- Pascal Mirindi ni mwanaharakati wa mazingira kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) anayepinga uchimbaji wa mafuta nchini humo.
- Mnamo mwaka 2022, wakati serikali ya DRC ilipokuwa ikitangaza maeneo mapya ya uchimbaji wa mafuta mashariki mwa nchi hiyo, Mirindi na wenzake walianzisha vuguvugu la kuielimisha jamii kuhusu hatari zinazotokana na uchimbaji wa mafuta na gesi.
- Mwishoni mwa mwaka wa 2024, serikali ya DRC ilianzisha mradi wa ukanda wa kijani ulioenea kutoka mashariki hadi magharibi mwa nchi, kwa lengo la kutengeneza “msitu mkubwa zaidi wa kitropiki uliolindwa duniani,” lakini miezi michache baadaye, nchi hiyo ilitangaza sehemu mpya za uchimbaji mafuta zinazochukua asilimia 60 ya eneo lote la nchi.
- Mirindi alizungumza na Mongabay mnamo mwezi Juni kuhusu harakati zake na mustakabali wa DRC.
Pascal Mirindi ni mwanaharakati wa mazingira anayeishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na alizaliwa mjini Goma. Aliwahi kuwa mwanachama wa vuguvugu lisilotumia nguvu la La LUCHA, ambalo lilipigania demokrasia nchini DRC. Ingawa La LUCHA ndilo lililomleta kwenye harakati zisizotumia nguvu, alitumia fursa hiyo kupigania mifumo ya ikolojia ya Kongo.
Tangu mwaka 2024, Mirindi amekuwa mstari wa mbele katika kupinga uchimbaji wa madini, mafuta, na gesi katika Bonde la Kongo. Kupitia kampeni na juhudi za kuielimisha jamii, wao na wenzao walifanikiwa kuzuia mipango ya utafutaji wa mafuta ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Virunga. Kwa sasa, Mirindi anapambana dhidi ya uchimbaji katika maeneo mapya 30 ya mafuta yanayochukua asilimia 72 ya Ukanda wa Kijani wa Kongo, mradi muhimu zaidi wa uhifadhi nchini humo unaoenea katika sehemu kubwa ya Bonde la Kongo, eneo ambalo ni makazi ya maelfu ya wanyama na tegemeo muhimu kwa jamii nyingi nchini DRC.
Mnamo mwezi Juni, Mirindi alizungumza na Mongabay kuhusu anachomaanisha kupinga uharibifu akiwa ndani ya nchi husika na kuleta mabadiliko katika ngazi ya kimataifa, huku akilinda makazi ya viumbe walio hatarini kutoweka kama vile sokwe wa milimani (Gorilla beringei beringei) na okapi au twiga wa msituni (Okapia johnstoni), ambao hupatikana katika eneo hilo pekee.

Mahojiano haya yametafsiriwa kutoka Kifaransa na kuhaririwa ili kuzingatia urefu na uwazi.
Mongabay: Pascal Mirindi ni nani?
Pascal Mirindi: Mimi ni raia wa Kongo; nilizaliwa Goma mnamo mwaka wa 1999. Nimekuwa mwanaharakati tangu nilipokuwa na umri wa miaka 15. Nilianza katika vuguvugu la kiraia la LUCHA.
LUCHA hujishughulisha kimsingi na masuala ya kijamii: kudai upatikanaji wa maji, umeme, na ajira. Baadaye, kutokana na mazingira ya kisiasa nchini Kongo na kwa kuwa sisi ni raia wa nchi hiyo, tulilazimika pia kushughulikia masuala hayo. Hivyo ndivyo, mnamo mwaka wa 2016, tulivyoanzisha kampeni ya kudai rais wa wakati huo, Joseph Kabila, aheshimu Katiba na kuandaa uchaguzi bila kugombea muhula mwingine. Hii ni kwa sababu sheria ya Kongo iko wazi: muhula wa urais unaweza kuhuishwa mara moja tu. Hapo ndipo nilipoanza harakati zangu.
Bila shaka, kulikuwa na changamoto mbalimbali. Kulikuwa na visa vya kukamatwa na majeraha yaliyonifanya nilazwe hospitali.
Leo, naratibu kampeni ya wananchi inayofahamika “Ardhi Yetu Bila Mafuta (Our Land Without Oil/Notre Terre Sans Pétrole).” Mnamo mwaka wa 2022, serikali ya Kongo ilianzisha mchakato wa kuuza vitalu vya mafuta katika maeneo yaliyohifadhiwa, kama vile Hifadhi ya Taifa ya Virunga. Wakati huo, tuliamua kuanzisha kampeni. Ni kampeni kubwa sana; ikiwa na mashirika wanachama zaidi ya 210, ambayo yametia saini mkataba wa kampeni hiyo.
Tunajitahidi kuzihamasisha jamii ili ziwe na msimamo thabiti wa kudai haki na kuwataka viongozi wao wawajibike. Pia tunajitahidi kuzipa jamii fursa za kudumisha utambulisho wao wa kijamii, tukitambua kuwa wao ndio wenye mamlaka ya juu kabisa.
Pia ninaushughulikia mradi wa Ukanda wa Kijani, nikifanya kazi moja kwa moja na taasisi inayosimamia mradi huo, ambayo ni wakfu wa Virunga. Ninaamini kuwa jamii sharti ziwe kiini cha mawazo yetu yote. Ni lazima jamii zishirikishwe kabla ya hatua yoyote kuchukuliwa, kwa sababu kuna msemo usemao: ukifanya jambo kwa ajili yangu bila kunishirikisha, kuna uwezekano mkubwa likachukuliwa kama jambo lililofanywa dhidi yangu.

Mongabay: Uliingiaje katika harakati za kutetea mazingira?
Pascal Mirindi: Kwangu mimi, LUCHA ilikuwa shule yangu. Ilikuwa ni jukwaa ambako nilijifunza jinsi ya kudai haki zangu na sababu za kuzidai. LUCHA ilinisaidia kuelekeza nguvu zangu na kuniongoza huku nikizingatia sheria. Na tulipofanya uchaguzi wa kwanza, kwa baadhi yetu, ilikuwa ni mafanikio.
Nakumbuka siku moja nilikwenda kumwona rafiki ambaye pia alikuwa mmoja wa wenzangu katika kuanzisha Vuguvugu la Upinzani [DRC]. Nilienda kumuona huko Rutshuru, mahali ambako baadhi ya wenzangu wa LUCHA walikuwa wamealikwa kwa sababu hawakuridhishwa na mambo fulani yaliyokuwa yakitokea eneo la Virunga. Kulikuwa na migogoro inayohusiana na ugawanyaji wa mipaka ya hifadhi, jambo lililosababisha matatizo mengi. LUCHA haikuwa na muda wa kushughulikia masuala ya mazingira pekee, bila shaka kulikuwa na changamoto nyingi katika nyanja mbalimbali nchini DRC.
Nilienda kumuona ili kuona kama tunaweza kufanya mazungumzo na uongozi wa Virunga na kutafuta suluhisho. Nilipowasili, nilipitia ndani ya Hifadhi ya Virunga; ilikuwa nzuri ajabu. Niligundua kulikuwa na tatizo kubwa kuhusu namna binadamu na mazingira wanavyoishi pamoja, na tatizo hilo lilihusiana na suala la mawasiliano.
Nilizungumza na wenzangu: “Jamani, je, tunaweza kufanya jambo lolote ili kusonga mbele? Tunakabiliwa na tatizo kubwa ambapo hifadhi hiyo iko hatarini kushambuliwa na kuharibiwa na jamii zinazoizunguka. Je, inawezekana sisi tukaingilia kati ili kusaidia jamii kuelewa kuwa hifadhi hii si mali ya Emmanuel de Merode, ambaye ni mkurugenzi wa Virunga?”
Si hifadhi ya ICCN [Taasisi ya Kongo ya Uhifadhi wa Asili]; ni mbuga yetu, ni chanzo chetu cha uhai na pumzi kama jamii. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa safari yangu.
Baada ya hapo, nilitembelea karibu vijiji vyote vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Virunga ili kuelewa changamoto zinazokabili jamii hizo. Tatizo kuu lilikuwa ukosefu wa mawasiliano. Hapo ndipo tulipoanzisha mazungumzo kati ya Shirika la Wakfu wa Virunga, jamii husika, na serikali ya Kongo. Muda mfupi baadaye, nilianza kushughulikia masuala yanayohusiana na sekta ya mafuta na haki za jamii.

Mongabay: Ni kwa nini watu wajali kuhusu misitu ya Kongo?
Pascal Mirindi: Najiuliza swali: Ni kwa nini tunapaswa kujali chanzo chetu cha hewa tunayovuta? Sote tunafahamu kwamba kama kusingekuwa na miti, tusingekuwa na hewa tunayovuta.
Sote tunafahamu vyema hali inayolikabili dunia kuhusiana na ongezeko la joto ulimwenguni, na misitu miwili mikubwa iliyosalia leo ni Amazon na Kongo. Hivi ni vyanzo vya uhai. Kutunza misitu hii kunamaanisha kuwajali watoto tutakaowaleta ulimwenguni; inamaanisha kujali vizazi vijavyo.
Ndiyo maana nasema watu lazima wajali misitu hii, chanzo chao cha uhai na kitu muhimu wanachoweza kuwaachia watoto wao. Itakuwa jambo la kusikitisha iwapo kesho watoto wao watawauliza: “Baba, ulifanya nini wakati misitu ya Kongo ilipokuwa ikikabiliwa na ukataji miti kiholela na uchimbaji wa mafuta?” Itakuwa jambo la kusikitisha iwapo hatutowajibu watoto wetu wakati huo.
Siku zote huwaambia watu: Kuheshimu misitu hii leo kunamaanisha kuacha maisha bora ya baadaye kwa ajili ya watoto wetu.
Mongabay: Je, raia wa kawaida wa Kongo anaweza kujua nini kuhusu hatari za utafutaji au uchimbaji wa mafuta katika Bonde la Kongo?
Pascal Mirindi: Kongo ni mojawapo ya nchi barani Afrika ambapo mafuta huchimbwa, jambo ambalo raia wengi wa Kongo hawalijui. Kwa takriban miaka 40, mafuta yamekuwa yakichimbwa huko Muanda, katika sehemu ya magharibi ya DRC, eneo pekee ambako nchi hiyo inapakana na bahari.
Ukifika Muanda, utagundua kuwa jamii za huko hazina hata huduma za maji safi ya kunywa, umeme, au barabara. Kama mfumo wa kiuchumi unaohusishwa na nishati ya mafuta ambao umekuwa ukisifiwa sana ungekuwa na matokeo halisi ya maendeleo, huenda leo Muanda ingekuwa kama Saudi Arabia.
Lakini hali hii imethibitisha kuwa mfumo wa kutegemea mafuta haujaleta maendeleo yaliyotarajiwa. Tulianzisha kampeni iliyoitwa “STAND UP MUANDA,” ambapo tulifanya matembezi ya siku tatu kutoka Kinshasa hadi Muanda. Tulianza safari tukiwa na takriban watu 40 kutoka Kinshasa, Goma na maeneo mengine, na tulipowasili Muanda, tulikuwa kundi la watu wapatao mia moja.

Mnamo mwaka wa 2022, serikali ya Kongo ilijisifu huku ikianzisha kaulimbiu kama vile ‘DRC, taifa la suluhisho.’ Nakubali kwamba DRC ni nchi ya suluhisho, lakini kwa ajili ya nani? Inapaswa kuwa nchi ya suluhisho kwa ajili ya wanadamu wote. Na sisi raia wa Kongo ni sehemu ya wanadamu hao.
Ilikuwa kaulimbiu nzuri lakini isiyo na maana ya msingi. Serikali ilianzisha mchakato wa kuuza vitalu vya mafuta vilivyojumuisha Hifadhi ya Taifa ya Virunga, Hifadhi ya Upemba na maeneo mengine. Kulikuwa na vitalu [27] vya mafuta na vitalu vitatu vya gesi. Tulianza kuhamasisha umma na kuiwekea serikali shinikizo kubwa. Mwishowe, serikali ya Kongo ilikiri kuwa ilikuwa ni wazo baya.
Mnamo mwaka wa 2024, serikali ilikubali kusitisha uuzaji wa vitalu vya mafuta. Hata hivyo, baadaye iliahidi kupitia upya ramani mpya ya vitalu vya mafuta. Jambo la kuhuzunisha ni kwamba waliwasilisha ramani mpya ya vitalu vya mafuta iliyojumuisha zaidi ya asilimia 60 ya eneo lote la Kongo.
Kila kitu kinachopaswa kufanywa ili kuilinda misitu kinakinzana na uchimbaji wa mafuta.
Ni lazima DRC ilinde misitu yake na kuanzisha uchumi wa kijani. Kile ambacho raia wa Kongo wanapaswa kujua ni kwamba serikali inaendelea kutudanganya kwa kusema inatufanyia mambo, lakini sivyo. Inawafanya hivyo ili kuendelea kuiba pesa za serikali.
Laiti viongozi wetu wangekuwa wanasiasa wazalendo wa kweli, wangewazia kile ambacho wangeiachia DRC, kwa vizazi vijavyo. Hivyo ndivyo mwanasiasa mzalendo alivyo. Lakini kwa bahati mbaya, wanasalia kuwa wanasiasa wanaofikiria tu maslahi yao tu, ambao hufikiria tu kile watakachowapa watoto wao. Kwangu mimi, hilo linabaki kuwa la kuhuzunisha sana. Na nina uhakika kwamba nguvu pekee inayoweza kuzuia misitu yetu kuharibiwa ni wananchi wenyewe.
Tunawezaje kuifanya jamii izuie mamlaka kuiweka rehani misitu yetu? Kwa kuwaelekeza katika harakati za kujipanga, kuwasaidia kuandaa sera, na kuwafanya watambue nguvu walizo nazo kama wenye mamlaka ya mwisho, bila shaka kwa kutumia mbinu za kutotumia nguvu za kimabavu.
Ilimradi hatuna jamii inayodai uwajibikaji, ni vigumu kuwa na mamlaka zinazowajibika. Kila mtu huwa na hamu ya kuvuka mipaka ya mamlaka aliyopewa, haswa pale ambapo hakuna mifumo ya ulinzi.

Mongabay: Ni lipi lengo la Notre Terre Sans Pétrole?
Pascal Mirindi: Notre Terre Sans Pétrole ni muungano uliobuniwa mwaka wa 2022 wakati serikali ilipozindua uuzaji wa vitalu vya mafuta, na tulihitaji nafasi ambapo tunaweza kuweka mkakati, kuratibu matendo yetu.
Mnamo Mei mwaka wa 2023, sote tulikutana nchini Kenya, ambako tulijadili ni mkakati gani tunafaa kuchukua, kwa sababu baadhi yetu walisema: Tunapinga unyonyaji wa aina zote za nishati za mafuta nchini DRC. Wengine walisema: DRC inaweza kuchimba mafuta yake, lakini Vitasi katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Baada ya majadiliano mengi, hatimaye tulikubaliana, kwa kauli moja juu ya wazo kwamba tunahitaji maendeleo ya haki, ya kijamii na yanayozingatia uchumi wa kijani, na si mtindo wa maendeleo unaohusishwa na uchimbaji wa mafuta.
Wakati huo, [mwaka 2024], tulizindua rasmi Notre Terre Sans Pétrole. Tulifanya shughuli nyingi huko Goma, Kinshasa na Beni. Lengo lilikuwa kuhamasisha jamii kuchukua jukumu la kupinga uuzaji wa vitalu vya mafuta na kuleta njia mbadala za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Notre Terre Sans Pétrole haikuanzishwa kwa ajili ya kupinga kila kitu tu; hatupo hapo ili kukataa mambo bila sababu. Tunapinga uuzaji wa vitalu vya mafuta na mfumo unaotegemea mafuta, lakini pia tunapendekeza njia mbadala. Lengo ni kuweka mfumo wa kiuchumi, kisiasa, kijamii na kimazingira, utakaoiwezesha DRC kuendelea bila kutegemea mafuta. Hivyo, DRC inaweza kupata maendeleo kupitia shughuli zisizoharibu mazingira na zinazoheshimu haki za watu asilia pamoja na jamii za Kongo.
Pia ni ukumbusho kwamba kuna mfumo ulioshindwa: mfumo wa mafuta ulioko Muanda. Tusirudie mambo yaliyoshindwa.
DRC ni nchi yenye suluhisho na uwezo mkubwa unaoweza kunufaisha wanadamu wote, lakini kwa upande mwingine, ni lazima pia ipate ufadhili wa kutosha.


Mongabay: Kampeni yako ya sasa inahusu nini, na kwa nini ni muhimu kipindi hiki?
Pascal Mirindi: Kampeni ya Notre Terre Sans Pétrole inajumuisha kampeni kadhaa ndogo: kuhusu eneo la gesi katika Ziwa Kivu; eneo la mafuta huko Muanda ambapo kampuni ya Perenco inafanya shughuli za uchimbaji; eneo la Ituri ambako pia kuna shughuli za uchimbaji; bomba la mafuta linalounganisha na Uganda; pamoja na eneo la Bonde la Kati.
Baadhi ya kampeni hizi zilipaswa kufanyika mapema zaidi. Kwa upande wa Muanda, hatua hizi zilipaswa kuchukuliwa muda mrefu uliopita. Lakini hatuwezi kuurudisha nyuma muda uliopita. Watu wanateseka. Hali ni mbaya sana. Na bado mamilioni ya dola, na hata ningeweza kusema mabilioni ya dola yanatokana na shughuli za uchimbaji wa mafuta. Kuna tatizo la uchafuzi na uharibifu wa mazingira. Uzalishaji wa kilimo umeathirika; wavuvi hawawezi tena kuvua samaki, na watu walipaswa kujipanga mapema zaidi ili kudai haki ya kupata maji.
Inasikitisha kuwa tunaanza leo, lakini tunajitahidi kutimiza wajibu wetu.
Sababu inayotufanya tulenge maeneo ya gesi ni kwamba si jambo la kawaida kuchimba gesi katika Ziwa Kivu. Hiyo ni aina ya uchimbaji usiyo wa kawaida na usiyozingatia uwajibikaji. Lazima tuonyeshe kuwa kuna mifumo madhubuti ya kiuchumi inayoweza kutumika kwa ajili ya Goma. Kwa hakika, Goma ni ushahidi kwamba iwapo kuna utashi wa kisiasa, eneo hilo linaweza kuendelezwa. Sasa Goma inapata umeme safi saa 24 kwa siku.
Sababu nyingine ya sisi kufanya hivi ni hii: Bonde la Kati ni eneo lenye uwezo mkubwa zaidi wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uzalishaji wa gesi chafuzi.
Nataka kuvutia umakini kuhusu jambo hili kwa sababu baadhi ya watu husema tunaweza kuchimba mafuta na bado tukalinda mazingira. Hii si kweli. Nilikuwa nchini Marekani, katika jimbo la California, mojawapo ya majimbo ya Marekani ambako mafuta huchimbwa. Nimeona watu wakiteseka kutokana na magonjwa ya mfumo wa kupumua yanayosababishwa na shughuli za uchimbaji wa mafuta.
Uchimbaji wa mafuta na utunzaji wa mazingira haviwezi kwenda sambamba. Marekani ina mifumo ya kisheria na teknolojia za kisasa zaidi. Hata hivyo, teknolojia hizo hazijawahi kufanikiwa kulinda jamii zinazoishi karibu na maeneo makubwa ya uchimbaji wa mafuta.
Kama Marekani inashindwa kuhakikisha uchimbaji wa mafuta unaozingatia uwajibikaji, sembuse sisi?

Mongabay: Ni athari zipi zimeletwa na Notre Terre Sans Pétrole?
Pascal Mirindi: Ni mafanikio makubwa kwamba serikali ya Kongo ilisitisha uuzaji wa vitalu hivi vya mafuta. Sisi ndio tuliwashinikiza viongozi kuachana na njia potofu waliyokuwa wakianza kuifuata.
Bila shaka, leo tunakabiliwa na suala jingine, nalo ni miradi ya EACOP [bomba la mafuta ghafi]. Tumefanikiwa kuzuia takriban benki 15 zilizotaka kufadhili mradi wa EACOP.
Tunajivunia kuendelea kuleta mwanga wa matumaini, si kwa watu wa Kongo pekee bali kwa wanadamu wote, ambao watakuwa na jukumu la kuitunza Afrika.
Mongabay: Tutumainie kufikia nini baada ya kampeni yenye mafanikio?
Pascal Mirindi: Mabadiliko chanya ni mchakato wa muda mrefu ambao hautokei mara moja. Hatua zisizo na vurugu na uhamasishaji usio na vurugu ndivyo vinavyoleta mabadiliko ya kweli. Hatua ya kwanza ni kuzionyesha jamii kuwa maisha wanayoishi si ya kawaida.
Baadhi ya watu hukuambia kwamba: “Kongo e kufa n’ango kala”, yaani, Kongo imekufa muda mrefu uliopita, hivyo wewe si mtu wa kuiletea mabadiliko. Hali hiyo si ya kawaida. Kuwa na nchi ambapo mamilioni ya mapipa ya mafuta yanachimbwa kila mwaka lakini jamii hazina maji safi ya kunywa, shule, na kadhalika; hii si hali ya kawaida.
Huko Muanda, kuna vijiji ambavyo ukifika unanusa harufu ya gesi. Mito imechafuliwa. Kuna mabomba ya mafuta yanayovuja na mafuta hayo kusambaa kila mahali: kwenye mashamba ya mahindi, mihogo, na mazao mengine. Hivyo, mama aliyetumia mwezi mzima kupanda mihogo yake hupoteza kila kitu alichopanda.
Tunakwenda kwa jamii hizo na kuwaambia: Hali mnayoishi si ya kawaida, lazima ibadilike. Na baada ya mazungumzo marefu na wao, wanaanza kuelewa.
Mongabay: Ni changamoto zipi kubwa zaidi unazokabiliana nazo?
Pascal Mirindi: Hila za kisiasa. Kuna maeneo unayokwenda ambapo watu wamepokea agizo kutoka kwa chifu. Ukilikataa agizo hilo, unaonekana kama mtu asiyempenda kiongozi. Hiyo ndiyo changamoto ya kwanza.
Changamoto ya pili ni miundombinu. Wakati mwingine inabidi uingie msituni ili kuzungumza na wenyeji asilia, hivyo unalazimika kutembea kwa miguu kwa siku nyingi. Hilo ni jambo linalochosha sana.

Mongabay: Una maoni gani kuhusu Ukanda wa Kijani wa Kivu-Kinshasa baada ya kufahamu kuhusu mikataba mipya ya vitalu vya mafuta?
Pascal Mirindi: Kuna ukosefu wa maono upande wa serikali kuelekea kwa wananchi. Mnaanzisha mradi unaoitwa Ukanda wa Kijani, eneo lililohifadhiwa linalosimamiwa na jamii wakati sheria ya mazingira inapiga marufuku uchimbaji au hata utafutaji wa mafuta katika eneo lililohifadhiwa. Kisha mnaniambia kuwa mmeanzisha uchimbaji wa mafuta katika eneo hilo. Ninaona utata katika nyanja zote, kwa sababu ni wazi kuwa hatuwezi kufanya shughuli za uchimbaji katika eneo lililohifadhiwa.
Ili mradi wa Ukanda wa Kivu-Kinshasa ufanikiwe, ni sharti serikali isimamishe mchakato wa kutoa vitalu vya mafuta katika Bonde la Kati na maeneo mengine yote. Hilo ndilo jambo la kwanza.
Jambo la pili ni kwamba, ili ukanda huu ufanikiwe, lazima kuwe na ushirikishwaji wa jamii katika hatua ya kuusanifu na katika kila kitu kinachohusiana nao. Naendelea kuwa na shaka, lakini pia niko tayari kusikiliza na nina imani na mtazamo chanya kuhusu ukanda huu. Suala hili halihusu mazingira pekee, bali pia kulinda jamii. Pia ni eneo ambalo tunajaribu kusaidia jamii za wakulima wanaolima kakao na michikichi, ili kuwasaidia kuuza mazao yao na kuyachakata ndani ya nchi. Ninaamini ukanda huu unaweza kuwezesha DRC kuwa na kitovu cha uzalishaji wa rasilimali zake za kilimo.
Nina hofu kuwa usimamizi mbaya unaofanywa na mamlaka unaweza kuathiri mradi huu na kusababisha kufeli kwake. Ikiwa mradi huu utaingizwa sana katika siasa, nina hofu kuwa unaweza kufeli.
Mongabay: Vipi unashughulikia masuala ya kiusalama yanayohusiana na kazi yako kama mwanaharakati, na unakabiliana vipi na hofu zako?
Pascal Mirindi: Sitojidai kwamba mimi ni mtu mwenye uwezo usio wa kawaida. Ndiyo, tuna hofu. Maisha yetu ya kila siku ni magumu na yenye changamoto nyingi. Hii inamaanisha kuhama-hama nyumba mara kwa mara; wakati mwingine hatulali nyumbani, tunalala nje. Ni maisha yaliyojaa vitisho. Ni maisha ambayo hatujui kesho italeta nini.
Kwa kweli hatujui ni nani anayetufuatilia. Mara kwa mara tunatazama nyuma ya bega ili kujua nani yuko karibu nasi. Lakini tunaendelea kuwa na matumaini. Tunafanya hivi kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Kwangu mimi, hii si vita yangu pekee. Mimi ni mtu tu ambaye nimetumiwa na Mungu kuanzisha harakati hizi. Nina uhakika kwamba hata nikifa, mtu mwingine ataendeleza mapambano haya. Napenda kusema hivi: Ima tupambane leo ili kutafuta suluhisho kwa ajili ya watoto wetu kesho, au tusifanye lolote na kuwaacha watoto wetu waendelee kuwa watumwa.
Nimekubali kuhatarisha uhuru wangu kwa sababu nataka kuwaachia watoto wangu Kongo iliyo bora zaidi, Kongo nzuri, na Kongo inayowajibika kwa watoto wangu.
Mongabay: Je, kuna jambo lolote ungependa kuongeza?
Pascal Mirindi: Kuwakumbusha watu kwamba Kongo hii imetupa kila kitu: utambulisho, jina, imani, na kila kitu tunachoweza kuwa nacho.
Kuwa raia wa Kongo, kuwa kile ambacho watu wanakiita kashfa ya kijiolojia na kuwa nchi ambayo ni suluhisho kwa wanadamu, ni jambo kubwa. Lazima tupiganie hilo. Lazima tupiganie nchi hii. Lazima tupiganie ili ipate nafasi yake stahiki. Si watu wengine watakaobadilisha nchi hii. Si watu wengine watakaojenga nchi hii. Sisi ndio wenye ndoto. Kila mmoja wetu ana maono kwa ajili ya Kongo hii. Kila mmoja wetu ana mambo anayotamani kuyaona katika nchi hii.
Ikimaanisha kuwa kila mmoja wetu ana kitu cha kuichangia Kongo hii, ili iwe Kongo ya ndoto zetu. Tujitahidi kuwaachia watoto wetu kitu cha mfano, cha kweli, thabiti, kizuri na kikubwa… kama ilivyo ukubwa wa nchi hii.
Picha ya juu: Mwanamume anaonyesha picha anayodai inaonyesha kemikali zenye sumu zilizomwagika kutokana na shughuli za uchimbaji wa mafuta, huko Muanda, magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mwaka wa 2023. Picha hii haihusiani na habari yenyewe na imetumika kwa madhumuni ya kielelezo pekee. Picha na AP Photo/Mosa’ab Elshamy.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 17/07/2026.