- Kenya ilizindua rasmi Ushirikiano wa Kitaifa wa Hatua dhidi ya Plastiki (NPAP) kwa ushirikiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa Hatua za Kudhibiti Plastiki (GPAP), mpango wa Jukwaa la Uchumi Duniani,katika mkutano wa Our Ocean uliofanyika Mombasa.
- Uchafuzi wa plastiki ni tishio kubwa kwa mifumo ikolojia ya baharini ya Kenya, uvuvi na maisha ya pwani, unaotokana na usimamizi duni wa taka au ukosefu wa mifumo bora ya usimamizi wa takaardhini, pwani na baharini.
- Mpango huo unalenga kuharakisha mpito hadi uchumi wa plastiki wa mviringo, ambao unalenga kupunguza uchafuzi wa plastiki, kuongeza thamani ya nyenzo ambazo kwa kawaida huchukuliwa kuwa takana kutoa fursa za kiuchumi katika mchakato huo
- Mongabay ilizungumza na Clemence Schmid, Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Hatua dhidi ya Plastiki (GPAP), kando ya mkutano wa Mombasaili kuelewa juhudi za ushirikiano zinajaribu kufanikisha nini nchini Kenya.
Wakati wa Mkutano wa 11 wa Our Ocean uliofanyika katika jiji la pwani la Mombasa, serikali ya Kenya, pamoja na Ushirikiano wa Kimataifa wa Hatua dhidi ya Plastiki (GPAP) wa Jukwaa la Uchumi Duniani na UNDP Kenya, walizindua rasmi Ushirikiano wa Kitaifa wa Hatua Dhidi ya Plastiki wa Kenya (NPAP Kenya).
Takriban tani milioni 14 za plastiki huishia baharini kila mwaka na zinachangia 80% ya uchafu wote wa baharini unaopatikana katika uso wa bahari na mashapo ya bahari kuu.
Kenya inakabiliwa na changamoto kubwa za uchafuzi wa plastiki, haswa katika vituo vya mijini na kando ya pwani yake. Plastiki huchangia takriban 20% ya tani 22,000 za taka zinazozalishwa kila siku nchini Kenya, kulingana na makadirio. Ni 27% tu ya taka za plastiki zinakusanywa, ambapo 8% huchakatwa tena na 19% zilizobaki hutupwa katika majaa ya taka au madampo holela. Taka za plastiki ambazo hazijakusanywa na kusimamiwa vyema mara nyingi huishia kwenye mito na baharini. Huvuruga mifumo ikolojia, huhatarisha wanyamapori, na huathiri utalii na uvuvi.
Mwaka wa 2017, Kenya ilianzisha marufuku ya matumizi, utengenezaji na uingizaji wa mifuko ya plastiki ya matumizi ya mara moja. Mnamo 2020, marufuku hiyo iliongezwa hadi plastiki zinazotumika mara moja katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Ushirikiano wa Kitaifa wa Hatua Dhidi ya Plastiki (NPAP Kenya) utasaidia kuharakisha mpito wa nchi hiyo kuelekea uchumi wa plastiki wa mviringo, kulingana na Clemence Schmid, Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Hatua dhidi ya Plastiki (Global Plastic Action Partnership – GPAP) katika Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum – WEF).

Mpango wa GPAP uliozinduliwa na WEF mwaka wa 2018 ni mpango wa wadau wengi wa kukabiliana na uchafuzi wa plastiki na kuunga mkono mpito kuelekea uchumi wa mviringo. Mpango huo unashirikiana na nchi washirika ili kutoa maarifa yanayotokana na data, kuunga mkono mikakati ya kitaifa na kuhamasisha hatua katika mnyororo wa thamani wa plastiki.
Ushirikiano wa Kitaifa wa Hatua Dhidi ya Plastiki umeanzishwa katika nchi 25 duniani kote, ikiwa ni pamoja na nane barani Afrika. Kenya ilijiunga na Ghana, Nigeria, Tanzania, Senegal, Angola, Zambia na Gabon katika kutekeleza mifumo kama hiyo.
Mongabay ilizungumza na Schmid kingoni mwa mkutano wa 11 wa Our Ocean ili kuelewa kile ambacho Ushirikiano wa Hatua Dhidi ya Plastiki unajaribu kufanikisha nchini Kenya.
Mongabay: Tishio la uchafuzi wa plastiki kwa viumbe hai wa baharini ni kubwa kwa kiasi gani?
Clemence Schmid: Takriban 80% ya uchafuzi wa baharini unatokana na plastiki. Kwa mfano, uchafu wa plastiki unapokwama kwenye miamba ya matumbawe, miamba hiyo ina uwezekano mara 20 zaidi wa kupata magonjwa, na kusababisha kuzorota kwa mfumo ikolojia. Lakini plastiki ikishafika baharini, huwa imechelewa sana kuchukua hatua dhidi ya uchafuzi wa plastiki. Jambo bora tunaloweza kufanya ni mbinu ya suluhu ya muda mfupi: kujaribu kuikusanya plastiki hiyo kabla haijasambaa zaidi.
Mongabay: Ni jukumu gani la WEF katika kuanzisha Ushirikiano wa Kitaifa wa Hatua Dhidi ya Plastiki nchini Kenya?
Clemence Schmid: Ushirikiano wa Kitaifa wa Hatua Dhidi ya Plastiki wa Kenya ni kitengo cha kitaifa cha mpango wa kimataifa wa GPAP. Tulizindua hili kwa ushirikiano na serikali ya Kenya, ambayo uongozi wake na maono yake yanalenga kukabiliana na uchafuzi wa baharini si tu baharini bali pia kupitia suluhisho za kuzuia uchafuzi kwenye chanzo chake.
Kama hatua ya kwanza, ushirikiano huu utasaidia uundaji wa Mpango wa Kitaifa wa Hatua dhidi ya Plastiki unaotambua vitendo vya kipaumbele, fursa za uwekezaji na njia za utekelezaji ili kupunguza uchafuzi wa plastiki, kuimarisha ufanisi wa rasilimali, kusaidia viwanda vya kijani na kuunda ajira.
Ushirikiano huu pia utaunda Ripoti ya Jinsia, Usawa na Ujumuishaji wa Kijamii (GESI) ili kusaidia kuhakikisha kwamba faida za mpito wa uchumi wa mviringo zinashirikiwa kwa upana katika jamii. Hii ni pamoja na kutambua na kuunga mkono majukumu ya wanawake, vijana na wakusanyaji taka wa sekta isiyo rasmi, ambao mara nyingi wako mstari wa mbele katika usimamizi wa taka za plastiki na ambao ni muhimu katika kujenga mifumo ya mviringo jumuishi na thabiti.
Tunakusudia kuwakutanisha serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia, sekta isiyo rasmi na wasomi ili kutathmini hali iliyopo na kubainisha suluhisho kwa pamoja. Sehemu ya pili inahusu hasa namna ya kujenga daraja kati ya kazi na malengo ya ngazi ya ndani na mjadala wa kimataifa. Nguvu ya mtandao huu wa nchi 25 [za GPAP] inasaidia kuwezesha mtiririko wa mawasiliano na maoni pande zote mbili.

Mongabay: Plastiki pia zinahusishwa na uzalishaji wa gesi chafuzi. Ni vipi juhudi za Kenya za kupunguza taka za plastiki zinaweza kuchangia malengo na ahadi zake pana za hali ya hewa chini ya Mkataba wa Paris?
Clemence Schmid: Hilo ni swali muhimu. Tunajua mnyororo wa thamani wa plastiki huchochea uzalishaji mkubwa wa hewa chafu. Pia tunajua ni muhimu kuushughulikia ili kufikia lengo la sifuri halisi. Mpango wa Kitaifa wa Hatua Dhidi ya Plastiki utatoa mapendekezo halisi ya kupunguza uchafuzi wa plastiki. Kama sehemu ya kazi hii, tutaweza pia kutoa mwelekeo kuhusu kiasi cha uzalishaji wa gesi chafuzi utakaopunguzwa.
Hatuangalii tu uchafuzi wa plastiki, bali pia tunapima athari chanya ambazo hatua hizi zinaweza kuwa nazo katika kufikia malengo ya Mkataba wa Paris.
Mongabay: Inakadiriwa kuwa uchumi wa mviringo unaweza kuunda ajira milioni 11 barani Afrika. Unaona kuna fursa gani kwa jamii za pwani, hasa kwa vijana, wanawake, na wakusanyaji taka wa sekta isiyo rasmi?
Clemence Schmid: Kazi inayofanywa na NPAP Kenya katika kusaidia mpito kuelekea uchumi wa mviringo inajumuisha sekta isiyo rasmi, hususan wakusanyaji taka, tangu mwanzo.
Tunajua kwamba mpito pekee unaowezekana ni mpito wa haki. Tunataka kuhakikisha kwamba mitazamo, maoni na mahitaji hayo yanazingatiwa tunapofikiria kuhusu mpito huu. Kupitia mtandao wa GPAP na mbinu yake inayotegemea ushahidi, NPAP Kenya ina uwezo wa kuvutia uwekezaji, kuimarisha miundombinu ya usimamizi wa taka, na kupanua mifumo salama ya kuchakata na kutumia tena, yote yakitegemea vipaumbele vya maendeleo ya kitaifa ya Kenya.
Kuna uhusiano kati ya utunzaji wa bahari, hatua za hali ya hewa, na mabadiliko ya kiuchumi, kwa sababu mpito wa haki kuelekea uchumi wa mviringo unaweza kutoa ajira hadi milioni 11 na fursa ya soko ya kila mwaka ya dola bilioni 546 kote Afrika ifikapo 2030, huku ikiimarisha ufanisi wa rasilimali, ushindani wa viwanda, na ustahimilivu wa kiuchumi. Ushirikiano huu pia unaunga mkono azma ya Kenya ya kuimarisha utengenezaji wa ndani, kuvutia uwekezaji na kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha kikanda cha uvumbuzi endelevu na viwanda vya kijani kibichi.
Mongabay: Kuhusu utekelezaji, ni aina gani za rasilimali zitapatikana kupitia aina hii ya ushirikiano?
Clemence Schmid: Sisi si shirika kama Benki ya Dunia au taasisi zingine, lakini kupitia kazi inayofanywa na Ushirikiano wa NPAP Kenya katika kuwakutanisha wadau wote, tunaweza kutoa fursa zaidi za uwekezaji kutoka pande mbalimbali; iwe ni sekta binafsi, Taasisi za Kifedha za Maendeleo (DFIs), au serikali.
Picha ya bango: Wanajamii wakikusanya taka za plastiki wakati wa zoezi la kusafisha ufukwe lililoandaliwa na shirika lisilo la faida la Coastal & Marine Resource Development (COMRED) katika pwani ya Kenya. Picha kwa hisani ya COMRED.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 7/07/2026.