.
Wanachama wa Team Lioness wako miongoni mwa askari zaidi ya 80 wa jamii ya Olgulului wanaopata msaada kutoka kwa International Fund for Animal Welfare (IFAW), shirika la kimataifa lisilo la faida, linalojikita katika uhifadhi wa wanyamapori.

IFAW hulipa mishahara ya askari hao kwa wakati na kuwapa mgao wa chakula, bima ya afya, sare, magari, redio, pamoja na vifaa vya ufuatiliaji na ukusanyaji wa data. Shirika hilo pia lilikarabati makao yao ili kuwawezesha akina mama wanaotaka kuishi na watoto wao wadogo, huku kila mwanakikosi akiwa na chumba cha kujitegemea.
Lakara anakiri kwamba mazingira ya kazi yameimarika sana tangu alipoajiriwa katika kikundi cha kwanza mwaka 2019. “Tunapewa vifaa kama GPS, redio, darubini, vifaa vya msaada wa kwanza, programu ya EarthRanger, viatu, na magari ya doria tunapokuwa uwanjani. Lakini havitoshi kila wakati,” alisema.
Kufikia mwaka 2025, idadi ya askari wanawake katika kikosi hicho ilikuwa imefikia 17, ambayo ni zaidi ya mara mbili ya waliokuwepo mwanzoni.
Hata hivyo, Lakara anataka kuona askari zaidi wakiajiriwa ili kudoria ipasavyo ardhi ya jamii yenye hekta 147,000, na wale waliopo tayari wapate mafunzo na vifaa vya kutosha.
Hisia hizo zinaungwa mkono na Naomi Simaloi, askari wa cheo cha constable ambaye alihamasika kujiunga na Team Lioness mwaka 2021 baada ya kuona jinsi wasichana wanane wa kwanza waliokuwa wameajiriwa walivyoheshimika katika jamii ya eneo hilo.
“Walibadilisha mtazamo wa watu wa eneo hili kuhusu kazi ya askari. Watu walikuwa wakiona kazi hiyo kama ya wanaume peke yao. Tukiwa wasichana, tuliwaona wakiheshimiwa sana katika jamii. Walinihamasisha kutaka kuwa askari nilipokuwa ningali shuleni, na fursa ilipopatikana, niliikamata,” Simaloi alisema.
Nyakati zinazompa Simaloi kuridhika zaidi kazini ni pale anaposhughulikia matukio ya migogoro kati ya binadamu na wanyamapori na kufanikiwa kuzuia mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya wanyamapori wanaoua mifugo au kuharibu mazao.
“Mara nyingi tunafika kwenye matukio kama hayo na kukuta umati wa watu wenye hasira, wengine hata wakitutishia. Lakini tumekuwa tukisuluhisha kila wakati kwa njia ya amani. Hata hivyo, ningependa kupata mafunzo bora zaidi ya ushirikiano na jamii ili kuboresha ujuzi wangu wa mahusiano,” aliongeza.
Utafiti wa mwaka 2025 uliochapishwa katika jarida la Frontiers for Conservation Science uligundua kwamba ukame mkali na wa muda mrefu, unaohusishwa na mabadiliko ya tabianchi, unachochea ongezeko la migogoro kati ya binadamu na wanyamapori pamoja na uhalifu wa wanyamapori katika maeneo yaliyolindwa nchini Kenya. Utafiti huo ulichanganua mashtaka 1,099 ya uhalifu wa wanyamapori katika mahakama za nchi hiyo, ukilenga kuelewa kiwango cha uhalifu na spishi zinazohusika. Ulibaini kwamba uhalifu kama malisho haramu na ujangili wa nyama ya porini ulifikia kilele wakati wa kiangazi.
Tembo ndiyo spishi iliyoathirika zaidi, ikifuatiwa na swala mdogo wa kifalme, twiga, nyati na pofu.
Dkt Tuqa Jirmo, mtafiti mshirika katika African Wildlife Economy Institute (AWEI), na mkaguzi mkuu wa zamani wa Hifadhi ya Taifa ya Meru na Hifadhi ya Wanyama ya Maasai Mara, anahusisha ongezeko la ujangili wa twiga na wanyama wadogo wanaokula majani na hali ngumu ya maisha inayosababishwa na ukame, watu wakilazimika kuua wanyamapori kwa ajili ya chakula.

“Maisha yanazidi kuwa magumu kwa jamii za wafugaji. Mifugo yao inakufa kutokana na ukame, ambao unazidi kuwa wa muda mrefu na wa mara kwa mara,” Jirmo alisema.
Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Ukame (NDMA) iliripoti vifo vya zaidi ya mifugo milioni 2 katika maeneo kame na nusu kame ya nchi hiyo wakati wa ukame mkali kati ya mwaka 2020 na 2022.
Jirmo, ambaye mwenyewe alianza kazi yake kama mgambo wa wanyamapori, anasema jukumu la askari la kulinda maeneo ya hifadhi na ardhi za jamii nchini limekuwa muhimu zaidi kuliko hapo awali.
Changamoto hizi zinajitokeza wazi zaidi huku dunia ikiadhimisha Siku ya Dunia ya Askari wa Wanyamapori tarehe 31 Julai. Sherehe hii ya kila mwaka hutambua kazi, kujitolea na kujitoa mhanga kwa walinzi wanaolinda wanyamapori na mifumo ya ikolojia, huku ikiwaheshimu wale waliopoteza maisha au kujeruhiwa wakiwa kazini. Maadhimisho ya mwaka huu pia yanafufua wito kwa serikali, mashirika ya uhifadhi na wafadhili kuboresha ustawi wa askari kupitia mishahara bora, mafunzo, vifaa na mazingira mazuri ya kazi.
Lakini kwa askari wengi wa jamii nchini Kenya, kama ilivyo kwa wenzao katika nchi nyingine za Afrika, kutambuliwa peke yake hakutoshi. Wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa nguvu kazi, huku ustawi duni ukidhoofisha uwezo wa wale waliopo kufanya kazi yao ipasavyo.
Licha ya kubeba majukumu yanayozidi kuongezeka, ikiwemo kushughulikia migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, kupambana na ujangili, na kufuatilia wanyamapori katika maeneo yanayozidi kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, walinzi wengi bado wanakabiliwa na changamoto za uhaba wa vifaa, mafunzo duni na mishahara isiyolipwa kwa wakati.
Inakadiriwa kuwa Afrika kwa sasa ina walinzi wa hifadhi wapatao 65,000 pekee, takriban moja ya tano ya walinzi 345,000 wanaohitajika ili kulinda ipasavyo maeneo yake ya uhifadhi.
Kenya Community Ranger Perception Survey 2024, iliyofanywa na WWF-Kenya na Kenya Wildlife Conservancies Association (KWCA), ilibaini kuwa ukosefu wa mafunzo ya kitaalamu, ukosefu wa vifaa vinavyofaa na hali zisizo thabiti za kazi ndizo changamoto tatu kuu zinazowakabili askari wa jamii.
Asilimia 40 tu ya askari walioshiriki katika utafiti huo waliripoti kupata mafunzo ya ushirikiano na jamii, huku asilimia 37 wakisema walikuwa wamefunzwa mbinu za doria. Asilimia 48 ya waliohojiwa walikuwa wamepata mafunzo kuhusu migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, asilimia 46 kuhusu ufuatiliaji, na asilimia 57 kuhusu utekelezaji wa sheria.
Matokeo pia yalionyesha kwamba asilimia 51 ya waliojibu walihisi hawakuwa na vifaa na miundombinu ya kutosha kuhakikisha usalama wao na kutekeleza majukumu yao. Takriban asilimia 52 walihisi kwamba makazi yaliyotolewa hayakutosha, huku asilimia 61 wakiripoti upungufu wa maji na usafi wa mazingira.
Askari wanawake, ambao walikuwa asilimia 6 tu ya nguvu kazi ya askari nchini Kenya kufikia mwaka 2025, waligundulika kukabiliwa na changamoto za ziada, hasa wanapotumiwa katika vituo vya mbali, ambapo huduma za msingi kama makazi yanayofaa kwa watoto, vyoo vya kutosha na maji safi vilikuwa vikikosekana.

Kwa askari wanaofanya kazi katika hifadhi za jamii kaskazini mwa Kenya, hali imezidi kuwa mbaya zaidi katika mwaka na nusu uliopita. Kupunguzwa kwa msaada wa kigeni kwa kasi na nchi za Magharibi kumesababisha askari wengi kukaa miezi mingi bila mishahara. Programu za uhifadhi zilizosaidiwa na United States Agency for International Development (USAID) zilisimama baada ya kuvunjwa kwake na utawala wa Donald Trump mwaka jana.
USAID ilikuwa moja ya wafadhili wakuu wa Northern Rangelands Trust (NRT), shirika la uanachama linalosimamia na kusaidia zaidi ya hifadhi 40 za jamii katika kaunti 10 nchini Kenya. NRT ililazimika kuwaachisha kazi karibu wafanyakazi 100 baada ya msaada wa USAID kusimama Januari 2025. NRT pia imekuwa ikisumbuliwa na migogoro ya uongozi na kesi za kisheria kuhusu uhalali wa hifadhi mbili mpya za jamii.
Msiba hauji peke yake
Hifadhi ya Jamii ya Cherab, mojawapo ya mashirika mawili yanayoshirikiana na NRT, yaliyokuwa katikati ya mzozo huo wa mahakamani, halikuathiriwa tu na kutatizika kwa shughuli zake; bali pia lilizama zaidi katika matatizo ya kifedha baada ya programu ya msaada wa Wakala wa Maendeleo wa Ufaransa (AFD) kumalizika karibu wakati huo huo.
“Ufadhili wa AFD ulituwezesha kulipa mishahara, kugharamia shughuli za kila siku, na kuweka mafuta kwenye magari ya doria. Tangu ufadhili huo ulipokoma, walinzi wetu wamekaa kwa miezi sita hadi saba bila mishahara. Licha ya hali hiyo, bado wanafanya doria kwa kiwango kidogo wakitumia pikipiki au kutembea kwa miguu,” Abdi Dima Mohamed, meneja wa Hifadhi ya Jamii ya Cherab, alisema.

Mohamed ni miongoni mwa viongozi wa uhifadhi wa jamii ambao wamekuwa wakizishawishi serikali za kaunti kaskazini mwa Kenya kuingilia kati na kuzinusuru hifadhi za jamii zinazokabiliwa na changamoto za kifedha.
“Tunaziambia serikali za kaunti kwamba hifadhi za jamii ni muhimu kwa uchumi wa eneo hili. Zinasaidia sekta ya utalii na zina uwezo wa kuongeza mapato ya serikali za kaunti. Lakini kumekuwa na ucheleweshaji wa kupitishwa kwa Miswada ya Hifadhi za Jamii ili kuwezesha serikali za kaunti kufadhili hifadhi hizo,” Mohamed aliongeza.
Kwa Lakara, changamoto zinazowakabili walinzi wa wanyamapori wa jamii ni zaidi ya mishahara iliyochelewa au vifaa visivyotosha. Zinazua maswali magumu kuhusu mustakabali wa uhifadhi katika maeneo ambapo jamii na wanyamapori wanategemeana na kuishi pamoja.
“Sisi ndio wa kwanza kufika na kuchukua hatua wakati tembo wanapoingia vijijini, wakati mifugo inaposhambuliwa au majangili wanapoingia katika hifadhi zetu za jamii,” anasema. “Walinzi wa hifadhi wasipopata msaada unaostahili, watu na wanyamapori wote wataathirika.”
Kadiri msaada wa kigeni unavyopungua na hifadhi za jamii zikitafuta vyanzo vipya vya ufadhili, wataalamu wa uhifadhi wanaonya kwamba kudumisha nguvu kazi ya walinzi wa hifadhi wenye motisha na vifaa vya kutosha kutahitaji uwekezaji mkubwa zaidi kutoka kwa serikali, sekta binafsi na jamii husika.
Bila msaada huo, itakuwa vigumu zaidi kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika kulinda wanyamapori wa Kenya na kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, hasa wakati ambapo athari za mabadiliko ya tabianchi zinazidi kuongezeka.
Picha ya bango: Mlinzi wa wanyamapori mwanamke akiwa kazini porini katika eneo la Amboseli. Picha kwa hisani ya IFAW.
It’s time we recognize the roles of rangers — and prioritize their safety (commentary)