- Upande wa mashitaka umedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
- Hakuna maelezo yaliyotolewa kwa nini mtuhumiwa hakuletwa mahakamani.
- Mshtakiwa anaendelea kusota rumande hadi Juni 23, kesi itakapotajwa tena.
Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili raia mmoja wa Korea Kaskazini, Un Hyok Ra (37), anayeshitakiwa kwa kukutwa akimiliki nyara za Serikali ambazo ni vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya TSh6.4 bilioni, imepigwa tarehe tena kwa madai kuwa upelelezi wake haujakamilika.
Shauri hilo limetajwa leo Juni 9, 2026 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Salome Mwasha.
Akiwakilisha upande wa Mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Florida Wenceslaus aliomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo kwa kile alichoeleza kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Mshtakiwa, ambaye anaendelea kusota rumande, hakuwepo mahakamani leo kama ilivyokuwa wakati kesi hiyo ilipotajwa Mei 25, na pia hakuwa na mwakilishi.
Hakimu Mwasha alikubali ombi la upande wa mashitaka na akaahirisha shauri hilo hadi Juni 23 mwaka huu, kesi itakapotajwa tena.
Mshtakiwa Ra alipanda kizimbani kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa Mei mwaka huu. Shauri lilipotajwa baada ya siku 14, yaani Mei 25 mwaka huu, mshtakiwa huyo hakufikishwa mahakamani na badala yake shauri liliahirishwa bila yeye kuwepo.
Kabla ya kuahirisha kesi hiyo, hakimu aliamuru hati ya kumfikisha mshtakiwa kortini itolewe ili kesi itakapotajwa Juni 9, 2026, mshtakiwa aletwe kortini. Hata hivyo leo mshtakiwa hakufikishwa kortini na hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa kwa nini mshatakiwa hakuwepo.
Awali upande wa Jamhuri ulidai katika hati ya mashtaka kuwa mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili, kukutwa akimiliki nyara za Serikali na kujihusisha na biashara hiyo bila kibali.
Ilidaiwa kuwa Aprili 19, 2026 katika eneo la Hoteli ya Golden Tulip–Masaki, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa akimiliki nyara za Serikali ambazo ni vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya
TSh6,476,534,750, mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali au leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika shtaka la pili, Ra ambaye ni Mkazi wa Mikocheni Dar es Salaam, anatuhumiwa kuwa tarehe hiyo na mahali hapo alijihusisha na biashara ya nyara za Serikali kwa kuuza vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya TSh6,476,534,750 mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali au leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Nchini Tanzania, kumiliki meno ya tembo bila kibali ni kosa la uhujumu uchumi. kisheria, meno ya tembo yanachukuliwa kuwa ni mali ya Serikali na umiliki wake unadhibitiwa na sheria.
Hivyo, kisheria, kumiliki, kununua, kuuza au kusafirisha nyara hizo bila kibali ni kosa linaloweza kusababisha adhabu ya kifungo cha muda mrefu na/au faini kubwa, pamoja na makosa mengine ya jinai chini ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori (Wildlife Conservation Act, No. 5 of 2009).
Picha ya bango: Nchini Tanzania, kumiliki meno ya tembo bila kibali ni kosa la uhujumu uchumi. Meno ya tembo yanachukuliwa kuwa ni mali ya Serikali na umiliki wake unadhibitiwa na sheria. Picha kutoka mitandaoni.