- Ufuatiliaji wa tembo katika Mlima Elgon, kwenye mpaka wa Uganda na Kenya, unaonyesha kundi la tembo lililovuka hadi upande wa Uganda, katika eneo ambalo walikuwa hawajaonekana kwa kiasi kikubwa tangu miaka ya 1970.
- Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda inasema kurejea kwao ni ishara chanya kwamba juhudi za kurejesha maeneo ya msitu yaliyoharibika katika Mbuga ya Kitaifa ya Mlima Elgon zinazaa matunda.
- Wakazi wa wilaya ya Bukwo, ambayo inapakana na hifadhi ya taifa, wanasema tembo waliharibu mazao mwaka wa 2025 lakini walinzi wa UWA hadi sasa wamezuia uharibifu huo mwaka wa 2026.
Kulingana na taarifa zilizopatikana kupitia kola za kufuatilia na Wakfu wa Mlima Elgon (MEF), mwaka jana tembo wasiopungua 60 walivuka kutoka Kenya hadi upande wa Uganda wa Mlima Elgon, mlima mkubwa wa volkeno ulioko mpakani mwa Uganda na Kenya, na kurudi kwenye sehemu ya asili yao ambapo hawajaonekana kwa zaidi ya miaka 40.
MEF hufadhili miradi ya jamii inayolenga kupunguza uharibifu wa misitu na kuongeza ufahamu wa masuala ya mazingira, pamoja na timu ya maskauti wa jamii 18 katika upande wa Kenya wa mlima, sehemu ya Mradi wa Tembo wa Mlima Elgon unaotekelezwa na Shirika la Wanyamapori la Afrika Mashariki. Mwenyekiti wa wakfu wa MEF, Chris Powles, aliiambia Mongabay kwamba mnamo mwaka 2022, maskauti walifuatilia tembo wanne wakivuka mto Suam, ambao unaashiria mpaka kati ya nchi hizo mbili.

Katika mahojiano kupitia barua pepe, Powles alisema sababu kadhaa zinaweza kuelezea kurudi kwa tembo, ingawa haiwezekani kusema kwa uhakika ni nini kiliwachochea kurejea katika eneo hilo. “[Hizi] ni pamoja na ongezeko la idadi ya tembo upande wa Kenya, kuongezeka kwa shinikizo la binadamu kwa upande wa Kenya, usalama wanaoupata wakiwa upande wa Uganda, ambako eneo hilo lote liko ndani ya mbuga ya taifa, tofauti na upande wa Kenya,” aliandika.
“Na, labda, tembo walio hai tangu wakati wengine wao waliuawa nchini Uganda sasa wamekufa kawaida na hivyo huenda kumbukumbu ya hatari zilizowakabili nchini Uganda imefifia kadri vizazi vilivyobadilika.”
Mwishoni mwa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa miaka ya 1980, tembo nchini Uganda na maeneo mengine ya Afrika Mashariki waliwindwa sana na wawindaji haramu wa pembe za tembo, ikiwa ni pamoja na wapiganaji katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Uganda.
Caroline Asiimwe, anayehusika na utafiti na ufuatiliaji wa ikolojia katika Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda, alisema kuvuka kwa tembo kutoka Kenya kurudi upande wa Uganda wa Mlima Elgon ni ishara ya mafanikio ya uhifadhi wa viumbe hai.
“Kihistoria, Mlima Elgon ulikuwa na idadi kubwa ya tembo, lakini baadaye walitoweka wakati makazi yao yalipoharibiwa. Hata hivyo, kutokana na juhudi za uhifadhi zinazotekelezwa na Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda, tumeona tembo wakirudi,” Asiimwe aliiambia Mongabay.
“Kwa kutumia teknolojia yetu ya ndege zisizo na rubani, tuliona kundi la tembo wakirudi, na tangu Novemba, hawajarejea Kenya.”

Misitu ya milimani ya Mbuga ya Kitaifa ya Mlima Elgon ni makazi ya zaidi ya spishi 300 za ndege, wakiwemo tai wenye ndevu walio kwenye hatari ya kutoweka (Gypaetus barbatus), na mamalia wakiwemo chui, swala aina ya taya (Ourebia ourebi) na tembo. Katika pande zote mbili za mpaka, mlima huo ni Hifadhi ya Mazingira ya UNESCO, lakini Asiimwe alisema jamii zinazoishi wilayani Bukwo na katika wilaya nyingine zinazozunguka mlima huo zimeharibu vibaya maeneo makubwa, na kusababisha tembo kuhamia upande wa Kenya.
“Baada ya shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo kupunguzwa, tulijaribu kurejesha makazi, ndipo tunaona tembo wakirudi,” Asiimwe alisema.
Mlima Elgon ni eneo muhimu la vyanzo vya maji, na afisa wa mamlaka ya UWA aliiambia Mongabay shirika lao limekuwa likifanya kazi kurejesha msitu ulioharibiwa. “Msitu unajirejesha wenyewe, ingawa mamlaka ya UWA inaendeleza upandaji wa baadhi ya miti,” Samuel Ngirio, mzee wa jamii kutoka kijiji cha Saptet wilayani Bukwo, aliiambia Mongabay. “Sasa tuna miti isiyo ya asili, ikiwemo miberoshi na mikaratusi, na tembo sasa wanaingia katika maeneo ambayo msitu umeanza kurejea.”
Watu wanaoishi karibu na mbuga hiyo wamekaribisha kwa tahadhari kurudi kwa tembo. “Jamii zinazozunguka mbuga hiyo zimekubali kurejea kwa tembo katika eneo hilo; kwa ujumla ni mchanganyiko wa majivuno, matumaini ya kiuchumi, wasiwasi mkubwa kuhusu usalama na hatari ya vifo, lakini [jamii] inazitaka mamlaka kutekeleza hatua za ulinzi kama vile uzio wa umeme, mitaro na fidia bora kwa hasara ya mazao na maisha,” alisema Arapptison Moses Malinga.
Yeye ni mwenyekiti wa Leaders Conservation Peace Initiative, shirika la jamii linalowaleta pamoja wazee wa jamii ili kukuza mazungumzo na kupunguza mivutano kati ya jamii na mamlaka ya UWA.
Ngirio aliiambia Mongabay kuwa mwaka wa 2025, tembo walifanya uharibifu mkubwa katika mashamba ya mahindi na migomba katika eneo hilo. “Nyumba yangu iko karibu sana na mbuga ya kitaifa,” alisema. “Mashamba ya majirani zangu wa karibu, Julius Musobo na kaka yake Ben Cheptegei, yaliathirika.”
Alisema wakazi wameiomba Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda kulipa fidia kwa hasara walizopata. Pia aliongeza kuwa wafanyakazi wa mamlaka ya UWA waliotumwa katika eneo hilo wamefaulu kuwatisha tembo kutoka kwenye mashamba ya wakulima mwaka huu.
Asiimwe wa UWA aliiambia Mongabay kwamba mamlaka ya wanyamapori inapanga kutoa mafunzo kwa jamii kupanda mimea ambayo haipendezi kwa tembo kama njia ya kupunguza migogoro inayoweza kutokea.
Pia alisema uwepo wa tembo unaweza kukuza utalii katika wilaya ya Bukwo. “Tembo ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii wa wanyamapori na wanaweza kuzalisha mapato, kutengeneza ajira kama vile waelekezi watalii na walinzi na kusaidia ufadhili wa uhifadhi,” Malinga alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda (UWA), James Musinguzi, alisema tayari jitihada zinaendelea ili kuhakikisha binadamu na wanyamapori wanaishi kwa amani, ambayo ni pamoja na kurejesha makazi, kuunda korido za wanyamapori ili kuruhusu usafiri salama wa tembo na kushirikisha jamii katika mipango ya uhifadhi na utalii wa mazingira.
Tembo kwenye Mlima Elgon wanajulikana kwa kuingia mapangoni kutafuta madini yenye sodiamu, wakichonga kuta za mapango hayo kuwa maumbo ya kipekee yaliyopinda. Mnamo mwezi wa Februari, Powles na wenzake kutoka Wakfu wa MEF walitembelea upande wa Uganda wa mlima, na kuona alama za zamani za meno ya tembo kwenye kuta za mapango pamoja na maumbo yaliyoundwa na uchongaji huo. Wenyeji pia walishiriki hadithi za jinsi tembo walivyotumia mapango hayo zamani.
Wakati tembo wanaporudi katika maeneo yao ya kihistoria katika Mlima Elgon, changamoto sasa iko katika kusawazisha mafanikio ya uhifadhi na ustawi wa jamii zinazoishi kandokando ya makazi ya tembo.
Wakati huo huo, wakazi kama Malinga wanaishinikiza mamlaka kuanzisha hatua kali zaidi za kuwazuia tembo wasiingie kwenye mashamba yao, ikiwa ni pamoja na uzio wa umeme, mitaro na uboreshaji wa fidia kwa uharibifu wa mazao na mali.
Picha ya bango: Mlima Elgon, Uganda. Picha imepigwa na Rod Waddington kupitia Flickr (CC BY-SA 2.0).
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 18/05/2026




