- Mvutano katika Ghuba uliovuruga usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz, ukisababisha bei ya mbolea kupanda. Licha ya mpango wa ruzuku wa serikali ya Kenya, wakulima wanapaswa kushughulika na gharama kubwa za mafuta na pembejeo.
- Angalau 26% ya usambazaji wa mbolea nchini Kenya hupitia Mlango-Bahari wa Hormuz. Hata hivyo, serikali imewahakikishia raia wake hifadhi ya kutosha ya mbolea, ikiwa na mipango ya kubadili vyanzo vya uagizaji wa mbolea.
- Wakati huo huo, wakulima wanaona mavuno yakipungua, licha ya mpango wa ruzuku wa serikali, huku bei za mbolea za kibiashara zikiendelea kupanda na gharama za mafuta kuongezeka.
- Kenya pia inapaswa kushughulikia uharibifu wa ardhi unaosababishwa na mmomonyoko wa udongo, mbinu duni za kilimo, matumizi kupita kiasi ya mbolea bandia na athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile mafuriko.
Mzee Philip Kitur anatembea katikati ya safu nadhifu za mabua ya mahindi, huku majani yanayoanza kuchipua yakitoa ishara ya mavuno tele. Mkulima huyo mwenye umri wa miaka 72 anamiliki shamba la ekari 41 katika kijiji cha Kipkeikei, Kaunti ya Trans-Nzoia.
Hata hivyo, nyuma ya tabasamu la Kitur kuna hofu ya kupoteza sehemu kubwa ya mavuno iwapo hatopata mbolea. “Mazao yanahitaji kuongezewa mbolea ya kukuzia, lakini sijapata mbolea ya aina ya urea; bila hiyo, naweza kupoteza hadi asilimia 30 ya mavuno yangu,” aliambia Mongabay.
Mutahi Kagwe, Waziri wa Kilimo nchini Kenya, anasema nchi ina akiba ya kutosha ya mbolea, ikiwa ni pamoja na mifuko milioni 2 ya mbolea ya nyongeza. Anasema Kenya inatafuta vyanzo mbadala vya mbolea ili kuhakikisha usalama wa chakula licha ya misukosuko ya kimataifa iliyosababishwa na mvutano kati ya Iran na Marekani.
“Ingawa hatuwezi kutabiri mgogoro wa Mashariki ya Kati utachukua muda gani, tumejadiliana kuhusu kupata mbolea ya urea kutoka Algeria na aina nyingine za mbolea kutoka Morocco,” Kagwe aliambia Mongabay katika mahojiano yaliyofanyika kwa njia ya mtandao.

Eneo kuu la uzalishaji wa chakula
Kaunti ya Trans-Nzoia ni mojawapo ya maeneo makuu ya uzalishaji wa chakula nchini Kenya, hasa mahindi, ambayo ni chakula kikuu. Kulingana na Ripoti ya Kitaifa ya Uzalishaji wa Kilimo ya mwaka 2025 kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu za Kenya, Trans-Nzoia ilichangia tani 423,156 (asilimia 10.5) kati ya tani 4,028,320 za mahindi zilizozalishwa mwaka 2024.
Hata hivyo, kumekuwa na changamoto kubwa katika uwezo wa Kenya kudumisha uzalishaji wake wa mahindi katika kipindi cha miezi sita iliyopita. Ripoti ya Soil Atlas 2025 inaashiria kuwa ni asilimia 20 pekee ya ardhi ya Kenya inayofaa kwa kilimo. Ripoti hiyo inasema, “Sehemu kubwa ya ardhi ya kilimo iko katika maeneo kame.”
Ripoti hiyo, iliyoandaliwa na Shirika la Heinrich Boell baada ya kuchambua tafiti mbalimbali za kisayansi zilizopitiwa na wataalamu, taarifa za Utafiti wa Udongo wa Kenya (Kenya Soil Survey), na data kutoka Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), inaonyesha kuwa angalau asilimia 40 ya ardhi ya Kenya imeharibika, huku hadi tani 26 kwa hekta zikipotea kutokana na mmomonyoko wa udongo kila mwaka.
Ripoti hiyo inaangazia athari za uharibifu wa udongo kwa usalama wa chakula na kuleta ushahidi wa kisayansi kuhusu afya ya udongo katika mjadala wa umma na mchakato wa utungaji sera.
“Nchini Kenya, 63% ya ardhi ya kilimo ina udongo wenye asidi, na 32% ya hiyo ina udongo ulioainishwa kama wenye asidi ya juu. Ingawa baadhi ya udongo una asidi kiasili, matumizi ya kupita kiasi ya mbolea ya viwandani yamezidisha tatizo,” ripoti inasema.
Lakini, kwa sasa, mbinu hizi ndizo zinazosaidia kilimo cha hadi hekta milioni 2.1 za mahindi, kulingana na ripoti ya IDEAS ya mwaka 2024, na huruhusu wakulima wadogo kulima chakula cha kutosha.

Mpango wa ruzuku ya mbolea wa Kenya
Mwaka huu wa fedha, serikali ya Kenya ilitenga dola milioni 139 kwa wakulima wanaostahiki kupata mbolea kwa nusu ya bei katika maduka ya pembejeo za kilimo yanayouza bidhaa hiyo iliyoagizwa na makampuni makubwa ya kimataifa kama Yara na ETG. Katika mwaka wa fedha wa 2025/2026 serikali ilitenga dola milioni 61, zilizokuwa za kima cha chini sana kuliko dola milioni 77 zilizopangwa kwa ajili yake mwaka wa 2024/2025.
Wakulima husajili majina yao, ukubwa na eneo la mashamba yao, na mazao wanayopanda kwenye Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Kilimo Jumuishi wa Kenya (KIAMIS) unaopatikana katika ofisi za machifu wa kata zao. KIAMIS huwatumia vocha kupitia SMS ili kudai pembejeo zao zilizofadhiliwa.
Kulingana na takwimu za serikali, kuna takriban wakulima wadogo milioni 7.5 nchini Kenya. Kufikia mwezi Novemba 2025, kulikuwa na wakulima milioni 7.2 waliosajiliwa katika mfumo wa KIAMIS.
Mnamo mwezi Machi 2026, wakulima wa Trans-Nzoia walilazimika kusimama kwenye foleni ndefu katika maghala ya serikali mjini Kitale ili kununua mbolea ya bei ya chini.
Wakati huo huo, katika maduka ya pembejeo za kilimo, bei ya gunia la kilo 50 la aina ya mbolea ya Diammonium Phosphate (DAP) au urea, inayotumiwa kwa ajili ya kurutubisha mimea baada ya kuota, ilikuwa dola 46 mwezi Januari, lakini mgogoro katika eneo la Ghuba ulisababisha bei ya kibiashara ya mbolea kupanda kwa kasi. “Mwezi Machi, bei ya gunia moja ilikuwa imepanda hadi takriban KSh8,000 ($62),” Josephine Ndonji, mkulima wa nyanya kutoka Kisumu, aliliambia shirika la Mongabay.
“Nilikuwa nimeagiza magunia 25. Sikupata magunia yote sehemu moja, hivyo ikanilazimu kuwasiliana na msambazaji mwingine kutoka Makueni. Mbali na gharama kubwa, pia ilinibidi kulipa kiasi cha ziada cha KSh2,000 ($15) ili kusafirisha mbolea hiyo hadi Kisumu na kisha hadi shambani kwangu huko Ahero.”

Mfumo wa ununuzi wa mbolea
Mkakati wa kitaifa wa mbolea wa Kenya unafanya kazi kupitia mfumo wa mikataba ya zabuni wazi na ununuzi wa kutoka Serikali hadi Serikali. Makubaliano ya muda mfupi hadi wa kati ya kununua kiasi maalum cha mbolea yanafikiwa na waagizaji wakubwa wa kibinafsi, wafanyabiashara wa bidhaa za kimataifa, na pia makampuni ya utengenezaji wa ndani na kimataifa.
Kulingana na World Integrated Trade Solution (WITS), Kenya iliagiza mbolea zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 418 mwanzoni mwa mpango wa ruzuku mwaka wa 2022, ikipitia soko la kimataifa lisilo tulivu lililovurugwa na kuzuka kwa vita vya Urusi na Ukraine.
Tangu Urusi ilipovamia Ukraine mwaka wa 2022, usambazaji wa mbolea chini ya NFSP sasa unategemea zaidi Morocco, huku Urusi, ikifanya kazi kupitia mikataba iliyopo na mifumo tata ya usafirishaji ikibaki kuwa chanzo cha pili kwa ukubwa licha ya vikwazo vya kijiografia na kifedha.
Saudi Arabia na Qatar zilitoa virutubisho vya nitrojeni na urea, huku nchi kadhaa za Ulaya na Misri zikijaza mapengo yaliyosalia ili kudumisha usambazaji wa mbolea licha ya soko la kimataifa lisilo imara.
Mfumo wa kupata mbolea kutoka vyanzo mbalimbali uliwezesha Kenya kudumisha upatikanaji wa mbolea katika kipindi cha mishtuko ya soko la kimataifa. Lakini huku Saudi Arabia na Qatar zikiwa wasambazaji wakuu wa mbolea ya nitrojeni chini ya NFSP, mgogoro katika Ghuba unaweza kuilazimisha Kenya kutazama zaidi ya eneo hilo kwa ajili ya usambazaji, jambo ambalo linaweza kuongeza gharama.
Wakati wa hotuba yake ya Hali ya Taifa mnamo Novemba 2025, Rais William Ruto alibainisha kuwa magunia milioni 7 (tani 350,000) ya mbolea ya ruzuku ilikuwa imesambazwa ili kuongeza uzalishaji wa mahindi nchini. Ripoti ya Utafiti wa Kiuchumi wa Kenya ya mwaka 2026 ilionyesha kuwa mavuno ya mahindi yaliongezeka kutoka magunia milioni 44.8 mwaka 2024 hadi magunia milioni 45.8 mwaka 2025. Wakati huo, Rais aliahidi kuongeza kiasi cha mbolea kitakachosambazwa mwaka 2026.
“Tunapanga kusambaza magunia milioni 12.5 (tani 625,000) katika kata zote 1,450, tukihakikisha kuwa kila mkulima anapata pembejeo kwa bei nafuu,” aliliambia Bunge.
Hata hivyo, hayo yalikuwa kabla ya mgogoro katika eneo la Ghuba, ambao ulivuruga usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz na kutatiza usambazaji wa mbolea.

Ghuba ya Uajemi ni mojawapo ya maeneo makuu duniani ya uzalishaji wa virutubisho vya nitrojeni na fosfeti, huku karibu theluthi moja ya biashara ya urea inayosafirishwa kwa njia ya bahari duniani ikipitia maji yake. Data kutoka kwa shirika la UM la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) inaonyesha kwamba Kenya huagiza takriban 26% ya jumla ya usambazaji wake wa mbolea moja kwa moja kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Kampuni za meli zinakabiliwa na gharama kubwa za bima dhidi ya hatari za vita, ada za ziada za mafuta ya meli, na ucheleweshaji wa muda mrefu bandarini. Baadhi ya meli hulazimika kupitia Rasi ya Tumaini Jema ya Afrika, na kuongeza wiki kadhaa kwa ratiba za usafiri na kuzidisha gharama za usafirishaji.
Kwa Kitur, misukosuko hii ni tishio la moja kwa moja kwa kipato chake. “Serikali imetoa ruzuku kwa mbolea; bei yake haijapanda. Lakini bei ya dizeli iko juu sana. Ni kana kwamba fedha zote nilizookoa kwa kununua mbolea yenye ruzuku zimeishia kununua mafuta ya matrekta ya kulimia,” Kitur aliambia Mongabay.
Mwaka wa 2026 ulianza kwa utulivu kiasi, huku bei ya rejareja ya dizeli ikiwa karibu KSh165.63 ($1.28) mwezi Februari, na kufikia KSh206.84 ($1.60) kufikia mwezi Aprili. Katikati ya mwezi Mei, Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Petroli (EPRA) ilitangaza bei ya rekodi ya juu ya KSh242.92 ($1.88) kwa lita jijini Nairobi.

Hata hivyo, kufuatia maombi na maandamano makubwa ya wadau wa usafiri wa umma kuhusu gharama kubwa ya maisha, mamlaka ya EPRA ilifanya marekebisho ya dharura katikati ya mwezi, ikipunguza bei kwa KSh10.06 ($0.078) na kufikia KSh232.86 ($1.80). Kwa sasa, lita moja ya dizeli inauzwa kwa KSh222.86 ($1.72).
Mwaka wa 2024 hadi katikati ya mwaka wa 2025, Kenya ilikuwa na bei ya chini ya awali ya ununuzi wa mahindi iliyowekwa kuwa KSh3,500 ($27.03) kwa gunia la kilo 90 la mahindi. Hata hivyo, mwaka wa 2026, Bodi ya NCPB ilitangaza kuwa itatekeleza bei ya chini ya KSh4,000 ($30.89) kwa kila gunia la kilo 90 la mahindi, ili kukabiliana na uhaba wa usambazaji katika soko la ndani na kuwalinda wakulima ambao bado walikuwa na akiba ya nafaka. Hatua hii, hata hivyo, ilizua malalamiko mengi, kwani baadhi ya wakulima walipendelea zaidi makampuni ya wasagaji binafsi wa mahindi ambao hununua gunia la kilo 90 kwa bei ya kati ya KSh4,200 ($32.43) na KSh4,400 ($33.98).
Hatua za Kuchukuliwa
Serikali ina matumaini ya kuwawezesha wakulima kuhimili mishtuko ya soko la kimataifa na kuimarisha usalama wa chakula nchini. Hata hivyo, licha ya kugeukia wauzaji wapya, Kenya ipo katika njia panda. Hadi Kenya itakapojenga uwezo wa kujitegemea zaidi katika uzalishaji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo, itaendelea kuathiriwa na mishtuko ya kimataifa, ambapo mzozo katika njia za usafirishaji za mbali unaweza kuamua moja kwa moja bei ya chakula nchini.
Picha ya bango: Philip Kitur, mkulima mwenye umri wa miaka 72 kutoka Trans-Nzoia, Kenya, anayenunua mbolea inayouzwa kwa ruzuku ya serikali. Picha na Achieng’ Otieno, Mongabay.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 3/07/2026.