- Taka za plastiki zinazozalishwa zinakadiriwa kufikia kati ya tani milioni 0.84 hadi 1.3 kwa mwaka.
- Taka zikiingia baharini, humezwa na samaki na kuingia kwenye mnyororo wa chakula wa binadamu.
- Bila hatua za haraka, Tanzania inaweza kupoteza hazina ya bahari yake.
- Mafanikio ya uhifadhi wa bahari yatategemea uwajibikaji wa kila mwananchi.
Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni mwaka huu kwa msisitizo wa kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Tanzania inaungana na mataifa mengine kuadhimisha siku hiyo huku ikikabiliwa na changamoto kubwa ya kulinda Bahari ya Hindi inayozidi kuathiriwa na uchafuzi wa mazingira, hasa ongezeko la taka za plastiki, uvuvi usio endelevu pamoja na uharibifu wa mifumo ya ikolojia ya pwani.
Hali ikoje?
Remy Lema, Meneja wa Kiufundi wa mradi wa ‘Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu’ kutoka International Union for Conservation of Nature (IUCN), anasema sehemu kubwa ya uchafuzi wa bahari inatokana na taka ngumu.
Anasema kuwa kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya uchafuzi unaopatikana baharini unatokana na taka ngumu, huku asilimia 10 hadi 12 ikihusishwa na vimiminika mbalimbali, yakiwemo mafuta, kemikali na taka nyingine za majimaji zinazomwagika kwenye mazingira ya bahari.
“Bila hatua za haraka za kulinda bahari, Tanzania inaweza kupoteza moja ya rasilimali zake muhimu zaidi za kiikolojia na kiuchumi katika miaka ijayo,” anasema Lema.
Uchafuzi wa bahari umegeuka kilio kwa wavuvi. Salum Khamis, anayefanyia kazi zake za uvuvi katika maeneo ya Kunduchi amelalamikia kuongezeka kwa uchafuzi wa bahari, akisema hali hiyo imeanza kuathiri shughuli zao za kila siku na kupunguza kipato kinachotegemea uvuvi.
“Kwa sasa plastiki nyingi zinaelea baharini na nyingine huzama. Samaki wanakufa au kuhama maeneo haya…hii inaathiri sana kiasi cha samaki kinachopatikana,” anasema.
Mvuvi mwingine kutoka eneo la Feri, Juma Said, anasema mara nyingi nyavu zao hunasa takataka badala ya samaki, jambo linalowaongezea gharama za matengenezo ya vifaa.
“Zamani tulikuwa tukipata samaki wengi karibu na ufukwe, lakini kwa sasa bahari imejaa takataka. Wakati mwingine tunatumia muda mwingi kusafisha nyavu kuliko kuvua,” anasema.
Mkazi wa Salasala, Joani Mfilinge ameiambia Mongabay kuwa zamani alikuwa anapenda sana kutembelea fukwe za bahari hasa maeneo ya Bagamoyo na Kunduchi lakini sasa hivi inakuwa vigumu kutokana na uchafuzi wa bahari unaoendelea. “Maji ya baharini siku hizi rangi yake hata haieleweki. Zamani unakuta maji rangi ya bluu na upepo mzuri lakini siku hizi mazingira ya bahari sio mazuri,” anasema.
Vyanzo vya uchafuzi wa bahari
Uchafuzi wa Bahari ya Hindi, hususan katika ukanda wa pwani wa Dar es Salaam, unaendelea kuwa changamoto kubwa inayotishia afya ya mifumo ya ikolojia ya baharini na maisha ya jamii zinazotegemea rasilimali za bahari. Uchafuzi huo unasababishwa na sababu mbalimbali.
Taka za plastiki, zinatajwa kuwa miongoni mwa vitu vinavyochangia uchafuzi wa bahari kwa kiasi kikubwa. Takwimu kutoka ofisi ya Makamu wa Rais (VPO) zinaonyesha taka za plastiki zinazozalishwa zinakadiriwa kufikia kati ya tani milioni 0.84 hadi 1.3 kwa mwaka, huku chini ya asilimia nne pekee zikirejelewa (recycled).
Tofauti kati ya kiasi cha taka kinachozalishwa na kile kinachorejelewa ni ishara ya changamoto kubwa ya usimamizi wa taka nchini Tanzania. Ili kuhakikisha ustawi na uhifadhi endelevu wa mazingira, ni muhimu taka zote zinazozalishwa zirejelewe au kushughulikiwa ipasavyo. Kiasi kikubwa cha taka kinapobaki bila kurejelewa, huongeza uwezekano wa taka hizo kuishia kwenye mazingira, ikiwemo mito na bahari na kusababisha uchafuzi.
“Tani nyingi za taka za plastiki huingia baharini kila mwaka, na changamoto kubwa ni vipande vidogo vidogo ambavyo haviozi…humezwa na samaki na kuingia kwenye mnyororo wa chakula wa binadamu,” inasema taarifa ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, NEMC, iliyotolewa kwa Mongabay.
Kwa mujibu wa takwimu za UNEP za 2025, kila mwaka, dunia huzalisha zaidi ya tani milioni 400 za plastiki, huku hadi asilimia 85 ya taka zote zinazopatikana baharini zikiwa ni za plastiki. Kati ya taka hizo, ni chini ya asilimia 10 pekee ya plastiki hiyo hurejelewa. Sehemu iliyobaki hutupwa kwenye dampo au kuishia kwenye mazingira, ikiwemo baharini. Kiasi kinachoingia baharini ni kati ya tani milioni 11 hadi 14.
Bila hatua madhubuti kuchukuliwa, kiasi cha taka za plastiki kinachoingia katika mifumo ya maji kinatarajiwa kuongezeka mara tatu kutoka takribani tani milioni 11 mwaka 2016 hadi kufikia karibu tani milioni 29 ifikapo mwaka 2040.
Taka nyingine ambazo ni hatari ni zile za hospitali. Kwa mujibu wa taarifa kutoka NEMC, IUCN na The Narture Conservancy, kutokana na mifumo dhaifu ya usimamizi wa taka, mabaki ya vifaa tiba kama sindano, glovu pamoja na kemikali kutoka hospitali na maabara, huingia kwenye mito na baharini.
“Taka za matibabu zisiposimamiwa ipasavyo, zinaweza kusababisha hatari za kiafya na kwa mazingira. Zikifika baharini zinaweza kubeba vimelea vya magonjwa na sumu kwa viumbe wa majini,” imesema taarifa hiyo.
Uchafuzi unaotokana na mafuta nao umetajwa kuwa changamoto inayoendelea kuchafua bahari kutokana na shughuli za meli, bandari na uvujaji wa mabomba ya mafuta, taarifa kutoka The Narture Conservancy inaeleza.
“Maji taka yasiyotibiwa kutoka majumbani na viwandani pamoja na mafuta yanayomwagika baharini huathiri ubora wa maji na maisha ya viumbe wa baharini,” anasema Elibariki Bajuta, Mkurungezi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria za Mazingira wa NEMC.
Chanzo kingine cha uchafuzi wa Bahari ya Hindi ni shinikizo la shughuli za binadamu pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
Umuhimu wa bahari
Kwa mujibu wa Lema, bahari yenye afya hutoa manufaa makubwa ya kiikolojia, kijamii na kiuchumi. Bahari pia huhifadhi viumbe mbalimbali kama samaki, matumbawe, mikoko na nyasi bahari ambazo zina mchango mkubwa katika uzalishaji wa chakula, kuhifadhi mazalia ya samaki na kulinda mwambao dhidi ya mmomonyoko.

“Iwapo bahari itatunzwa vizuri, Tanzania itanufaika kupitia kuongezeka kwa samaki, utalii na fursa nyingine za uchumi wa buluu. Pia kipato cha wananchi wanaotegemea shughuli za baharini kitaongezeka,” anasema.
Mbali na uchumi, bahari pia imeendelea kuwa chanzo cha bidhaa mbalimbali muhimu ikiwemo mwani unaotumika katika tiba mbadala na bidhaa za viwandani. Nyasi bahari na mikoko pia zina mchango mkubwa katika uzalishaji wa oksijeni na kunyonya hewa ya ukaa inayochangia mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Elibariki, bahari ina mchango mkubwa sana katika kufyonza hewa ya ukaa kupitia nyasi bahari na mikoko. Anasema hadi sasa Tanzania ina takribani aina 12 za nyasi bahari ambazo pia zina mchango mkubwa katika uzalishaji wa oksijeni.
Ripoti ya State of the Coast for Mainland Tanzania ya mwaka 2024, inaonyesha kuwa maji ya ukanda wa pwani wa Tanzania yana jumla ya aina 12 tofauti za nyasi bahari (seagrass). Nyasi bahari ni sehemu muhimu ya mfumo wa ikolojia ya baharini kwani licha ya kutoa makazi na maeneo ya kuzaliana kwa samaki na viumbe wengine wa majini, husaidia kulinda fukwe dhidi ya mmomonyoko wa ardhi na huboresha ubora wa maji kwa kunasa mashapo na uchafu.
Aidha, imeelezwa kuwa misitu ya mikoko na miamba ya matumbawe hufanya kazi kama kinga asilia dhidi ya mawimbi makali na mmomonyoko wa fukwe, hasa katika maeneo ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Kwa mujibu wa Elibariki, zaidi ya asilimia 25 ya viumbe wa baharini hutegemea matumbawe kwa chakula, makazi na mazalia, jambo linaloifanya sekta ya uvuvi kuwa tegemeo kubwa la ajira na chakula nchini.
Wataalamu wanaeleza kuwa matumbawe yanapoharibika, samaki hupoteza mazalia na maeneo ya kujisitiri, hali inayosababisha kupungua kwa samaki na kuathiri moja kwa moja maisha ya wavuvi.
“Sheria zipo wazi kabisa kuhusu matumizi ya baruti au nyavu haramu lakini bado baadhi ya watu wanaendelea kufanya shughuli hizo ambazo zinaharibu sana matumbawe na viumbe wa baharini,” anaeleza Lema. Sheria ya Hifadhi za Baharini na Maeneo Tengefu ya Bahari ya mwaka 1994 Sura ya 146, inaunda maeneo maalum yaliyolindwa kisheria ili kulinda bioanuwai iliyo hatarini kutoweka au yenye umuhimu wa kipekee.
Sheria ya Meli za Biashara, sura ya 165, inatoa wajibu wa kisheria kwa vyombo vya baharini. Kwa mujibu wa sheria hiyo, ni kosa la jinai kwa nahodha au mmiliki wa chombo chochote kuruhusu mafuta au mchanganyiko wa mafuta kuvuja au kumwangwa makusudi baharini. Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003 Sura ya 22, inakataza mtu yeyote kufanya shughuli za uvuvi bila kupata leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Uvuvi au afisa aliyeidhinishwa.
Katika ukanda wa pwani wenye urefu wa takribani kilomita 1,424 kutoka Tanga hadi Mtwara, bahari imeendelea kuwa mhimili muhimu wa maisha ya mamilioni ya wananchi wanaotegemea uvuvi, utalii, usafirishaji na biashara.
Kwa mujibu wa wataalamu, zaidi ya Watanzania milioni 12 wanaishi katika maeneo ya pwani huku takribani watu milioni 4.5 wakitegemea sekta ya uvuvi moja kwa moja au kwa njia zisizo za moja kwa moja.
“Bahari yenye afya inawezesha uvuvi endelevu kwa wavuvi wadogo na wa viwanda, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa,” inasema taarifa ya The Nature Conservancy.
Bahari pia inachangia kati ya asilimia 30 hadi 40 ya shughuli za kiuchumi zinazohusiana na rasilimali za asili kupitia uvuvi, utalii na biashara ya baharini.
Emmanuel Mpina, Kaimu Meneja wa Programu ya Bahari kutoka the Nature Conservancy (TNC) Tanzania, anasema bahari ni moja ya mifumo muhimu zaidi duniani katika kudhibiti mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza maisha ya binadamu.
Uchafuzi wa bahari ni pigo pia kwa sekta ya utalii. Kwa mujibu wa Emmanuel, katika miaka ya karibuni, maeneo ya pwani ya Tanzania yameendelea kuvutia watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani.
“Karibu asilimia 50 ya watalii wa kimataifa husafiri kwenda maeneo ya pwani kutokana na vivutio vya bahari na fukwe. Zanzibar, Kisiwa cha Mafia, Tanga na Mtwara ni miongoni mwa maeneo yanayovutia watalii kutokana na matumbawe, viumbe wa baharini pamoja na shughuli za utalii wa pwani,” anasema.
Anasema katika kisiwa cha Mafia, watalii wengi huvutiwa na papa nyangumi, hali inayochangia kuongezeka kwa mapato ya utalii na ajira kwa jamii zinazozunguka maeneo hayo.
Athari za uchafuzi wa bahari
Uchafuzi wa bahari una athari kubwa kwa mazingira, mifumo ya ikolojia na kwa jamii zinazotegemea rasilimali za baharini kwa maisha yao.
Kwa mujibu wa Emmanuel, vipande vidogo vidogo vya plastiki huingia kwenye mnyororo wa chakula. Hii inaweza kusababisha changamoto kubwa za kiafya kwa binadamu, ikiwemo magonjwa yanayohusishwa na saratani.
Wadau wengine wa mazingira wanasema Tanzania inaweza kushuhudia kuongezeka kwa mmomonyoko wa pwani, kupungua kwa samaki na kushuka kwa mapato ya utalii katika kipindi cha miaka mitano hadi 10 ijayo, iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa. “Mfumo wa bahari ukiharibika, athari zake zinaenda moja kwa moja kwa jamii. Wavuvi watapata samaki wachache, utalii utaathirika na hata usalama wa chakula utakuwa kwenye hatari,” anasema Lema.
Athari hizo pia zinatarajiwa kuongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha kuongezeka kwa joto la maji ya bahari, hali inayochangia kufa kwa matumbawe na kubadilika kwa mifumo ya maisha ya viumbe wa baharini.
Ghaamid Abdulbasat, ambaye ni mtaalamu wa mazingira anasema taka ngumu zinaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya mifumo ya ikolojia ya bahari, akisisitiza kuwa viumbe vya majini vinahitaji mazingira safi ili kuendelea kuwa na afya nzuri.
Anafafanua kuwa taka za plastiki, hasa chupa, mara nyingi haziingii baharini zikiwa tupu bali hubeba mabaki ya vimiminika au kemikali zinazoweza kusababisha madhara makubwa kwa viumbe wa majini.
“Wakati mwingine chupa zinaingia baharini zikiwa na vimiminika fulani ndani yake. Hizi zinaweza kuua viumbe wa baharini na kufanya bahari pamoja na fukwe kuwa kwenye hali ya kukosa hewa,” anasema.
Kwa mujibu wa Abdulbasat, uchafuzi wa bahari pia una madhara ya moja kwa moja kwa afya ya binadamu kupitia samaki wanaoliwa. Anasema kemikali na uchafu huingia kwenye mlolongo wa chakula kupitia mchakato wa bioaccumulation na biomagnification (mkusanyiko wa kemikali katika viumbe na kuongezeka kwake katika mnyororo wa chakula).
“Samaki wanaishi kwenye mazingira yaliyochafuliwa, hivyo wanabeba pia ule uchafu unaowazunguka. Mwisho wa siku binadamu anayekula samaki hao naye anaathirika,” alieleza.
Aidha, anasema uchafuzi wa bahari unaathiri hata viumbe wa kina kirefu cha bahari ambao wana jukumu muhimu la kufyonza hewa ya ukaa (carbon), hali inayoweza kuvuruga mifumo ya ukanda wa pwani na mazingira ya bahari kwa ujumla.
Pia anaonya kuhusu madhara ya uchafuzi unaotokana na mafuta yanayomwagika baharini kutoka kwenye meli na magari.
“Mafuta yanayomwagika yana kemikali nzito sana. Kuna baadhi ya kiwango bahari inaweza kujisafisha yenyewe, lakini kiwango kinapokuwa kikubwa au mafuta hayo kuwa na vimiminika hatari, madhara yake yanakuwa makubwa zaidi,” alisema.
Nini kinafanyika kuokoa bahari?
Elibariki anasema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisheria na kiufundi kulinda Bahari ya Hindi, ikiwemo kufanya ukaguzi wa viwanda na miradi ya pwani kuhakikisha maji taka yanatibiwa kabla ya kumwagwa baharini.
“Pia tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha uchakataji wa majitaka unafanyika kabla ya maji taka kutiririshwa kwenye mazingira,” anasema.
Serikali pia imeendelea kusimamia upigaji marufuku wa mifuko ya plastiki, hatua iliyosaidia kupunguza taka ngumu baharini.
Katika jitihada za kukabiliana na changamoto hizo, serikali imeendelea kutekeleza sheria na sera mbalimbali za mazingira ikiwemo kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, uamuzi ulioanza kutekelezwa mwaka 2019.
Sheria ya Hifadhi za Baharini na Maeneo Tengefu ya Bahari ya mwaka 1994 Sura ya 146, inaunda maeneo maalum yaliyolindwa kisheria ili kulinda bioanuwai iliyo hatarini kutoweka au yenye umuhimu wa kipekee. Sheria ya Meli za Biashara, sura ya 165, inatoa wajibu wa kisheria kwa vyombo vya baharini.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, ni kosa la jinai kwa nahodha au mmiliki wa chombo chochote kuruhusu mafuta au mchanganyiko wa mafuta kuvuja au kumwangwa makusudi baharini. Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003 Sura ya 22, inakataza mtu yeyote kufanya uvuvi haramu au kutumia njia zilizopigwa marufuku katika shughuli za uvuvi.
Sheria kuu zinazohusika na uhifadhi wa bahari ni pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Sheria ya Hifadhi za Baharini na Maeneo Tengefu ya Bahari ya mwaka 1994, pamoja na Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003.
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira inaweka mfumo wa kudhibiti uchafuzi wa mazingira, usimamizi wa taka, tathmini za athari za mazingira (EIA), na viwango vya ubora wa maji. Sheria hiyo pia inatoa mamlaka kwa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kusimamia utekelezaji wa sheria za mazingira.
Sheria ya Hifadhi za Baharini na Maeneo Tengefu ya Bahari ya mwaka 1994, inalinda hifadhi za bahari, matumbawe, mikoko na viumbe wa baharini huku ikipiga marufuku shughuli kama matumizi ya baruti, sumu na uvuvi haramu ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa. Sheria ya Uvuvi inadhibiti uvuvi haramu, matumizi ya nyavu zisizoruhusiwa na uharibifu wa mazalia ya samaki.
Kuhusu usimamizi wa sheria, NEMC inafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye viwanda, hoteli za pwani na miundobinu mingine ili kuhakikisha maji taka yanatibiwa kabla ya kutiririshwa.
Chini ya usimamizi wa sheria hizo, matumizi ya mifuko ya plastiki yamepungua kwa kiasi kikubwa, na sasa serikali inaanzisha na kuimarisha mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji endelevu ili kudhibiti uchafuzi mapema kabla haujafika kwenye vyanzo vya maji.
Ili kuimarisha uhifadhi wa viumbe vya baharini na uchumi wa bluu nchini Tanzania, Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Asili na Maliasili (IUCN) unatekeleza mradi wa “Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu” wenye thamani ya Euro milioni 11.4 (takriban TSh33 bilioni).

Chini ya mradi huo wa miaka minne ulioanza Novemba 2024, jamii zinasaidiwa kuanzisha shughuli mbadala za kiuchumi kama ufugaji wa nyuki, useremala, kilimo cha mwani na ufugaji wa kaa ili kupunguza utegemezi mkubwa wa moja kwa moja kwenye misitu ya mwambao na rasilimali za bahari.
Changamoto
Licha ya Tanzania kuwa na sheria na sera mbalimbali za mazingira chini ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), pamoja na taasisi nyingine, wataalamu wanasema changamoto kubwa bado ipo kwenye utekelezaji.
Kikwazo kikubwa, inaelezwa, ni watu kushindwa kubadili tabia kuhusu ulinzi wa bahari na pia viongozi kushindwa kuziwajibisha taasisi zinazochafua bahari kwa manufaa binafsi.
Kwa upande wa Emmanuel, uhaba wa fedha, vitendea kazi na rasilimali watu, na mifumo ya usimamizi iliyojikita zaidi katika ngazi za kati badala ya kufikia ngazi za jamii, ni miongoni mwa mambo yanayoendelea kudhoofisha juhudi za kusimamia mazingira ya bahari.
“Pamoja na juhudi za serikali na taasisi mbalimbali, mafanikio ya uhifadhi wa bahari yatategemea pia uwajibikaji wa kila mwananchi. Kila mtu ana jukumu. Kama tunataka kuokoa bahari yetu, tunapaswa kuanzia kwenye namna tunavyotupa taka, matumizi ya plastiki na kufuata sheria za mazingira,” anasema Emmanuel.
Siku ya Mazingira Duniani
Remy Lema, Meneja wa Kiufundi wa mradi wa ‘Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu’ kutoka International Union for Conservation of Nature (IUCN), akizungumzia maadhimisho ya siku ya mazingira duniani, anasema kwa sasa dunia inalazimika kuchukua hatua za haraka kupunguza uchafuzi wa mazingira na kurejesha mifumo ya ikolojia iliyoharibika.
“Kaulimbiu ya mwaka huu inahamasisha watu kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Dunia inasisitiza hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kupunguza uchafuzi na kurejesha mifumo ya ikolojia, na bahari ni sehemu muhimu ya mfumo huo,” alisema.
Wakati wataalamu wakitoa tahadhari kuhusu hatari ya kuendelea kwa uchafuzi wa mazingira ya bahari, ujumbe mkuu wa Siku ya Mazingira Duniani unabaki kuwa mmoja, bila hatua za haraka za kulinda bahari, Tanzania inaweza kupoteza moja ya rasilimali zake muhimu zaidi za kiikolojia na kiuchumi katika miaka ijayo.
Picha ya Bango: Mvuvi katika eneo la Kudunchi, Salum Khamis akiongelea kuhusu kuongezeka kwa uchafuzi wa bahari. Picha na Hellen Nachilongo.