- Njia za kusafirisha gesi zitapita maeneo ya bahari muhimu kiikolojia na kibaiolojia.
- Mabomba yanayotarajiwa kujengwa yanaweza kuathiri makazi ya viumbe.
- Serikali yasema mradi uko katika hatua za mwisho kabla ya kusainiwa kwa makubaliano ya mwisho.
Wakati Serikali ya Tanzania ikijiandaa kutia saini makubaliano ya mwisho kabla ya kusainiwa kwa makubaliano ya mwisho wa mradi wa kuchakata na kusafirisha gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG), ripoti mpya iliyotolewa na mashirika zaidi ya kumi imeweka wazi athari mbalimbali zinazoweza kusababishwa na upanuzi wa miradi ya mafuta na gesi katika maeneo ya pwani na baharini.
Ripoti hiyo inayojulikana kama “Fossil Fuel Threats to the Ocean: Marine Life and Coastal Communities at Risk” pamoja na mambo mengine, inaeleza kuwa upanuzi wa shughuli za mafuta na gesi baharini unaweza kusababisha madhara makubwa yatokanayo na uchimbaji wa visima, umwagikaji wa mafuta, uchimbaji wa sakafu ya bahari (deep-sea mining) pamoja na kuongezeka kwa shughuli za usafirishaji wa meli.
Ripoti hiyo ilitolewa Juni 4, 2026 na shirika la Earth Insight kwa ushirikiano na mashirika 12 ya kiraia, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani inayoadhimishwa Juni 8.
Ripoti iliandaliwa kutokana na utafiti uliohusisha nchi 11 kutoka sehemu mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.
Katika utafiti huo, Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi ambazo zinaendelea kuhamasisha uwekezaji mkubwa katika sekta ya mafuta na gesi. Nchi nyingine zilizotajwa ni Kenya, Australia, Cameroon, Indonesia, Jamaica, Norway, Trinidad na Tobago, Argentina na Mexico.
Kwa Tanzania, mradi huo unapangwa kujengwa katika eneo la Likong’o, kusini mwa mkoa wa Lindi. Lengo ni kuchakata gesi asilia inayopatikana baharini na kuibadilisha kuwa gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) kwa ajili ya kuuzwa katika masoko ya kimataifa.
Ripoti hiyo imetolewa siku chache baada ya Waziri wa Nishati, Dkt Deogratius Ndejembi, kuliambia Bunge kwamba makubaliano ya kibiashara na kodi kati ya serikali na wawekezaji wa mradi wa LNG yamekamilika, na kilichobaki ni hatua za mwisho za kisheria kabla ya kusainiwa kwa makubaliano ya mwisho.
Waziri alisema hayo Aprili 24, 2026 mjini Dodoma wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2026/27.
“Makubaliano ya kibiashara yamefikiwa, makubaliano ya kodi yamefikiwa, na sasa tupo katika hatua ya kisheria,” alisema Ndejembi.
Wakati msimamo wa Serikali ya Tanzania ni kuendelea na mradi huo, ripoti ya shirika la Earth Insight na mashirika 12 ya kiraia, inaainisha maeneo kadhaa ambayo utekelezaji wa mradi huo unaweza kuathiri.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, njia zinazotarajiwa kutumiwa na meli kubwa za kusafirisha gesi zinapita katika maeneo mawili ya bahari yenye umuhimu mkubwa wa kiikolojia na kibayolojia. Maeneo hayo ni makazi ya viumbe walio katika hatari ya kutoweka, wakiwemo papa nyangumi (whale shark), kasa aina ya hawksbill (kasa mdomo wa mwewe) na green turtle (kasa wa kijani), pamoja na dugong.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, eneo linalotarajiwa kuathiriwa zaidi liko ndani ya mfereji wa Msumbiji (Mozambique Channel) na Mfereji wa Kaskazini wa Msumbiji, maeneo yanayotambuliwa kimataifa kwa uzalishaji mkubwa wa viumbe baharini na utajiri wa bayoanuwai.
Maeneo hayo pia yana miamba ya matumbawe, njia za viumbe wanaohama kutoka sehemu moja kwenda nyingine na makazi muhimu ya mamalia na viumbe wengine wa baharini kama nyangumi wenye nundu, dugong, papa na nyangumi.
Aidha, miundombinu ya nchi kavu inayohusiana na mradi huo pia imeelezwa kuwa inakabiliwa na hatari. Mabomba yanayotarajiwa kujengwa pamoja na miundombinu mingine yanaweza kuathiri baadhi ya makazi ya viumbe katika maeneo ya pwani, ikiwemo sehemu zinazopita ndani ya Lindi Creek Key Biodiversity Area (KBA), eneo linalotambuliwa kwa umuhimu wake katika uhifadhi wa spishi na makazi ya viumbe hai.
Katika eneo la bahari la Lindi pekee, ripoti hiyo inasema kuna takribani kilomita za mraba 25 za misitu ya mikoko, kilomita za mraba 35 za maeneo ya hifadhi za baharini na pwani, pamoja na kilomita za mraba 46 za maeneo muhimu ya bayoanuwai ya baharini na pwani.
Mwezi Juni 2022, Serikali ya Tanzania ilisaini makubaliano ya awali (Framework Agreement) na kampuni za Equinor na Shell yaliyobainisha haki na wajibu wa kila upande katika utekelezaji wa uwekezaji huo. Hata hivyo, makubaliano ya mwisho yamekuwa yakicheleweshwa mara kadhaa.
Mwezi Aprili 2025, serikali iliwaeleza wabunge kuwa ucheleweshaji huo ulitokana na juhudi za Tanzania kuhakikisha inalinda zaidi maslahi ya taifa katika mikataba hiyo, kwa lengo la kuepuka makosa yaliyotokea katika baadhi ya mikataba ya uwekezaji ya awali. Wakati huo, serikali ilieleza kuwa ilitarajia mikataba hiyo kusainiwa ndani ya mwaka 2025 na uzalishaji wa gesi kuanza ifikapo mwaka 2030.
Mapema mwaka huu, serikali ilitoa tena hakikisho kwa umma kuwa makubaliano hayo yangekamilishwa kabla ya mwezi Juni.
Mradi huo mkubwa wenye thamani ya $42 bilioni unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na muungano wa kampuni za kimataifa za nishati, ambapo Shell na Equinor ni waendeshaji wakuu wa mradi huo, huku ExxonMobil ikiwa miongoni mwa washirika wake.
Serikali na wadau wa sekta ya nishati wanautaja mradi huo kama uwekezaji mkubwa zaidi kuwahi kupangwa nchini Tanzania.
Kabla hata ya kuchapishwa kwa ripoti hiyo, mradi huo ulikuwa tayari umeibua mjadala kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kwa mifumo ya ikolojia ya baharini katika eneo la Lindi, ikiwemo mikoko, matumbawe, viumbe wa baharini na baadhi ya jamii za pwani ambazo tayari zimeathiriwa na mipango ya upatikanaji wa ardhi na uhamishaji wa wananchi.
Hata hivyo, serikali imeendelea kuutetea mradi huo ikisema utaleta uwekezaji mkubwa, ajira, mapato ya taifa na maendeleo ya miundombinu kwa Lindi na Tanzania kwa ujumla.
Picha ya bango: Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Dkt Deogratius Ndejembi, akihutubia bunge hivi maajuzi.