- Sagalla caecilian, amfibia anayepatikana pekee katika Msitu wa Sagalla, anatishiwa na mikaratusi, ukataji miti ya kiasili na mabadiliko ya tabianchi.
- Jamii ya Sagalla imeungana na wadau wa uhifadhi kuondoa mikaratusi, kupanda miti ya kiasili na kuhamasisha kilimo endelevu ili kurejesha makazi ya kiumbe huyo.
- Wataalamu wanasema Sagalla caecilian husaidia kuboresha rutuba ya mchanga na kuhifadhi unyevunyevu, hivyo kunufaisha kilimo na ikolojia.
- Zaidi ya miti 10,000 ya kiasili imepandwa, lakini juhudi zaidi zinahitajika kulinda makazi ya kiumbe huyo na kuhakikisha anaendelea kuishi.
TAITA TAVETA, Kenya – Kusini mashariki mwa Kenya, ndani ya msitu mnene wa Sagalla, kunapatikana mnyama wa kipekee wa jamii ya amfibia anayejulikana kama Sagalla caecilian (Boulengerula niedeni).
Mlima huo wa Sagalla, wenye urefu wa zaidi ya mita 1,400 kutoka usawa wa bahari, una miti ya aina mbalimbali inayounda makazi ya Sagalla caecilian.
Kiumbe wa kipekee ulimwenguni
Kilomita 18 kutoka tambarare za mji wa Voi, Mongabay ilizuru msitu huo wa Sagalla unaoweza kufikiwa kwa gari na pikipiki hadi sehemu fulani, na sehemu iliyosalia hufikiwa kwa miguu.

Mongabay ilitaka kufahamu iwapo jamii inatambua spishi hii na faida zake kwa ikolojia, na ilifanikiwa kukutana na wanajiji wakiwa katika shughuli zao za kila siku shambani. “Mimi sikuwa nafahamu mnyama huyu. Nilikuwa namuona shambani kisha namkatakata kwa jembe au namgonga kwa mawe ili afe, kwa sababu anafanana na nyoka,” anasema Jemimah Mwaiga.
Sasa Mwaiga anafahamisha Mongabay kuhusu umuhimu wa kiumbe huyo, na kufafanua jinsi walihusishwa katika kutafuta jina lake la kinyumbani, “kilima mrota”.
“Tulijifunza kuwa kiumbe huyo husaidia katika ukulima na ubora wa mchanga kwa kuchanganya mchanga na virutubisho vilivyo mchangani na kuongeza rutuba ya asili ya mchanga,” Mwaiga anaelezea Mongabay.
Mwanasayansi wa masuala ya mchanga na mazingira Kenneth Macharia wa shirika la Edge of Existence, anasema kiumbe huyu ni wa kipekee katika mlima wa Sagalla. Huishi katika mazingira yenye unyevunyevu, na mchanga wenye rutuba. Macharia anaongeza: “Jamii zinaweza kuimarisha kilimo pamoja na utunzaji wa mazingira kwa kutumia mbinu bora katika mchanga kama vile kupanda miti ya kiasili, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kudumisha rutuba ya asili ya mchanga”.

“Mchanga wenye afya unaogeuzwa na kuchanganywa na kiumbe huyu hushikilia maji vyema na kupunguza athari za ukame kwa mimea. Wakulima wanafaa kupanda nyasi aina ya Vetiver na miti asili ili kuzuia mmomonyoko wa udongo. Hivyo watakuwa wanachangia uhifadhi wa kiumbe huyu pamoja na kuboresha uzalishaji wa kilimo, na hatimaye kuimarisha ikolojia inayosaidia wadudu wachafushaji mimea kama vile nyuki, na pia kuzuia wadudu waharibifu kama viwavi,” Macharia alielezea Mongabay.
Mtaalamu wa wanyama wa jamii ya amfibia katika makumbusho ya kitaifa ya Kenya, Dkt Patrick Malonza, naye anasisitiza upandaji wa miti ya kiasili kama vile Nuxia congesta, Bridelia micrantha (Mwera), Croton megalocarpus, Markhamia species, Ficus species, Melia volkensii (kirumbutu), Albizia gummifera (msuruwache), Newtonia buchananii na Warburgia ugandensis.
“Hii ndio miti iliyopandwa na inaendelea kupandwa. Japo kuna changamoto ya kuendelea kuishi kwa miche kutokana na kiangazi, jamii imejitolea kuendeleza juhudi hizo, haswa wakati kunaponyesha, ili tuondoe mikaratusi,” anasema Malonza.
Faida kwa jamii, tishio kwa kiumbe
Christopher Mwakio, mkulima kutoka Sagalla, anaelezea Mongabay: “Japo shingo upande, lisilo budi kutendwa lazima litendwe. Mimi binafsi naipenda mikaratusi kwa kuni na mbao, kwa sababu imenifaidi muda mrefu. Lakini ni muhimu iondolewe na kupandwe miti ya kiasili ili kuweza kuwahifadhi viumbe hao na mazingira. Sasa mimi nimegeukia biashara ndogondogo ya vyakula vya shambani na ukulima”.
“Kwanza majani ya mikaratusi hii hayakauki kabisa kama mingine, lakini yanafunika ardhi kama vile karatasi za plastiki na kusababisha udongo usichanganywe na viumbe hao,” alifafanua.

Utafiti unaonyesha kuwa mbali na topografia ya milima ya Sagalla na mabadiliko ya tabianchi, miti ya mikaratusi imechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa kiumbe huyu kwa kunyonya maji na kukausha ardhi.
Amfibia huyu alitambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2005 na kisha kuorodheshwa kuwa hatarini na shirika la kimazingira la IUCN mwaka 2013. Tangu wakati huo, hakujakuwa na taarifa mpya kuhusu hali ya kiumbe huyo.
Aidha, wataalamu wa amfibia wanasema kiumbe huyu huishi vyema kwenye mazingira yaliyo na miti mingi isiyokauka, ambayo huweka unyevunyevu unaomwezesha kuishi, na ambapo pia hupata chakula chake.
Hamasa muhimu kwa jamii
Utafiti unaonyesha kuwa ukosefu wa ufahamu wa kutosha miongoni mwa jamii, kukatwa kwa miti ya kiasili pamoja na mabadiliko ya tabianchi vinatishia kutoweka kwa amfibia huyu.
Daniel Mwaiga, mwenyekiti wa kikundi cha kijamii linalojulikana kama Kirani Self Help Group, ambaye pia ni mzee wa kijiji eneo la Kishamba Juu, Sagalla, anasema awali hawakufahamu faida zake, lakini kutokana na hamasa za mara kwa mara kutoka kwa wadau wa mazingira, jamii imekumbatia spishi hii. “Sasa wanajamii wameelewa maana na faida za Sagalla caecilian. Ikifika wakati wa mvua, kila mmoja anapanda miti ya kiasili,” anasema Mwaiga.
Kulingana na mtaalamu wa masuala ya bioanuai na misitu kaunti ya Taita Taveta James Mwang’ombe, mikaratusi ilipandwa wakati wa uongozi wa ukoloni ili kuzalisha mbao zilizotumiwa kama mataluma ya reli wakati wa ujenzi, pamoja na kutumika kama kuni kwa injini za mvuke.
“Ilikuwa ni njia moja ya kuzuia uharibifu wa misitu ya kiasili, kwa sababu miti ilihitajika kutumika katika ujenzi wa reli. Walipanda mikaratusi, ambayo ni miti migumu inayokuwa kwa muda mfupi, kwa utumizi wa mbao. Serikali ilipendekeza mikaratusi ipandwe kwa wingi kutimiza mahitaji ya jamii kama vile kuni na mbao za kujengea. Wakati huo bioanuai haikutiliwa mkazo kama sasa. Hivyo ndivyo mazingira yaliendelea kudorora,” anasimulia Mwang’ombe.
Mkurugenzi huyo anasema muungano wa Taita Taveta Wildlife Forum, ukishirikiana na Chuo Kikuu cha Kent nchini Uingereza, pamoja na ushirika wa Zoological Society of London, kwa msaada kutoka wakfu wa Darwin Initiative, walianzisha mchakato wa kuanza kushinikiza mabadiliko ili kuboresha mazingira katika mlima Sagalla kupitia kupanda miti ya kiasili katika sehemu zilizo tupu, pamoja na mashambani.
“Jamii ilitengeneza vitalu vya miche au miti ya kiasili na ikaanza kupanda miti chini ya uangalizi wa Sagalla Community Forest Association. Hii ilikuwa ni pamoja na shughuli mbalimbali kama vile kubadili mifumo ya ukulima hadi kilimo endelevu, kuwapa mafunzo na kukataza utumizi wa kemikali shambani. Pia walihimiza upandaji wa migomba ili kuboresha mazingira yanayofaa kwa kiumbe huyo, kufuga samaki na nyuki kwa kipato mbadala,” aliambia Mongabay.

Anasisitiza kuwa juhudi zaidi zinahitajika kuendelea kumhifadhi kiumbe huyo, na kuboresha mazingira kwa jumla, akisema kwa sasa ni hekta sita pekee za eneo ambazo zimepandwa miti ya kiasili.
Mabadiliko ya tabianchi
Malonza anasema mabadiliko ya tabianchi, kulima kandokando ya vyanzo vya maji, ukataji miti na utunzaji mbovu wa mchanga na mazingira, vimeongeza shinikizo kwa mazingira hayo yaliyo tayari kuwa tete.
Anahimiza kuwa, ili kukabiliana na haya na kuilinda Sagalla caecilian, ni lazima jamii, wadau na watetezi wa mazingira na viumbe hai, wanasayansi na viongozi washikamane.
“Tulibuni mfumo wa kuboresha na kurejesha hali ya mwanzo ya mazingira kwa jamii, tukilenga pakubwa kuondoa mikaratusi na kupanda miti ya kiasili, na kuimarisha ukulima endelevu. Miti zaidi ya 10,000 imepandwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, ikiwemo Taita Taveta Wildlife Forum, Nature Kenya, Kenya Forest Service, na vikundi vya kijamii. Juhudi hizo zinaendelezwa na wanajamii,” anasema Malonza.
Kwa mujibu wake, njia moja iliyowezesha jamii hiyo kukumbatia juhudi za kumtunza na kumhifadhi Sagalla caecilian ilikuwa ni kuwahusisha jamii katika kumpa jina la kinyumbani. “Mwaka 2013, jamii hiyo ilimpa Sagalla caecilian jina ‘Kilima mrota’, likimaanisha kuwa hunenepa akiwa katika mazingira mazuri na hukonda anapowekwa juani,” asema Malonza.
Macharia anasema juhudi za jamii za sasa za kupanda miti asili na kulinda vyanzo vya maji zimeonyesha hatua bora za kurudisha hali ya misitu asili. “Elimu inayotolewa mara kwa mara kwa jamii na warsha za kuwafunza kuhusu uhifadhi wa mazingira na viumbe mbalimbali itaendelea kujenga uhusiano mwema kati ya afya ya mchanga, viumbe wasiopatikana kwingineko duniani, na kilimo hakika endelevu,” alisema.
Wanasayansi wanaonya kuwa kuendelea kupungua kwa viumbe vya amfibia kama vile Sagalla caecilian ni ishara ya kuendelea kudorora kwa mazingira. Macharia na Malonza wanaelezea kuwa hili si suala la kijamii tu, ila inafaa kukumbusha ulimwengu kuwa kupotea kwa bioanuai huanza kimya kimya katika misitu midogo, viumbe wasioangaziwa pakubwa na katika kila maamuzi yanayotolewa katika utumizi wa ardhi, ambayo taratibu yameendelea kubadili mustakabali wa mazingira asili.
Hakuna takwimu kamili
Malonza anasema hakuna takwimu kamili za kuashiria kupungua au kuongezeka kwa viumbe hao, ila idadi yao inaweza kukadiriwa kutokana na ongezeko la viumbe wanaoonekana katika eneo hilo. “Wananchi wengi walinunua miche wakapanda kwenye mashamba yao kwa manufaa ya mbao, fito za kujengea, na kuni. Serikali ilipanda miti hiyo pamoja na misonobari (pine) kuongeza idadi ya miti,” Malonza aliambia Mongabay.
Aidha, anasema hakuna maelezo kamili kuhusu miti ya mikaratusi iliyoondolewa kufikia sasa, kwa sababu inaondolewa kwa sehemu na kupanda miti mbadala.
“Wanajamii wengine hawajapendelea suala la kuondolewa kwa mikaratusi, mashambani mwao, kwa sababu inawafaidi kwa mbao na kuni, na fedha za kujikimu maisha. Wanaendelea kupewa hamasa kuhusu njia mbadala za kupata fedha. Pia kwa upande wa misitu ya serikali, zoezi hilo linafanyika kwa hatua, kwani kukata miti yote kwa pamoja italeta mmomonyoko wa udongo na kupoteza idadi ya miti pamoja na kuongeza halijoto,” anaelezea Malonza.

Mwang’ombe anaelezea kuwa idadi ya viumbe hawa haiwezi kubainika, kwa sababu asili yao ni ya “Subterranean”. Hii ina maana kuwa maumbile yao ni ya chini ya ardhi. “Takwimu za mwaka 2024, zinaorodhesha viumbe hivyo kuwa 900 katika kila hekta moja, kwa sababu ya kuendelea kuharibiwa kwa mazingira yao ya unyevu, inaweza kusemekana kuwa idadi yao inapungua,” Mwang’ombe aliambia Mongabay.
Mkurugenzi huyo anasema, suluhu ni kupunguza athari zinazoweka viumbe hawa hatarini, ikiwemo kuondoa kabisa mikaratusi na misonobari, na kuhimiza kilimo endelevu.
“Kufikia sasa, mikaratusi ingalipo. Itakuwa vyema iwapo serikali itachukua jukumu kwa haraka kubuni mwelekeo wa kuziondoa mikaratusi na kupanda miti ya kiasili,” aliongeza Mwang’ombe.
“Sisi kama jamii tumejitolea kumhifadhi spishi hii baada ya kupewa ufahamu kumhusu na manufaa yake katika mchanga, kilimo na ikolojia kwa ujumla,” Mwaiga aliambia Mongabay.
Picha ya bango: Mnyama wa kipekee wa jamii ya amfibia anayejulikana kama Sagalla caecilian (Boulengerula niedeni). Picha kwa hisani ya Edge of Existence.