- Mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuwa tishio kwa ikolojia ya bahari ya Zanzibar na mafanikio ya uchumi wa buluu, licha ya juhudi za uhifadhi.
- Hemed Suleiman Abdulla amesema athari kama kupanda kwa kina cha bahari, kupauka kwa matumbawe na dhoruba kali zinahatarisha utalii na uvuvi.
- Wataalamu wanasisitiza uwekezaji katika uchumi wa kaboni ya buluu kupitia mikoko na nyasi bahari ili kusaidia uhifadhi na kunufaika na masoko ya kaboni.
- Serikali inahimiza miundombinu himilivu, mifumo ya tahadhari ya mapema na ushirikishwaji wa vijana katika ubunifu wa uchumi wa buluu, licha ya changamoto za uvuvi haramu.
Licha ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhifadhi ikolojia ya bahari kupitia usimamizi endelevu wa rasilimali zake, mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuwa tishio kubwa kwa mazingira hayo na ustawi wa jamii zinazoyategemea.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zinahatarisha mafanikio ya uchumi wa buluu kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari, kupauka kwa miamba ya matumbawe, dhoruba kali pamoja na kupungua kwa samaki baharini.

Aliyasema hayo katika Warsha ya 29 ya Mwaka ya Utafiti iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umasikini [REPOA], iliyowaweka pamoja serikali za Tanzania bara na Zanzibar pamoja na wadau wa bahari kujadili namna ya kuimarisha ikolojia hiyo.
Abdulla alisema Zanzibar imekuwa kivutio kikubwa cha utalii duniani kutokana na utajiri wa ikolojia yake ya bahari, utamaduni wa watu wake na mazingira ya amani na utulivu lakini ongezeko la joto duniani linaendelea kuathiri mifumo ya bahari inayochangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Zanzibar kupitia utalii, uvuvi na shughuli nyingine za kiuchumi zinazotegemea bahari.
Nini kifanyike
Makamu wa Pili wa Rais alishauri kujengwa kwa miundombinu himilivu na mifumo madhubuti ya tahadhari ya mapema ili kulinda ikolojia ya bahari na maisha ya wananchi.
Alishauri kuwepo ushirikiano kati ya taasisi za mafunzo ya uvuvi na bahari pamoja na vyuo vikuu katika kuendeleza uchumi wa buluu kwa muda mrefu, sambamba na kuingiza elimu ya bahari katika mitaala ya shule.
“Nawasihi kwamba uchumi wa buluu ni zaidi ya sekta ya kiuchumi. Ni safari ya pamoja ya taifa inayohitaji uwajibikaji, ubunifu, tafiti imara na ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuhakikisha mafanikio yake,” alisema.
Ushirikishwaji wa vijana
Makamu wa Pili wa Rais pia alisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha vijana katika shughuli za uhifadhi wa ikolojia ya bahari kupitia miradi inayowawezesha kiuchumi kwani wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko kupitia ubunifu na teknolojia katika sekta ya uchumi wa buluu, ikiwemo utalii wa bahari, bidhaa zinazotokana na viumbe baharini, huduma za kidijitali za baharini na ujasiriamali wa teknolojia za bahari.
“Jambo hili linaonesha kuwa uchumi wa buluu hauishii kwenye uvuvi na usafirishaji wa baharini pekee, bali pia ni eneo la ubunifu, teknolojia na ujasiriamali,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejizatiti kuwekeza katika mafunzo ya ujasiriamali wa baharini kwa vijana, ikiwemo kilimo cha mwani, matumizi ya ndege zisizo na rubani (drone), ufugaji wa kisasa wa viumbe maji pamoja na uundaji wa mifumo ya kisasa ya bahari.

Prof Yunus Daud Mgaya, Mtaalamu wa Biolojia ya Bahari katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliiambia Mongabay kuwa ili kuhifadhi ikolojia ya bahari serikali inatakiwa kuwekea mkazo uchumi wa kaboni ya buluu (blue carbon) kwa kuwa una nafasi kubwa kusaidia uhifadhi wa mazingira ya bahari kupitia utunzaji wa mikoko na nyasi bahari ambazo zina uwezo mkubwa wa kufyonza kaboni.
Aidha, alisema uwekezaji katika mifumo hiyo unaweza kusaidia Tanzania kunufaika na masoko ya kimataifa ya kaboni huku ukichangia uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo ya bahari.
“Ili nchi iweze kunufaika kikamilifu na fursa hizo, kuna haja ya kuimarisha mifumo ya upimaji wa kaboni, kuhakikisha uwazi katika mgawanyo wa faida pamoja na kujenga ushirikiano wa kuaminika unaounga mkono uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya wananchi,” alisema Prof Mgaya.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Captain Hamad Bakar Hamad, alisema juhudi zinazoendelea za uhifadhi wa bahari zimeongeza uzalishaji wa samaki na mwani, sekta zinazowanufaisha zaidi ya watu 100,000. Hata hivyo, alisema Zanzibar bado inakabiliwa na changamoto za uvuvi haramu na uharibifu wa mazingira.
Picha ya Bango: Kulinda ikolojia ya Zanzibar ni hatua muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kujenga uchumi wa buluu wenye tija. Picha kutoka mtandaoni.