- Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro imeitupilia mbali rufaa ya Jamhuri, na kudumisha uamuzi wa kuwaachia huru Yahaya Juma na Masima Mlugu waliokuwa wakishtakiwa kwa kumiliki meno ya tembo.
- Washtakiwa walidaiwa kukutwa na vipande 18 na meno matatu ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 120,000 bila kibali halali.
- Mahakama ilibaini mkanganyiko katika ushahidi wa upande wa mashtaka, hasa kuhusu tarehe za kukamatwa na mlolongo wa vielelezo, jambo lililoibua shaka ya msingi.
- Jaji Stephen Magoiga alihitimisha kuwa mashtaka hayakuthibitishwa pasipo shaka, hivyo akatupilia mbali rufaa ya Jamhuri.
Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro imeitupilia mbali rufaa ya Jamhuri ya kupinga hukumu iliyowaachia huru Yahaya Juma na mwenzake.
Washitakiwa hao walikuwa wanadaiwa kukutwa na vipande 18 na meno matatu ya tembo yenye thamani ya Dola za Marekani 120,000.
Hukumu ya Mahakama hiyo ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Stephen Magoiga baada ya kusikiliza mawasilisho ya pande zote mbili.
Rufani hiyo iliyowasilishwa na Wakili wa Serikali Paulina Massawe ilitokana na uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Morogoro uliowaachia huru Yahaya Juma na Masima Mlugu waliokuwa wakikabiliwa na shtaka la kukutwa na vipande 18 na meno matatu ya tembo yenye thamani ya Dola za Marekani 120,000 bila kibali halali.
Mahakama ya Wilaya
Katika Mahakama ya Wilaya, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita, akiwemo mtunza vielelezo, askari aliyefanya ukamataji, shahidi huru aliyeshuhudia upekuzi na ukamataji, mhifadhi wa wanyamapori aliyefanya uthamini wa meno ya tembo, askari wa TANAPA aliyeshiriki operesheni pamoja na mpelelezi wa kesi.
Upande wa mashtaka uliwasilisha vielelezo saba, vikiwemo vipande 18 vya meno ya tembo, meno matatu kamili ya tembo, magunia mawili ya salfeti yaliyobebea meno hayo, pikipiki aina ya FEKON yenye namba T43 CNF, hati ya ukamataji na ripoti ya uthamini iliyoonyesha kuwa nyara hizo zilikuwa na thamani hiyo.
Kwa upande wa utetezi, washtakiwa wote wawili walitoa ushahidi wao wenyewe. Mshtakiwa wa kwanza aliwasilisha pia flashi diski iliyokuwa na video ya YouTube akidai kuwa meno ya tembo yaliyoonyeshwa kwenye taarifa ya habari hayakuwa na alama, tofauti na yale yaliyowasilishwa mahakamani kama vielelezo.
Mahakama ya Wilaya ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha shtaka pasipo mashaka na hivyo ikawafutia mashtaka na kuwaachia huru washtakiwa.
Upande wa Jamhuri
Akipinga uamuzi wa kuachiwa huru washtakiwa hao, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) alikata rufaa akidai mahakama ya wilaya ilikosea kisheria na kimantiki kwa kuhitimisha kuwa mashtaka hayakuthibitishwa pasipo shaka.
Wakili wa Serikali Pauline Massawe alidai ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka ulitosha kuwatia hatiani washtakiwa na kwamba hitilafu ya tarehe iliyojitokeza ilikuwa ndogo na isiyoathiri msingi wa kesi.
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, washtakiwa walikamatwa Agosti 17, 2024 baada ya polisi kwa kushirikiana na maofisa wa TANAPA kupata taarifa za siri kuhusu umiliki haramu wa nyara za Serikali.
Ilidaiwa kuwa operesheni hiyo iliongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OCCID) wa Morogoro, ambapo kibali cha upekuzi kilipatikana kabla ya kuwakamata washtakiwa katika eneo la Barabara ya Iringa karibu na mashamba ya Chuo Kikuu Cha Kilimo (SUA).
Polisi walidai walikuta vipande 18 na meno ya tembo matatu kamili yakiwa ndani ya magunia mawili yaliyokuwa yamefungwa kwenye pikipiki.
Hata hivyo, washtakiwa walikana madai hayo. Mshtakiwa wa kwanza alidai kuwa alikamatwa katika nyumba ya kulala wageni inayoitwa Ngurasi eneo la Maelewano karibu na Stendi ya Mabasi ya Mafiga, huku mshtakiwa wa pili akidai alikamatwa Kasanga alipokuwa akisubiri usafiri kwenda Mikumi.
Hukumu
Akitoa hukumu baada ya kusikiliza mawasilisho ya pande zote mbili, Jaji Magoiga alieleza kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha shtaka hilo pasipo kuacha shaka kutokana na kuwepo kwa mkanganyiko mkubwa kuhusu tarehe ya kukamatwa kwa watuhumiwa na kukamatwa kwa meno hayo ya tembo.
Awali, Jamhuri ilidai kuwa Agosti 18, 2024 watuhumiwa walikamatwa eneo la Mashamba ya SUA, Mafiga, Manispaa ya Morogoro wakiwa na meno matatu ya tembo na vipande 18 vya meno ya tembo bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori, jambo lililowafanya kufunguliwa mashtaka ya kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria.
“Mahakama Kuu ilibaini kuwa shahidi wa sita wa upande wa mashtaka (mpelelezi) alieleza kuwa vielelezo vilipokelewa Julai 18, 2024, ilhali mashahidi wengine walidai watuhumiwa na meno hayo ya tembo walikamatwa Agosti 17, 2024,”alisema Jaji Magoiga .
Jaji Magoiga alisema tofauti hiyo iligusa msingi wa mlolongo wa uhifadhi wa vielelezo na kuibua shaka ya msingi ambayo haikufafanuliwa wakati wa usikilizwaji wa kesi.
Alisema upande wa mashtaka haukumhoji tena shahidi huyo ili kuondoa mkanganyiko huo hivyo ushahidi wake uliendelea kubaki kama ulivyokuwa na kuathiri uaminifu wa kesi nzima.
Mahakama ilisisitiza kuwa katika mashauri ya jinai, shtaka lazima lithibitishwe pasipo kuacha shaka yoyote ya msingi.
Kutokana na sababu hizo, Mahakama Kuu ilihitimisha kuwa rufaa ya Jamhuri haina msingi, ikaifuta na kudumisha uamuzi wa Mahakama ya Wilaya wa kuwaachia huru Yahaya Juma na Masima Mlugu.
Picha ya Bango: Biashara haramu ya pembe za ndovu inaendelea kuwa tishio kubwa kwa uhifadhi wa tembo, ikichochea ujangili na kuhatarisha juhudi za kulinda wanyamapori nchini na duniani. Picha kwa hisani ya African People &Wildlife.