- Mbinu mpya za uchakachuaji wa mwani kuwa kichocheo cha kibiolojia cha mimea (biostimulant) zinawapa wakulima wa Kwale soko la uhakika kwa kununua mwani mbichi kila siku moja kwa moja kutoka mashambani.
- Wakulima wa mwani, hasa wanawake wa Kibuyuni, wanasema soko hilo jipya limewaongezea kipato, kupunguza gharama na kazi ya kukausha mwani, na kuboresha maisha ya familia zao.
- Wataalamu wanasema mwani una manufaa ya kiuchumi na kimazingira, ikiwemo kunyonya kaboni, kupunguza uchafuzi wa maji na kutumika kutengeneza bidhaa rafiki kwa mazingira kama mbolea za kibiolojia.
- Majaribio ya biostimulant inayotokana na mwani nchini Kenya yameonyesha kuongeza mavuno ya mazao kwa zaidi ya asilimia 10 hadi 15 na kusaidia mimea kustahimili ukame na joto kali.
KWALE, Kenya – Kila siku asubuhi maji yanapopungua katika ufuo wa bahari wa Kibuyuni, Kaunti ya Kwale kusini mwa pwani ya Kenya, Salim Ahmed na wakulima wenzake wa mwani huelekea baharini kuangalia mashamba yao.
Ahmed amefanya ukulima wa mwani kwa miaka mitatu sasa. Ukosefu wa ajira na uhaba wa fursa za kiuchumi vilimsukuma kutafuta njia mbadala ya kujikimu kimaisha. Kilimo cha mwani kikawa jibu lake, akaamua kujiunga na wanakijiji wenzake wanaofanya ukulima huo.
Mwani ni kundi la viumbe wa majini wanaofanana na mimea inayokua katika maji ya chumvi, hasa maeneo ya pwani yenye kina kifupi. Hupandwa kwa kufungwa kwenye vitiji na kamba baharini. Mwani huchukua kati ya siku 45 na 60 kufikia kiwango cha kuvunwa.
Mwani hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile vipodozi, sabuni, dawa, virutubisho vya lishe, vinywaji na malighafi za viwandani.
Kwa wakulima wengi wa mwani katika eneo la Kwale, baada ya kuvuna wao huukausha kisha kuuuza kupitia chama cha ushirika cha mwani katika eneo la Kibuyuni.
Ukulima wa mwani ulishirikisha wanawake wengi katika eneo la Kibuyuni ili wapate fursa ya kupata manufaa ya bahari ambayo imekuwa tegemeo la upatikanaji wa riziki kwa familia nyingi eneo la Pwani. Hii ni kutokana na kuwepo kwa mila na tamaduni zilizomwekea vikwazo mwanamke kuingia baharini kuvua samaki.

Lakini ukulima huo sasa umeanza kuvutia hata wanaume kama Ahmed, kutokana na faida ambazo wameziona kwa wanawake, wakiwa na matumaini ya kupata kipato cha kujiendeleza kimaisha.
Lakini licha ya wakulima wa mwani kuongezeka kwa kasi, wanakabiliwa na changamoto ya kupata soko la kila siku la wanunuzi. Mara nyingi hubaki na mazao yaliyohifadhiwa majumbani wakisubiri wanunuzi.
Kutokana na pengo hilo la kibiashara, mashirika mbalimbali yamekuja na mbinu ambazo zitasaidia wakulima wa mwani kupata soko kila siku.
Kulingana na Dkt Fiona Wanjiku, mwanzilishi mwenza wa shirika la Mawimbi Ocean Innovations, ambaye pia ni mtafiti wa kisayansi, mwani ni zao linalounganisha bahari na kilimo, wanawake na ajira, pamoja na sayansi na maendeleo ya jamii. “Nilipokuwa nafanya utafiti wangu wa masomo (PhD) nchini Ireland kuhusu bioteknolojia ya baharini, nilikuwa najiuliza kila mara kwa nini Kenya haijafaidika kikamilifu na mwani ilhali uwezo upo,” Wanjiku aliiambia Mongabay.
“Wakulima wengi wamekuwa wakivuna mwani na kuukausha, lakini hakuna wanunuzi wa uhakika. Wengine hadi leo bado wana magunia ya mwani wa mwaka jana yakiwa yamehifadhiwa bila soko,” aliongezea Wanjiku.
Kulingana naye, suluhisho sio kuwafundisha watu kulima mwani pekee, bali kujenga masoko yatakayohakikisha mkulima anauza mazao yake kila siku.
Kupitia shirika lao, wameanza kuchakachua mwani kuwa kichocheo cha kibiolojia cha mimea (biostimulant), aina ya mbolea ya kisasa inayosaidia mazao kukua vizuri, kustahimili ukame na magonjwa, huku ikiongeza afya ya udongo na kulinda mazingira.
Kiwanda hicho kilichoko eneo la Shimoni, Kaunti ya Kwale, kinanunua mwani mbichi moja kwa moja kutoka kwa wakulima kila siku.
Tofauti na mfumo wa zamani uliowalazimu wakulima kukausha mwani huku wakisubiri wanunuzi kwa miezi mingi, mfumo huu mpya unahakikisha kipato cha mara kwa mara kwa wakulima wa mwani.
Kwa wakulima wengi, hii imeondoa mzigo wa kuanika mwani kwa muda mrefu huku wakihofia mvua, uharibifu au kukosa wanunuzi.
“Kile tunachotengeneza si mbolea ya kawaida; ni bidhaa inayosaidia mimea kuwa imara zaidi dhidi ya changamoto za tabianchi na wadudu. Tunataka wakulima wajue kwamba ukulima wa mwani unaweza kuwa biashara ya kuaminika. Tunataka waweze kuamka kila siku wakijua kuna soko,” alisema Wanjiku.
Ahmed ni mmoja wa wakulima ambao sasa wanauza mwani katika kiwanda hicho. Alisema sasa ana uhakika wa kuuza mwani wake kila siku huku pia akipunguziwa kazi ya kuanika ili ukauke kisha autafutie soko.
“Nyakati za nyuma tulikuwa tunalima lakini hatukuwa na mnunuzi wa uhakika. Sasa tumepata morali zaidi ya kufanya kazi kwa sababu tunajua kuna soko,” alisema Ahmed.
Tima Bakari, ambaye amekuwa mkulima wa mwani kwa miaka minne, anasema kazi hiyo imebadili maisha yake na ya familia. “Ukulima wa mwani umenisaidia kusomesha watoto na kupata chakula nyumbani kila siku. Zaidi, imenisaidia kujenga nyumba yangu iliyokuwa ya udongo kwa kutumia mawe,” alisema.
Tima pia alikuwa akiuza mwani wake katika ushirika wa chama cha mwani Kibuyuni. Alisema alikuwa akiuza kilo moja ya mwani mkavu (uliokaushwa) kwa KSh50. Sasa amepata soko jipya na ana matumaini kuwa mapato yake yataongezeka maradufu, huku akiwa na muda zaidi wa kulima na kuvuna. Pia atakuwa akiuza mwani wake moja kwa moja bila kupoteza muda wa kukausha.
“Tayari nimeuza mwani wangu mbichi mara mbili kwa kiwanda hiki na naona faida. Pia imenipunguzia muda kwa sababu sasa sina haja ya kuanika mwani ninapoutoa baharini. Na kwa upande wa soko, sasa sina wasiwasi kwani ninapotoa mwani baharini, naupeleka sokoni moja kwa moja na napata pesa zangu,” alisema Tuma.
Shamu Swaleh, mmoja wa wanawake wanaofanya kazi katika kiwanda hicho, alisema alikuwa mfanyibiashara mdogo wa chakula lakini akaacha kazi hiyo na kujiunga na kazi ya kuchakachua mwani. Alisema kazi hiyo imempa fursa ya kujua umuhimu wa mwani baharini na kwenye nchi kavu. “Tangu nianze kufanya kazi hii ya mwani sasa naweza kulisha familia yangu kila siku. Sio lazima nisubiri mwanamume alete pesa nyumbani. Pia nasomesha watoto wangu,” alisema Shamu.
Meneja wa Uratibu wa Ukusanyaji wa Mazao na Mahusiano ya Jamii wa Mawimbi Ocean Innovations Mohamed Fuad alisema utafiti waliofanya katika jamii nyingi za wakulima wa mwani katika eneo hilo ulionyesha kuwa wakulima wengi wamehifadhi mwani mkavu majumbani wakisubiri wanunuzi.
“Tulikuta tani nyingi za mwani mkavu zimehifadhiwa kwenye nyumba za wakulima kwa sababu ya ukosefu wa soko,” alieleza Fuad. “Sisi huwa tunanunua mwani mbichi halafu tunakamua tupate yale maji yake ndio tutengeneze mbolea. Zaidi, kiwanda chetu kiko Shimoni, karibu na mkulima wa mwani,” aliongeza Fuad.

Kwa mujibu wa Fuad, gunia la kilo 50 la mwani mbichi hununuliwa kwa KSh600 kutoka kwa wakulima mbalimbali katika vijiji vya Kibuyu, Kijiweni na Bati. Kiwanda hicho kina jumla ya wafanyikazi watano, wawili wakiwa wanawake.
Bernard Fulanda, mtaalamu wa masuala ya sayansi ya baharini na mabadiliko ya tabianchi kutoka Chuo Kikuu cha Pwani kilichopo katika Kaunti ya Kilifi, Pwani ya Kenya, alisema mbali na mwani kuunda fursa za kazi na kuwawezesha wanawake kiuchumi. Pia husaidia bahari kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Prof Fulanda alisema mwani una uwezo wa kunyonya virutubisho vingi, kama vile nitrojeni na fosforasi kutoka kwa maji, na kusaidia kupunguza uchafuzi wa maji.
Zaidi alisema bidhaa zinazotengenezwa kutokana na mwani, ikiwemo mbolea, ni rafiki kwa mazingira na wakulima wanaweza kutumia badala ya mbolea za kemikali, kwani hazina sumu na haziharibu mazingira.
Kulingana na Profesa Fulanda, tafiti pia zimeonyesha kuwa mwani unaweza kuchukua kati ya megatoni 61 na 268 za kaboni kwa mwaka, na wastani wa megatoni 173.
Kulingana na ripoti ya Frontiers ya kilimo cha mwani, mwani husaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Mwani una jukumu kubwa katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kunyonya uzalishaji wa kaboni, kuzalisha upya mazingira ya baharini, kuunda nishati ya mimea na plastiki inayoweza kutumika tena, pamoja na kuzalisha protini ya baharini.
Hata hivyo, licha ya faida zake, kilimo cha mwani hakikosi changamoto zake. Mwani pia hukumbana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha mwani kuchujuka na kupoteza rangi na ubora wake.
China ndio mzalishaji mkubwa zaidi wa mwani ulimwenguni, ikizalisha asilimia 57%. Hata hivyo, uzalishaji wa mwani umeongezeka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, huku ikizalisha zaidi ya $59 bilioni kufikia mwaka wa 2019.
Ripoti ya hivi karibuni ya Benki ya Dunia imeonyesha masoko 10 ya mwani duniani yenye uwezekano wa kukua kwa $11.8 bilioni zaidi ifikapo mwaka wa 2030 kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Nchini Kenya, ili kuimarisha ukulima wa mwani kwa kutumia mbinu endelevu, serikali, kwa ushirikiano na mashirika mengine, ikiwemo Taasisi ya Kenya ya Utafiti wa Viumbe vya Baharini (KMFRI), wameanzisha mradi wa matumizi ya kamba ziitwazo biopolymer.

Kamba hizi zinaoza na zimeundwa kupunguza uchafuzi wa bahari kwa kupunguza matumizi ya kamba za plastiki. Kamba hizo huoza katika kipindi cha miaka miwili bila kuacha taka zozote zile za sumu kwenye bahari. Tayari wanawake katika kijiji cha Kibuyuni wameanza kuzitumia.
Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani alisema wataimarisha uzalishaji wa mwani katika eneo hilo kwa kuwapa wakulima wa mwani mafunzo ya kuwajengea uwezo na kuwapa nyenzo za upanzi ili waweze kuongeza mapato yao.
Wanjiku aliiambia Mongabay kuwa wao pia huwapa wanawake mafunzo ya kusimamia uzalishaji kiwandani, kuhakikisha ubora wa bidhaa na kuelewa taratibu za usindikaji.
Kwa sasa, spishi ya mwani wanayotumia sana ni ile ya Spinosum (Eucheuma denticulatum) ambayo inapandwa sana eneo la Kibuyuni. Pia wanatarajia kuanzisha upanzi wa spishi ya Cottonii (Kappaphycus alvarezii) katika eneo hilo.
Utafiti wa kilimo unaonyesha kuwa biostimulant inayotokana na mwani inaweza kufanya kazi sawa na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, lakini kwa gharama nafuu zaidi na rafiki kwa mazingira.
Mbolea (biostimulant) hiyo imeonyesha mafanikio makubwa kwa wakulima katika maeneo mbalimbali ya nchi. Kulingana na Nelson Wafula, mtafiti wa bidhaa za shamba, ikiwemo mbolea, hiyo biostimulant ilijaribiwa katika mashamba ya maua, maharagwe na broccoli miongoni mwa mboga nyengine.
Katika mashamba ya maua, mbolea hiyo iliongeza mavuno kwa zaidi ya asilimia 15.
Katika majaribio yaliyofanyika katika baadhi ya mashamba katika kaunti za Kirinyaga, Murang’a, Trans Nzoia na Makueni, mbolea hiyo ilionyesha uwezo mkubwa wa kusaidia mimea kustahimili mazingira magumu kama ukame na joto kali, huku wakulima wakiongeza zaidi ya asilimia 10 katika mavuno ya mboga zao.
Faida nyingine kubwa iliyobainika ni ukuaji bora wa mizizi. Mimea iliyotumia mbolea hiyo ilikuwa na mizizi mirefu zaidi, jambo lililosaidia kufyonza maji na virutubisho kwa ufanisi mkubwa.
“Japo bidhaa hii iko katika hatua ya majaribio, tayari tumeona manufaa yake na itafaidisha wakulima wengi. Teknolojia hii ni ya kipekee kwa sababu inatengenezwa hapa Kenya kwa kutumia rasilimali za bahari ya Kenya, tofauti na mbolea nyingi zinazotoka nje ya nchi,” alisema Wafula.
Wanjiku alisema kwa sasa bidhaa hiyo bado ipo katika hatua za mwanzo za uzalishaji, lakini tayari kuna ishara za uwepo wa soko kutoka kwa wakulima nchini Kenya na mataifa mengine kama vile Brazil na Namibia.
Alisisitiza kuwa ndoto yao kubwa si kuuza nje pekee, bali kujenga soko la ndani ambalo litawanufaisha wakulima wa Kenya kwanza. “Tunataka wakulima humu nchini wawe wa kwanza kufaidika na rasilimali za bahari yetu,” alisema.
Picha ya bango: Wakulima wa Mwani wakivuna mwani eneo la Shindambe, Lamu , Kenya. Picha na Karel de la Cruz Victoria.