- Biashara ya kuokota na kuuza chupa za plastiki jijini Dar es Salaam inasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuziba mifereji na hatari ya mafuriko, huku ikitoa ajira na kipato kwa wanawake na vijana.
- Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) linasema shughuli hiyo imechangia kuboresha usafi wa mazingira, lakini bado chupa za rangi na mifuniko ya plastiki hukosa soko na mara nyingi huachwa kutapakaa mitaani.
- Waokotaji wa chupa wanakabiliwa na changamoto za mazingira yasiyo salama ya kazi, ukosefu wa vitendea kazi kama glovu na buti, ujira mdogo, na wakati mwingine kutuhumiwa kwa uhalifu wanapofanya kazi mapema alfajiri.
- Waokotaji wanaitaka Serikali kuanzisha vituo maalum vya ukusanyaji wa chupa, kutoa vitambulisho vya utambuzi na kuimarisha utekelezaji wa sheria za urejelezaji ili kuongeza ufanisi wa sekta hiyo na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
DAR ES SALAAM, Tanzania – Kushamiri kwa biashara ya uokotaji wa taka hasa chupa za plastiki katika maeneo ya mijini, huenda kuleta mageuzi katika kushughulikia changamoto za mazingira katika miji mikubwa likiwemo la Dar es Salaam.
Kwa muda mrefu, chupa za plastiki zimekuwa zikitajwa kuwa chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira mijini. Zile ambazo hutupwa kwenye mifereji zimekuwa zikiziba njia za maji na kuchangia mafuriko. Aidha, chupa zinapochomwa, moshi wake husababisha maradhi na pia kuathiri mazingira kutokana na asili yake ya kuchelewa kuoza.
Hata hivyo, kuibuka na kukua kwa biashara ya chupa za plastiki zilizotumika, ambayo mara nyingi hufanywa na akinamama na vijana, kunaendelea kubadilisha historia. Hivi sasa badala ya kushuhudia barabara zenye mifereji iliyojaa chupa tupu, kinachoonekana ni akinamama na vijana waliobeba viroba vikubwa vyenye chupa hizo.
Wakusanyaji wadogo huuza chupa hizo kwa wakusanyaji wakubwa au kwa kampuni zinazojishughulisha na ukusanyaji na urejelezaji wa chupa hizo baada ya matumizi.
Taimuru Hamad, Meneja Uzingatiaji Sheria kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), anakiri kwamba biashara hiyo imeleta faida kubwa katika ustawi na ulinzi wa mazingira.

“Kuokotwa kwa hizi chupa kunasaidia sana. Kwanza, kunasaidia katika suala zima la ustawi wa mazingira, lakini pia kwenye suala la usafi. Kama zingekuwa haziokotwi, mazingira yangeendelea kuathirika sana na pia yangekuwa machafu sana,” alisema Taimuru katika mahojiano na Mongabay.
Chupa za rangi
Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na waokotaji wa chupa za plastiki hapa nchini, bado kuna mapungufu.
“Chupa za plastiki zenye rangi haziokotwi sana. Wanaofanya biashara hiyo wanadai kwamba matumizi ya chupa hizo ni madogo na hivyo hazina soko ukilinganisha na zile nyeupe,” anasema Taimuru.
Kwa mujibu wa Taimuru, viwanda vinavyouziwa hupendelea chupa za plastiki nyeupe ambazo husagwa na unga wake hutumika kutengenezea bidhaa mbalimbali zikiwemo chupa nyingine pamoja na nguo aina ya tisheti.
Changamoto nyingine ya biashara hiyo ni kwamba waokotaji huchukua chupa tu na kutupa mifuniko ovyo, hali inayopingana na malengo ya zoezi zima ambayo ni kuleta ustawi kwa mazingira.
Ingawa biashara hiyo ya uokotaji chupa za plastiki inaleta chembe za matumaini kwenye harakati za kutunza na kuhifadhi mazingira, Taimuru anakiri kwamba mfumo wa biashara hiyo unakidhi mahitaji kwa kiasi kidogo sana. Anasema hicho kinachofanyika ni sehemu ndogo tu ya juhudi kubwa za uhifadhi wa mazingira.
Taimuru amesisitiza kuwa pamoja na uokotaji wa chupa za plastiki kuleta manufaa, ni lazima wahusika kufuata sheria za utunzaji wa mazingira na mikataba ya kimataifa kuhusu mazingira.
“Kanuni za Udhibiti wa Taka za Plastiki za mwaka 2019 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022, inabidi itekelezwe kwa vitendo,” alisema Taimuru.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo, kampuni zinazozalisha bidhaa zinazotumia chupa za plastiki zinapaswa kushiriki katika ukusanyaji na urejelezaji wa chupa hizo baada ya matumizi, kama sehemu ya kulinda mazingira.
Waokotaji wa chupa
Baadhi ya waokotaji wa chupa za plastiki katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam wanasema ingawa kazi hiyo inawasaidia kujipatia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yao, lakini si salama kwa afya zao na pia ujira wake ni mdogo sana.
“Kwa kawaida chupa huwa na uzito mdogo sana. Unaweza kuokota siku nzima lakini ukajikuta unaambulia kilo zisizozidi kumi,” anasema Moses Mayalla anayefanyia shughuli zake Magomeni.
“Wakati mwingine tunaingia kwenye mitaro ya maji machafu bila buti wala glovu na kuokota chupa. Ingawa kufanya hivyo si salama lakini hali duni ya maisha inatulazimisha kufanya hivyo,” anasema Martha Mlangwa.
“Kwa kuokota chupa tunasaidia kuhifadhi mazingira, kitu ambacho kina manufaa ya muda mrefu kwa jamii. Lakini tunapouza chupa hizo pia tunapata pesa ya kujikimu,” anasema Kasavilla Nelson.

“Hizi chupa, ukiwa na malengo unafaidika. Hukosi hela ya kula, ukipata elfu 3,000, elfu 4,000 umekosa nini,” anasema Godfrey Nicholas, kauli inayoungwa mkono na Ibrahim Ali.
Rai kwa Serikali
Ili kuendelea kufanya kazi hiyo kwa ari, waokotaji wa taka walioongea na Mongabay waliiomba Serikali katika ngazi za mitaa kuhamasisha wananchi ili wawaunge mkono.
“Kutokana na kazi hii tunapata riziki lakini pia tunasaidia kutunza mazingira. Serikali kupitia ngazi za mitaa inaweza kuanzisha sehemu maalum ambazo watu watakuwa wanapeleka chupa pale, ili kazi yetu iwe kuzifuata tu. Hilo litatupunguzia kazi na pia kutupa hamasa,” anasema Aisha Maulid.
James Handiko anasema mitaa inaweza pia kujitolea kuchangia vitendea kazi ili viwasaidia kufanya kazi katika mazingira salama.
Changamoto
Miongoni mwa changamoto za shughuli hiyo ni pamoja na baadhi ya chupa hasa zile za rangi kutopokelewa na makampuni yanayohusika na urejelezaji.
“Kutokana na hali hiyo, baadhi ya waokotaji wa taka wanachukua tu zile chupa wanaoweza kuuza. Nyingine wanaziacha mitaani zikizagaa. Hilo ni tatizo kwa sababu hizo chupa zilizosalia zinaendelea kuathiri mazingira,” anasema Handiko.
Changamoto nyingine inayowakabili ni kuonekana kama wezi. “Sisi shughuli zetu za kuokota chupa tunaanza mapema alfajiri. Wakati mwingine unapozunguka mtaani na kwa bahati mbaya eneo hilo kukawa kumetoa wizi, kabla ya wewe kufika pale, unaambiwa wewe ndiye umeiba,” alieleza Juma Musa Lechipya.
Anasema kwa vile shughuli wanayofanya inasaidia pia jamii kwa kuhifadhi mazingira, ni vema Serikali iwasaidie wapate vitambulisho vitakavyowatambulisha mitaani.
Kauli ya Serikali
Kurejelezwa kwa taka na kuzalisha bidhaa nyingine ni miongoni mwa mikakati iliyowekwa na Serikali kupunguza kiasi cha taka.
Mwezi Aprili 2025, “Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)…” Reuben Kwagilwa alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa taka za plastiki katika maeneo ya fukwe za bahari na maziwa zimepungua kwa takribani asilimia 60 na hivyo kupunguza hatari kwa viumbe wa majini.
Naibu Waziri alibainisha kuwa Serikali imeweka jitihada madhubuti za kuhakikisha taka hususani zile za plastiki zinazozalishwa katika maeneo mbalimbali nchini zinarejelezwa ili kuzalisha bidhaa nyingine.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali inahakikisha katika majiji, kama vile Dar es Salaam, inajenga madampo makubwa yatakayoambatana na viwanda vitakavyofanya shughuli ya urejelezaji na kuchakata taka kuwa bidhaa, hatua itakayosaidia kudhibiti taka.
Picha ya bango: Kwenye barabara nyingi za mijini, ni kawaida kukutana na mikokoteni au baiskeli zilizobeba mifuko mikubwa yenye chupa za plastiki kama inavyoonekana pichani. Picha na Joyce Bazira.