- Kutokana na mahitaji makubwa katika biashara ya wanyama wa kufugwa majumbani (pet trade) pamoja na uharibifu wa makazi yake ya asili, mijusi aina ya gecko wamepungua kwa kiwango kikubwa, hali iliyowaweka katika hatari ya kutoweka nchini Tanzania.
- Vizuizi vya kimataifa vya biashara na hatua za ulinzi wa spishi hiyo vimesaidia mijusi hao kuanza kuongezeka tena baada ya miaka mingi ya uvunaji kupita kiasi.
- Juhudi za wanasayansi pamoja na uhifadhi unaoongozwa na jamii, ikiwemo kuondoa miti vamizi na kupanda upya miti ya asili, zimewapa mijusi hao na wanyamapori wengine fursa ya kuongezeka tena katika msitu wa hifadhi wa Kimboza.
Uzuri ni laana – angalau kwa mjusi mdogo wa rangi ya samawati (turquoise dwarf gecko) anayepatikana katikati mwa Tanzania. Kati ya Desemba 2004 na Julai 2009, mahitaji ya mjusi huyu kutoka kwa wakusanyaji wa wanyama barani Ulaya yaliongezeka sana, jambo lililosababisha kukamatwa na kusafirishwa nje ya Tanzania kwa takriban mijusi 40,000 ya aina hii iliyokuwa na mwonekano wa kuvutia.
“Nakumbuka nilipowaona kwa mara ya kwanza katika maonyesho ya wanyama, bei yao ilikuwa dola za Marekani 700 kwa kila mmoja ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi za Tanzania milioni 1.8,” alisema Dennis Rödder, mtaalamu wa wanyama watambaao kutoka Leibniz Institute for the Analysis of Biodiversity Change nchini Ujerumani, katika mahojiano na Mongabay yaliyofanyika kwa njia ya video. “Nadhani ndani ya miaka mitatu au minne, spishi hii ilikuwa imeenea kote Ulaya. Ilikuwa ni rahisi kuinunua kutoka duka lolote la wanyama wa kufugwa.”
Mijusi hawa wanaojulikana kisayansi kama (Lygodactylus williamsi) hukua hadi kufikia urefu wa sentimita 6–9 (takriban inchi 2.5–3.5). Wanapatikana tu katika maeneo mawili madogo ya misitu nchini Tanzania: Hifadhi ya Misitu ya Kimboza na Hifadhi ya Ruvu. Maeneo haya yaliyohifadhiwa yana ukubwa wa jumla ya kilomita za mraba 34 (takriban maili za mraba 13).
Majike waliokomaa wana rangi ya kijani-kahawia inayofanana na majani ya miti wanayoishi, jambo linalowasaidia kujificha dhidi ya maadui. Hata hivyo, madume huwa na ngozi ya samawati ang’avu inayovutia sana. Rangi hii ni miongoni mwa rangi adimu zaidi kupatikana kiasili, na hutumika kuwavutia majike wakati wa uzazi.

Mjusi wa aina hii ambaye hufanya kazi zake wakati wa mchana, ana uwezo mkubwa wa kulinda eneo lake. Huwafukuza watoto wake mara tu wanapoanguliwa kutoka kwenye mayai ili waondoke kwenye miti wanamoishi na kwenda mbali kujitafutia riziki. Mjusi huyu ambaye hapendi kuchanganyikana huishi kwenye miti yenye majani marefu na miiba mikali (maarufu kama screwpines), miti hii hupatikana nchini Kenya na Tanzania. Miti hii hukua hadi kufikia urefu wa mita 3 hadi 20 (takriban futi 66) na huwa na majani marefu yenye miiba pamoja na umbo linalofanana na chemchemi ya maji. Muundo huu huifanya kuwa makazi bora kwa mijusi hawa, kwani huwapa mahali pa kujificha na kuzaliana, sehemu ya kujipatia joto la jua, na eneo la kupata chakula ambapo maji na wadudu hukusanyika.
“Haya ndiyo mazingira wanayoyapendelea,” alisema Charles Kilawe, mtaalamu wa ikolojia ya misitu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, katika mahojiano na Mongabay yaliyofanyika kwa njia ya video. “Majani ya miti wanayopendelea yana miiba, na hiyo huwakinga mijusi hawa dhidi ya wanyama wanaowawinda kama nyoka au tai.”
Hata hivyo, utegemezi wa mijusi hawa kwa mti kama kinga dhidi ya maadui wa asili umewaweka katika hatari zaidi kutoka kwa adui mwingine: binadamu. Wawindaji haramu hutumia mapanga kukata miti mikubwa ili kuwakamata mijusi waliomo hasa wale wasioweza kujitetea. Ukataji huu wa miti kwa ajili ya kuwakamata mijusi ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba kufikia mwaka 2009, miti ya screwpine ilipungua kutoka kufunika zaidi ya nusu ya eneo la Hifadhi ya Msitu wa Kimboza hadi kufikia asilimia 17.6 tu ya eneo lote la hifadhi hiyo.
Mwaka huo, watafiti walikadiria kuwa mijusi hawa wanaovutia waliosalia porini walikuwa takriban 150,000 pekee. “Nilipoanza kufanya kazi huko mwaka 2016, ilikuwa vigumu sana kuwaona,” alisema Kilawe.
Mwaka 2009, mtaalamu wa wanyama watambaao, Morris Flecks na wenzake kutoka Taasisi ya Leibniz walihoji kundi moja la wakusanyaji wa mijusi kutoka jamii zinazozunguka Hifadhi ya Msitu wa Kimboza. Walikadiria kuwa kundi hilo lilikuwa limekamata kati ya mijusi 32,000 na 42,000 aina ya turquoise dwarf gecko kutoka hifadhi hiyo katika kipindi cha miaka mitano iliyotangulia. Watafiti hao walibainisha kuwa idadi hiyo, ambayo waliamini ilikuwa angalau asilimia 15 ya idadi yote ya mijusi hao waliokuwa porini wakati huo, huenda ilikuwa kubwa zaidi kwa sababu haikujumuisha mijusi waliokusanywa na makundi mengine mengi yaliyokuwa yakifanya shughuli hizo ndani ya msitu.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, ukamataji au usafirishaji wa mijusi hao, au spishi nyingine yoyote ya wanyamapori kutoka katika hifadhi ya msitu iliyolindwa, ulihitaji kibali rasmi. Hata hivyo, maafisa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) waliwaeleza watafiti kuwa hakuna vibali vya aina hiyo vilivyowahi kutolewa.
Ukusanyaji huu mkubwa wa mijusi kwa ajili ya biashara ya wanyama wa kufugwa majumbani (pet trade), pamoja na uharibifu wa haraka wa makazi yao ambayo tayari ni machache, ulisababisha kupungua kwa kasi kwa idadi yao. Kutokana na hali hiyo, Rödder, Flecks na wataalamu wengine wa wanyama watambaao walipendekeza spishi hiyo itambuliwe na Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) kama spishi iliyo katika hatari kubwa ya kutoweka.
Hatimaye, mwaka 2012, spishi hiyo iliwekwa katika kundi hilo. Miaka mitano baadaye, biashara ya kimataifa ya mijusi hao ilipigwa marufuku rasmi baada ya spishi hiyo kuingizwa katika Kiambatisho cha Kwanza cha mkataba wa kimataifa unaosimamia biashara ya wanyamapori, maarufu kama Mkataba wa CITES.
Kufikia wakati huo, ukamataji mkubwa wa mijusi hao katika maeneo ya chini ya Milima ya Uluguru ulikuwa umepungua kwa kiasi kikubwa. Hii ilitokana na ukweli kwamba masoko ya nje ya nchi hayakuwa na mahitaji makubwa tena. Ingawa mijusi hao waliendelea kupendwa na wafugaji wa wanyama wa kipekee, wale waliokuwa wakizalishwa kwenye vituo vya ufugaji huko bara la Ulaya walikuwa tayari wamefikia idadi ya kutosheleza mahitaji yao ya wakati huo. Hali hiyo ilisababisha bei ya mijusi hao kushuka kutoka dola 1,500 za Marekani kwa mnyama mmoja hadi takribani dola 40 pekee.
“Idadi ya mijusi hawa imerudi na kuwa kama ilivyokuwa kabla ya kuanza kwa ukamataji mkubwa. Hilo ni jambo jema,” alisema Rödder katika mahojiano na Mongabay.
“Jambo lisilo zuri sana ni kwamba miaka michache baada ya utafiti wetu, kulitokea moto mkubwa wa msituni katika mojawapo ya hifadhi hizi.”

Kupotea kwa makazi kutokana na ukataji miti haramu, ukusanyaji wa kuni, ubadilishaji wa misitu kuwa mashamba ya kilimo, shughuli za uchimbaji madini, pamoja na kuenea kwa mti vamizi wa Spanish cedar (Cedrela odorata) ndani na nje ya hifadhi mbili za misitu ambako mjusi aina ya Lygodactylus williamsi hupatikana, kunaendelea kuongeza shinikizo kwa spishi hiyo.
Mti wa Spanish cedar uliletwa katika Msitu wa Kimboza mwaka 1960, kwa lengo la kupunguza shinikizo la ukataji wa miti ya asili. Wazo lilikuwa kwamba mti huo wenye asili ya Amerika, unaokua kwa haraka, ungeweza kutoa chanzo cha uhakika cha mbao bora na kuni.
Hata hivyo kinyume na matarajio, mti huo wa kigeni, ambao unaweza kufikia urefu wa mita 40, uligeuka kuwa spishi vamizi. Kwa kuwa huzalisha mbegu mara mbili kwa mwaka ambazo husambazwa na upepo na kuota kwa urahisi katika maeneo yanayobaki wazi baada ya ukataji haramu wa miti na uchomaji wa misitu, umechukua nafasi ya miti ya screwpine katika maeneo mengi.
“Mnamo mwaka 2016, mti wa Cedrela ulikuwa miongoni mwa miti iliyotawala zaidi katika msitu huo, ikichukua karibu asilimia 32 ya eneo lenye miti mikubwa,” Kilawe aliiambia Mongabay.
Mwaka 2022, Kilawe alichapisha utafiti kuhusu Kimboza uliolenga kubaini kama mijusi aina ya turquoise dwarf gecko waliathiriwa moja kwa moja na uwepo wa miti ya Spanish cedar. Aligundua kuwa miti ya screwpine bado ilikuwa ikistawi katika maeneo yenye unyevunyevu na kwenye miamba ya chokaa.
Tofauti na utafiti uliofanyika miaka 40 iliyopita ambao ulibaini uwepo wa miti aina ya pandanus rabaiensis katika zaidi ya nusu ya maeneo yaliyofanyiwa uchunguzi, katika utafiti wa Kilawe miti hiyo ilionekana ikiwa ni chini ya nusu ya maeneo yaliyokaguliwa, hali inayoonyesha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa makazi ya mijusi hao. Kwa upande mwingine, uwepo wa miti ya Spanish cedar uliongezeka kwa kasi. Mwaka 1982, miti hiyo ilionekana katika asilimia 16 ya maeneo yaliyofanyiwa uchunguzi, wakati katika utafiti wa Kilawe ilionekana katika asilimia 52 ya maeneo hayo.
Ingawa Kilawe alibaini kuwa mijusi aina ya turquoise dwarf gecko bado walipatikana kwa kiwango sawa kwenye miti ya screwpine iliyokuwa chini ya miti mirefu ya cedar, matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa idadi ya mijusi ilikuwa ndogo zaidi katika maeneo yaliyofunikwa na kivuli kizito cha miti hiyo ya kigeni ikilinganishwa na maeneo yenye miti michache ya cedar au yasiyokuwa nayo kabisa.
Bado kuna haja ya kufanya tafiti zaidi ili kuelewa kwa undani athari za moja kwa moja za miti ya Spanish cedar kwa mijusi hao. Hata hivyo, kuendelea kuenea kwa miti hiyo katika maeneo ya msitu yaliyoachwa wazi na moto au baada ya miti kuanguka, kunazua hofu kwamba itaendelea kuchukua nafasi ya makazi ya asili ya mijusi hao. Athari kama hizo kwa bioanuwai ya asili zimeripotiwa pia katika maeneo mengine ambako mti huo umepandwa, ikiwemo Ghana na Visiwa vya Galápagos.

Leo, wakazi wa vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Msitu wa Kimboza wanashirikiana na askari wa uhifadhi katika kusimamia na kulinda msitu huo, amesema Kilawe. Chini ya uongozi wake, jamii hizo zimekata karibu miti 100,000 ya Spanish cedar tangu mwaka 2016 na kufanikisha kupunguza matukio ya moto wa misituni kwa takribani asilimia 80.
Pia, tangu mwaka 2018 wamekuwa wakipanda takribani miti 5,000 ya asili kila mwaka, wakifanya kazi hatua kwa hatua kurejesha muundo wa awali wa msitu wa Kimboza. Kilawe aliiambia Mongabay kuwa “mabalozi” 10 kutoka vijiji mbalimbali hulipwa kwa kazi hiyo, huku kuongoza watalii kukiwa chanzo kingine cha mapato kinachotokana na juhudi za kulinda mfumo huo wa ikolojia.
“Tuna matumaini kwamba ikiwa zoezi la kuondoa miti hiyo litaendelea, huenda ndani ya miaka mitano ijayo msitu ukawa hauna tena miti ya Cedrela,” alisema Kilawe. “Kushirikiana na jamii katika shughuli za uhifadhi, ni muhimu sana na kunaleta matokeo makubwa.”
Baada ya kuwa katika hatari kubwa ya kutoweka kutokana na biashara ya wanyama na uharibifu wa makazi yake, mjusi aina ya turquoise dwarf gecko sasa anaendelea kuimarika kutokana na juhudi hizi za upandaji na urejeshaji wa misitu pamoja na kupigwa marufuku kwa biashara yake duniani kote. Kilawe alisema kuwa urejeshaji wa misitu ya Kimboza pia umewezesha kurejea kwa wanyamapori wengine, wakiwemo nyani wa buluu (Cercopithecus mitis) na ndege aina ya alethe mwenye kifua cheupe (Chamaetylas fuelleborni). Hali hii inaonyesha kuwa ushirikiano na juhudi za pamoja zinaweza kuokoa spishi na mifumo muhimu ya ikolojia dhidi ya hatari ya kutoweka.
Picha ya bango: Mjusi aina ya Turquoise dwarf gecko. Picha: © Ardgard Essau kupitia iNaturalist (CC BY-NC 4.0).
Nukuu:
Flecks, M., Weinsheimer, F., Böhme, W., Chenga, J., Lötters, S., & Rödder, D. (2012). Watching extinction happen: The dramatic population decline of the critically endangered Tanzanian Turquoise Dwarf Gecko, Lygodactylus williamsi. Salamandra, 48(1), 12-20. Retrieved from https://www.salamandra-journal.com/index.php/contents/2012-vol-48/270-flecks-m-f-weinsheimer-w-boehme-j-chenga-s-loetters-d-roedder
Kilawe, C. J., Mchelu, H. A., & Emily, C. J. (2022). The impact of the invasive tree Cedrela odorota on the Electric Blue Gecko (Lygodactylus williamsi) and its habitat (Pandanus rabaiensis) in Kimboza Forest Reserve, Tanzania. Global Ecology and Conservation, 38, e02225. doi:10.1016/j.gecco.2022.e02225
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 06/06/2026
