- Miradi mingi ya kaboni haihusishi jamii tangu hatua ya kubuni wazo hadi utekelezajiwake.
- Malalamiko hayo yanaakisi changamoto kubwa inayokabili sekta ya kaboni: kutoshirikishwa kwa jamii tangu hatua za mwanzo za kubuni miradi.
- Mbinu mpya ya fidia ya kaboni inayotumia teknolojia imeanza kuleta mabadiliko.
- Mfumo mpya huwashirikisha wafugaji katika usimamizi endelevu wa malishona kusaidia kurejesha imani katika miradi ya fidia ya kaboni.
Naito Leshao alionyesha hisia za kuchoshwa na miradi ya biashara ya fidia ya hewa ukaa katika mkutano wa kimataifa uitwao Global Landscapes Forum (GLF) wa mwaka 2026 uliofanyika Nairobi, Kenya.
Akiwa na hisia kali, Leshao aliuliza maswali kadhaa: kwa nini miradi mikubwa ya kaboni inayodaiwa kuwa kwa ajili ya watu waliolinda ardhi kwa miaka mingi hupitia mikononi mwa watu wengi kiasi kwamba malipo yanapowafikia wanajamii, wanapata kiasi kidogo sana?
Leshao, aliyekuwa akiwakilisha jamii yake kutoka Maasai Mara, aliendelea kwa swali jingine: Je, mnatarajia jamii za kiasili ziendelee kuhifadhi ardhi huku zikilinda mifumo yao ya malisho, wakati matatizo yao hayasikilizwi kuhusu namna mabadiliko ya tabianchi yanavyowaathiri?
Maswali tata
Maswali yake si mapya katika mijadala ya uhifadhi wa mazingira. Yameendelea kujitokeza tangu Mkataba wa Paris ulipoweka msingi wa ushirikiano wa kimataifa katika biashara ya kaboni kupitia Kifungu cha 6 kama njia ya kupambana na ongezeko la joto duniani huku ukiwa na lengo la kupambana na ongezeko la joto duniani na kuzalisha mapato.
Hata hivyo, vigezo vya mfumo huo mara nyingi vimekuwa vikionekana kuwa vya upendeleo, vikiegemea zaidi kwa waendelezaji wa miradi katika mnyororo wa biashara ya kaboni.
“Wanakuja na asilimia fulani, lakini nani anaamua hizo asilimia? Nani anasema kwamba jamii hii inapaswa kupata asilimia 10 au 15? Unajuaje kwamba hicho ndicho kiasi kinachokidhi uendeshaji wa jamii hii? Pamoja na kukosekana kwa usawa katika mchakato huu, bado dunia inazihitaji jamii za kiasili kuhifadhi mazingira,” alisema Leshao.
Hakukuwa na majibu ya haraka kwa maswali yake, licha ya makadirio mapya kuonyesha kwamba mapato yanayotokana na soko la kimataifa la kaboni yataongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 14 mwaka 2025 hadi zaidi ya dola za Marekani bilioni 69 mwaka 2036.
Lakini ripoti ya Carbon Market Watch inathibitisha kile kinachochochea wasiwasi wa Leshao. Hofu hiyo inatokana na uchunguzi uliohitimisha kuwa jamii hizo ziko kwenye hatari ya kupokonywa ardhi yao kutokana na miradi ya fidia ya kaboni, na hayo yalibainika baada ya kupitia takribani miradi 2,000 inayoingia sokoni.

Kwa mujibu wa Wendy Chamberlin, mshauri mwandamizi wa masuala ya tabianchi na masoko katika shirika lisilo la kiserikali la kimataifa linalojulikana kama Trickle Up, hatari hizo zinatokana na ukweli kwamba miradi mingi haihusishi jamii tangu hatua ya kubuni wazo hadi utekelezaji. Alisema shida nyingine ni muundo unaosababisha ukosefu wa usawa katika umiliki na mgawanyo wa faida.
“Siamini katika miradi ya kaboni. Fedha zinapoingia kwenye jamii, hicho ndicho kinachotarajiwa tushangilie. Lakini hakuna uwazi kuhusu fedha hizo zinatoka wapi, zinaenda wapi na maamuzi yanafanywaje,” alisema Chamberlin wakati wa kikao alichohudhuria Leshao.
Kadiri mkutano wa GLF ulivyoendelea, ndivyo baadhi ya maswali yaliyokuwa yakimsumbua Leshao yalivyoanza kupata majibu. Miongoni mwa majibu hayo ni namna mbinu mpya ya fidia ya kaboni inayotumia teknolojia inavyobuni na kutekeleza miradi katika Afrika Mashariki, huku ikibadili mfumo wa ushirikiano na mgawanyo wa faida kati ya jamii na waendelezaji wa miradi.
Joshua Laiser, mwanzilishi na mratibu wa Tanzania Conservation Community Initiative, anasema mfumo huo unawashirikisha wafugaji katika ufugaji endelevu wa malisho, ambapo mifugo huhamishwa kutoka eneo moja la malisho kwenda jingine kwa utaratibu maalumu.
Anasema lengo linakuwa kuvunja udongo wa juu, kusambaza samadi kwa mpangilio mzuri, na kuruhusu maeneo yaliyotumika kupumzika ili nyasi na uoto wa asili viweze kurejea.
Mabadiliko makubwa
Kadiri uoto wa asili unavyorejea, ndivyo kaboni zaidi inavyohifadhiwa ardhini. Hapo ndipo mabadiliko makubwa yanapoanzia, kwa kuwa uhifadhi wa mazingira unageuzwa kuwa njia ambayo jamii zinaweza kupata mapato kupitia mauzo ya mikopo ya kaboni inayotokana na ongezeko la kaboni inayohifadhiwa ardhini, anafafanua.
Kabla ya mradi kuanza rasmi, jamii husika lazima zitoe ridhaa yao. Baada ya hapo hufuata tathmini mbalimbali kabla ya utekelezaji kamili kuanza, mchakato ambao unaweza kuchukua miaka kadhaa ya ushirikishwaji wa jamii, kwa mujibu wa Laiser.

Laiser pamoja na timu yake walitambulisha programu iliyobuniwa na Afriscout, shirika la kijamii linalofanya kazi nchini Kenya, Tanzania na Ethiopia, ambalo kwa zaidi ya miaka miwili limekuwa likizielimisha jamii kuhusu usimamizi wa maeneo ya malisho na namna ya kuanzisha miradi ya fidia ya kaboni.
Programu hiyo inaendeshwa kwa msaada wa akili bandia (AI). Kwa kushirikiana na maafisa wa Afriscout waliopo katika maeneo ya kazi, wanajamii hutumia programu hiyo kuchora ramani za uoto wa asili kutathmini ubora wa udongo na kufuatilia hali ya malisho, jambo linalowezesha jamii kufuatilia na kusimamia maeneo yao ya malisho.
Maafisa hao huingiza taarifa mbalimbali katika mfumo huo, zikiwemo mipango iliyokubaliwa na jamii wakati wa mikutano, ratiba ya malisho, pamoja na mwongozo wa uhamishaji wa mifugo.
Wafugaji wanaweza kufungua na kupata taarifa hizo kupitia programu ya simu inayotumia akili bandia.
“Teknolojia hii inawasaidia kutathmini na kurahisisha mtiririko wa taarifa kuhusu usimamizi wa maeneo ya malisho, na hapo ndipo umuhimu wa matumizi ya akili bandia unapoonekana. Jamii zimeridhia kabisa na matumizi ya teknolojia hii. Sasa tunaelekea katika hatua ya kuthibitisha miradi ya kaboni,” alisema Laiser.
Kwa mujibu wa Laiser, mfumo huo mpya unasaidia kurejesha imani katika miradi ya fidia ya kaboni, huku ukiwezesha usimamizi bora wa maeneo ya malisho, kurejea kwa uoto wa asili, kupunguza vifo vya mifugo, na kuboresha uwezo wa jamii kufanya maamuzi kuhusu uhifadhi wa mazingira.
Hata hivyo, kwa mujibu wa wataalamu, changamoto nyingi zinazokumba miradi ya fidia ya hewa ukaa huanza tangu hatua za awali za kubuni miradi hiyo.
Kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa ufugaji wa kurejesha mazingira kwa kiwango kikubwa, ambao sasa umeunganishwa na teknolojia za kisasa za fidia ya hewa ukaa, maeneo hayo yalikuwa tayari yakihifadhi hewa ukaa kutokana na miaka mingi ya usimamizi wa asili uliofanywa na jamii za kiasili.
Kutumiwa vibaya kwa fursa
Hata hivyo, Laiser anasema, waendelezaji wa awali wa miradi ya hiari ya hewa ukaa, walitumia fursa hiyo vibaya kwa kuanzisha miradi iliyoungwa mkono na wanasiasa wa maeneo husika huku wakizitenga jamii za kiasili, jambo lililosababisha migogoro ya ardhi nchini Kenya na Tanzania.
Hali hii ilimaanisha kuwa ardhi hizo hazingeruhusiwa kutumika kwa shughuli nyingine zozote isipokuwa kuzalisha mikopo ya hewa ukaa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20. Anasema jambo hilo liliwasumbua wananchi wa maeneo hayo kutokana na sababu za msingi zinazotokana na historia ya ukoloni.
Kwa mfano nchini Kenya, Sheria ya Ardhi ya mwaka 1902 (Crown Lands Ordinance, 1902), ilifafanua upya ardhi ya jamii kama ardhi tupu au isiyotumika pale inapokuwa haina makazi ya kudumu au hailimwi. Haya ni kwa mujibu wa Vivian Silole, mkuu wa ushirikiano wa kimkakati, programu na ubia katika shirika la IMPACT Kenya, ambalo linatetea haki za jamii za kiasili.
Silole anasema kuwa hatua hiyo ilifanywa kimkakati ili kufanya mifumo ya maisha ya wafugaji ionekane kama haijazingatiwa au kutambuliwa kikamilifu, au kuhalalisha uporaji wa ardhi yao, kwa lengo la kubadili matumizi ya maeneo ya malisho ili yaendane na mifumo ya kikoloni. Athari za ukoloni huo zimeendelea kujidhihirisha kwa muda mrefu na kusababisha dhuluma za kihistoria za ardhi katika jamii za kiasili.
Kuendelea kwa simulizi hizi za kikoloni hata baada ya Kenya kupata uhuru kuliunda mfumo unaodhani kuwa jamii za kiasili hazina sheria, uratibu wala uwajibikaji. Hata hivyo, ardhi za wafugaji zinaongozwa na sheria za kimila zilizo wazi na zina mifumo ya maarifa ya jadi na maamuzi ya pamoja ya kijamii, alisema Silole.

“Hii ndiyo sababu migogoro ya ardhi imeendelea kudumu kwa muda mrefu, na naamini inaendelea kutokana na kutotambulika kwa mfumo wa maeneo ya malisho. Watu wengi hawaelewi hasa maeneo ya malisho ni nini. Haya ni mifumo ya wafugaji ambayo hubadilika kulingana na misimu, na haiwezi kuingizwa kirahisi katika ramani na sera zisizobadilika, jambo linalofanya maeneo hayo kupuuzwa mara nyingi,” alisema Silole wakati wa mjadala wa jopo katika kongamano la GLF.
Migogoro hiyo sasa imeenea hadi katika miradi ya fidia ya kaboni. Hata hivyo, mbinu mpya ya kubuni miradi inayotumia akili bandia (AI) inalenga kupinga dhana hizo na kushirikiana na jamii kuunda mifumo endelevu, jambo ambalo linahitaji muda. Kwa mfano, imechukua takribani miaka minne kuanzisha mradi wa fidia ya hewa ukaa nchini Ethiopia kwa kutumia mbinu hii mpya, ili kuhakikisha jamii zina uelewa wa mradi huo na zinafahamu athari na wajibu unaoambatana nao, alisema Laiser.
“Akili bandia haipo ili kuwanyang’anya wananchi mamlaka ya kufanya maamuzi. Inaweza kurahisisha mchakato wa kufanya maamuzi, lakini haiwezi kufanya maamuzi yenyewe, kwani mamlaka hayo yapo mikononi mwa wafugaji wenyewe,” alisema Laiser.
Picha ya bango: Vivian Silole, mkuu wa ushirikiano wa kimkakati, programu na ubia katika shirika la IMPACT Kenya (kushoto), akiwa kama mjumbe katika Global Landscapes Forum jijini Nairobi, Kenya.