- Zaidi ya nyati 100 wameuawa katika hifadhi hiyo tangu mwaka 2015.
- Ukaribu na kambi ya wakimbizi umechochea kushamiri kwa biashara ya nyama ya porini.
- Utekelezaji duni wa sheria unachangia kuendelea kwa tatizo hilo.
- Rasilimali na vitendea kazi vya kutosha vitasaidia kuimarisha ulinzi wa hifadhi.
Unapoingia ofisini kwa msimamizi wa hifadhi, kitu cha kwanza unachokiona ni picha za mafuvu na mifupa ya nyati, pundamilia na wanyama wengine. Wanyama hawa ambao kwa miaka mingi wamekuwa fahari kwa Burundi, huenda wakatoweka na kubaki historia iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuzuia kuuawa kwao katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu.

Hifadhi hiyo inayoingia katika mikoa minne ambayo ni Muyinga, Cankuzo, Ruyigi na Karusi, inaundwa kwa asilimia 75 na uoto wa savana, asilimia 15 ni misitu na asilimia 8 ni maeneo ya majani. Kulingana na mipaka yake iliyowekwa mwaka 1991, hifadhi ina urefu wa kilometa 62 na upana wa kati ya kilometa 5 hadi 13.
Athanasie Mpawenimana, Afisa wa Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu anasema hapo awali mtandao wa ujangili ulikuwa mdogo na usio na mpangilio. Hata hivyo anasema katika miaka ya karibuni umepanuka kwa kasi, kuwa na muundo na kuvuka mipaka ya nchi.
“Awali, matukio yalikuwa ya hapa na pale. Leo hii tunazungumzia mitandao iliyopangwa vizuri inayofanya kazi kwa kushirikiana na watu wa ndani na nje ya hifadhi,” anaeleza.
Anataja pia kuwepo kwa biashara ya nyama ya porini ambapo inaelezwa kuwa wanyama huuawa na nyama kuuzwa nchi za jirani. Anasema; “Wawindaji haramu humuua mnyama, huchukua nyama haraka na kutoweka. Kinachobaki ni mafuvu na mizoga ambayo mara nyingi hutupwa karibu na milango ya kuingilia kwenye hifadhi,” anaongeza.
Anafafanua kuwa kuongezeka kwa biashara hii haramu pia kunahusishwa kwa sehemu na ukaribu wa kambi ya wakimbizi ya Kavumu, ambako baadhi ya watu wanadaiwa kujihusisha na uuzaji wa nyama ya porini kwa raia wa Kongo waliopo kambini humo.
Anatole Niyonzima, mlinzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, anasema zaidi ya nyati 100 wameuawa katika hifadhi hiyo tangu mwaka 2015.
Parrain Doris Cubahiro, kutoka OBPE (Ofisi ya Burundi ya Ulinzi wa Mazingira) anasema takwimu hizi zinawakilisha sehemu tu ya hali halisi kutokana na ugumu wa kupata takwimu sahihi, unaosababishwa na uhaba wa rasilimali watu, vifaa na mifumo mizuri ya kiutendaji. Anasema kwa sasa kuna walinzi 62 pekee wanaolinda eneo lenye ukubwa wa hekta 50,800.
Mojawapo ya mifano halisi ni idadi ya nyati ambapo mwaka 2016, waraka mmoja ulikadiria kuwa idadi ya wanyama hao katika hifadhi hiyo ilikuwa 1,101 wakati waraka mwingine uliotolewa mwaka huohuo ulitoa makadirio ya nyati 817, hali inayoonyesha utofauti mkubwa wa takwimu.

Kama ilivyo katika huduma nyingi nchini Burundi, suala la takwimu sahihi bado ni changamoto kubwa. Ni vigumu kujua kwa usahihi idadi ya sasa ya wanyama katika hifadhi.
Mwaka 2024, aliyekuwa Waziri wa Mazingira wa Burundi, Albert Mbonerane katika mahojiano na gazeti la Iwacu alitangaza kuwa nyati ni miongoni mwa spishi zilizokuwa katika hatari kubwa ya kutoweka na akatoa mifano kuunga mkono kauli yake.
Uwindaji Haramu
Sababu kadhaa zimetajwa kuwa chanzo cha tishio linalowakumba wanyama katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, na hivyo kuchangia kupungua kwao.
OBPE (Ofisi ya Burundi ya Ulinzi wa Mazingira) inasema kuwa ujangili, ambao umekuwa ukiendelea kwa miongo kadhaa, ni mojawapo ya sababu kuu za kupungua kwa kasi kwa wanyamapori katika hifadhi hiyo.
“Ujangili una historia ndefu katika mahusiano kati ya jamii na rasilimali za asili nchini Burundi. Mbinu za wawindaji haramu zimekuwa zikibadilika kadiri muda unavyopita,” anasema Parrain Dorain.
Anaeleza kuwa kabla ya kipindi cha ukoloni, uwindaji na ukusanyaji wa chakula vilikuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya jamii, lakini taratibu hizo zilipungua polepole bila kutoweka kabisa.
“Kadiri Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu ilivyoendelea katika miaka ya 1990 na 2000, uwindaji ulifanyika kwa kutumia mitego rahisi. Kuanzia miaka ya 2010, mbinu zilianza kuwa hatari zaidi, zikitumia nyaya za chuma na mashimo ya kunasa wanyama. Leo hii, ujangili umekuwa wa kisasa zaidi, wakati mwingine ukihusisha mbwa na hata moto ili kuwafukuza wanyama,” anaongeza.

Mpawenimana anaeleza kuwa wawindaji haramu sasa wamejipanga vizuri na wanafahamu kikamilifu mapungufu ya mifumo ya ulinzi wa hifadhi. Anasema wahalifu hao wanatumia uhaba wa watumishi kama upenyo wa kufanya uhalifu huo.
Anatole Niyonzima, mlinzi wa misitu kandokando ya Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, anasema kutokana na tatizo la uwindaji haramu, makundi ya wanyama yaliyokuwa yakionekana miaka ya nyuma, hayapo tena. Anasema: “Miaka ya nyuma ilikuwa rahisi kuona makundi ya nyati au pundamilia lakini hivi sasa walinzi wanaweza kupiga doria kwa muda mrefu bila kuona mnyama yeyote”.
Licha ya uhaba wa watumishi, anasema kazi hiyo inaweka maisha ya walinzi hatarini. Anafafanua kuwa kuna wakati mlinzi mmoja alishambuliwa vikali na mbwa wakati wa doria na akalazwa hospitalini akiwa katika hali mbaya. Mfanyakazi mwingine alijeruhiwa mguuni kwa mkuki akiwa kazini.
“Tunakabiliwa na makundi hatari, yaliyojipanga vizuri na yenye rasilimali za kutosha,” anasema Niyonzima, kauli iliyoungwa mkono na mlinzi mwingine akisema: “Wanakuja kwa idadi kubwa, wanaijua vizuri hifadhi na mara nyingi hutushitukiza. Wakati mwingine hatupati hata muda wa kujibu, kwa sababu hatuna vifaa vya kuweza kuwakabili”.
Anaongeza kuwa idadi kubwa ya wawindaji haramu hutoka katika mkoa wa Karusi, ambapo matukio ya ujangili yameripotiwa kuwa mengi zaidi, kabla ya kuenea taratibu hadi eneo la Cankuzo.
Kwa mujibu wa Mpawenimana, udhaifu wa adhabu za kisheria unachangia kuendelea kwa tatizo hilo. Anasema watu wanaokamatwa, mara nyingi huachiwa baada ya kulipa faini ya takribani faranga za Burundi 100,000 ($33.3), jambo ambalo halina nguvu ya kuzuia uhalifu huo.
Moto kwenye misitu
Moto kwenye misitu ni njia nyingine inayochangia kutokomea kwa wanyama hao. “Wakati wa kiangazi, sehemu mbalimbali za hifadhi huharibiwa kupitia moto unaowashwa ama na wawindaji ili kufukuza wanyama au na wananchi wanaofanya hivyo ili kurahisisha shughuli za kijamii kama kurina asali na kutafuta malisho kwa wanyama. Moto huo huharibu makazi na kuwafanya wanyama wakimbie mbali zaidi,” anasema Mpawenimana.
Hatari nyingine inayoikumba hifadhi ya taifa ni barabara kuu ya taifa inayounganisha mikoa ya Cankuzo na Muyinga. Kwa mujibu wa Parrain Doris Cubahiro, matukio ya magari hasa malori makubwa hupita haraka bila kujali kwamba njia hizo zinapita katika eneo la hifadhi lenye wanyama.
Athari za kupungua kwa wanyama
Parrain Dorain Cubahiro, mkuu wa maeneo yaliyohifadhiwa na ukuzaji wa utalii wa ikolojia katika Ofisi ya Burundi ya Ulinzi wa Mazingira, anaeleza wasiwasi wake kutokana na kupungua kwa kasi kwa spishi mbalimbali. Anasema: “Mnyama anapouawa, inamaanisha mambo mawili: kwanza kupungua kwa idadi ya wanyama, na pili kupotea kwa uwezo wake wa kuzaliana”.
Anaongeza kuwa upotevu huu wa polepole wa wanyamapori una athari ya moja kwa moja katika sekta ya utalii wa ikolojia na mapato ya hifadhi.
Anasema kwa sasa, wageni hulipa takribani faranga za Burundi 5,000 ili kuingia katika hifadhi hiyo, lakini iwapo kungekuwa na wanyama wengi zaidi, wageni wangekuja kwa wingi zaidi na mapato ya hifadhi yangeongezeka kwa kiasi kikubwa.
“Kupungua kwa wanyama kunapunguza mvuto wa hifadhi na huenda kukasababisha kushuka kwa idadi ya watalii wanaoitembelea,” anasisitiza.

Aidha anasema kupungua kwa wanyama katika hifadhi kunaweza kusababisha kutokuwepo kwa uwiano wa kiikolojia na upotevu usioweza kurekebishwa wa bioanuwai, jambo linalohatarisha kabisa dhima ya msingi ya hifadhi hiyo.
Changamoto
Juhudi za kukabiliana na mambo yanayohatarisha wanyama katika hifadhi hiyo, zinakwamishwa na changamoto mbalimbali.
Uhaba wa rasilimali umetajwa kama sababu mojawapo inayokwamisha juhudi za kukabiliana na wawindaji haramu ambao wamekuwa wakibadilisha mbinu kila wakati.
“Wawindaji wanakuja katika makundi ya watu kati ya 20 hadi 30. Wanaweka mitego ya nyaya za chuma, ili kuwanasa na kuwaua kwa ajili ya kuwala,” anaeleza Anatole.
“Mbinu nyingine wanayotumia ni mbwa ambapo nyati wanapopanda kwenye kilima, mbwa hupiga kelele, zinazowashtua wanyama hao na kufanya warudi chini ambako wawindaji kwa kutumia mikuki, mishale na mipanga, huwaua,” anasema.
Marc Bakundintwari, Msimamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, anasema wawindaji haramu pia hutishia maisha ya wananchi wanaolinda hifadhi. Anasema: “Miezi michache iliyopita, wawindaji haramu walijeruhi kiongozi mmoja sehemu ya mkono. Pia kuna mlinzi mmoja aliyekamatwa, kupigwa na kujeruhiwa kichwani kwa mapanga”.
Utekelezaji duni wa sheria pia ni kikwazo kingine. Kwa mujibu wa Bakundintwari, licha ya sheria namba 1/21 ya Oktoba 2018, inayozungumzia ufugaji wa kudumu inapiga marufuku wanyama wa kufungwa kuzunguka bila usimamizi kwenye ardhi ya Burundi, watu wamebuni mbinu nyingine ambapo huwaleta ng’ombe kwa siri kwa ajili ya malisho. Anasema hayo yote yanatokea kwa sababu ya sheria kutotekelezwa ipasavyo.
Nini kifanyike?
Ofisi ya Burundi inayohusika na kulinda mazingira ina mikakati mbalimbali kuokoa wanyama hao. Mkakati wa kwanza ni kuhakikisha wanatoa vitendea kazi kwa walinzi wa hifadhi ikiwa ni pamoja na silaha ili waweze kujilinda dhidi ya wawindaji haramu.
“Wawindaji haramu hawana uoga na vifaa visivyo vya kisasa vinavyotumiwa na wanaolinda mazingira na kupigana nao bila kuwa na silaha ni kuhatarisha maisha yao,” anasema Niyonzima.
Hatua nyingine ni kuongeza idadi ya walinzi wa hifadhi, kuboresha rasilimali za kiutendaji (magari, mawasiliano na vifaa vya ufuatiliaji) pamoja na kuanzisha teknolojia za kisasa kama vile droni na mifumo ya ufuatiliaji wa GPS ili kudhibiti vyema shughuli ndani ya hifadhi.
“Wanyama katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu wanahitaji kuokolewa. Vinginevyo, spishi nyingi zinakabiliwa na hatari ya kutoweka,” anasema Bakundintwari.
Picha ya bango: Kundi la nyati likiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, nchini Burundi. Picha na Lionel Jospin Mugisha.