- Raia wa Korea Kaskazini, Un Hyok Ra (37), ameachiliwa huru na Mahakama ya Kisutu baada ya DPP kuwasilisha nolle prosequi, akieleza kuwa Jamhuri haina nia ya kuendelea na kesi hiyo.
- Mahakama pia imeamuru Ra aondoke nchini Tanzania, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ombi la kumtangaza kuwa persona non grata.
- Ra alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kumiliki na kufanya biashara ya vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya zaidi ya TSh6.47 bilioni ($2.45 milioni) bila kibali.
- Kesi hiyo ya uhujumu uchumi ilikuwa imeahirishwa mara kadhaa kwa madai ya upelelezi kutokamilika, kabla ya DPP kusitisha mashtaka, hatua ambayo kisheria haizuii kufunguliwa tena kwa shauri hilo endapo itahitajika.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imemwachilia huru na kuamuru aondoke nchini Raia wa Korea Kaskazini Un Hyok Ra (37) aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya Uhujumu Uchumi baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuomba hivyo kwa maelezo kwamba upande wa Jamhuri hawana nia ya kuendelea na shauri hilo.
Maombi hayo ya Jamhuri yaliwasilishwa mahakamani na Wakili wa Serikali Mkuu, Twawabu Issa mbele ya Hakimu Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mwasha aliyekuwa akisikiliza shauri hilo dhidi ya mshtakiwa Ra aliyedaiwa kukutwa na vipande 504 vya meno ya tembo bila kibali.
Wakili Twawabu alidai kuwa DPP kwa mamlaka aliyonayo kisheria aliwasilisha uamuzi wa kusitisha mashtaka (nolle prosequi) (chini ya Kifungu cha 92 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023 ambapo zamani kilikuwa Kifungu cha 91 kabla ya marekebisho ya 2022) akionyesha kuwa Jamhuri haina nia ya kuendelea na shauri hilo hivyo akaomba mahakama imwachie huru mshtakiwa.
Mshitakiwa atakiwa kuondoka nchini
Upande wa mashtaka pia uliwasilisha maombi “persona non grata” kuonyesha kuwa mshtakiwa huyo hatakiwi kuendelea kubaki nchini Tanzania na anatakiwa kuondoka.
Mahakama baada ya kusikiliza maombi hayo iliyakubali na kuamuru mshtakiwa aachiliwe huru na aondoke nchini.
Katika shauri lolote la jinai na katika hatua yoyote kabla ya hukumu au uamuzi, DPP anaweza kuwasilisha nolle prosequi kwa kuitaarifu Mahakama kuwa Jamhuri haitaendelea na mashtaka lakini haizuii kumshtaki tena mshtakiwa pale inapohitajika kufanya hivyo.
Ra alifikishwa mahakamani mara ya kwanza Mei 5 , 2026 akikabiliwa na mashtaka mawili, kukutwa akimiliki nyara za Serikali ambazo ni vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya TSh6,476,534,750 ($2453235) na kujihusisha na biashara hiyo haramu.
Shauri hilo la Uhujumu Uchumi namba 10054 la mwaka 2026 lilikuwa likitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Salome Mwasha na liliahirishwa mara kadhaa kwa kile kilichoelezwa kuwa upelelezi haukuwa umekamilika huku mshtakiwa akiwa mahabusu.
Mshtakiwa Ra baada ya kupanda kizimbani mara ya kwanza shauri lake lilitajwa tena baada ya siku 14 yaani Mei 25 mwaka huu bila mshtakiwa kuwepo mahakamani. Juni 9, 2026 wakati shauri lilipotajwa tena Ra hakufikishwa mahakamani na kesi iliahirishwa. Hata hivyo Juni 23, 2026 tarehe ambayo kesi ingeletwa tena kortini, ilibainika kuwa shauri hilo limeshaondolewa.
Awali ilidaiwa katika hati ya mashtaka kuwa Aprili 19, 2026 katika eneo la Hoteli ya Golden Tulip–Masaki, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa akimiliki nyara za Serikali ambazo ni vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya TSh6,476,534,750 ($2453235), mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali au leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika shtaka la pili, Ra ambaye ni Mkazi wa Mikocheni Dar es Salaam, alituhumiwa kuwa tarehe hiyo na mahali hapo alijihusisha na biashara ya nyara za Serikali kwa kuuza vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya TSh6,476,534,750 ($2453235) mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali au leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Picha ya Bango:Raia wa Korea Kaskazini Un Hyok Ra (37) aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya Uhujumu Uchumi ameachiwa huru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuomba hivyo kwa maelezo kwamba upande wa Jamhuri hawana nia ya kuendelea na shauri hilo. Picha kutoka mtandaoni.