Hatua zinazopendekezwa na waandaaji wa Kombe la Dunia lijalo la FIFA hazitatosha kuwalinda wachezaji na mashabiki dhidi ya hatari ya joto kali na unyevunyevu unaotarajiwa katika mashindano ya mwaka huu, mtaalamu wa matibabu anaonya.
Mnamo Desemba mwaka 2025, FIFA ilitangaza kuwa kutakuwa na mapumziko ya dakika tatu kwa ajili ya kunywa maji kwa wachezaji katika kila nusu ya kila mchezo “ili kuhakikisha hali bora zaidi kwa wachezaji”. Hata hivyo, uchambuzi wa hivi majuzi unasema Kombe la Dunia la 2026, lililoandaliwa kwa pamoja na Marekani, Meksiko na Kanada, litakuwa na joto kali zaidi kuliko mashindano ya Marekani ya ’94.
Wanasayansi kutoka World Weather Attribution (WWA), mtandao wa kimataifa wa watafiti wanaochunguza mchango wa mabadiliko ya tabianchi katika matukio ya hali mbaya ya hewa, wanaonya kuwa mabadiliko ya tabianchi yameongeza karibu mara mbili uwezekano wa joto kali tangu wakati huo.
Hiyo inafanya iwe vigumu zaidi kuondoa joto mwilini, alisema Chris Mullington, mshauri wa kutia ganzi na mhadhiri mkuu wa kliniki katika Imperial College London.
“Hiyo ni muhimu kwa sababu wanasoka huzalisha kiasi kikubwa cha joto mwilini wanapokimbia mara kwa mara, kuongeza kasi na kucheza kwa kiwango cha juu cha ushindani,” alisema katika mkutano na waandishi wa habari. “WBGT inapoongezeka, mifumo ya kawaida ya kupoeza ya mwili inakuwa dhaifu.”
WBGT ni kipimo cha joto kinachojumuisha halijoto ya hewa, unyevunyevu, mionzi ya jua na kasi ya upepo, na hutoa “hisia halisi” ya joto kwenye mwili wa mwanadamu.
Mullington alisema viwango vya juu vya WBGT vinaweza kulazimisha wachezaji “kupunguza kasi ya kukimbia mara kwa mara, kujiendesha kwa uangalifu zaidi, na uwezo wao wa kufanya maamuzi unaweza kuathirika kadiri shinikizo la joto linavyoongezeka.”
Uchanganuzi wa shirika la WWA ulibainisha miji ya Miami, Kansas City na New York/New Jersey kuwa miongoni mwa miji itakayokuwa wenyeji wa mashindano iliyo katika hatari ya joto na unyevunyevu mwingi. Mechi ishirini na sita huenda zikachezwa katika WBGT ya nyuzi joto 26 Selsiasi (79° Fahrenheit) au zaidi, shinikizo la joto linapokuwa hatari sana, waandishi wanasema. Pia kuna uwezekano wa theluthi moja kwamba WBGT itazidi nyuzi joto 28°C (82°F) – hali inachukuliwa kuwa si salama kwa uchezaji; waandishi huongeza.
Mullington alisema utafiti wa fiziolojia unapendekeza kuongeza muda wa mapumziko, na kuweka maeneo ya kupulizia maji baridi ili kupunguza kikamilifu shinikizo la joto.
Pia alitoa wito kwa ustawi wa mashabiki. “Ikiwa muda wa mapumziko utaongezwa na mechi zikawa ndefu zaidi, mashabiki watakaa nje katika hali hizo kwa muda mrefu zaidi,” Mullington alisema. “Kwa hivyo katika kupunguza hatari kwa wachezaji, unaweza kuongeza hatari kwa mashabiki.”
Ili kupunguza hatari kwa watazamaji, Mullington alipendekeza waandaaji kutotoza maji. “Nadhani shabiki wako wa kawaida wa kandanda hawezi kulipa pauni 8 [karibu $11] kwa chupa ya maji,” aliiambia Mongabay katika mkutano huo. “Lakini iwapo wangepewa bure, wangeipokea kwa furaha.”
Mwishowe, Mullington alisema, ni juu ya kuongeza ufahamu wa hatari kwa mashabiki. “Sidhani kama mashabiki wengi wanafahamu kuwa wanaweza kujiweka hatarini katika hali hii, kwa hivyo kutoa taarifa wazi kuhusu hatari hiyo [ili waweze] kufanya maamuzi yao wenyewe kuhusu jinsi ya kujilinda,” alisema.
Picha ya bango: Uwezekano wa kila mchezo wa Kombe la Dunia 2026 kuchezwa katika viwango vya halijoto ambavyo waandishi wa utafiti wanaviona kuwa si salama kwa uchezaji. Picha kwa hisani ya World Weather Attribution.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 18/05/2026