- Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imempa dhamana Mohamed Hamad Sulemani, anayekabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi yanayohusisha biashara haramu ya vipande 19 vya meno ya tembo vyenye thamani ya zaidi ya TSh bilioni 2.9.
- Jaji Amold Kirekiano aliamua kuwa mwombaji ana haki ya dhamana baada ya upande wa Jamhuri kutopinga ombi hilo na kutokuwepo ushahidi unaoonyesha angekimbia, kuharibu ushahidi au kuingilia mwenendo wa kesi.
- Masharti ya dhamana yanamtaka Sulemani kuweka TSh368.7 milioni taslimu au hati ya mali yenye thamani sawa, kuwa na wadhamini wawili, kutotoka nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama, kukabidhi pasipoti yake na kuhudhuria vikao vyote vya kesi.
DAR ES SALAAM, Tanzania – Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imempa dhamana Mohamed Hamad Sulemani, anayekabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi yanayohusisha kufanya biashara haramu ya nyara za Serikali zenye thamani zaidi ya TSh bilioni 2.9 ($1,104,763).
Mahakama hiyo mbele ya Jaji Amold Kirekiano ilitoa uamuzi Juni 15, 2026 baada ya kusikiliza maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na Mohammed dhidi ya Jamhuri.
Sulemani anakabiliwa na mashtaka matatu, shtaka la kuongoza genge la uhalifu, kushiriki biashara haramu ya nyara na kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria, akiwa pamoja na washtakiwa wengine watatu katika kesi ya Uhujumu Uchumi namba 10770 ya mwaka 2026 inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.
Katika maombi yake ya dhamana, Wakili wa mshtakiwa, Meschack Dede, aliiomba Mahakama Kuu izingatie kuwa makosa yanayomkabili mteja wake yanadhaminika na kwamba thamani ya mali inayodaiwa, nusu ihesabiwe kwa kugawanywa kwa washtakiwa wote wanne.
Ombi la wakili lapita
Upande wa Jamhuri haukupinga ombi hilo la wakili na wala haukuwasilisha kiapo cha kupinga maombi.
Wakili wa Serikali Grace Kibaki aliiomba mahakama izingatie hati ya mashtaka pamoja na masharti ya Sheria ya Uhujumu Uchumi kuhusu utoaji wa dhamana.
Baada ya kusikiliza maombi hayo, Jaji Kirekiano alikubali kumpatia mwombaji dhamana kwa kuzingatia masharti ya kisheria kuhusu kiwango cha fedha kinachotakiwa kuwekwa mahakamani.
Alisema kifungu cha 36(5)(a) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi kinamtaka mshtakiwa kuweka fedha taslimu au mali yenye thamani ya nusu ya fedha au mali inayohusika katika kosa.
Jaji alitegemea maamuzi ya awali ya mahakama, ikiwemo kesi ya Arafat Hussein Nasri dhidi ya Jamhuri na kesi ya Silvester Hillu Dawi na wenzake dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ambazo ziliruhusu mahakama kutumia busara ili kuhakikisha haki inatendeka.
Jaji asema kuwa kwa vile ombi halikupingwa na upande wa Jamhuri na hakukuwa na ushahidi wowote ulioonyesha kuwa mshtakiwa angeweza kukimbia, kuharibu ushahidi au kuingilia mwenendo wa kesi mahakama haikuwa na sababu ya kutoendelea kuzingatia ombi la dhamana kwa mujibu wa sheria.
Jaji Kirekiano alisema hakuna sababu zilizowasilishwa mahakamani zinazoonyesha kuwa mwombaji hastahili kupewa dhamana.
“Katika kesi hii, thamani ya mali inayodaiwa kuhusika, shtaka la kwanza TSh983,233,052, Shtaka la pili TSh983,233,052 na shtaka la tatu TSh983,233,502 ambayo jumla thamani yake ni TSh2,949,699,156,” alisema Jaji.
Nusu ya jumla ya thamani ni TSh1,474,849,578, ikigawanywa kwa washtamiwa wote wanne, kiasi kinachotakiwa kwa kila mshitakiwa ni fedha taslimu TSh368,712,394.50 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani sawa au zaidi iliyopo Dar es Salaam.
Masharti ya dhamana
Masharti ya dhamana yaliyotolewa kwa washitakiwa ni wadhamini wawili waliotakiwa kusaini dhamana ya maandishi ya TSh184,356,197.25 kila mmoja na sharti lingine wadhamini wawe na kitambulisho cha Taifa (NIDA) na hati ya kusafiria ama leseni ya udereva.
Masharti mengine ni kutotoka nje ya jiji la Dar es Salaam bila kibali cha mahakama, kukabidhi pasipoti na nyaraka nyingine za kusafiria mahakamani, kuhudhuria vikao vyote atakavyoitwa na kutofanya kosa lolote linaloweza kusababisha kifungo wakati akiwa nje kwa dhamana.
Jaji Kirekiano alisema uthibitishaji wa wadhamini na nyaraka za dhamana utafanywa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mara tu mwombaji atakapokuwa tayari kutimiza masharti hayo.
Washitakiwa Mohamed Hamad Sulemani, Faki Juma Shaal, Khamis Hussein Hassan na Keneth Jacob Tweve wanashtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mashtaka matatu yakiwemo kumiliki isivyo halali nyara za Serikali.
Katika hati ya mashtaka ilidaiwa katika shtaka la kwanza kuwa kati ya Machi na Mei mwaka 2026 mkoani Mtwara na Dar es Salaam, kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu kwa kukusanya, kumiliki na kupatikana na vipande 19 vya meno ya tembo vyenye thamani ya $38,000 sawa na TSh983,233,502 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa kati ya Aprili 30 mwaka 2026 na Mei mosi mwaka huo jijini Dar es Salaam, washtakiwa walijihusisha na kusafirisha vipande 19 vya meno ya tembo vyenye thamanj ya TSh983,233,502 bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Shtaka la tatu ilidaiwa kuwa Mei 11 mwaka 2026, washtakiwa wakiwa maeneo ya Goba walikutwa wakimiliki vipande hivyo 19 vya meno ya tembo vyenye thamani ya TSh983,233,502 isivyo halali.
Shauri hilo linasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ahmed Bilal na lilipangwa kutajwa Juni 29 mwaka huu na washtakiwa wote wako rumande.
Picha ya bango: Super tusker Craig akiwa katika Hifadhi ya Kitaifa ya Amboseli, nchini Kenya, siku chache kabla hajaaga dunia. Meno ya tembo yameendelea kuwa miongoni mwa nyara za serikali zinazotafutwa zaidi katika biashara haramu. Picha na Elodie Toto, Mongabay.