- Mradi wa Dangote wa dola bilioni 17 wa kiwanda cha kusafisha mafuta Lamu wazua mjadala kati ya serikali na wanaharakati wa mazingira.
- Wanaharakati waonya kuwa mradi unaweza kuhatarisha mikoko, miamba ya matumbawe na maisha ya jamii za pwani.
- Wavuvi na mashirika ya mazingira wanataka Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) ifanywe kwa uwazi kabla ya ujenzi kuanza.
- Serikali inasema mradi huo utazalisha ajira 60,000 na kuimarisha biashara ya mafuta Afrika Mashariki na Kati.
LAMU, Kenya – Pendekezo la bilionea wa Nigeria Aliko Dangote kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta cha $17 bilioni katika Kaunti ya Lamu, nchini Kenya, limezua mjadala mkali, huku serikali ikikitaja kama kichocheo cha uchumi, na wanaharakati wakionya kuhusu athari zake kwa ikolojia na maisha ya jamii za pwani.
Dangote achagua Kenya
Baada ya miezi kadhaa ya uvumi kuhusu iwapo kiwanda hicho kingejengwa Kenya, Uganda au Tanzania, kampuni ya Dangote Industries ilichagua Kenya kuwa mwenyeji wa uwekezaji huo.
Katika ripoti iliyochapishwa na Reuters, Makamu Rais wa Kitengo cha Mafuta na Gesi wa Dangote Industries Limited, Edwin Devakumar, alithibitisha kuwa kiwanda hicho chenye uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku kitajengwa katika Kisiwa cha Lamu na kinatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu.
Mafuta ghafi yanatarajiwa kupatikana kutoka nchi za Afrika Mashariki, zikiwemo Uganda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Iwapo mradi huo utakamilika, utafuata mfano wa kiwanda cha Dangote kilichopo karibu na Lagos, Nigeria, chenye uwezo wa kusafisha mapipa 650,000 kwa siku, na ambacho kilianza uzalishaji mwaka 2024 na ndicho kikubwa zaidi barani Afrika.
Serikali yaeleza manufaa
Rais William Ruto, akimteua naibu wake Kithure Kindiki kusimamia mradi huo, alisema Kenya imefikia makubaliano na Dangote ya kuendeleza mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta.

Kwa mujibu wa Ruto, kiwanda hicho kitahudumia masoko ya Afrika Mashariki na Afrika ya Kati, na kinatarajiwa kuunda takribani nafasi za ajira 60,000 wakati wa ujenzi na uendeshaji wake.
Wanaharakati wapinga
Wakati serikali ikisisitiza manufaa ya kiuchumi ya uwekezaji huo, wanaharakati wa mazingira wanataka mchakato wa tathmini ya athari kwa mazingira ufanywe kwa uwazi na ushirikishe wananchi, wakisema uamuzi wowote kuhusu mradi huo unapaswa kuzingatia si tu faida za kiuchumi, bali pia athari zake kwa mazingira, urithi wa kitamaduni na maisha ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Mnamo Julai 14, Greenpeace Africa ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari, ikieleza wasiwasi kwamba mpango wa serikali ya Kenya kushirikiana na Dangote kujenga kiwanda hicho unaweza kuhatarisha mfumo dhaifu wa ikolojia ya pwani ya Afrika Mashariki, huku ukiingiza Kenya katika mustakabali hatarishi “wa kuendelea kutegemea nishati ya mafuta ya kisukuku”.
“Kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta cha kiwango hiki kinaweza kusababisha uharibifu wa makazi ya viumbe hai, kuzorota kwa mazingira ya baharini, kuongeza hatari ya umwagikaji wa mafuta na kuchangia uchafuzi hatari wa hewa,” Greenpeace Africa ilieleza.
Aidha, shirika hilo lilisema kuwa ahadi ya nafasi 60,000 za ajira “haiwezi kutumiwa kuficha gharama halisi za uwekezaji huu. Miradi mikubwa ya mafuta ya kisukuku mara nyingi huunda ajira za muda mfupi huku ikidhoofisha vyanzo vya mapato vilivyopo tayari, hususan katika sekta za uvuvi, utalii na uchumi wa jamii za wenyeji unaotegemea biashara ndogo ndogo,” Greenpeace Africa ilieleza.
Vile vile, shirika la Power Shift Africa limeeleza kuwa Lamu, ambayo imetambuliwa na UNESCO kama eneo la Urithi wa Dunia, ina mifumo muhimu ya ikolojia, ikiwemo misitu ya mikoko, miamba ya matumbawe na nyasi za baharini zinazotegemewa na sekta ya uvuvi, utalii na jamii za wenyeji.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Mohammed Adow, amesema mradi huo hautatoa suluhisho la changamoto ya upatikanaji wa umeme kwa mamilioni ya Waafrika, akisisitiza kuwa Kenya inapaswa kuendelea kuwekeza katika nishati isiyochafua mazingira badala ya kuongeza utegemezi wa mafuta.
“Kenya imejijengea sifa duniani kama moja ya mataifa yanayoongoza barani Afrika katika matumizi ya nishati mbadala kupitia jotoardhi, upepo na nishati ya jua,” Adow anasema. “Viongozi wake bado wana nafasi ya kufuta kibali hiki na kulinda moja ya maeneo ya kipekee zaidi barani Afrika.”
Kwa upande wake, Omar Elmawi wa Africa Movement of Movements amesema kuwa ingawa bado hakuna taarifa za kina kuhusu mradi huo, uzoefu wa viwanda vya kusafisha mafuta katika mataifa mbalimbali unaonyesha kuwa mara nyingi gharama za kimazingira huzidi manufaa ya kiuchumi kwa jamii zinazozunguka miradi hiyo.
Elmawi anasema sheria za mazingira nchini Kenya zinaitambua miradi ya kusafisha mafuta kuwa miradi yenye hatari kubwa kwa mazingira, hivyo ni lazima ifanyiwe Tathmini ya Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment – EIA) kabla ya kuidhinishwa.
“Ikiwa mchakato wa EIA utafuatwa kikamilifu na wananchi watapewa nafasi ya kushiriki, basi kama ilivyokuwa kwa pendekezo la mradi wa kinu cha kuzalisha umeme kwa makaa ya mawe cha Lamu, kuna uwezekano mkubwa mradi huu usitekelezwe,” amesema Elmawi. “Kwa mtazamo wetu, huu ni mradi ambao ukitekelezwa utakuwa kosa kubwa, si kwa kizazi cha sasa pekee bali pia kwa vizazi vijavyo vitakavyobeba athari zake,” Elmawi aliiambia Mongabay kupitia simu.
Mifano ya athari katika mataifa mengine
Elmawi amesema Bara la Afrika tayari lina mifano ya viwanda vya kusafisha mafuta katika nchi kama Sudan, Afrika Kusini na Nigeria. Amesema kiwanda cha Dangote nchini Nigeria kimeibua wasiwasi kuhusu athari za kimazingira, ikiwemo uharibifu wa udongo, mmomonyoko wa maeneo ya pwani na kuathiri shughuli za uvuvi.
Ameongeza kuwa katika maeneo mengine duniani, nchini Marekani kuna eneo karibu na mji wa New Orleans linalojulikana kama “Cancer Alley”, jina linalotokana na viwango vya juu vya visa vya saratani vinavyohusishwa na shughuli za viwanda.
Kwa mujibu wa wanaharakati hao, iwapo kiwanda kitajengwa Lamu, kuna hofu ya uchafuzi wa bahari, kupungua kwa mazalia ya samaki, na kuathirika kwa uzalishaji wa asali ya mikoko endapo kutakuwa na uvujaji wa mafuta au uchafuzi mwingine utokanao na shughuli za kiwanda.
Wavuvi waeleza hofu
Mwenyekiti wa Muungano wa Vikundi vya Usimamizi wa Fukwe za Uvuvi (Beach Management Units, BMUs), Lamu, Somo Mohammed, amesema bado hawajapewa taarifa rasmi kuhusu eneo litakapojengwa kiwanda hicho, lakini iwapo kitajengwa karibu na Bandari ya Lamu, athari kwa sekta ya uvuvi zinaweza kuwa kubwa.

Amesema wavuvi wana hofu ya kupungua kwa idadi ya samaki, kuathirika kwa shughuli za kilimo na uwezekano wa baadhi ya wananchi kuhamishwa kupisha mradi huo, hali ambayo inaweza kuongeza umaskini katika jamii za wenyeji.
Mohammed ameitaka serikali kuhakikisha jamii zinashirikishwa kikamilifu kabla ya mradi huo kuanza na kwamba tathmini ya athari kwa mazingira ifanywe kwa uwazi.
“Kwa sasa tunasikia taarifa hizi kupitia vyombo vya habari. Katiba inataka wananchi washirikishwe kabla ya mradi wowote mkubwa kutekelezwa,” Somo aliambia Mongabay.
Hadi sasa, serikali haijatangaza tarehe ya kuanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho wala kuchapisha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA), hatua ambayo wanaharakati na jamii za wenyeji wanasema ni muhimu kabla ya mradi kuendelea.
Picha ya bango: Bilionea wa Nigeria Aliko Dangote. Picha kwa hisani ya The Habari Network.