- Ufugaji wa viumbe vya majini waweka rekodi mpya: Mwaka 2024, uzalishaji wa viumbe vya majini kupitia ufugaji ulifikia tani milioni 103 kwa mara ya kwanza, ukichangia asilimia 53 ya uzalishaji wote wa wanyama wa majini duniani.
- Biashara ya mazao ya majini yafikia dola bilioni 186: Biashara ya dunia ya bidhaa za majini na mwani ilifikia dola bilioni 186 mwaka 2024, ikihusisha maeneo 230 ya kiuchumi na kuonyesha umuhimu wa sekta hiyo katika uchumi wa dunia.
- Zaidi ya watu milioni 600 wanategemea sekta hiyo: Uvuvi na ufugaji wa viumbe vya majini uliajiri zaidi ya watu milioni 65 na kusaidia maisha ya zaidi ya watu milioni 600 duniani kupitia ajira, kipato na lishe.
- FAO yaonya kuhusu changamoto za uendelevu: Licha ya mafanikio ya uzalishaji, mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira, uvuvi haramu na uharibifu wa mifumo ikolojia vinaendelea kutishia mustakabali wa sekta hiyo muhimu.
Kufikia mwaka 2024, biashara ya bidhaa za majini duniani ilifika $186 bilioni. Kati ya hizo, $184 bilioni zilihusishwa na biashara ya bidhaa za majini pekee, ilhali $2 bilioni zilihusishwa na biashara ya mwani na mazao mengine. Biashara hiyo ilihusisha maeneo ya kiuchumi 230 kote ulimwenguni.
Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa [FAO] ambayo pia imeeleza kuwa sekta hiyo inayohusiana na uvuvi na ufugaji wa samaki na viumbe wengine wa majini iliajiri wafanyakazi zaidi ya milioni 65, na hivyo kuwa tegemeo la maisha ya watu zaidi ya milioni 600 kote duniani.
FAO ilizindua ripoti hiyo mpya ya Hali ya Uvuvi na Ufugaji wa Viumbe vya Majini Duniani (SOFIA 2026) kwenye mkutano wa 11 wa Bahari Yetu [11th Our Ocean Conference] uliofanyika jijini Mombasa, nchini Kenya.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa uzalishaji wa uvuvi na ufugaji wa viumbe vya majini duniani ulifikia rekodi ya tani milioni 235 kwa mwaka 2024. Pia uzalishaji wa wanyama wa majini ulifikia tani milioni 195 na umeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 3.2 kwa mwaka tangu miaka ya 1950.
Pia ripoti ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa imeonyesha kuwa uvuvi wa asili umeendelea kuwa thabiti kwa kiasi kikubwa tangu mwishoni mwa miaka ya 1980, hali inayochangiwa na juhudi za usimamizi wa uvuvi na uhifadhi wa mazingira katika baadhi ya maeneo.
Aidha, ilibainika kuwa ufugaji wa viumbe vya majini ulizalisha tani milioni 103 za wanyama wa majini, rekodi ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa. Hii ni sawa na asilimia 53 ya uzalishaji wote wa viumbe vya majini duniani, na zaidi ya asilimia 59 ya chakula cha wanyama wa majini kinachotumiwa na binadamu.

Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa uzalishaji huo wa tani milioni 103 za viumbe vya majini unaofugwa ulikuwa na thamani ya takribani $371 bilioni katika kiwango cha shambani, jambo linaloonyesha mchango mkubwa wa sekta hiyo katika uchumi wa dunia. Kwa mara ya kwanza katika historia, uzalishaji wa viumbe vya majini unaotokana na ufugaji ulivuka kiwango cha tani milioni 100, hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa umuhimu wa ufugaji wa viumbe vya majini katika kukidhi mahitaji ya chakula duniani.
Katika taarifa ya utangulizi ya ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu alisema kuwa ripoti hiyo inakuja wakati muafaka, ikiwa imebaki chini ya miaka mitano kufanikisha Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu.
Dongyu alisema: “Inatoa maarifa thabiti, yanayotokana na ushahidi na yenye mwelekeo uliozingatia sayansi na ujuzi wa hali ya juu ili kusaidia njia halisi na hatua za kufikia uvuvi na ufugaji endelevu wa viumbe vya majini.”
Mkurugenzi huyo alisema ripoti hiyo inawasilisha takwimu zilizohuishwa na kuthibitishwa kuhusu ufugaji wa viumbe vya majini na uvuvi duniani, na inaonyesha jinsi FAO, wanachama wake, jamii za wenyeji, taasisi za kitaifa, sekta husika na washirika wanavyoshirikiana kuendeleza sekta hiyo.
Je, vyakula vya majini vinahitajika kiasi gani duniani?
Shirika la FAO linakadiria kuwa asilimia 89 ya uzalishaji wa viumbe vya majini duniani imelengwa kwa matumizi ya binadamu. Ripoti imeeleza kuwa upatikanaji wa viumbe vya majini kama chakula kwa kila mtu duniani ulifikia kilo 21.1 mnamo mwaka 2023, na inakadiriwa kuwa uliongezeka zaidi hadi kufikia kilo 21.3 mnamo 2024.
Samaki na vyakula vingine vya majini vinatambulika sana kwa thamani yao ya lishe, vikitoa protini ya kiwango cha juu pamoja na vitamini muhimu, madini, na asidi za mafuta.
“Kadri idadi ya watu inavyoendelea kuongezeka na shinikizo kwenye mifumo ya chakula ya nchi kavu linavyozidi, vyakula vya majini vinakuwa sehemu muhimu zaidi ya mikakati ya usalama wa chakula duniani,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo ambayo hutolewa kila baada ya miaka miwili.
Ripoti inaonyesha kuwa uvuvi na ufugaji wa viumbe vya majini unasalia kuwa chanzo muhimu cha ajira, kipato, na lishe, hasa katika nchi za kipato cha chini na cha kati ambapo vyakula vya majini mara nyingi hutoa chanzo kinachopatikana kwa urahisi zaidi cha protini ya wanyama.
Ufugaji ulivyoongezeka kwa kasi duniani
Takwimu za ripoti hiyo zinaonyesha mabadiliko yaliyokuwa yakijitokeza kwa miongo kadhaa iliyopita.
Wakati uvuvi wa asili ukitajwa kuwa thabiti kwa kiasi kikubwa tangu mwishoni mwa miaka ya 1980, ufugaji wa viumbe vya majini umeibuka kama kichocheo kikuu cha ukuaji katika uzalishaji wa chakula cha majini.
Mwaka 2024, uvuvi wa asili ulizalisha takriban tani milioni 92 za bidhaa za chakula kutoka majini, wakati uvuvi uliotokana na ufugaji ulichangia tani milioni 103.
Sasa ripoti hiyo pia inaeleza kuwa ukijumuisha uzalishaji wa mwani, uzalishaji wa mazao ya majini ulifikia takriban tani milioni 142 wenye thamani inayokadiriwa kufikia $391 bilioni.

Dongyu alisema jumuiya ya kimataifa bado inaeleza wasiwasi kuhusu vitisho vya athari ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira, na uharibifu wa mifumo ikolojia katika mifumo ya maji ya bahari na maji yanayopatikana kwenye maeneo ya nchi kavu.
“Ripoti inatuonesha kwamba sayari yenye afya inahitaji bahari na mifumo salama ya maji ya bara,” alisema.
Katika mapendekezo, Dongyu alisema kuna haja ya kuhakikisha kuwa juhudi zote stahiki zinachukuliwa ili kuzuia kuporomoka kwa uendelevu na kulinda uwezo wa sekta hiyo kwa muda mrefu, kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kwa sasa ufugaji hutoa zaidi ya asilimia 59 ya vyakula vyote vya majini vinavyoliwa duniani kote ambapo maendeleo yake yamechangiwa na maboresho ya teknolojia ya uzalishaji, chakula bora cha samaki, udhibiti mzuri wa magonjwa, mifumo imara ya utawala na uwekezaji unaoongezeka katika mbinu endelevu za uzalishaji.
Bara la Asia linatajwa kuchangia karibu asilimia 89 ya uzalishaji wa ufugaji duniani, huku Uchina ikiendelea kuwa mzalishaji mkubwa zaidi duniani.

India, Indonesia, Vietnam, na Bangladesh pia zinaendelea kuchukua nafasi kubwa katika kuchochea uzalishaji huo.
Kwa wataalamu wengi, kuongezeka kwa ufugaji kunaonyesha mahitaji ya dunia kwa vyakula vya majini hayawezi tena kutimizwa kwa kuvuna samaki kutoka kwenye vyanzo asilia vya maji pekee.
Ni sekta ya mabilioni ya dola duniani
Sekta ya uvuvi na ufugaji wa viumbe vya majini (mazao ya majini) imekuwa mojawapo ya sekta za chakula zenye thamani kubwa zaidi duniani, ikizalisha zaidi ya $186 bilioni mwaka 2024.
Ripoti inaeleza kuwa zaidi ya theluthi moja ya uzalishaji wa wanyama wa majini inauzwa kimataifa, ikiongozwa na minyororo ya ugavi inayozidi kuwa ya kisasa inayounganisha wazalishaji na watumiaji katika mabara yote.
Hata hivyo, ukuaji wa kibiashara unatajwa kuchangiwa na viwango vya juu vya uzalishaji, mtandao ulioboreshwa wa usafiri, maendeleo katika teknolojia za usindikaji na ufikiaji ulio rahisi wa masoko.
Kwa nchi nyingi zinazoendelea, mauzo ya nje ya uvuvi yanaendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato ya kigeni na ukuaji wa uchumi.
Rasilimali isiyopatikana kwa usawa
Licha ya ongezeko la uzalishaji duniani, upatikanaji wa vyakula vya majini unatofautiana kati ya maeneo mbalimbali kwani barani Asia, wastani wake ni kilo 26.3 kwa mtu kwa mwaka wakati barani Afrika, upatikanaji ni kilo 9.1 pekee kwa mtu ikiwa ni chini ya nusu ya wastani wa dunia.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa vyakula vya majini huchangia takriban asilimia 19 ya protini yote ya wanyama inayotumiwa kote barani humo, na hivyo kuvifanya kuwa sehemu muhimu ya usalama wa chakula na lishe.
Shirika la FAO linaonya kuwa kuongeza uzalishaji pekee hakutaboresha usalama wa chakula moja kwa moja bali panahitajika uwekezaji katika miundombinu, vyumba vya baridi, usafiri, usindikaji na masoko ili kupunguza athari kwa jamii zilizo hatarini.
Je, tutegemee uvuvi wa asili?
FAO inaeleza kuwa uvuvi wa samaki wa mwituni bado ni muhimu kwa mifumo ya chakula duniani licha ya ukuaji wa haraka wa ufugaji wa samaki.
Mnamo 2024, uvuvi wa baharini ulizalisha takriban tani milioni 80 za wanyama wa majini, wakati uvuvi wa nchi kavu ulifikia rekodi ya tani milioni 12.3, na kufanya jumla ya samaki wa mwituni kufikia takriban tani milioni 92.
Hata hivyo, wasiwasi kuhusu uendelevu unaendelea ambapo shirika la FAO linasema kuwa mwaka 2023 ni asilimia 62.4 tu ya samaki wa baharini waliofanyiwa tathmini ya kuvunwa ndani ya viwango endelevu vya kibaiolojia.
Aidha, ripoti hiyo pia ilibainisha kuwa asilimia 72.6 ya samaki wote waliovuliwa baharini mwaka 2023 walitoka katika hifadhi za samaki zilizokuwa ndani ya viwango endelevu vya kibaiolojia, ishara kwamba hatua za usimamizi wa uvuvi zimechangia ongezeko la mavuno kutoka kwa hifadhi zinazovuliwa kwa njia endelevu.

Takwimu za uvuvi zilionyesha hali ya kutia moyo mwaka 2024 ambapo uvuvi wa jodari duniani ulifikia rekodi ya tani milioni 9.3, huku mavuno ya samaki aina ya anchoveta yakiongezeka zaidi ya mara mbili, hali iliyochangiwa na ustahimilivu wa mifumo ikolojia ya majini na ufanisi wa usimamizi wa uvuvi.
Ripoti hiyo ilieleza kuwa makundi mengine ya aina nyingine za samaki yaliathiriwa kwa kiasi kikubwa na uvuvi haramu, uharibifu wa sehemu ya mazalia pamoja na mabadiliko ya hali ya mazingira.
Mabadiliko ya tabia nchi yatajwa kuleta changamoto kubwa ya muda mrefu katika uvuvi na ufugaji wa samaki.
Pia kupanda kwa halijoto, uharibifu wa mazingira, misukosuko ya kiuchumi na mivutano ya kisiasa ya kimataifa vinatatiza mifumo ikolojia ya majini.
Ili kukabiliana na changamoto hizi, FAO inapendekeza mbinu kadhaa za kusaidia kulinda mazao yatokayo majini (Blue Transformation) ambazo ni ufugaji wa samaki unaozingatia hali ya hewa, usimamizi endelevu wa uvuvi, matumizi ya sayansi, minyororo thabiti ya thamani, na kupambana na uvuvi haramu.
Mpango wa Blue Transformation wa FAO unalenga kuboresha uendelevu, uzalishaji na ushirikishwaji katika sekta ya uvuvi na ufugaji wa viumbe vya majini.
Kama hayo yatazingatiwa, shirika hilo linaamini kuwa ifikapo mwaka 2034 kiwango cha uzalishaji wa wanyama wa majini kitafikia tani milioni 214.
Picha ya bango: Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya FAO ya Hali ya Uvuvi na Ufugaji wa Viumbe wa Majini Duniani (SOFIA), uzalishaji wa viumbe wa majini kupitia ufugaji wa samaki na viumbe wengine wa majini (aquaculture) ulivuka tani milioni 100 kwa mara ya kwanza mwaka 2024. Picha kwa hisani ya FAO.