- Wavuvi wa pwani ya Kenya wanasema kelele za baharini zinachangia kupungua kwa viumbe kama nguva, pomboo na nyangumi, na kuhatarisha uvuvi.
- Kongamano la 11 la Our Ocean lilitambua kelele za chini ya maji kama tishio linaloongezeka kwa viumbe vya baharini.
- IFAW na HACQO zinasema ongezeko la shughuli za kiuchumi baharini linaongeza uchafuzi wa kelele unaovuruga maisha ya viumbe vya baharini.
- Wataalamu wanataka utafiti zaidi, sera bora na ushirikiano ili kupunguza kelele baharini na kulinda ikolojia ya bahari.
Katika eneo la jeti, Mtangawanda, Kaunti ya Lamu, kwenye ufuo wa Bahari ya Hindi, mwendo wa saa sita mchana, Omar Shafi ameketi kwenye kivuli cha banda la wavuvi, akikarabati kwa makini nyavu yake ya kuvulia samaki.
Ni shughuli ambayo anaifanya kila siku baada ya kutoka baharini kuvua samaki. Anapomaliza, yeye huiweka sehemu salama kwa ajili ya uvuvi kesho yake. “Tangu nianze uvuvi miaka 40 sasa, nimekuwa nikitumia nyavu hizi za uzi kuvua samaki kwa sababu haziharibu mazingira ya bahari,” anasema Shafi.

Kulingana naye, ujio wa zana mbalimbali za kuvulia samaki umeharibu mazingira ya bahari kiasi cha kwamba samaki na viumbe wengine baharini wamepungua sana.
“Kuna zana nyingi ambazo wavuvi wanatumia, ambazo zinaharibu utulivu wa bahari. Hivyo husababisha baadhi ya viumbe baharini kupungua,” anasema.
Vifaa vinavyosababisha kelele baharini ni kama meli kubwa za mizigo na abiria, boti za mwendo kasi, zana za kuvulia samaki kama trola, mitambo ya utafiti na uchimbaji na mitambo ya ujenzi wa miundombinu ya baharini. Vifaa hivi vimetajwa kusababisha kelele ambazo huathiri uwezo wa viumbe hao kuwasiliana, kusafiri na kusaka chakula.
Kama anavyoeleza Shafi, nguva ni miongoni mwa wanyama baharini ambao alikuwa akikutana nao mara kwa mara alipoanza uvuvi hasa katika maeneo ya Manda na Dodori, kaunti ya Lamu. Lakini sasa imekuwa vigumu sana kwake kuwaona.
Nguva bado yuko
“Kwa maoni yangu, mnyama huyu nguva bado yuko, lakini kwa sababu bahari haina utulivu kutokana na kelele za vyombo vya uvuvi, nguva hukimbia, siwaoni tena,” anasema Omar.
Taswira hiyo haielezwi na Shafi peke yake, bali pia na wavuvi katika ukanda wa pwani wenye urefu wa zaidi ya kilomita 600. Wanaeleza hofu yao kwamba hali ilivyo hivi sasa inaweza kuchangia kuzorota kwa sekta ya uvuvi zaidi.
Omar Bwana, kutoka eneo la Ngomeni Malindi, ni mvuvi mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 30, na ni mmoja wa wavuvi ambao walikuwa na uhusiano wa karibu sana na mnyama nguva, kiasi cha kwamba alikuwa na eneo lake maalum la tengefu baharini alikokuwa akiwalea nguva wawili; mama na mwanawe.
Anasema alikuwa akiwapitia kila asubuhi kabla aanze uvuvi ili kuhakikisha kuwa tengefu yake ndogo haiingiliwi na mvuvi yeyote. Akimaliza kuvua, hupitia tengefu hiyo kuwaangalia kabla ya kurudi nyumbani.
“Mimi nilikuwa na sehemu maalum ambayo nilikuwa nawalinda wanyama hawa nguva, na kila asubuhi nilikuwa nikiwapitia, na walikuwa wamenizoea,” anasema Bwana. Lakini Bwana anasema siku moja alifika eneo hilo la tengefu na kupata nguva wote wawili hawapo. Licha ya kupitia eneo hilo mara kwa mara, hajawahi kuwaona tena. Anashuku kwamba hili lilisababishwa na kelele za boti za kutumia mashine ambazo zilianza kupita eneo hilo.
Bwana anasema nguva hula kwenye maji madogo baharini au nyasi za baharini, na hupenda mazingira tulivu. Endapo watasumbuliwa na chakula chao kuharibiwa, basi wao hutoroka.
Mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa plastiki baharini na uvuvi mbaya ni miongoni mwa athari ambazo zimekuwa zikitajwa kuathiri mazingira ya bahari na kuongeza wasiwasi kwa zaidi ya watu milioni 600 duniani wanaotegemea uvuvi kujipatia kipato cha kila siku.
Kelele baharini ni kilio cha wavuvi wengi katika pwani ya Kenya, ambao wanasema inaathiri viumbe vya bahari. Sasa kilio hicho kimepata msukumo wa kimataifa.
Tatizo linaloibuka
Katika kongamano la 11 la Our Ocean lililokamilika hivi majuzi jijini Mombasa, Kenya, kelele za baharini zilitajwa kama tatizo ambalo wanasayansi wanasema linaibuka. Tayari wataalamu wanasema baadhi ya viumbe vya baharini vinaendelea kuathirika. Wanasema linafaa kupewa kipaumbele kwa mataifa kulifanyia utafiti zaidi na kuja na mbinu za kukabiliana nalo.
Miongoni mwa viumbe wanaoathiriwa ni nguva, ambao hupenda mazingira matulivu.
Shirika la International Fund for Animal Welfare (IFAW) liliongoza mjadala ulioangazia tishio hilo na athari zake katika ikolojia ya bahari ili kupaza sauti kuhusu athari za kelele baharini kwa mataifa mbalimbali.

Lilian Mulupi, afisa wa mipango, kitengo cha uhifadhi wa Bahari kutoka shirika la IFAW, alielezea kuwa mbali na athari kama vile mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa plastiki baharini na uvuvi mbaya, tishio la kelele baharini halifai kupuuzwa kutokana na ongezeko la shughuli za kiuchumi na biashara katika Bahari ya Hindi.
Mulupi anaelezea kuwa kelele huchangia usumbufu na mtafaruku katika maisha ya viumbe vya baharini, huku akitoa mfano wa spishi nyingi za baharini, ikiwemo samaki, nyangumi, pomboo, nguva, na wanyama wasio na uti wa mgongo, ambao hutumia sauti kuwasiliana, kusafiri, kutafuta chakula, na kuepuka wanyama wanaokula wenzao.
“Ongezeko la kelele kutoka kwa meli, shughuli nyingine za binadamu, na maendeleo huhatarisha maisha na kuchangia mgogoro wa viumbe hai, na kufanya bahari isistahimili mabadiliko ya tabianchi.
“Wakati mfumo wa ikolojia wa baharini unapovurugika, uvuvi huathiriwa. Jamii zilizo kando ya pwani yetu hutegemea sana samaki kwa ajili ya usalama wa chakula na riziki nyingine. Hivyo tusipoilinda bahari dhidi ya kelele, huenda tukapoteza viumbe vya baharini vingi sana,” anaeleza Mulupi.
Muungano wa Mataifa Yenye Dhamira ya Juu kwa Bahari Tulivu (High Ambition Coalition for a Quiet Ocean – HACQO), unasema moja ya hoja zilizochipuka katika kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari lililofanyika Nice, nchini Ufaransa mwaka 2025 ni kwamba kelele chini ya maji inayosababishwa na shughuli za binadamu inaweza kuathiri vibaya viumbe vya baharini katika uwezo wao wa kuogelea, kula, kuwasiliana, kuzaana na hata kuepuka kuliwa.
Licha ya kuwa utafiti haujafanywa humu nchini Kenya kujua haswa kiwango cha kelele ambazo zinatolewa na zana mbalimbali na umbali ambao kelele hizo zinafika baharini, Kerry Max, afisa wa masuala ya kimataifa wa HACQO nchini Canada alisema utafiti waliofanya unaonyesha kuwa kila baada ya miaka 10, kelele za baharini zinaongezeka maradufu.

Muungano huo umeungana na mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ambayo yamekuwa yakitoa wito wa kupunguzwa, kama si kuondolewa kabisa kwa kelele baharini.
Hatua za haraka zahitajika
Wito huo umetolewa hasa kwa nchi 10 zinazounda Bahari ya Hindi Magharibi (WIO), ambazo ni Somalia, Kenya, Tanzania, Msumbiji, Afrika Kusini, Madagascar, Comoro, Mauritius, na Seychelles kuchukua hatua za haraka kabla ya tishio hilo kuleta madhara makubwa.
WIO ina zaidi ya watu milioni 65 wanaoishi kando ya mwambao wake ambao wanategemea bahari kujikimu. Pia ina moja ya mifumo ya ikolojia ya pwani na baharini iliyo hai zaidi ulimwenguni.
Hivyo basi, endapo tishio hilo la kelele halitashughulikiwa kwa wakati, basi huenda mamilioni ya watu wanaotegemea bahari eneo la WIO wakakosa kujitegemea kiuchumi.
Kwa mfano, sekta ya uchumi wa samawati nchini Kenya huchangia KSh37 bilioni ($286,045,612.5) za pato la taifa kila mwaka, huku ikitoa ajira kwa zaidi ya watu milioni 1.2.
Stellamarris Muthike, afisa mkuu wa mazingira ya baharini kutoka Mamlaka ya Bahari Kenya (Kenya Maritime Authority), anasema kuna baadhi ya sheria ambazo zinalinda maeneo ya bahari dhidi ya usumbufu wa kelele.
Anasema kuna baadhi ya maeneo ya hifadhi ambayo wameweka masharti yanayozuia boti na meli kufika ili kulinda viumbe vya baharini.
“Tulipotengeneza mpango wa kulinda maeneo ya bahari, tulichora ramani ya maeneo ambayo vyombo vikubwa kama meli hupitia kwa wingi na tukachambua kwa kina kiwango cha usafirishaji katika njia kuu za baharini. Muongozo huo ndio unatusaidia kuongoza hatua za kupunguza kelele za chini ya maji na kuongeza juhudi za uelewa miongoni mwa jamii kuhusu athari zake,” anafafanua Muthike.
Zaidi, anasema Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (the International Maritime Organization – IMO) limeunda muongozo wa kuhakikisha kuwa kelele za baharini zimepunguzwa, huku Kenya, kama nchi mwanachama wa mkataba wa IMO, ikitarajiwa kutekeleza mwongozo huo.
Haja ya kufanywa tafiti zaidi
Muthike hata hivyo anasema tafiti chache zimefanywa kuhusu athari za shughuli za usafirishaji wa meli, hususan kelele za chini ya maji kwa viumbe vya baharini. Hivyo kuna haja ya kufanywa tafiti zaidi kuhusu athari zake kwa viumbe vya baharini, na kisha kujumuishwa katika mfumo wa kimataifa wa bayoanuwai.
Dkt Nina Wambiji, mwanasayansi wa uvuvi wa baharini kutoka Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi Kenya (KMFRI), ambaye pia ni makamu wa rais wa Western Indian Ocean Marine Science Association (WIOMSA), ni miongoni mwa wanasayansi waliojadili kwa kina suala hilo la kelele baharini kwenye kongamano hilo.
Alikiri kuwa suala la kelele baharini limekuwa tatizo sugu, lakini kwa muda halijapewa kipaumbele, hasa Afrika, kutokana na kwamba halikuwa limefanyiwa utafiti kikamilifu kutokana na ukosefu wa miundombinu, ikiwemo nguvukazi, na fedha za kufanya utafiti huo kwa kina.
“Wakati majadiliano kuhusu uhifadhi wa baharini yalipoanza miaka iliyopita, mkazo ulikuwa katika masuala ya usalama. Hata uchafuzi wa plastiki ulikuwa bado haujapata umakini kama ulivyo leo. Tishio la kelele halikupewa kipaumbele,” Wambiji anaiambia Mongabay.
Hata hivyo, anaamini suala hilo halifai kupuuzwa tena.
“Uchumi samawati unajumuisha uvuvi, bandari, meli, madaraja, uchimbaji wa visima baharini na maendeleo mengine mengi. Katika shughuli hizi zote kuna kelele, kwa hivyo lazima tuelewe athari zake kwa mfumo wa ikolojia wa bahari,” anasema Wambiji.
Anasema kuna haja ya washikadau wote kuungana na kuunda mbinu ambazo zitatumiwa kufanya utafiti na kuandaa suluhisho mbalimbali. Anasema hatua mojawapo ambayo imeanzishwa ni kuleta mjadala huo kwenye majukwaa ya kimataifa kama ilivyoanza kwenye kongamano la 11 la Our Ocean.
HACQO pia imependekeza mataifa kujiunga na muungano huo ili kuunda zana, mikakati, na kutekeleza teknolojia za kupunguza kelele za baharini. Aidha, kwa kujiunga na muungano huo, nchi wanachama hujitolea kushughulikia kelele za baharini, kuendeleza suluhisho kwa kutumia sera na kutafuta fursa za ushirikiano.
Wambiji anasema ukusanyaji wa takwimu kwa ushirikiano kati ya wanasayansi wa baharini na jamii zinazoishi kando ya maeneo ya pwani kutasaidia sana katika ufuatiliaji na utafiti wa kelele tofauti-tofauti baharini.
“Hatuwezi kudhibiti kile ambacho hatukijui, hivyo basi lazima utafiti uanze sasa,” anasema Wambiji.
Picha ya bango: Omar Shafi akishona nyavu yake yakuvulia samaki katika eneo la Mtangawanda kaunti ya Lamu, Kenya. Picha na Ruth Keah, Mongabay.