- Kesi imesikiliza na jumla ya mahakimu watano tofauti.
- Washitakiwa wengine waliachiwa baada ya kuingia kwenye maridhiano na DPP.
- Washtakiwa waliobaki wanaendelea kusota rumande.
Ile kesi ya kukutwa na meno ya tembo ambayo iko mahakamani kwa miaka 10 sasa huku watuhumiwa wakiendelea kusota rumande, imeendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, Jijini Dar es Saalam.
Washtakiwa walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza mwaka 2018, na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde.
Baada ya kusomewa mashtaka, shauri lilifutwa, lakini muda mfupi baadaye wakasomewa mashtaka upya mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile, ambaye sasa hivi ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Washitakiwa walikuwa 11
Wakati kesi inaanza, washitakiwa walikuwa 11, lakini idadi hiyo ilipungua baada ya washtakiwa watano kuingia kwenye maridhiano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), ambapo walikiri makosa yao na kuachiliwa baada ya kutimiza makubaliano waliyoafikiana.
Washtakiwa waliobakia katika shauri hilo ni Victor Mawanda, Mussa Abdallah, Abbas Jabu, Haruna Kasa na Halfani Kahengele.
Awali ilidaiwa katika hati mashtaka kuwa kati ya Januari mwaka 2006 na Juni mwaka 2016, washtakiwa walipanga njama ya kuongoza genge la uhalifu Jijini Dar es Salaam.
Walidaiwa kuuza, kupokea, kununua, kuhamisha, kusafirisha na kumiliki vipande 660 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh 4,656,795,000 ambayo ni nyara za serikali.
Ilidaiwa pia kuwa kati ya Aprili mosi na Juni 24 mwaka 2016, maeneo ya Mbezi Msakuzi wilayani Ubungo, washtakiwa walikutwa wakimiliki vipande hivyo vya meno ya tembo bila kuwa na kibali ama leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Washitakiwa walikana mashitaka na wako gerezani kwa kuwa kesi yao ya uhujumu uchumi haina dhamana.
Korti kusikiliza shahidi wa 10
Hadi sasa shauri hilo limeshasikilizwa na mahakimu zaidi ya watano katika vipindi tofauti. Mwaka 2023, shauri hilo lilikuwa linasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mary Mrio. Kabla ya hapo, lilikuwa linasikilizwa na Hakimu Rhoda Ngimilanga.
Kwa sasa kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahimu Mushi na inaendelea kusikilizwa ambapo shahidi wa tisa, WP 10462, Sajenti Julieth aliyeshiriki kwenye upelelezi wa shauri hilo, amekamilisha kutoa ushahidi wake.
Shauri hilo liliahirishwa hadi Juni 23, 2026, kwa ajili ya kuendelea kusikiliza shahidi wa 10.
Wakati huohuo Jeshi la Magereza limetekeleza amri iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam ya kuwafikisha mahakamani washtakiwa wanne wanaokabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kumiliki vipande 19 vya meno ya tembo bila kuwa na kibali.
Washtakiwa katika shauri hilo ni Faki Shaal (54), Khamisi Hassan (40), Kenneth Twelve (54) na Mohammed Suleiman (43).
Akiwakilisha upande wa Jamhuri Wakili wa Serikali, Erick Mabagala aliomba mahakama iahirishe shauri hilo kwa kile alichokieleza kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Wakili huyo alikubali maombi ya upande wa mashtaka la kuahirisha shauri hadi tarehe itakayopangwa na Mahakama.
Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mkuu Ahmed Bilal ambaye alikuwa na udhuru aliahirisha shauri hilo hadi Juni 29 mwaka huu, shauri litakapoletwa kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa hao ambao ni wafanyabiashara wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 10770/2026.
Katika shtaka la kwanza, upande wa Jamhuri ulidai kuwa kati ya Machi na Mei mwaka 2026, mkoani Mtwara na Dar es Salaam kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu kwa kukusanya, kumiliki na kupatikana na vipande 19 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 38,000 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa kati ya Aprili 30 mwaka 2026 na Mei mosi mwaka huo, jijini Dar es Salaam washtakiwa walijihusisha na kusafirisha vipande 19 vya meno ya tembo bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika shtaka la tatu ilidaiwa kuwa Mei 11 mwaka 2026 washtakiwa wakiwa maeneo ya Goba walikutwa wakimiliki vipande hivyo 19 vya meno ya tembo isivyo halali.
Wakati kesi inatajwa Juni Mosi mwaka huu, shauri hilo halikusikilizwa kwa kuwa mtandao ulikuwa unasumbua. Kufuatia hali hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Chalo aliomba Mahakama itoe hati ya wito washtakiwa waletwe mahakamani na upande wa utetezi walikubaliana na maombi hayo.
Hakimu Bilal alikubali maombi hayo na kutoa hati ya wito akiwaamuru Magereza kuwafikisha washtakiwa mahakamani Juni 15 mwaka huu kusikiliza shauri lao. Magereza walitekeleza amri hiyo na washtakiwa waliletwa mahakamani.
Picha ya bango: Mshtakiwa Halfani Kahengele na wenzake wakitoka mahabusu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam wakisindikizwa kuelekea chumba cha Mahakama kwa ajili ya kusikiliza shauri lao. Picha na Tumaini Mgeni.