- Wahifadhi nchini Kenya wanatumia teknolojia za GPS na setilaiti kufuatilia twiga wa Maasai katika Eneo la Uhifadhi la Tsavo ili kuelewa athari za maendeleo ya miundombinu na shughuli za binadamu kwa mienendo yao.
- Upotevu na kugawanyika kwa makazi kutokana na ujenzi wa barabara, reli, uzio na upanuzi wa makazi ya watu vinaendelea kuwa miongoni mwa vitisho vikubwa kwa maisha ya twiga barani Afrika.
- Takwimu zitakazokusanywa kutoka kwa twiga 20 waliotiwa alama zinatarajiwa kusaidia kuboresha mikakati ya uhifadhi na usimamizi wa twiga wa Maasai nchini Kenya.
- Ingawa idadi ya twiga nchini Kenya imeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, wahifadhi wanaonya kuwa ongezeko la watu, migogoro ya matumizi ya ardhi na mabadiliko ya tabianchi vinaendelea kuhatarisha mustakabali wa spishi hiyo.
Dunia inapoadhimisha Sikuu ya Twiga leo, siku inayolenga kusherehekea na pia kuhamasisha kuhusu changamoto zinazowakabili mamalia hawa warefu zaidi duniani, mjadala sasa unaelekezwa katika namna bora ya kuwahifadhi si kama spishi moja pekee, bali kama spishi nne tofauti, huku ongezeko la watu na maendeleo ya miundombinu yakiendelea kuwa tishio kwa maisha yao.
Kufuatia pendekezo la ujenzi wa Barabara Kuu ya Kasi ya Nairobi-Mombasa (Nairobi Mombasa Expressway – NME), barabara ya njia mbili itakayojengwa sambamba na Reli ya Kisasa (SGR), mpango wa Twiga Tracker Initiative uliwatia alama twiga 20 (majike 11 na madume 9) ili kufuatilia mienendo na matumizi ya maeneo ya twiga wa Maasai katika ukanda wa Nairobi-Mombasa kabla, wakati na baada ya ujenzi huo ndani ya Eneo la Uhifadhi la Tsavo.
Kupitia teknolojia bunifu za ufuatiliaji, na kwa ushirikiano na mfumo wa EarthRanger, programu ya wakati halisi inayosaidia juhudi za uhifadhi wa wanyamapori, watafiti waliwafunga twiga vifaa vyepesi vya GPS vilivyounganishwa na setilaiti kwenye mikia yao ili kupata taarifa muhimu kuhusu namna wanavyohama, jinsi wanavyotumia makazi yao, na athari za shughuli za binadamu kwa mienendo yao.
Mpango wa Twiga Tracker, unaotekelezwa na Giraffe Conservation Foundation (GCF), kwa sasa unafuatilia twiga tisa katika Hifadhi ya Taifa ya Tsavo Mashariki, wanane katika Hifadhi ya Taifa ya Tsavo Magharibi na watatu katika ranchi za Taita.
Shirika la GCF lilitekeleza zoezi hili kwa ushirikiano na Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS), Tsavo Trust, Taasisi ya Utafiti na Mafunzo ya Wanyamapori (WRTI), Wildlife Works na Sheldrick Wildlife Trust.
Kwa mujibu wa GCF, Eneo la Uhifadhi la Tsavo ni muhimu sana kwa kuwa linatumika kama njia kuu ya kupitisha wanyamapori mbalimbali.

Hata hivyo, shirika hilo linaonya kuwa muunganiko huo wa ikolojia unazidi kutishiwa na upanuzi wa makazi ya watu na miundombinu inayounganisha miji miwili mikubwa zaidi nchini Kenya – Nairobi na Mombasa.
“Takwimu tayari zipo kuhusu namna tembo wa savana wa Afrika (Loxodonta africana) wanavyotembea katika eneo hili, lakini mienendo ya twiga wa Maasai bado haijafahamika vya kutosha,” GCF ilisema.
Takwimu zilizokusanywa katika zoezi hilo lililofanyika kati ya Mei 16–22, 2026 zinatarajiwa kusaidia kuboresha mikakati ya uhifadhi na usimamizi wa twiga wa Maasai nchini Kenya.
Twiga wa Maasai ni mojawapo ya spishi nne za twiga zilizotambuliwa rasmi katika uamuzi muhimu wa mwaka 2025 wa Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) baada ya miaka ya tathmini za kina za kisayansi. Uamuzi huo ulifuta mtazamo wa awali uliokuwa ukiwaainisha twiga wote duniani kama spishi moja.
Uamuzi huo ulitokana na mapito ya kitaalamu ya taksonomia, ambao ni mfumo wa kisayansi wa kuainisha viumbe hai, yaliyoendeshwa na Kikosi Kazi cha Taksonomia Chini ya Kikundi Maalumu cha Twiga na Okapi cha Tume ya IUCN ya Kuokoa Spishi (GOSG) na (SSC).
Mbali na twiga wa Maasai (Giraffa tippelskirchi), spishi nyingine tatu zilizotambuliwa ni twiga wa kaskazini (Giraffa camelopardalis), twiga wa wavu (Giraffa reticulata) na twiga wa kusini (Giraffa giraffa).
Kwa mujibu wa wahifadhi, utambuzi wa spishi hizi nne umefungua njia kwa kila moja kutathminiwa kivyake kulingana na ukubwa wa idadi yake, eneo la usambazaji na vitisho vinavyoikabili. Hapo awali twiga walizingatiwa kama spishi moja yenye jamii ndogo kadhaa, hali iliyoweza kuficha hatari zinazowakabili baadhi ya makundi yao.
Kwa mujibu wa GCF, idadi ya twiga barani Afrika ni takribani 117,000, ikiwa ni upungufu wa karibu asilimia 30 katika kipindi cha miaka 35 iliyopita licha ya mafanikio ya uhifadhi yaliyopatikana katika baadhi ya maeneo.
Mojawapo ya mafanikio hayo yameripotiwa nchini Kenya, ambapo Sensa ya Wanyapori ya mwaka 2025 ilionyesha ongezeko la asilimia 5.4 la idadi ya twiga. Kwa mujibu wa sensa hiyo, twiga walifikia takribani 43,000.
Mafanikio hayo yalihusishwa na “miongo kadhaa ya juhudi za kukomesha ujangili katika hifadhi, uhamishaji wa twiga kwa malengo ya uhifadhi, utekelezaji mkali wa sheria, uhifadhi unaoongozwa na jamii na kuimarishwa kwa muunganiko wa ikolojia.”
“Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo ambayo kwa muda mrefu yalichukuliwa kuwa makazi bora ya twiga, idadi yao imepungua kwa hadi asilimia 95 katika kipindi hicho hicho,” GCF ilisema.
Arthur Bienvenu Muneza, mwanaikolojia wa wanyamapori na mratibu wa GCF Afrika Mashariki, anasema kutambuliwa kwa spishi nne tofauti kunaruhusu tathmini sahihi zaidi ya hali ya kila spishi kutokana na vitisho maalumu vinavyoikabili.
“Orodha Nyekundu ya IUCN ni nyenzo muhimu ya uhifadhi inayobainisha hali ya mimea na wanyama ili kusaidia na kuchochea hatua za uhifadhi pamoja na mabadiliko ya sera. Hili ni muhimu hasa kwa sababu spishi hizi nne zinastahili kuainishwa katika viwango tofauti vya hatari kulingana na changamoto zinazozikabili,” alisema Muneza.
Ingawa tathmini tofauti za Orodha Nyekundu bado zinaendelea, wahifadhi wanatarajia kutakuwa na tofauti kubwa katika hadhi ya uhifadhi wa spishi hizo nne kutokana na tofauti za idadi na vitisho vinavyokabili kila moja katika maeneo mbalimbali ya Afrika.
Twiga ni sehemu muhimu ya mazingira ya Afrika kwa sababu wanachangia kudumisha mifumo ya ikolojia. Wanachukuliwa kuwa “wahandisi wa ikolojia” kwa kuwa husaidia kuunda na kudumisha savana kupitia ulaji wa majani, usambazaji wa mbegu na kuhifadhi uwiano wa mazingira.
Kwa sasa wahifadhi wanatumia teknolojia za kisasa za GPS na ufuatiliaji kwa setilaiti kufuatilia na kuhifadhi twiga.
“Hili ni muhimu kwa sababu upotevu na kugawanyika kwa makazi, hasa kutokana na shughuli za binadamu, ni miongoni mwa vitisho vikubwa kwa maisha ya twiga katika maeneo mengi wanamoishi,” alieleza Muneza.
Hadi sasa, vifaa vya ufuatiliaji vya GCF vimetumika katika nchi 17 za Afrika kulingana na mahitaji ya uhifadhi. “Kwa mfano, vinaweza kutumika kufuatilia mienendo ya kuvuka mipaka, athari za uzio au barabara, na ufuatiliaji baada ya kuhamisha wanyama,” alisema.
Jamii za wenyeji ni wadau muhimu kwa kuwa hushirikiana na twiga katika matumizi ya ardhi. Ushiriki wao katika kupanga na kutekeleza shughuli za uhifadhi, ikiwemo kubainisha maeneo ya kutia alama twiga na kusaidia ufuatiliaji baada ya zoezi hilo, ni muhimu kwa mafanikio ya juhudi hizo.
“Hili lina umuhimu mkubwa nchini Kenya, ambako ongezeko la watu na maendeleo ya miundombinu vina athari kubwa kwa idadi ya twiga, hasa twiga wa Maasai,” Muneza aliiambia Mongabay kupitia barua pepe.
Kenya ina nafasi muhimu katika uhifadhi wa spishi mpya za twiga kwa sababu ni makazi ya spishi tatu kati ya hizo nne, zikiwa ni twiga wa Maasai, twiga wa wavu na twiga wa kaskazini.
Philip Muruthi, mwanachama wa Kikosi Kazi cha Njia za Uhamaji wa Wanyamapori nchini Kenya na Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Uhifadhi wa Twiga, anasema Siku ya Twiga Duniani ni fursa muhimu ya kutafakari changamoto kuu zinazowakabili twiga.
“Miongoni mwa masuala yanayohitaji tafakari ya kina zaidi siku hii ni namna upotevu wa makazi unavyoendelea kuwa tishio la moja kwa moja kwa uhai wa twiga,” alisema Muruthi.
Mbali na upotevu wa makazi, twiga pia wanakabiliwa na changamoto za kugawanyika kwa makazi kutokana na ujenzi wa barabara na uzio, uwindaji haramu, upanuzi wa makazi ya watu na ukame wa muda mrefu unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi. Shinikizo hizi hupunguza uhuru wa kutembea, upatikanaji wa chakula na maji, na huwatenga makundi ambayo tayari yako hatarini.
Muruthi anasema ongezeko la watu, linalochochewa na ushindani wa ardhi na rasilimali chache, limesababisha uvamizi mkubwa wa makazi ya wanyamapori na kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.

Hata hivyo, utafiti wa hivi karibuni utafiti wa hivi karibuni ulibaini kuwa kuna kiwango kikubwa cha uvumilivu kwa twiga katika baadhi ya maeneo ya Kenya wanamoishi.
“Wengi wa waliohojiwa waliwaona twiga kama wanyama wenye hatari ndogo, na zaidi ya nusu yao waliripoti kutopata uharibifu wowote wa ardhi au mali,” alisema Abdullahi Ali, mwandishi mkuu wa utafiti huo. “Muhimu zaidi, wasiwasi uliotolewa ulijihusisha zaidi na ushindani wa maji, uvamizi wa makazi na changamoto pana za maisha kuliko twiga wenyewe.”
“Bila shaka, mabadiliko ya tabianchi yanazidisha hali hii yote, jambo linalohitaji juhudi za makusudi zaidi za uhifadhi,” Muruthi aliiambia Mongabay kwa njia ya simu.
Katika zoezi la hivi karibuni la GCF la kufuatilia twiga katika Eneo la Uhifadhi la Tsavo, timu ya watafiti ilimkagua tembo wa savana wa Afrika aliyekuwa amejeruhiwa baada ya kugongwa na gari.
“Tukio kama hili linaonyesha umuhimu wa zoezi la kutia alama twiga na haja ya kuelewa zaidi mienendo ya twiga wa Maasai katika mandhari hii,” GCF ilisema katika hitimisho lake.
Shirika hilo liliongeza kuwa taarifa za mtandaoni za ufuatiliaji wa twiga wote 20 wa Maasai zitashirikiwa na washirika wote kupitia EarthRanger, huku uchambuzi na ripoti za maendeleo zikitarajiwa kutolewa mara mbili kwa mwaka.
Siku ya Twiga Duniani huadhimishwa kila tarehe 21 Juni, siku ambayo huwa ndiyo ndefu zaidi ya mwaka katika nusu ya dunia ya Kaskazini. Maadhimisho ya siku hiyo yalianzishwa na GCF mwaka 2014 ili kuongeza uelewa kuhusu changamoto za uhifadhi wa twiga barani Afrika.
Picha ya bango: Twiga waonekana wakivuka barabara katika hifadhi moja nchini Kenya. Picha kwa hisani ya GCF.