- Taka nyingi huingizwa nchini kwa kivuli cha vifaa vya kielektroniki vilivyotumika.
- Kati ya tani 35,000 za taka zinazozalishwa kwa mwaka, ni chini ya 5% tu hurejelezwa.
- Taka hizi huharibu makazi ya viumbe na kuvuruga mifumo ya ikolojia.
- Usimamizi thabiti wa uingizaji wa bidhaa hizo nchini ni hatua muhimu.
Ni mchana wa Jumapili tulivu mjini Iringa. Penina Mtatifikolo anaandaa chakula kwa ajili ya familia yake. Mama huyu hana habari kuwa ugali, kambale na mchicha anaoandaa unaweza kuwa sababu ya madhara makubwa ya kiafya kwake na familia yake kwa kuwa vyakula vyote hivi huenda vina viambata-sumu.
Mahindi na mchicha vililimwa katika eneo lililo karibu na jalala ambamo zinatupwa takataka mbalimbali hatari, zikiwemo zile za kielektroniki, huku kambale akiwa amevuliwa katika bwawa lililochafuliwa na taka za aina hiyo.

Katika maeneo mengi, hasa mijini, wananchi hula vyakula ambavyo vina uwezekano mkubwa wa kuwa na sumu zinazotokana na taka za kielektroniki bila wao kufafahamu. Kadhalika mazingira katika maeneo hayo nayo hayako salama kutokana na taka hizo kuchafua udongo, maji, hewa na kuharibu makazi ya viumbe na kuhatarisha bioanuwai.
Ongezeko la taka za kielektroniki
Taka za kielektroniki ni vifaa vya elektroniki kama simu za mkononi, kompyuta, televisheni, jokofu, betri, viyoyozi, mashine za kufulia, chaja, nyaya na vifaa vingine vilivyoharibika, kupitwa na wakati au visivyotumika tena, na vinavyotupwa bila tahadhari.
Kadri matumizi ya vifaa vya kielektroniki yanavyoongezeka nchini ndivyo uzalishaji wa taka hizo unavyoongezeka.
Kulthum Shushu, Ofisa Mazingira wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), anasema Tanzania huzalisha wastani wa tani 35,000 za taka za kielektroniki kwa mwaka, lakini ni chini ya asilimia tano tu ndiyo hurejelezwa na kuchakatwa kutokana na ukweli kuwa urejelezaji wa taka hizo hatarishi ni ghali sana.
Hali hiyo, anasema, husababisha taka kujikusanya katika mazingira na mzigo wa kuzisimamia huongezeka siku hadi siku.
Ongezeko la taka za kielektroniki
Katika mahojiano na Mongabay, Kulthum anasema tatizo hilo linachochewa zaidi na uingizaji nchini wa vifaa vya kielektroniki ambavyo baadhi havikidhi viwango vinavyotakiwa na hivyo kuwa sawa na taka zinazoingizwa nchini kwa kivuli cha vifaa vya kielektroniki vilivyotumika.
“Hakuna viwango vya vifaa vilivyotumika kwa kuwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lina viwango kwa vifaa vipya tu na kusababisha vifaa vilivyotumika kuingia nchini bila udhibiti unaojulikana na unaoweza kusimamiwa kisheria,” anaeleza.
Hamad Taimuru, Meneja wa Uzingatiaji na Utekelezaji Sheria wa NEMC, anaunga mkono hoja hiyo akisema kuwa licha ya vifaa visivyo na viwango, lakini kuna wafanyabiashara wengine wanaoingiza nchini vifaa vilivyobakiza muda mfupi kufikia mwisho wa muda wake wa matumizi, ambavyo baadhi yake huingizwa ‘kwa njia za panya’.
Anasisitiza kuwa waingizaji wanaweza kuingiza nchini kontena lililojaa kompyuta au majokofu na baada ya kufika ndipo huchambuliwa kufahamu kipi cha kuuza na kipi cha kutupa.
“Kwa vile huu ni uingizaji wa taka kwa njia ya vifaa ambavyo vimetumika, tuwaombe wenzetu wa taasisi zinazoshughulikia ushindani wa kibiashara pamoja na uingizaji wa bidhaa ambazo zimetumika, kuweka udhibiti madhubuti,” anasema Taimuru.

Yusuf Abdulrahim Yusuf, Ofisa Uoteshaji Tishu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar (ZAHILI), anasema kuongezeka kwa matumizi ya simu, kompyuta na vifaa vingine vya kielektroniki vinaifanya Tanzania kuwa na ongezeko la taka hizo.
Athari za taka za kielektroniki
Daria Leonard wa kampuni ya Electronic Waste Management Solution (WEEE), anaongeza kuwa taka za kielektroniki zina athari kubwa si tu kwa mazingira bali pia kwa afya ya binadamu na uhifadhi endelevu wa rasilimali endapo hazitasimamiwa ipasavyo.
“Vifaa hivi vina kemikali na metali nzito kama risasi, zebaki, kadmiyamu, arseniki, nikeli na kromiamu. Metali hizi nzito ni hatari kwani yanapotupwa ovyo huchafua udongo, maji na hewa, uchafuzi ambao huharibu makazi ya viumbe, kupunguza bioanuwai na kuvuruga mifumo ya ikolojia,” anabainisha.
Kwa mujibu wa Daria taka za aina hii zinapochomwa, huchangia uzalishaji wa gesi chafu na kemikali hatari zinazochafua hewa na kuchochea mabadiliko ya tabianchi.
“Ndiyo maana tunashauri sana taka za aina hii zirejelezwe ili kupunguza athari hizi na kuhakikisha zinaendelea kutumika zikiwa katika muundo mwingine,’’ anafafanua.
Anasema taka za kielektroniki hudumu katika mazingira kwa muda mrefu kuliko taka zinazooza baada ya muda mfupi huoza na kupotea.
“Aina nyingi za taka hizo zina viambata vya plastiki na shaba ambavyo baada ya vifaa hivyo kutupwa, vinapaswa kutenganishwa mapema na kuchakatwa kutengeneza vitu vingine; la sivyo vinakaa muda mrefu katika mazingira na kuleta uchafuzi,” anaeleza.
Kwa upande wa athari za taka hizo kwa mimea, Yusuf anabainisha kuwa uchunguzi wa tishu za mimea katika maabara umebaini kuwa mimea na mifugo mingi imeathiriwa na madini hatarishi yanayotokana na utupaji holela wa taka za kielektroniki.
Tafiti zinasemaje?
Usimamizi wa taka za kielektroniki Tanzania huongozwa na Kanuni ya Usimamizi wa Mazingira (Udhibiti na Usimamizi wa Taka za Vifaa vya Umeme na Kielektroniki 2021). Kanuni hiyo inaongozwa na misingi mitatu ya kulinda mazingira; kuzuia madhara kabla hayajatokea, mchafuzi kulipa na mzalishaji kuwajibika na suala la usalama wa kifaa hadi mwisho wa maisha ya kifaa hicho.
Tafiti tatu zilizofanywa maeneo tofauti nchini Tanzania zinatoa matokeo ya kuogofya: kwamba vyakula mbalimbali vinavyoliwa mijini vimechafuliwa kwa madini yanayokuwa sumu mwilini mwa binadamu pindi yanapoingia kupitia mnyororo wa chakula.
Tafiti hizi ni zile zilizofanywa na wataalam wa ndani katika miji ya Dar es Salaam, Iringa na Mbeya, maeneo hayo yakitumika kama uwakilishi wa maeneo mengine yenye mazingira yanayofanana.
Katika utafiti uitwao, ‘Heavy Metal Contamination in Soil and Food Crops and Associated Human Health Risks in the Vicinity of Iringa Municipal Dumpsite, Tanzania’ uliofanywa na Victor Fanuel Sanga na Christina Fabian Pius (2024), karibu na dampo la Manispaa ya Iringa, ilibainika kuwa kiasi cha madini ya kadmium, arseniki na nikeli kwenye udongo kilivuka viwango vinavyoruhusiwa. Kadhalika kiwango cha madini ya risasi kwenye mahindi na maharagwe kilikuwa juu ya kiwango kinachokubalika. Madini haya kwa kiasi kikubwa hutokana na vifaa vya kielektroniki vilivyotupwa kwenye dampo hasa betri.
Viwango vikubwa vya metali hizo kwenye udongo kinaelezwa kuwa na athari mbalimbali. Zebaki na metali nyingine nzito kwenye udongo zinadaiwa kusababisha uchafuzi wa mazingira, kupunguza rutuba kwenye udongo, kuharibu makazi ya viumbe na kuvuruga mifumo ya ikolojia.
Aidha katika utafiti huo ilibainika kuwa uchafuzi wa mazingira na usimamizi hafifu wa taka, hasa zile zisizooza kirahisi kama vile za kielektroniki unaweza kuleta athari za kiafya. Utafiti huo ulibaini uwepo wa metali nzito (heavy metals) mbalimbali kwenye mazao ya chakula kama vile mahindi, maharage na mbogamboga.
Utafiti uliofanywa na Dkt Samwel Ntapanta wa Chuo Kikuu cha Aarhus nchini Finland, ‘Gathering Electronic Waste in Tanzania: Labor, Value, and Toxicity’ ulibaini kuwa tatizo la taka za kielektroniki ni kubwa zaidi katika nchi za Kusini mwa dunia (Global South) kutokana na kutokuwepo kwa mikakati madhubuti ya usimamizi wa taka hizo tofauti na hali ilivyo katika nchi za Kaskazini mwa dunia (global North).
Dk. Ntapanta alieleza kuwa taka za kielektroniki huingiza sumu kwenye mazingira hasa kupitia shughuli zisizo rasmi za uchakataji kama kuchoma nyaya ili kupata metali, na kumwaga ovyo mabaki ya vitu hivyo. Taratibu hizi huachilia kemikali hatari kama risasi, zebaki na kadmium, ambazo huingia kwenye udongo, maji na hewa.
Kamati ya Pamoja ya Wataalam wa Viambata Kwenye Chakula wa Shirika la Afya Duniani na Shirika la Chakula na Kilimo (JECFA) imeainisha viwango vinavyokubalika vya kemikali hatarishi kwenye chakula. Tafiti zinaonyesha kuwa nchini Tanzania viwango hivyo vimepitiliza kutokana na tatizo la taka za kielektroniki.
Othman C. Othman wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika utafiti wake. “Heavy metals in green vegetables and soils from vegetable gardens in Dar es Salaam, Tanzania” uliochapishwa katika jarida la Tanzania Journal of Science alibainisha uwepo wa viwango vya juu vya metali nzito kama vile risasi, kadmiyamu (cadmium), zinki, nikeli na shaba katika aina tano za mbogamboga katika maeneo ya Tabata, Buguruni, Sinza, Ukonga na Kiwalani, Jijini Dar es Salaam.
Uwepo wa madini haya unahusishwa na ulimaji wa mbogamboga hizo karibu na madampo na kutumia majitaka kumwagiliwa mbogamboga hizo na hivyo kuwa na hatari za kiafya kwa watumiaji.

Kwa ujumla, mboga za mijini zilikuwa na viwango vikubwa zaidi vya madini hatarishi kuliko vinavyokubalika na viwango vya FAO/WHO.
Changamoto
Usimamizi hafifu wa uingizaji wa vifaa vya kielektroniki ni miongoni mwa changamoto zinazorudisha nyuma juhudi za kukabiliana na taka za kielektroniki
Nyendo Kinyonga, Mtaalam wa Mabadiliko ya Tabianchi na Jinsia, anaona kukosekana kwa viwango vya TBS kwa vifaa vilivyotumika kama changamoto nyingine.
“Napendekeza kuwe na viwango vya vifaa vya kielektroniki vinavyoingizwa nchini ili kupunguza matumizi ya bidhaa zisizo na ubora. Kwa mfano, unakuta kuna jagi la kuchemshia maji linaunzwa TSh10,000 ($4), halafu likitumika miezi miwili tu linakufa na kutupwa. Sasa fikiria kukiwa na watu 1,000 walionunua haya majagi na wakayatupa, ni uchafuzi kiasi gani utakuwa umefanyika?” anaongeza Nyendo.
Changamoto nyingine ni uelewa mdogo miongoni mwa wananchi kuhusiana na masuala ya taka za kielektroniki.
“Nimefanya tafiti kuhusu masuala ya taka ngumu kwa ujumla katika ngazi ya familia, na matokeo yanaonyesha bado kuna pengo katika kutoa elimu na ufuatiliaji wa sheria. Lakini pia bado kuna pengo katika miundombinu ya kukusanya taka katika ngazi ya familia ambayo ndio mwanzo mkubwa wa uzalishaji taka,” anasema.
Nini kifanyike kupunguza tatizo hili?
Kwa mujibu wa Taimuru, mambo mbalimbali yanaweza kufanyika kudhibiti tatizo la taka za kielektroniki. Anataka usimamizi thabiti, hususan katika eneo la uingizaji wa bidhaa hizo nchini kama hatua muhimu. Pia anashauri kuongeza ushirikiano kati ya taasisi zinazohusika.
Anasema hali hii itapunguza uingiaji wa bidhaa hafifu za kielektroniki licha ya kukosekana kwa viwango vya TBS kwa vifaa vilizotumika.
Kwa mujibu wa Taimuru, usimamizi thabiti wa Mkataba wa Basel utasaidia kudhibiti kisheria uingizaji holela wa bidhaa hizo.
Usafirishaji wa vifaa vya kielektroniki kutoka nchi moja kwenda nyingine unasimamiwa na Mkataba wa Basel ambao Tanzania ni mwanachama.
Kulthum anasema kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa Mkataba huo, basi kama mkataba huo yatasimamiwa ipasavyo, hakuna kifaa kibovu au kilichokaribia kumaliza muda wake wa matumizi kitakachoingia nchini na hiyo kuokoa mazingira kwa kiasi kikubwa.
“Hata TV iliyotumika ambayo kitufe kimoja hakifanyi kazi huhesabiwa kuwa ni taka hatarishi na kwa masharti ya Mkataba wa Basel, kifaa kama hicho inatakiwa kirudishwe nchi kilichotoka,” anaongeza.
Mkataba huo pia unazitaka nchi wanachama kupunguza uzalishaji taka hatarishi ‘kadri inavyowezekana’, kusimamia na kupunguza madhara ya taka hizo ili kulinda afya za binadamu na mazingira, na kudhibiti taka hatarishi zisivuke mipaka, hasa kupelekwa kiholela katika nchi zinazoendelea na ikiwa ni lazima kuzisafirisha, nchi zinakotoka zinapaswa kupata ruhusa ya nchi zinakopelekwa.
Matakwa mengine ni kuhakikisha taka zinachakatwa karibu na mahali zinapozalishwa na kushirikiana kimataifa katika kubadilishana taarifa, teknolojia na kusaidiana kusimamia taka hizo.
Hatua nyingine ya kudhibiti hali hiyo ni utekelezaji makini wa Kanuni ya Usimamizi wa Mazingira (Udhibiti na Usimamizi wa Taka za Vifaa vya Umeme na Kielektroniki, 2021) na uwekezaji wa rasilimali fedha kwenye usimamizi wa taka ni moja ya suluhisho la tatizo hili.
Kauli ya Serikali
Naibu Waziri (Ofisi ya Makamu wa Rais) Muungano na Mazingira, Reuben Kwagilwa, anasema Serikali ya Tanzania inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya usimamizi wa taka zinazozalishwa maeneo mbalimbali.
Akizungumza bungeni hivi karibuni, Kwagilwa alisema katika kufanikisha hatua hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya uhifadhi wa mazingira ikiwemo udhibiti wa taka.
Waziri alitoa maelezo hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Lucy Edward Mwakyembe aliyetaka kujua Serikali kwa kushirikiana na Mikutano ya Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP) na Michango Iliyoamuliwa Kitaifa (NDCs) itasimamiaje uchakataji wa taka na matumizi ya nishati.
Alifafanua kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Taka wa miaka mitano (2025 – 2030) wenye lengo la kuimarisha mfumo wa usimamizi wa taka kwa dhana ya uchumi rejeshi ambapo taka zinazozalishwa zinaweza kutumika tena kama malighafi viwandani.
Kinyonga anashauri kuwepo kwa viwango vya kupima ubora wa vifaa vya kielektroniki vinavyoingizwa nchini hata vile vilivyokwishatumika.
“Nimefanya tafiti kuhusu masuala ya taka ngumu kwa ujumla katika ngazi ya familia, na matokeo yanaonyesha bado kuna pengo katika kutoa elimu na ufuatiliaji wa sheria. Lakini pia bado kuna pengo katika miundombinu ya kukusanya taka katika ngazi ya familia ambayo ndio mwanzo mkubwa wa uzalishaji taka,” anasisitiza.
Aidha, utekelezaji makini wa Kanuni ya Usimamizi wa Mazingira (Udhibiti na Usimamizi wa Taka za Vifaa vya Umeme na Kielektroniki, 2021) na uwekezaji rasilimali fedha kwenye usimamizi wa taka ni moja ya suluhisho la tatizo hili kwa kuongeza uwekezaji katika usimamizi wa Kanuni hiyo.
Picha ya Bango: Taka za kielektroniki zikikusanywa kwa ajili ya kutengeneza vitu vingine. Picha kwa hisani ya WEEE Centre.