Wakati wa mapambazuko katika ufukwe wa Paga, Kaunti ya Kisumu, wavuvi wanaonekana wakivuta boti zao hadi ufuoni baada ya kukesha usiku mzima katika Ziwa Victoria. Lakini tofauti na miaka iliyopita, wengi wao walirejea na samaki wachache sana.
Mvuvi Hesbone Otieno anasema kupungua kwa akiba ya samaki hakutishii tu riziki zao bali pia kunalazimisha jamii zinazotegemea ziwa hilo kutafakari upya mustakabali wa uvuvi katika ziwa hilo, ambalo ndilo kubwa zaidi barani Afrika.
“Wakati mwingine nakaa ziwani usiku mzima na kurudi na kati ya samaki 300 na 359 pekee,” anasema Otieno, ambaye amevua katika Ziwa Victoria kwa miongo kadhaa. “Samaki ni wachache na kipato pia kinapungua. Kama mvuvi, naona njia ambayo imebakia ni kukumbatia vizimba vya samaki ili tuweze kuendelea kuishi.”

Ziwa Victoria ni chanzo cha kujikimu kwa jamii za wavuvi nchini Kenya, Uganda na Tanzania, kupitia uvuvi na biashara zinazohusiana nao. Hata hivyo, kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa mwaka 2023, katika miaka ya hivi karibuni, Ziwa Victoria na eneo lake la vyanzo vya maji vimeathirika vibaya kutokana na “uvuvi kupita kiasi, umwagikaji wa mafuta, utiririshaji wa taka ambazo hazijatibiwa, kuenea kwa spishi vamizi, uchotaji wa maji kupita kiasi kutoka bonde la ziwa, na mabadiliko ya tabianchi, miongoni mwa sababu nyingine.”
Kushuka kwa uzalishaji wa samaki
Kwa mujibu wa Shirika la Huduma za Uvuvi Kenya (KeFS), uzalishaji wa samaki katika Ziwa Victoria umeshuka kutoka takriban tani za metriki 94,349 mwaka wa 2021 hadi 67,575 mwaka wa 2024. Huu ni upungufu wa zaidi ya tani 27,700 katika kipindi cha miaka mitatu. Upungufu huo unaonekana wazi katika fukwe mbalimbali za Kisumu, ambako uvuvi umekuwa uti wa mgongo wa jamii kwa miongo kadhaa.
Otieno anasema mifumo isiyotabirika ya hali ya hewa imefanya uvuvi kuwa mgumu zaidi. Mvua kubwa, upepo mkali, na hali zisizotabirika za hewa zimefanya shughuli za uvuvi kuwa hatari zaidi. “Mabadiliko ya tabianchi yametuathiri sana. Wakati mwingine mvua ni mingi kupita kiasi, na wakati mwingine hali ya hewa hubadilika ghafla tukiwa bado ziwani.”
Pia analaumu ongezeko la matumizi ya boti zenye injini na mbinu haramu za uvuvi kwa kuharakisha upungufu wa samaki. “Hapa ziwani tuna boti ambazo zinatumia nyavu haramu zinazovua kila kitu, ikiwemo samaki wadogo na mayai ya samaki. Pia boti zenye injini huharibu nyavu zilizowekwa na wavuvi wadogo,” Otieno anafafanua.
Kadri mavuno yanavyoendelea kupungua, ndivyo wavuvi wengi katika ufukwe wa Paga sasa wanaangalia ufugaji wa samaki kwa vizimba kama chanzo mbadala cha kipato.


Vizimba vya samaki ni miundombinu inayoelea majini ambamo samaki, hasa sato, hufugwa katika mazingira yanayodhibitiwa hadi kufikia ukubwa wa kuvuliwa. Wavuvi wanasema kuwa vizimba vikisimamiwa vyema vinaweza kusaidia kuziba pengo linaloongezeka kati ya mahitaji ya samaki na kupungua kwa akiba ya samaki ziwani.
Moses Odhiambo, kiongozi katika kitengo cha Usimamizi wa Ufukwe (BMU) wa Paga, anasema ufugaji wa samaki kwa vizimba unazidi kuwa mkakati wa kuendelea kuishi kwa jamii za wavuvi.
“Vizimba vinalenga kuongeza uzalishaji ili kufidia kupungua kwa akiba ya samaki ziwani. Ni wakati wa kuchukua hatua kwa sababu kuna hatari ya kupoteza chakula na kipato cha familia zetu. Katika ufukwe wa Paga, kuna vizimba 98 vinavyofanya kazi. Vinamilikiwa na watu binafsi na vikundi,” Odhiambo aliiambia Mongabay.
Odhiambo anasema ufugaji kwa vizimba unaweza kuleta faida ndani ya miezi sita hadi kumi, ikitegemea ukubwa wa uwekezaji na uzalishaji wa samaki.
Hata hivyo, licha ya kuonekana kama suluhisho, wavuvi wengi wadogo wana hofu kuwa wanaweza kuachwa nje kutokana na gharama kubwa za kuanzisha mradi. “Kuanzisha kizimba kimoja kidogo kunahitaji angalau KSh500,000 ($3,867), na gharama zinaweza kufikia hadi KSh3,000,000 ($23,202),” Odhiambo anasema.
Kwa wavuvi wakongwe kama Otieno, kupata mtaji huo ni changamoto kubwa, ukizingatia familia na hali ngumu ya uchumi. “Ndiyo, nahitaji kizimba. Lakini tatizo ni jinsi ya kuanza. Kwa sasa, vizimba hivi vinaonekana kuwa vya wastaafu na wawekezaji wenye uwezo mkubwa, si wavuvi wa kawaida.”

Wataalamu wa mazingira pia wameonya kuwa ufugaji kwa vizimba, iwapo hautasimamiwa ipasavyo, unaweza kuleta shinikizo jipya la kiikolojia katika Ziwa Victoria kupitia taka za samaki, uchafuzi wa maji na msongamano mkubwa wa samaki kwenye vizimba.
Otieno anaamini kuwa ufugaji wa samaki unaweza kuwa jambo lisiloepukika kadiri uvuvi wa jadi unavyoendelea.
Kwa jamii ambazo zimekuwa zikilitegemea ziwa hilo kwa vizazi, mabadiliko kutoka uvuvi wa asili kwenda ufugaji wa samaki yanaakisi uhalisia mpana zaidi.
Hata hivyo, iwapo ufugaji wa samaki kwa vizimba utakuwa suluhisho endelevu au utazua changamoto mpya za kimazingira, itategemea namna serikali, watafiti na jamii watakavyosimamia mfumo dhaifu wa ikolojia wa ziwa hilo katika miaka ijayo.
“Upungufu wa samaki katika Ziwa Victoria unasababishwa na mabadiliko ya tabianchi, kupungua kwa viwango vya maji kutokana na uvukizaji, na uchafuzi kutoka vyanzo vya moja kwa moja na visivyo vya moja kwa moja, ikiwemoUfugaji shughuli za kilimo na mjini,” anasema Dkt Elizabeth Obado, mhadhiri wa Uvuvi na Ufugaji wa Samaki katika Chuo Kikuu cha Maseno.
Athari za ubora duni wa maji
“Mabadiliko haya yanaathiri mfumo wa ikolojia wa samaki kupitia ubora duni wa maji, kama vile kiwango cha oksijeni iliyoyeyushwa na viwango vya juu vya pH vinavyochochewa na shughuli za viwandani,” Obado anaambia Mongabay.
Anafafanua kuwa uvuvi kupita kiasi pia umechangia hali hiyo. “Idadi ya jamii inaongezeka na kuna mahitaji ya upatikanaji wa chakula endelevu. Hali hii imesababisha kukamatwa kwa samaki wachanga,” anasema.
Anasema uvamizi wa maeneo ya ardhioevu pia umechangia uchafuzi. “Wakati wa mvua, maji ya mtiririko hubeba uchafu, kuuingiza ziwani, na kuongeza viwango vya amonia na virutubisho vinavyoweza kusababisha eutrofikesheni na ukuaji wa mimea ya majini kama gugu maji. Kwa njia hiyo, shughuli za kilimo huchangia uchafuzi wa ziwa hilo.”
Anafafanua zaidi: “Kwa sasa siwezi kutaja kiwango halisi cha athari za mabadiliko ya tabianchi katika kupungua kwa akiba ya samaki, kwa sababu bado tafiti zinaendelea.
Jinsi halijoto huathiri uzazi wa samaki
Hata hivyo, halijoto ni kipimo muhimu kwa sababu inaathiri uzazi wa samaki. Samaki huzaliana vyema katika halijoto ya kati ya nyuzi 28°C na 32°C, hasa kwa Sato (Oreochromis niloticus) na kambare (Clarias gariepinus). Mabadiliko yoyote ya halijoto yanaweza kuchelewesha mzunguko wa uzazi kwa sababu joto likiwemo chini sana, viwango vya kuzaliana hupungua.”

Obado pia anaelezea kuwa samaki hutegemea mifumo ya mvua kama ishara ya upatikanaji wa chakula. Mvua ikichelewa, uzalishaji wa samaki huathirika na kuathiri idadi yao kwa ujumla.
Anasema lengo la vizimba ni kuongeza uzalishaji wa samaki, kwa sababu idadi ya sasa katika maji ya wazi haiwezi kukidhi mahitaji. “Ufugaji kwa vizimba utasaidia kukidhi mahitaji ya protini kwa binadamu. Hata hivyo, haitachukua nafasi ya uvuvi wa jadi kwa sababu hatuwezi kupoteza mfumo wetu wa ikolojia wa ziwa,” anasema.
Anaonya dhidi ya ufugaji wenye msongamano: “Samaki wengi wakizuiliwa katika eneo moja, mabaki ya chakula na taka zao zinaweza kuchafua mazingira yao. Baadhi ya vifaa vinavyotumika kuunda vizimba ni metali. Vinapopata kutu, huachilia kemikali zinazobadilisha ubora wa maji kwa samaki walioko vizimbani na wale wa asili.”
Pendekezo lake ni kuwa ufugaji wa vizimba usimamiwe kwa uagalifu kupitia uteuzi sahihi wa maeneo ili kuepusha kuhatarisha maisha ya samaki. “Kwa mujibu wa tafiti, sato (Oreochromis niloticus) ndiyo spishi inayofaa zaidi kwa ufugaji wa vizimba. Tafiti zinaendelea kuhusu spishi zingine kama vile sangara.”
Ushirikiano ni muhimu
Kwa mujibu wa mhadhiri huyo, kinachoitajika kwa sasa ni ushirikiano kati ya wavuvi, watafiti na mashirika kama vile Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA), ili kuimarisha sera za uhifadhi wa mazingira kupitia utekelezaji na ufuatiliaji sahihi wa shughuli za uvuvi.
Utafiti wa 2024 uliochapishwa katika jarida la Journal of Great Lakes Research, ulioongozwa na Dkt Christopher Aura, mwanasayansi katika Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi Kenya (KMFRI), ulibaini kuwa ufugaji wa samaki kwa vizimba una uwezo wa kuongeza uzalishaji wa samaki katika Ziwa Victoria. Hata hivyo, utafiti huo unaeleza kuwa upanuzi wa ufugaji huo unapaswa kuambatana na mbinu bora ili kuzuia madhara kwa mfumo wa ikolojia wa ziwa.
Wataalamu wa mazingira pia wanasema kuwa ufugaji wa samaki kwa vizimba pekee hauwezi kuwa suluhisho la muda mrefu katika Ziwa Victoria bila juhudi za kurejesha ikolojia na kuimarisha usimamizi endelevu wa sekta ya uvuvi.
“Urejeshaji wa maeneo ya ardhioevu, ulinzi wa maeneo ya kando ya ziwa, pamoja na kupunguza uchafuzi unaoingia katika Ziwa Victoria ni muhimu ili kulinda mfumo wa ikolojia. Hii ni kwa sababu ardhioevu inatumika na samaki kama mahala pa kuzalia na makazi ya wale wachanga, huku ikifanya kazi ya kuchuja uchafuzi unaoelekezwa ziwani,” Dkt Jenniffer Atieno, mhadhiri wa sayansi ya mazingira katika Chuo Kikuu cha Maseno, aliiambia Mongabay.

Kwa mujibu wa Atieno, juhudi za kurejesha makazi hazitatosha kukomesha kupungua kwa akiba ya samaki ikiwa hakutaambatana na usimamizi madhubuti wa rasilimali za uvuvi. “Lazima kukuwe na ufuatiliaji wa kisayansi, utekelezaji wa sheria na kanuni za mazingira, ushirikiano wa karibu kati ya Kenya, Uganda na Tanzania, pamoja na ushirikishwaji wa jamii za wavuvi katika kusimamia rasilimali za ziwa,” anasema.
Uendelevu wa shughuli za uvuvi
Mapendekezo ya Atieno yanaendana na utafiti uliochapishwa mwaka 2022 katika jarida la People and Nature. Utafiti huo unabainisha kuwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi pamoja na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni hatua muhimu katika kuhakikisha uendelevu wa shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria.
Atieno anasema jamii zinazozunguka ziwa hazina budi kujiandaa kukabiliana na hali ya hewa inavyozidi kutotabirika.
“Lazima tujue mbinu za matumizi ya ardhi inayozingatia mabadiliko ya tabianchi, ulinzi wa maeneo ya ardhioevu yanayopunguza athari za mafuriko, kupunguza uchafuzi unaoingia ziwani kutokana na maji ya mvua, pamoja na kuimarisha tahadhari za mapema. Hizi zitakuwa hatua muhimu kukabiliana na hatari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya uvuvi,” anapendekeza Atieno.
Picha ya bango: Mvuvi Hesbone Otieno wakati akihojiwa na mwandishi wa Mongabay katika ufukwe wa Paga. Picha na Kelvin Matuku, Mongabay.