Heri ya Siku ya Kimataifa ya Sokwe. Tarehe 14 Julai dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Sokwe, mojawapo ya viumbe wanaokaribiana zaidi na binadamu kwa asili. Hapa chini ni muhtasari wa baadhi ya habari za hivi karibuni za Mongabay kuhusu sokwe na maisha yao:
Sokwe kwenye vita katika Hifadhi ya Taifa ya Kibale
Kama binadamu, sokwe pia huingia katika migogoro mikubwa wao kwa wao. Mwandishi wa Mongabay, Keith Anthony Fabro, aliripoti kuhusu kile kilichoelezwa kama “vita vya wenyewe kwa wenyewe” vya sokwe katika Hifadhi ya Taifa ya Kibale nchini Uganda.
Kabla ya mgawanyiko huo, kundi la Ngogo lilikuwa na sokwe kati ya 150 na 200, na hivyo kuwa miongoni mwa makundi makubwa zaidi ya sokwe kuwahi kurekodiwa porini. Baadaye kundi hilo liligawanyika katika makundi mawili yanayojulikana kama Kundi la Kati (Central) na Kundi la Magharibi (Western), yaliyotajwa kutokana na maeneo ya msitu walikokuwa wakipatikana.
Kati ya mwaka 2018 na 2024, kundi la Magharibi lilifanya mashambulizi 24 dhidi ya kundi la Kati, na kuua angalau madume saba yaliyokomaa pamoja na sokwe wachanga 17. Migogoro hiyo bado inaendelea na inaweza kuwa na athari za muda mrefu kwa idadi ya sokwe katika eneo hilo. Utafiti unaonyesha jinsi mabadiliko ya mahusiano ya kijamii yanavyoweza kusababisha mgawanyiko na vurugu hata katika jamii za wanyama.
Ni kwa namna gani sokwe na Ringo Starr wanafanana?
Kupiga ngoma huku ukiimba kwa wakati mmoja ni kipaji kinachovutia, iwe kwa mwanamuzi kama Karen Carpenter au kwa Ringo Starr. Lakini inaonekana sokwe pia wana uwezo huo. Mwandishi wa Mongabay, Liz Kimbrough, alieleza kuhusu Ayumu, sokwe dume mwenye umri wa miaka 26 katika taasisi ya Chuo Kikuu cha Kyoto inayoshughulika na utafiti kuhusu asili ya tabia za binadamu (EHUB). Ayumu amekuwa aking’oa mbao kutoka kwenye njia ya kutembea, kuzitumia kama ala za muziki na kupiga kwa mpangilio maalum huku akitoa sauti.
Watafiti walirekodi maonyesho 89 na kubaini kuwa mpigo wa ngoma haukuwa wa kubahatisha, bali ulikuwa na mpangilio wa kimdundo unaofanana na miito ya kawaida ya sokwe. Aidha, Ayumu alionekana akicheka na kuonyesha ishara za kufurahia kitendo hicho, jambo linaloashiria kuwa tabia hiyo humletea hisia chanya. Utafiti huo unaunga mkono nadharia kwamba muziki wa kutumia ala huenda ulitokana na mawasiliano ya kihisia kupitia sauti.
Watoto wa sokwe ni majasiri zaidi
Kwa binadamu, ujana ndiyo kipindi ambacho watu wengi hufanya mambo bila kuogopa athari zake. Wanasayansi walidhani hali hiyo ingekuwa hivyo pia kwa sokwe, ambao ni ndugu wa karibu wa binadamu katika mageuzi. Hata hivyo, John Cannon kutoka Mongabay aliripoti kuwa sokwe wachanga ndio wenye tabia ya kuthubutu zaidi.
Watafiti nchini Uganda walibaini kuwa sokwe wadogo ndio wenye tabia ya kuthubutu zaidi, wakijirusha kutoka mti mmoja hadi mwingine licha ya hatari ya kuumia. Watafiti wanaamini kuwa kwa binadamu, uangalizi mkubwa kutoka kwa wazazi unaweza kupunguza uwezekano wa watoto kuchukua hatari kama hizo.
Kwa wasomaji wadogo, Mongabay Kids iliripoti habari inayoonyesha kuwa sokwe na nyani wakubwa wengine hupenda kutaniana kwa michezo. Watafiti walitumia saa 75 wakiwachunguza sokwe waliokuwa kwenye bustani ya wanyama na kurekodi matukio 142 ya utani wa kimchezo. Matukio mengi yalihusisha sokwe wadogo wakiwatania sokwe watu wazima.
Picha ya bango: Sokwe wa Mashariki (Pan troglodytes schweinfurthii) kwenye Msitu wa Budongo, Uganda. Picha na Julie Larsen © Wildlife Conservation Society.