- KWS yashutumiwa kuwazuia na kuwanyanyasa walalamikaji wenza wakati wa ukaguzi wa mahakama kuhusu ujenzi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nairobi.
- Zaidi ya Wakenya 4,642 wametia saini ombi wakitaka mahakama iamue uhalali wa ujenzi wa BICC na uhamishaji wa Kituo cha Wanyama Yatima.
- Wanamazingira waonya mradi huo utahatarisha msitu wa asili na makazi ya faru weusi walio katika hatari ya kutoweka.
- KWS yatetea mradi, ikisema utaboresha huduma za uhifadhi wa wanyamapori na kutoa ajira kwa takriban watu 500.
NAIROBI, Kenya – Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya (KWS) limeshutumiwa kwa kuwazuia na kuwanyanyasa walalamikaji wenza katika kesi inayopinga uhamishaji wa Kituo cha Kuhifadhi Wanyama Yatima cha Nairobi (Nairobi Animal Orphanage).
Mnamo Julai 16, Mahakama ya Mazingira na Ardhi jijini Nairobi ilimwagiza Naibu Msajili wake, Vincent Kiplagat, kutembelea eneo linalobishaniwa akiwa pamoja na pande zote katika kesi hiyo ili kuandaa na kuwasilisha ripoti mahakamani.
Katika taarifa iliyotumwa kwa Mongabay, shirika la Save the Nairobi National Park (SaveNNP) lililaani kile lilichokiita “vitisho na vitendo vya kutisha” kutoka kwa maafisa wa KWS, pamoja na hatua ya kuwanyima wanaharakati hao ruhusa ya kuingia katika eneo la ziara.
SaveNNP ilisema hatua hiyo inapingana na mwaliko wa KWS kwa vyombo vya habari kushiriki katika ziara hiyo ya mahakama.

Mongabay iliona barua ya KWS iliyowaalika wanahabari kuhudhuria ziara ya eneo hilo iliyoongozwa na Msajili wa Mahakama ya Mazingira.
Katika taarifa yao, SaveNNP na JustAct ziliishutumu KWS kwa kutaka “kudhibiti simulizi” kuhusu mradi huo na kuhakikisha sauti za Wakenya hazisikiki mahakamani wala kupitia vyombo vya habari wakati wa ukaguzi wa eneo hilo. Madai kama hayo pia yalitolewa na Friends of Nairobi National Park.
Msemaji wa KWS, Duncan Wanyama, alisema wageni hao hawakuzuiwa kuingia, na kwam ba askari wa wanyamapori walikuwa wakitekeleza tu taratibu za kawaida zinazotumika ndani ya hifadhi hiyo, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Wanaharakati hao walisema walalamikaji wenza waliruhusiwa kuingia baadaye, lakini ni baada ya maafisa wa mahakama, wawakilishi wa KWS, wanahabari na mwakilishi pekee wa kisheria wa walalamikaji aliyeruhusiwa kuingia hifadhini kukamilisha ukaguzi wa eneo hilo.
Hadi sasa, Wakenya 4,642 wametia saini ombi linaloitaka Mahakama ya Mazingira na Ardhi kuamua iwapo ujenzi wa kituo hicho unaweza kuendelea bila kuzingatia sheria husika na Katiba.
Wanamazingira wanaonya kuwa kutenga takriban ekari 76 hadi 89 za Hifadhi ya Taifa ya Nairobi kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Bomas (Bomas International Conference Complex – BICC), kuhamisha Kituo cha Kuhifadhi Wanyama Yatima cha Nairobi na kujenga maegesho ya magari 1,300 kutahatarisha msitu wa asili unaolindwa pamoja na makazi ya faru weusi, ambao wako katika hatari kubwa ya kutoweka.
Kwa upande wake, KWS imetetea mradi huo ikisema utajumuisha miundombinu ya kisasa zaidi, ikiwemo hospitali ya wanyamapori, huduma bora kwa wageni na nafasi kubwa zaidi ya kushughulikia wanyamapori wanaookolewa. Shirika hilo pia linasema mradi huo utachochea uchumi wa eneo hilo na kutoa ajira kwa takriban watu 500.
Kituo cha sasa cha kuhifadhi wanyama yatima kilianzishwa mwaka 1964. Mkurugenzi Mkuu wa KWS, Erastus Kanja, amesema maboresho yanayopangwa yataongeza uwezo wa kuwaokoa na kuwakarabati wanyamapori pamoja na kuimarisha elimu ya uhifadhi.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Kanja alisema kituo kipya “kitatuwezesha kuwa na eneo linalofanana zaidi na mazingira ya porini ambapo tunaweza kuanza kuwarejesha wanyama. Wanyama ambao tumefanikiwa kuwarejesha porini hadi sasa ni faru weusi, faru weupe na tembo.”
Hata hivyo, wanaharakati wanasema tukio la Julai 22 linaonyesha ukosefu wa uwazi katika utekelezaji wa mradi huo.
“Kilichotokea jana kinaonyesha ukosefu wa uwazi, dharau kwa ushiriki wa umma na mwelekeo wa kutumia nguvu pale ambapo KWS haipati inachotaka,” walisema. “Hii inafuatia matumizi ya nguvu kupita kiasi na kukamatwa kwa waandamanaji wa amani wiki chache zilizopita.”
Picha ya bango: Simba wakipumzika ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nairobi. Picha kwa hisani ya SaveNNP.
Makala hii imesasishwa ili kujumuisha maoni ya KWS kuhusu madai kwamba iliwazuia wahusika katika kesi inayopinga ujenzi mpya katika Hifadhi ya Taifa ya Nairobi kuingia katika eneo lake.
Bioanuwai hatarini: Uhamisho wa kituo cha wanyama yatima wazua wasiwasi miongoni mwa wahifadhi