- Lengo ni kupunguza uzalishaji wa gesi ya kaboni dioksidi (CO₂) inayotokana na mafuta ya magari.
- Taasisi za umma zaagizwa kujumuisha ununuzi wa magari yanayotumia umeme na gesi asilia.
- Mwongozo wa Kitaifa wa Sera ya Magari ya Umeme umeanza kutekelezwa.
- Mpaka sasa kituo cha kuchajia magari ya umeme kwa nchi nzima kiko kimoja.
Na Mpango wa Tanzania wa kuhamia matumizi ya nishati safi katika usafiri ili kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa inayotokana na mafuta ya magari, umeanza kutekelezwa. Hadi sasa baadhi ya hatua za mpango huo zinaendelea kutekelezwa kwa mafanikio ingawa pia kuna changamoto kadhaa zinazohitaji kushughulikiwa.
Juni 12, mwaka huu, serikali ya Tanzania ilitangaza dhamira yake ya kuhamia matumizi ya nishati safi kwenye vyombo vya usafiri kwa kuzielekeza taasisi zote za umma kuanza kujumuisha ununuzi wa magari yanayotumia umeme na gesi asilia katika mipango na bajeti zao.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omari, wakati akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, alisema lengo la mpango huo ni kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa inayotokana na mafuta ya magari ambayo huchochea athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupunguza gharama kubwa za kununua mafuta.

Hatua hiyo pia ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Michango ya Taifa Iliyoamuliwa (NDCs) chini ya Mkataba wa Paris ambapo Tanzania imeahidi kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kupitia sekta za nishati na usafiri.
Uzalishaji wa hewa ya ukaa
Mpango wa kutumia nishati safi kwenye vyombo vya usafiri nchini Tanzania, iwapo utafanikiwa, utapunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa hewa ukaa inayotokana na mafuta ya magari ambayo huchochea athari za mabadiliko ya tabianchi.
Msololo Onditi, Mtaalam wa mabadiliko ya tabianchi na Mshauri wa Masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika Shirika la Maendeleo la Ujerumani Tanzania (GIZ), anasema kila lita moja ya petroli inayochomwa katika injini za vyombo vya usafiri kama magari, huzalisha karibu kilo 2.3 za gesi ya kaboni diokside (CO₂) huku lita moja ya dizeli ikizalisha takribani kilo2.7 za gesi hiyo.
Gesi hiyo hujikusanya kwenye anga kwa miaka mingi na hufanya kazi kama blanketi linalonasa joto la jua na kuongeza joto la dunia. Kadiri magari yanavyoongezeka, ndivyo kiwango cha gesi hiyo kinachoingia angani kinavyoongezeka na kusababisha kuongezeka kwa joto duniani ambalo ni kichocheo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati (International Energy Agency – (IEA) sekta ya usafiri inachangia takribani robo ya uzalishaji wa gesi ya kaboni diokside, huku usafiri wa barabarani ukiwa ndiyo sehemu kubwa zaidi ya mchango huo.
“Hii ina maana kwamba bila kupunguza utegemezi wa magari yanayotumia petroli na dizeli, itakuwa ngumu kwa dunia kufikia malengo ya kupunguza ongezeko la joto hadi nyuzi joto 1.5°C kama yalivyowekwa katika Mkataba wa Paris,” anasema.
Mahfoudh anasema kwa kuwa magari ya umeme hayatoi moshi kupitia bomba la kutolea nje (zero tailpipe emissions) matumizi ya nishati safi kwenye vyombo vya usafiri yatapunguza kwa kiwango kikubwa uchafuzi wa hewa mijini na kupunguza uzalishaji wa gesi zinazochochea mabadiliko ya tabianchi.
Nishati kutokana na gesi asilia
Fredrick Mushi, Mkurugenzi wa Programu na Uendeshaji wa Elico Foundation anasema Tanzania inaweza kuhamia nishati ya umeme na gesi kwenye vyombo vya usafiri kwa sababu ina rasilimali za kutosha za kuzalisha umeme kupitia maji, gesi asilia, jua, upepo na jotoardhi.
“Tanzania ina akiba kubwa ya gesi asilia kama nishati ya kuendeshea magari. katika magari kama ile ya Songosongo na Madimba ambayo hutoa kiwango kidogo cha kaboni kuliko petroli na dizeli,” anasema Mushi.
Mikakati iliyopo
Katika kupunguza uzalishwaji wa hewa chafu kupitia vyombo vya usafiri, mwaka 2024, Serikali ya Tanzania iliandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Sera ya Magari ya Umeme ambayo imeanza rasmi utekelezaji wake.
Juni 12, mwaka huu, Serikali ya Tanzania ilitangaza mpango wa kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi kwenye vyombo vya usafiri kwa kuzielekeza taasisi zote za umma kuanza kujumuisha ununuzi wa magari yanayotumia umeme na gesi asilia katika mipango na bajeti zao.
Ngereja Mgejwa, Jiolojia Mkuu katika Wizara ya Nishati, anasema kutekeleza mpango huo serikali imefanya yafuatayo: imejenga vituo 18 vya kujaza gesi asilia (CNG) katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Mtwara na kukamilisha ujenzi wa kituo cha kwanza cha kuchaji magari ya umeme jijini Dodoma, huku ikiwa imepanga kujenga vituo vingine 49 ifikapo Novemba mwaka huu ili kuanzisha mtandao wa kitaifa wa huduma za kuchaji magari hayo.
“Tulianza kwa kuweka mazingira wezeshi kupitia Mfumo wa Kitaifa wa Sera ya Magari ya Umeme, kuandaa kanuni na miongozo, pamoja na kutoa vivutio vya uwekezaji. Sasa tupo katika hatua ya utekelezaji kwa kujenga miundombinu na kuhamasisha matumizi ya magari yanayotumia umeme na gesi asilia,” anasema Mgejwa.
Ameongeza kuwa Serikali pia imepunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa baadhi ya magari yanayotumia umeme, ili kupunguza gharama za uagizaji na kuongeza upatikanaji wake nchini.
Aidha, serikali imeendelea kurahisisha mazingira ya uwekezaji kwa kutoa vibali kwa kampuni na taasisi binafsi kuagiza, kuingiza na kuuza magari yanayotumia umeme nchini, pamoja na kuwekeza katika huduma za kuchaji na matengenezo ya magari hayo.
“Lengo letu ni kujenga mazingira ambayo yataifanya sekta binafsi iwe mshirika mkuu wa serikali katika kuharakisha matumizi ya teknolojia za magari ya umeme na gesi asilia,” anasema.
Kwa mujibu wa Mgejwa, Wizara ya Nishati inaendelea kupanua miundombinu ya kuchaji magari ya umeme na kujaza gesi asilia, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi, kuandaa wataalamu wa matengenezo ya teknolojia hizo na kuhimiza taasisi za umma kuwa watumiaji wa mwanzo wa magari ya umeme na gesi.
Anasema lengo la muda mrefu ni kuwa na mfumo wa usafiri unaotumia nishati zinazozalishwa nchini, kupunguza matumizi ya mafuta ya petroli na dizeli, kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kuimarisha usalama wa nishati wa taifa.

Aidha Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omari, wakati akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma Juni 12, mwaka huu alisema katika bajeti kuu ya mwaka huo, serikali imependekeza kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa baadhi ya magari yanayotumia umeme katika hatua inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala nchini.
Aidha Serikali imependekeza kutoa unafuu wa ushuru wa forodha kwenye betri za umeme zinazotumiwa na wazalishaji au waunganishaji wa magari na pikipiki za umeme pamoja na kuendelea kutoa vivutio vya kikodi kwa waunganishaji na wazalishaji wa vyombo vya moto vinavyotumia umeme na gesi.
Uharibifu wa mazingira
Tanzania ilikuwa na takribani vyombo vya usafiri milioni 8.85 mwaka 2023 vikijumuisha magari, pikipiki, bajaji, malori na mabasi na zaidi ya asilimia 99 ya vyombo hivyo, vikiendeshwa na injini zinazotumia mafuta ya petroli au dizeli, ripoti kuhusu tathmini ya mpito kutoka matumizi ya mafuta ya petroli kwenda gesi asilia katika sekta ya usafiri wa barabarani Tanzania pamoja na mwongozo wa Sera ya Taifa wa Magari ya Umeme (2024), zinaonyesha.
Utegemezi huu mkubwa wa mafuta kwenye magari unaongeza uzalishaji wa gesi chafu kama kaboni dioksidi (CO₂), oksidi za nitrojeni (NOₓ) na methane ambazo huchafua hewa na kusababisha mmagonjwa nakuchochea athari za mabadiliko ya tabianchi.
Magari ya umeme Tanzania
Ili kutimiza azma ya serikali ya kupunguza au kumaliza uzalishwaji wa hewa ukaa, wataalam wanashauri matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia gesi na umeme vinavyotokana na nishati safi, pamoja na kuimarisha usafiri wa umma na teknolojia zenye ufanisi wa matumizi ya nishati.
Dkt. Pius Victor, Mhadhiri Katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Mwenyekiti wa Chama cha Usafiri wa Umeme (TAEMA), anasema lazima umeme unaotumika kuchaji vyombo vya usafiri utokane na nishati safi kama vile maji, upepo na jua.
Anasema kama idadi kubwa ya vyombo vya usafiri kama magari, bajaji na pikipiki za umeme vitakuwa vinachajiwa na umeme unaozalishwa na nishati inayotoa hewa chafu kama gesi na mafuta, tatizo bado litakuwa pale pale kwa sababu uzalishwaji wa hewa chafu utakuwa unaendelea.
Anaishauri serikali kupitia wizara ya nishati kuongeza uzalishwaji wa umeme kupitia maji kutoka kiasi cha sasa cha asilimia 54 na umeme jua kutoka asilimia moja iliyopo sasa, ili yaweze kumudu kuchaji idadi kubwa ya magari yatakayoingia nchini.
Mwongozo wa Sera
Dkt Pius anasema kuna haja ya Serikali kutengeneza sera itakayotoa mwongozo wa namna ya kuendesha sekta ya magari ya umeme ikiwamo kutengeneza mazingira rafiki kwa sekta binafsi kuendeleza teknolojia ya vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati safi nchini.
“Kwa sasa vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati safi gharama yake ni kubwa ukilinganisha na vinavyotumia mafuta, kwa sababu gharama za kuingiza nchini ni kubwa. Kukiwa na sera na miongozo inayoweka mazingira rafiki ya uwekezaji ikiwamo kutoa ruzuku, itasaidia kupunguza gharama na kuhamasisha Watanzania wengi kununua magari hayo,” anasema Dkt Pius.
Anasema Tanzania inatakiwa kujifunza kutoka Serikali ya Rwanda ambayo ilitoa msamaha wa kodi za uagizaji, kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa baadhi ya vyombo vya usafiri vya umeme na pia imewekeza katika vituo vya kuchaji.
Kenya pia imefanikiwa kutengeneza mazingira rafiki kwa kampuni binafsi zinazozalisha au kuunganisha pikipiki, mabasi na magari ya umeme pamoja na mifumo ya kubadilisha betri.
Changamoto
Fredrick Mushi, Mkurugenzi wa Programu na Uendeshaji wa Elico Foundation anasema kuwa uhaba wa vituo vya kuchajia magari na kujaza gesi unaweza kurudisha nyuma juhudi za serikali za kuhamia kwenye vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati safi.
Akitoa mfano, anasema mpaka sasa kituo cha kuchajia magari ya umeme kwa nchi nzima kiko kimoja mkoani Dodoma huku serikali ikitoa ahadi ya kuongeza vingine 50. Hali hiyo inasababisha wanaomiliki vyombo hivyo kwa sasa kuchajia magari kwenye nyumba na kutumia zaidi ya saa tatu, jambo ambao linachelewesha shughuli za maendeleo.
Anasema kuwa mtumiaji wa vyombo hivyo anapaswa kuwa na uhakika kwamba anaweza kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro au Dodoma kwa urahisi, kama ilivyo kwa magari yanayotumia mafuta, jambo ambalo haliwezekani bila kuwa na vituo vya kuchaji vilivyosambazwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Mmiliki wa kampuni inayo jihusisha na uuzaji wa magari ya umeme mkoani Dar es Salaam, Stephen Msikwa anasema kukosekana kwa vituo vya kuchajia magari ya umeme kwa haraka kuna katisha tamaa watumiaji kununua aina hizo za usafiri.

“Mfano gari za bei rahisi zinahitaji kuchajiwa kila baada ya mwendo wa kilometa 200 au 300 kwa hiyo watumiaji wanakosa uwanda mpana wa kutembea na magari haya kwa muda mrefu kutokana na uhaba wa vituo,” anasema.
Gharama za magari
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Zanzibar Climate Change Alliance (ZACCA), Mahfoudh Shabani Haji, anasema iwapo utekelezaji wa mpango huo utafanikiwa, hatua hiyo inaweza kuwa sehemu muhimu ya safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kijani unaopunguza uchafuzi wa mazingira, kuimarisha usalama wa nishati na kuchangia juhudi za dunia za kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi,” alisema.
Picha ya bango: Dk Pius Victor Mhadhiri Katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Mwenyekiti wa Chama cha Usafiri wa Umeme (TAEMA), akionyesha kituo cha kuunda vyombo vya usafiri wa umeme katika chuo hicho. Picha na Jenifer Gilla, Mongabay.