- Ushoroba umepungua kutoka kilomita za mraba 600 hadi 274.
- Uhamaji wa wanyama unaepusha hatari ya wanyama wenye nasaba moja kuzaliana.
- Ongezeko la shughuli za kibinadamu, makazi na mifugo huzidi kuubana ushoroba.
- Ili ushoroba ubaki hai, lazima wanajamii waone faida ya uhifadhi.
Ushoroba wa Kwakuchinja, ambao katika toleo la kwanza la mfululizo wa makala kuhusu manufaa ya ushoroba nchini Tanzania, ulielezwa kuleta manufaa makubwa kwa uhifadhi na pia kwa jamii zinazozunguka hifadhi ya Burunge, uko hatarini kutokana na kuendelea kupungua siku hadi siku.
Ushoroba huo uko Kaskazini mwa Tanzania, kati ya Hifadhi za Taifa za Tarangire na Ziwa Manyara, na unaokatiza maeneo ya Babati, Monduli na Simanjiro, umeendelea kuwa kiunganishi muhimu cha mifumo ya ikolojia katika ukanda huo wenye utajiri mkubwa wa viumbe hai. Kwa miongo kadhaa umekuwa njia muhimu ya kupita kwa wanyamapori wanaohama kutoka eneo moja kwenda lingine.

Revocatus Meney, mtafiti kutoka TAWIRI, anasema ushoroba huo umekuwa ukipungua siku hadi siku kutokana na ongezeko la shughuli za kibinadamu. Makazi, kilimo na mifugo vinaendelea kuubana mwaka hadi mwaka na kuufanya uwe finyu.
Kwa mujibu wa tafiti za TAWIRI, miaka ya 1970, ushoroba wa Kwakuchinja ulikuwa na ukubwa unaofikia kilomita za mraba 600.
Hata hivyo, Meney anasema kutokana na ongezeko la shughuli za kibinadamu ikiwemo makazi, kilimo na matumizi mengine ya ardhi, eneo hilo limeendelea kupungua na kufikia takribani kilomita za mraba 274.45 kwa sasa.
Kupungua huku kunamaanisha kuwa zaidi ya nusu ya eneo la awali la ushoroba limepotea ndani ya kipindi cha takribani miongo mitano.
Meney anasema hakuna kiwango kimoja cha upana kinachotumika kwa ushoroba kwa sababu hutegemea aina ya wanyama wanaoutumia na mazingira husika.
Hata hivyo, anasema kadri ushoroba unavyokuwa mpana na usio na vikwazo vya shughuli za kibinadamu ndivyo unavyokuwa na uwezo mkubwa wa kuruhusu uhamaji salama wa wanyamapori. “Kwa tembo na wanyama wengine wakubwa wanaohama kwa makundi, ushoroba mwembamba sana huongeza hatari ya migogoro na binadamu na kupunguza matumizi yake kwa wanyama,” anasema Meney.
Athari za kupungua kwa ushoroba
Miongoni mwa athari za kupungua kwa ushoroba huo ni kukwamisha uhamaji wa tembo, pundamilia, nyumbu na wanyama wengine wanaotegemea njia hiyo kusafiri kati ya mifumo ya hifadhi.

Kwa mujibu wa tathmini ya “Kwakuchinja Wildlife Corridor Ecological Viability Assessment” ya mwaka 2019, ongezeko la mifugo ndani ya eneo la ushoroba limeendelea kuwa tishio kubwa kwa uendelevu wa mfumo huo wa ikolojia.
Akizungumzia tishio hilo, Zacharia Laizer, Mkurugenzi Mtendaji wa Asilia Giving, taasisi inayojishughulisha na uhifadhi kupitia miradi inayoelimisha juu ya umuhimu wa wanyamapori na binadamu kuishi pamoja, anasema ongezeko kubwa la mifugo ndani ya ushoroba husababisha ushindani wa rasilimali kati ya mifugo na wanyamapori, hasa maji na malisho.
“Mifugo inapokuwa mingi kwa wakati mmoja kwenye maeneo ambayo wanyamapori wanategemea kwa ajili ya mapito na kupata chakula, baadhi ya wanyama huanza kubadilisha njia zao za asili au kuchelewesha uhamaji wao,” anasema Laizer.
Anaongeza kuwa uwepo wa watu wengi wanaoambatana na mifugo huongeza usumbufu katika maeneo ambayo yanapaswa kuwa salama kwa wanyamapori kupita. Anasema hali hiyo inapunguza ubora wa ushoroba na kuathiri kazi yake ya msingi ya kuunganisha mifumo ya ikolojia ya Tarangire na Manyara.
Aidha Meney anasema kuwa kupungua kwa ushoroba huo kutahatarisha mfumo wa kuzaliana kwa wanyama hasa wale wanaohitaji kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine.
“Ushoroba unapozibwa, wanyama wanapoteza uhuru wa kutembea. Hii inaathiri hata uwezo wao wa kuzaliana na kuendelea kuwepo kwa muda mrefu. Wanyamapori wanahitaji maeneo makubwa na mapito ya uhakika. Sasa ushoroba unapopungua, wanyama wanakosa njia za kupita na matokeo yake, migogoro kati yao na binadamu huongezeka,” anasema Meney.
Meney anasema athari nyingine ya kupungua kwa eneo hilo ni kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, hasa tembo ambao wana kumbukumbu sana ya njia wanazotumia.
Kwa upande wa wadau wengine wa uhifadhi, kupungua kwa ushoroba kunaweza kuathiri hata uchumi wa utalii unaotegemea uwepo wa wanyamapori.
Sheria na utekelezaji
Juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau wengine kulinda ushoroba wa Kwakuchinja, zinakumbana na upinzani mkali kutokana na mgongano wa maslahi baina ya wananchi na wahifadhi.

Wahifadhi matakwa yao ni ushoroba kuachwa huru ili wanyamapori waendelee kuutumia katika hali ya uhuru na usalama.
Ruth Philemon, Afisa Mhifadhi Daraja la Kwanza wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), anasema uhamaji wa wanyama ni muhimu kwenye masuala ya kuzaliana na kwamba wakikaa sehemu moja kuna hatari ya wanyama wenye nasaba moja kuzaliana.
“Wanyama kwa asili yao, hawawezi kukaa sehemu moja, wanahitaji kuhama kutoka eneo moja kwenda lingine, na uwepo wa ushoroba unawapa uhuru wa kupita,” anasema Ruth.
Anasema Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009 pamoja na kanuni zake, imetambua umuhimu wa maeneo haya na kutoa mamlaka kwa serikali kuyasimamia. Hata hivyo anasema utekelezaji wake unakuwa mgumu kutokana na changamoto ya ongezeko la watu na mahitaji ya ardhi.
Akizungumzia namna ambayo maslahi tofauti yanavyoathiri ushoroba, Christopher Laizer, Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Babati, anasema, tofauti na wahifadhi, watu wanahitaji maeneo ya malisho, makazi na kilimo.
“Maeneo yaliyopo hayatoshelezi kutokana na kuongezeka kwa watu pamoja na shughuli. Mambo hayo yanaongeza msukumo wa kuendelea kumega eneo la ushoroba,” anasema Christopher.
Licha ya ugumu huo, Anna Mbogo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, anasema mamlaka za serikali za mitaa zinaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kupunguza migogoro inayochochewa na changamoto kubwa ya mahitaji ya ardhi.
Nini kifanyike?
Zacharia anasema ili kuokoa ushoroba ni lazima kubuni mikakati itakayonufaisha pande zote, yaani wanyamapori na binadamu. “Tukitaka ushoroba ubaki hai, jamii lazima ione faida ya uhifadhi. Lakini pia ni lazima kuwe na uwazi kwenye mifumo ya hifadhi,” anasema Zacharia.
Kuanzishwa kwa maeneo mapya ya usimamizi wa wanyamapori, utoaji wa elimu, ufugaji wenye tija (mifugo michache), na kuimarisha mipango ya matumizi bora ya ardhi, ni mambo mengine yanayopendekezwa ili kunusuru ushoroba huo.
Ruth anasema Serikali kwa kushirikiana na taasisi husika inaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa wanyamapori na mazingira yao ambayo ni pamoja na ushoroba hiyo, jinsi tunaweza kuzitunza.
“Pia tunafanya doria kuzuia uharibifu wa mazingira katika maeneo hayo,” anasema Ruth.
“Kwa sasa bado tunaona tembo, nyumbu na wanyamapori wengine wakitumia ushoroba huu. Hiyo inaonyesha kuwa bado una uhai na umuhimu wake wa kiikolojia haujapotea. Lakini ukweli ni kwamba shinikizo la shughuli za kibinadamu linaendelea kuongezeka kila mwaka. Tusipochukua hatua sasa, tunaweza kufika mahali ambapo wanyama watakosa kabisa njia hii muhimu ya kupita,” anasema Ruth.
Anaongeza: “Changamoto tuliyonayo sasa si kwamba ushoroba umepotea, bali ni jinsi ya kuuzuia usiendelee kupungua. Hilo ndilo jukumu kubwa la serikali, wadau wa uhifadhi na jamii zinazouzunguka”.
Picha ya bango: Miongoni mwa matukio ambayo ni nadra kutokea katika ushoroba wa Kwakuchinja ni kuonekana kwa wanyama wote wakubwa; simba akiwa juu ya mti na tembo akiwa chini ya mti huohuo.(Picha na Isack Dickson)