- Jumuiya ya kimataifa imeweka malengo kabambe ya kulinda asili, lengo la hivi punde zaidi ni kulinda asilimia 30 ya sayari ifikapo 2030. Walinzi wa wanyamapori ndio kitovu cha juhudi hii. Kulingana na Shirikisho la Walinzi wa Kimataifa, wana jukumu muhimu katika kulinda maeneo yaliyohifadhiwa na kufikia malengo ya uhifadhi wa kimataifa.
- Lakini katika maeneo mengi yaliyohifadhiwa, walinzi wanazidi kukabiliwa na vurugu, mara nyingi hukabiliana na makundi yenye silahakwa usaidizi mdogo, hasa katika maeneo yasiyo na utulivu kama vile mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
- Kwa Emmanuel Bahati Lukoo, ukweli huu si wa kufikirika bali ni wa kibinafsi sana. Mnamo mwaka wa 2018, alinusurika shambulio la karibu kutoka kwa wapiganaji wa Mai-Mai(kundi lililojihami linalofanya kazi katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo). Tofauti na walinzi wengi ambao wamepoteza maisha wakilinda asili mashariki mwa DRC, alinusurika. Zaidi ya walinzi 100 wanaaminika kuuawa katika Hifadhi ya Kitaifa ya Virunga katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
- Akitafuta kuangazia hali halisi na mazingira ya kazi ya walinzi nchini DRC, hivi majuzi Bahati alichapisha kitabu kiitwacho Conservation at the ‘Cost of My Youth: The Survival of a Ranger’, ambamo anasimulia maisha ya mlinzi wa mbuga mashariki mwa DRC.
Katika Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afrika ya kati, kulinda asili kunaweza kugharimu maisha yako. Kwa miaka mingi, walinzi wanaofanya kazi katika mbuga za wanyamapori kama Virunga na Kahuzi-Biega wamefanya kazi katikati ya makundi yenye silaha, usafirishaji haramu wa maliasili, mivutano ya kijamii na vurugu za kudumu ambazo tayari zimegharimu maisha ya mamia ya wenzao. Hata hivyo, licha ya jukumu lao kuu katika kulinda bayoanuwai na baadhi ya misitu muhimu zaidi ulimwenguni, wengi wanaendelea kufanya kazi wakiwa na usaidizi mdogo, mishahara midogo, na hali hatarishi sana.
Kwa Emmanuel Bahati Lukoo, ukweli huu ni wa kibinafsi sana. Aliwahi kuwa mlinzi katika mbuga ya kitaifa ya Virunga ambapo kwa sasa ni afisa katika Hifadhi ya Kitaifa ya Kahuzi-Biega, alinusurika kifo katika shambulizi la kushutukizia mnamo mwaka wa 2018 na kikundi cha wanamgambo wa jamii kinachojulikana kama Mai-Mai. Wenzake kadhaa waliuawa kwa kuviziwa. Alipigwa risasi, alijeruhiwa na kupata kiwewe cha kisaikolojia, na baadaye kufunguliwa mashitaka mbele ya mahakama ya kijeshi katika kesi iliyohusishwa na ulinzi wa hifadhi, angeweza kuondoka. Badala yake, Bahati alichagua kusimulia hadithi yake katika kitabu kiitwacho Conservation at the Cost of My Youth: The Survival of a Ranger, simulizi ghafi ya dhabihu, hofu, shinikizo za kisiasa, na mara nyingi hali halisi isiyoonekana inayowakabili walinzi wa misitu mashariki mwa DRC.
Kwenye mahojiano ya ana kwa ana na Mongabay, Bahati anatafakari safari yake, shambulizi lililokaribia kumuua, kiwewe walichopata walinzi, migogoro kati ya uhifadhi na maisha ya jamii ya eneo hilo, na uingiliaji wa kisiasa unaotatiza ulinzi wa maeneo yaliyohifadhiwa. Zaidi ya hadithi ya kibinafsi, hata hivyo, ushuhuda wake pia ni wito wa kuchukua hatua: hatimaye kutambua walinzi kama wahusika muhimu katika uhifadhi wa kimataifa, kabla ya kuwa mashujaa baada ya kufariki.
Bahati aliiambia Mongabay kuwa shinikizo la kisiasa linabaki kuwa mojawapo ya changamoto kuu zinazokabili uhifadhi nchini DRC, ambapo wakati mwingine walinzi huvamiwa, kupigwa, kuzuiliwa au kupelekwa mahakamani katika kesi zinazohusishwa na maeneo yaliyohifadhiwa.

Mongabay: Ni kitu gani kilichokusukuma kuandika kitabu hiki?
Emmanuel Bahati Lukoo: Motisha yangu hutokana na mambo kadhaa. Mapema sana, niligundua kuwa walinzi wa mbuga za uhifadhi hawakuwa wakisimulia hadithi zao wenyewe. Mara nyingi ni waandishi wa habari, watafiti, au wanahistoria wanaoandika kutuhusu, ingawa hawaishi maisha tunayoishi.
Mimi ni mlinzi wa mbuga za wanyamapori. Najua maana ya usiku wa kukosa usingizi, vitisho, kutengwa na familia, shida za kila siku. Nilijisemea kuwa ni sharti niandike jambo hata kidogo ili dunia ielewe mazingira wanayofanya walinzi wa mbugani, hasa katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Pia nilitaka kuipa changamoto serikali ya Kongo. Tunafanya kazi kubwa kulinda ubinadamu na bado hakuna utambuzi wa kweli. Mara nyingi, Walinzi huchukuliwa kuwa mashujaa tu wanapofariki. Sipendi wazo hili kwamba mtu huwa shujaa baada ya kifo. Walinzi wanatakiwa kutambuliwa wakiwa bado wako hai.
Mongabay: Hukuogopa kuandika kitabu hiki na kuwanyooshea vidole wanasiasa fulani?
Emmanuel Bahati Lukoo: Nilichagua taaluma hii nikijua hatari iliyopo. Nilipoona changamoto na ugumu wa maisha unaohusishwa na uhifadhi, nilijiambia kuwa ni sharti zikabiliwe.
Kuhusika kwa wanasiasa fulani katika uharibifu wa mbuga ni ukweli. Baadhi yao humiliki sehemu za maeneo yaliyohifadhiwa kinyume cha sheria. Na walinzi wa wanyamapori au maafisa wa uhifadhi wanapowapinga, wanakuwa walengwa.
Binafsi, nimekamatwa, kufunguliwa mashtaka, kushambuliwa na askari na wanasiasa kwa sababu nilikataa kushirikiana katika uharibifu wa mbuga. Nimeona wenzangu wengi wakifa. Nimehudhuria mazishi mengi ya walinzi. Wakati fulani, unahisi unapaswa kuzungumza.

Mongabay: Ni kipi kilikusukuma, katika umri mdogo, kujiunga na uwanja huu licha ya hatari na ukosefu wa usalama?
Emmanuel Bahati Lukoo: Nilijiunga na Taasisi ya Kongo ya Uhifadhi wa Mazingira (ICCN) nikiwa bado mwanafunzi. Nilikuwa nimesomea uhifadhi wa mazingira katika Taasisi ya Juu ya Utalii na Usimamizi.
Mwanzoni, niliwasiliana na mkurugenzi wa Hifadhi ya Kitaifa ya Virunga, Emmanuel de Merode. Nyakati fulani nilipeleka barua mbugani. Siku moja aliniuliza nilichokuwa nikijifunza, nami nikajibu “uhifadhi.” Alikuwa ni mtu aliyenitia moyo sana.
Nilivutiwa na jinsi alivyowatendea walinzi. Siku moja, yeye binafsi alimsafirisha mlinzi aliyejeruhiwa hadi hospitali kwa gari lake mwenyewe. Hilo lilinigusa sana moyoni.
Baadaye, kazi ya kuajiri walinzi ilipofunguliwa, nilituma ombi. Wakati huo nilikuwa kijana na mwanariadha; Nilicheza soka. Nilichaguliwa na kufunzwa huko Rumangabo (Rumangabo ni kituo cha kijeshi kilicho kaskazini mwa Goma huko Kivu).
Mongabay: Familia yako ilifanya nini ulipochukua mkondo huu?
Emmanuel Bahati Lukoo: Nilibahatika kuwa na wazazi ambao waliniruhusu kujichagulia njia yangu mwenyewe. Hawakuwahi kunilazimisha kazi.
Lakini baadaye, kwa sababu ya hatari za kazi hiyo, wanafamilia yangu wengi walianza kuwa na wasiwasi. Baada ya shambulio la kuvizia ambalo karibu timu yangu yote iliuawa, jamaa kadhaa walikuja kuniona hospitalini na kunitaka niache kazi hiyo.
Lakini kwangu, kutoendelea kungehisi kama kuacha kumbukumbu ya wenzangu walioangushwa. Kuendelea ilikuwa njia ya kuwaheshimu.

Mongabay: Tuzungumze kuhusu lile shambulizi la mwaka 2018. Ulilisimulia kwenye kitabu. Unaweza kutuambia kilichotokea?
Emmanuel Bahati Lukoo: Wakati huo, niliamuru kitengo maalum cha mbuga kilichopewa kazi ya kupambana na vikundi vyenye silaha. Dhamira yetu ilijumuisha kulinda baadhi ya maeneo ya hifadhi na kulinda ujenzi wa uzio wa umeme unaokusudiwa kupunguza migogoro kati ya tembo na jamii za wenyeji.
Mnamo Aprili 9, mwaka wa 2018, tulikuwa tumeenda kusimamia doria ya timu. Barabarani, katika eneo liitwalo Oro, tulivamiwa kwenye shambulio la kuvizia. Ilikuwa kwenye savanna, mahali ambako hakuna mtu angetarajia shambulio.
Milio ya risasi ikaanza mara moja. Dereva aliingiwa na hofu. Gari lilitumbukia kwenye shimo. Wenzetu kadhaa waliuawa papo hapo. Mimi mwenyewe nilijeruhiwa. Nilifanikiwa kujificha na kurudisha ufyetulianaji risasi.
Nilipigwa risasi kadhaa, silaha yangu ilikwama, lakini niliweza kuitengeneza kwenye makabiliano hayo ya risasi. Hatimaye nilifaulu kutorokea eneo salama zaidi kabla ya kuhamishwa hadi hospitalini.
Siku hiyo, tulipoteza watu sita: walinzi watano na dereva mmoja raia.
Mongabay: Baada ya shambulizo hilo, je ulipata msaada wa kutosha wa kisaikolojia?
Emmanuel Bahati Lukoo: Niliathiriwa na kiwewe cha kisaikolojia. Shukrani kwa Mkurugenzi de Merode, nilitunzwa na kupokea matibabu kutoka kwa mwanasaikolojia huko Goma kwa miezi mitatu. Baadaye niliacha shughuli za viwanjani na kupata nafasi ya usimamizi nilipokuwa nikiendelea kupata nafuu. Lakini ukweli ni kwamba hakuna msaada wa athari za kisaikolojia kwa walinzi wengi. Wengi wanateseka kimya kimya. Serikali ya Kongo inafaa kuanzisha mfumo wa msaada kwa wanaume na wanawake hawa wenye kuathiriwa na kiwewe kikuu.
Kuwa mlinzi wa mbuga ni kiwewe kikubwa sana. Wakati mwingine unakuwa mbali na familia yako kwa miezi mingi. Upo katika shinikizo za kila mara. Kunapaswa kuwa na utaratibu halisi wa msaada wa kisaikolojia kwa walinzi.

Mongabay: Umetaja mishahara pia. Je, hali ikoje leo?
Emmanuel Bahati Lukoo: Mshahara wa mlinzi wa mbuga ni mdogo sana. Tunaishi kutokana na marupurupu yanayolipwa na washirika wa kibinafsi au mashirika yasiyo ya kiserikali yaani NGOs. Kiasi hiki hakijaongezeka licha ya kupanda kwa bei na hatari zinazoongezeka.
Bado walinzi wanafanya kazi mchana na usiku, mbali na familia, katika maeneo ya vita. Watoto wetu wanapaswa kupata elimu bora ikiwa afisa atakufa akiwa kazini.
Kiukweli, walinzi hawana mshahara wa kweli. Kinachoturuhusu kuishi ni mafao ya marupurupu yanayotolewa na washirika wa kimataifa. Lakini pamoja na vita na kupanda kwa gharama za maisha, marupurupu hayo hayatoshi tena. Hata hivyo hatari huongezeka kila siku.
Mongabay: Tuambie kuhusu kesi ya Nzulo, unayoisimulia kwenye kitabu, iliyosababisha kuzuiwa kwao.
Emmanuel Bahati Lukoo: Nzulo iko eneo la magharibi mwa Goma. Wanasiasa na machifu wa kimila walinyakua ardhi ya mbuga huko. Nilipojaribu kutekeleza sheria, walinishutumu kwa uporaji na vurugu. Askari tisa walikuja kunikamata. Nilipigwa na kuzuiliwa kwa saa mbili gerezani.
Tangu wakati huo, nimekuwa nikiitwa kila juma mbele ya mahakama ya kijeshi kwa mashtaka yasiyo na msingi. Nyuma ya haya yote kuna siasa. Lakini ninatembea kifua mbele.

Mongabay: Kwenye kitabu chako, pia unaeleza kwamba baadhi ya jamii za wenyeji zilikuona kama “mtu mbaya.” Kwa nini?
Emmanuel Bahati Lukoo: Kwa sababu kazi yetu ni kupambana na shughuli haramu ndani ya mbuga za wanyamapori. Katika baadhi ya jamii maskini sana, hiyo inakufanya kuwa adui.
Watu niliowajua tangu utotoni waliniambia hivi: “Wazungu wataondoka, lakini wewe utabaki hapa.”
Kwangu, suluhisho liko katika uhifadhi shirikishi. Jamii sharti ifahamu kwamba kulinda hifadhi pia ni kwa manufaa yao. Njia mbadala za kiuchumi na kazi karibu na mbuga lazima zibuniwe.
Ndio maana tulizindua miradi na vijana, haswa kuhusu ya michezo. Nilitengeza shule ya soka ili kuwaleta vijana karibu na walinzi na kukuza uhifadhi.
Mongabay: Pia umetaja uingiliaji wa kisiasa katika usimamizi wa hifadhi. Tatizo hili ni kubwa kwa kiasi gani?
Emmanuel Bahati Lukoo: Ni tatizo kubwa sana. Wanasiasa wengine huwadanganya wenyeji wa eneo hilo kwa kuwaahidi kupata ardhi ya mbuga wakiwapigia kura.
Hii inahimiza uvamizi haramu, utumiaji mbaya wa rasilimali na wakati mwingine hata vikundi vyenye silaha. Kisha ni walinzi wanaopaswa kukabiliana na matokeo yake vijijini.

Mongabay: Leo, kutokana na vita kati ya M23 (kundi la waasi wa kijeshi) na serikali, kuna athari gani katika uhifadhi?
Emmanuel Bahati Lukoo: Uharibifu ni mkubwa sana. Kuna ukataji miti kiholela, ukataji miti ovyo na uchimbaji madini kiharamu, na uharibifu mkubwa wa makazi asilia.
Leo, baadhi ya maeneo ya hifadhi hayafikiki. Tuko katika hali ngumu sana.
Mongabay: Je, ni aina gani ya usaidizi unaoweza kuleta mabadiliko kwa walinzi?
Emmanuel Bahati Lukoo: Kwanza kabisa, ni usalama. Kisha mazingira mazuri ya kazi na malipo bora. Walinzi pia wanapaswa kuwa na uhakika kwamba watoto wao wataweza kusoma na kuishi vizuri. Wengi hujitolea maisha yao yote kulinda nafasi hizi.
Mongabay: Licha ya hayo yote, unaendelea na kazi hii. Unapowatazama watoto wako, unatumai uhifadhi wa wakati ujao gani?
Emmanuel Bahati Lukoo: Natumai siku moja kuona mbuga zetu kwa mara nyingine tena kuwa sehemu zinazotembelewa na watalii kutoka duniani kote. Mandhari yetu ni miongoni mwa mazuri na viumbe hai vyema ulimwenguni, lakini hatuwezi kufaidika na utajiri huu kwa sababu ya migogoro. Ndoto yangu ni kuona mbuga za Kahuzi-Biega, Virunga, Maïko na hifadhi zingine kuwa alama za amani na ustawi kwa mara nyingine.
Picha ya bango: Kwa sasa, Emmanuel Bahati Lukoo ni naibu mkurugenzi wa Hifadhi ya Kitaifa ya Kahuzi-Biega. Picha kwa hisani ya Emmanuel Bahati Lukoo.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 19/05/2026