- Kenya imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika na ya pili duniani kunufaika na ufadhili wa Hasara na Uharibifu wa tabianchi, unaolenga kusaidia waliopata athari za majanga ya hali ya hewa.
- Fedha kiasi cha KSh90 milioni (dola 700,000) kutoka Santiago Network zitaelekezwa kwa jamii zilizoathiriwa na ukame, mafuriko na uharibifu wa mazao.
- Kenya itatumia fedha hizo kufanya tathmini ya kitaifa ya hasara na uharibifu wa tabianchi katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
- Wadau wamesema hatua hiyo ni mafanikio makubwa yanayoonyesha uongozi wa Kenya katika ajenda ya tabianchi Afrika.
Kenya imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika na ya pili duniani kunufaika na ufadhili huo wa kukabiliana na majanga ya tabianchi, msaada unaolenga kusaidia waliopata hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Fedha hizo, kiasi cha KSh90 milioni ($700,000) kutoka Santiago Network on Loss and Damage, mfumo wa Umoja wa Mataifa wenye makao yake nchini Uswisi unaofadhiliwa kupitia michango ya hiari kutoka kwa nchi zilizoendelea na jumuiya ya kimataifa, zitatolewa kupitia serikali na kusambazwa kwa jamii mbalimbali nchini zinazokabiliwa na majanga mbalimbali yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi.
Majanga hayo ni pamoja na ukame wa mara kwa mara, mafuriko, kupungua kwa uzalishaji wa mazao, uharibifu wa mazao na matukio mengine ya hali mbaya ya hewa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu wa Kenya, Festus Ng’eno, alisema msaada huo ni hatua muhimu sana. Ng’eno alisema hatua hiyo inaifanya Kenya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika na ya pili duniani kunufaika na mfuko huo. Vanuatu, taifa la funguvisiwa lenye maeneo mengi ya mwinuko wa chini, ndiyo iliyokuwa nchi ya kwanza duniani kupata ufadhili huo.
Ng’eno alitoa taarifa hiyo katika mazungumzo yaliyofanyika sambamba na mazungumzo ya kiufundi ya tabianchi ya UNFCCC Subsidiary Bodies (SB64) yanayoendelea huko Bonn, Ujerumani.
Katika taarifa aliyochapisha mtandaoni, akithibitisha habari iliyochapishwa na gazeti la People Daily mnamo Juni 10, Dkt Ng’eno alisema kuwa licha ya Kenya kupitia baadhi ya majanga makubwa zaidi ya tabianchi katika Afrika Mashariki, nchi hiyo haijawahi kupima kikamilifu kiwango halisi cha hasara iliyopata kutokana na majanga hayo. “Hali hiyo sasa itabadilika,” alisema.
Kwa mujibu wa chapisho la shirika la utangazaji la serikali ya Kenya KBC, fedha hizo zitatumika kusaidia Kenya kufanya tathmini ya kina ya kitaifa kuhusu hasara na uharibifu uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.
Fred Njehu, mtaalamu wa mikakati ya kisiasa wa Greenpeace Afrika, aliliambia gazeti la Daily Nation kwamba hatua ya kuifanya Kenya kuwa miongoni mwa nchi za kwanza kuongoza katika tathmini na uwekaji kumbukumbu wa hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi, ni maendeleo chanya katika juhudi za kukabiliana na changamoto hiyo.
“Imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu kwa nchi zilizo mstari wa mbele katika changamoto za tabianchi kupata msaada wa kujenga ustahimilivu. Mgao wa Kenya unaashiria mabadiliko ya hatua za tabianchi kutoka kwenye mifumo, ramani za utekelezaji na mijadala kwenda kwenye utekelezaji halisi,” alisema.
Maendeleo haya yamekuja wakati nchi za Afrika zikiendelea kudai haki ya tabianchi na fidia zaidi kutoka kwa mataifa yanayotajwa kuwa na mchango mkubwa katika ongezeko la joto duniani.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kenya Climate Change Working Group, Jeremiah Kioli, haya ni mafanikio makubwa kwa Kenya, nchi ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kutetea hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia malengo kabambe ya kupunguza athari zake.
Aliiambia Mongabay kwamba kutambuliwa kwa Kenya kama kinara katika juhudi za kushughulikia hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi, ni uthibitisho wa dhamira ya nchi hiyo katika hatua inazochukua kukabiliana na athari pamoja na uhamasishaji katika kutafuta rasilimali zinazohitajika. “Hii ni hatua kubwa mbele,’’ alisema.
Akifafanua namna fedha hizo zinavyoweza kutumika, Kioli, ambaye pia ni Kamishna katika Tume inayoshughulikia masuala ya mito ya Nairobi, aliiambia Mongabay: “Matumizi ya fedha hizi yatajikita zaidi katika kujiweka tayari na kuweka mifumo. Zitasaidia kufanya tathmini na kubaini hasara na uharibifu unaostahili kufidiwa. Unapimaje hasara na uharibifu? Unahitaji mifumo madhubuti, kama ilivyo kwa Mfuko wa Kijani wa Tabianchi (Green Climate Fund)”.
Katika miaka ya karibuni, Kenya imekuwa ikiongoza juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku Rais William Ruto mara kwa mara akitaka kuwepo kwa mifumo bora ya kifedha ili kuharakisha ukuaji wa uchumi wa Afrika.
Katika miaka ya karibuni, nchi hiyo imekumbwa na majanga makubwa ya hali ya hewa yaliyosababisha vifo na uharibifu mkubwa, hali iliyoongeza umuhimu wa upatikanaji wa fedha za Hasara na Uharibifu (Loss and Damage), wakati juhudi za kupunguza na kuhimili athari za tabianchi zikiendelea.
“Ufanisi huu unaonyesha uongozi bora wa Kenya katika hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na dhamira yake ya kujenga ustahimilivu dhidi ya athari zinazoongezeka za mabadiliko hayo,” ilisema Wizara ya Mazingira.
Picha ya bango: Mafundi wanajaribu kuokoa sehemu za gari lililosombwa kutoka kwenye karakana ya wazi wakati wa mafuriko ya Machi 2026, yaliyosababisha vifo vya angalau watu 110 na kuwafanya watu 34,700 kuhama makazi yao katika maeneo mbalimbali nchini Kenya. Picha na Maxwell Agwanda.