- Atuwa Omari, mwenye umri wa miaka 23, anaelezwa kuwa mwanamke pekee Zanzibar anayeshiriki uzamiaji wa kurejesha miamba ya matumbawe, akifanya kazi chini ya Bahari ya Hindi karibu na Kisiwa cha Mnemba.
- Miamba ya matumbawe ya Mnemba iliharibiwa na uvuvi usiodhibitiwa na msongamano wa watalii, hali iliyosababisha Serikali ya Zanzibar kuweka hatua za uhifadhi ikiwemo kupunguza idadi ya wageni, kusitisha uvuvi kwa muda na kuongeza ada za uhifadhi.
- Juhudi za urejeshaji zimeanza kuzaa matunda, huku ikielezwa kuwa takribani asilimia 80 ya matumbawe yamepona au yamerejeshwa, na samaki wameanza kurejea katika maeneo yaliyokuwa yameharibiwa.
- Licha ya changamoto za kazi ya uzamiaji na mitazamo ya kijamii kuhusu wanawake kufanya kazi za baharini, Atuwa anaendelea kuwa mfano wa kuigwa, akihamasisha wasichana kushiriki katika uhifadhi wa mazingira ya bahari na kulinda urithi wa vizazi vijavyo.
Zaidi ya futi 40 (takriban mita 12.2) chini ya Bahari ya Hindi, karibu na Kisiwa cha Mnemba kilichopo Zanzibar, Atuwa Omari na wahifadhi wengine huzama hadi kwenye sakafu ya bahari kwa lengo la kushiriki katika urejeshaji wa miamba ya matumbawe iliyoharibika.
Anapokuwa katika eneo hilo, mawimbi humsukuma huku makundi ya samaki yenye rangi mbalimbali kama vile wa bluu, njano na kijani hupita juu ya kichwa chake huku mwanga wa jua ukionekana kwa mbali ndani ya maji.
Juu ya uso wa bahari, watalii huwa wanazunguka katika maji bila kufahamu kuhusu mfumo dhaifu wa ikolojia unaopambana kuendelea kuishi chini yake.
Kwa mujibu wa waajiri wake, Atuwa, mwenye umri wa miaka 23, anaelezwa kuwa mwanamke pekee Zanzibar anayeshiriki kazi hiyo ya uzamiaji wa urejeshaji wa matumbawe.
Mamlaka za Zanzibar zinaeleza kuwa miaka mitatu iliyopita, eneo la Mnemba ambako Atuwa hufanya kazi, ambalo lina baadhi ya miamba muhimu ya matumbawe ya Zanzibar, liliharibika.
Makame Omar Makame, Mkurugenzi wa Idara ya Uhifadhi Baharini Zanzibar, anasema eneo hilo la Mnemba liliathiriwa na shughuli za kibinadamu zilizokithiri.
“Kulikuwa na shughuli nyingi za uvuvi zisizofuata utaratibu, msongamano wa watalii, ambapo takribani boti 200 zenye watalii zilikuwa zikiingia katika eneo la mita 200 za ukanda wa pwani kila siku,” Makame aliieleza Mongabay.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, ili kulinda mazingira, Serikali ya Zanzibar iliamua kupunguza idadi ya wageni hadi 80 kwa siku na kuongeza ada ya uhifadhi kutoka $3 hadi $25 kwa mtalii mmoja, kusitisha kwa muda shughuli za uvuvi na pia kutoa elimu kwa jamii.
Hilo lilikuwa jambo muhimu kwa Atuwa na wenzake ambao wanaamini jamii zao zilihitaji mazingira salama.
Atuwa alizaliwa na kukulia karibu na mwambao wa Bahari ya Hindi. Makazi ya familia yake yalikuwa jirani na fukwe, na alikuwa akiwaona wavuvi wakiondoka jioni kwenda baharini huku watoto wakitumia mchana kuogelea baharini.
Kadri muda ulivyopita, alijijengea ukaribu na bahari, bila kujua kuwa siku moja ingekuwa sehemu muhimu ya maisha yake. Mwanzoni alipata changamoto kuzoea mazingira hayo.
“Kujifunza kupumua chini ya maji haikuwa rahisi,” anasema na kuongeza kuwa wakati mwingine mawimbi huwa makubwa na maji ni baridi sana, lakini kadri muda ulivyopita alizoea na kuwa imara.
Mama yake ndiye aliyemtia moyo kujikita kwenye kazi hiyo ya uzamiaji na utunzaji mazingira. “Bado nakumbuka mama yangu akiniambia kuwa kila fursa huja na baraka zake,” anasema Atuwa.
Kilichoanza kama nafasi ya kazi baadaye kiligeuka kuwa jambo muhimu zaidi kwake. Kwa Atuwa, kazi hiyo inahitaji nguvu na uvumilivu mkubwa.
Kabla ya kila uzamiaji, Atuwa huandaa mitungi ya hewa iliyobanwa na vifaa vya chini ya maji kisha hushuka baharini kwa saa kadhaa. Mawimbi makali na maji baridi hufanya kazi kuwa ngumu zaidi.

Anapokuwa chini ya bahari, kazi yake ni kufunga kwa uangalifu vipande vya matumbawe kwenye miundo maalum iliyowekwa chini ya maji ili miamba iweze kukua tena taratibu.
Bila miamba yenye afya, wataalamu wanasema jamii zinazotegemea uvuvi na utalii zinaweza kukumbwa na madhara makubwa ya kiuchumi na kimazingira.
Baada ya miezi kadhaa ya urejeshaji, samaki huanza kurejea katika maeneo ambayo matumbawe yaliharibika.
Hali hiyo imeongeza umuhimu wa miradi ya urejeshaji wa matumbawe karibu na Mnemba, ambako makundi ya uhifadhi na mamlaka za Zanzibar zinajaribu kufufua miamba iliyoharibika kwa kupanda na kulinda matumbawe.

Hata hivyo, wataalamu wa uhifadhi wa mazingira ya bahari wanaonya kuwa miamba hiyo inaendelea kuwa hatarini kutokana na ongezeko la joto la bahari, kubadilika kwa hali ya hewa, uvuvi haramu, uchafuzi wa mazingira na shinikizo linalotokana na shughuli za utalii.
Makame, ambaye ni mtafiti mbobevu, anasema kuwa matumbawe katika maeneo mengi visiwani humo yalikuwa kwenye hali mbaya katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2021.
“Uharibifu ulikuwa mkubwa. Serikali iliamua kufanya eneo hilo la Mnemba kuwa eneo la uhifadhi la Serikali na hapa sheria ilianza kutumika kudhibiti shughuli katika eneo hilo wakati urejeshaji ukiendelea,” anasema mtafiti huyo.
Makame anasema kwa sasa sehemu kubwa ya matumbawe yamerejea na jitihada zaidi zinaendelea, zikiwemo kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutunza miamba hiyo.
Mnamo Septemba 2021, jamii ilianza kushirikiana na shirika la &Beyond katika urejeshaji wa miamba hiyo, kulinda eneo la hifadhi ya baharini, na kusaidia katika uvuvi endelevu.
Atuwa na wenzake wamekuwa sehemu ya juhudi za urejeshaji katika eneo la Mnemba, ambapo inaelezwa kuwa hadi sasa takribani asilimia 80 ya matumbawe yamepona au yamerejeshwa.
Hija Uledi, ambaye ni mhifadhi kwenye kisiwa hicho, anasema: “Kwa zaidi ya miaka minne sasa tumerudisha uhai kwenye miamba. Sasa samaki wameanza kuongezeka katika eneo hili lenye matumbawe, lakini pia kuna mabadiliko makubwa ukilinganisha na hali ilivyokuwa.”

Juma Mshenga, ambaye amefanya shughuli za uvuvi kwa takribani miaka 30 katika eneo hilo, anasema: “Mabadiliko yapo. Wakati tulianza kazi hiyo, hali ilikuwa tofauti. Hapo awali samaki walikuwa wengi, lakini walipungua katika miaka ya karibuni. Sasa samaki wameongezeka baada ya Serikali kusitisha uvuvi kwenye eneo hili (Mnemba).”
Juhudi za Atuwa na wenzake zinaelezwa kuzaa matunda. “Kuona maisha yakirejea kwenye miamba iliyoharibika hunifanya nijivunie kazi tunayofanya na wanaume ninaozamia nao,” alisema Atuwa.
Hata hivyo, changamoto anazokutana nazo hazipo baharini pekee. Katika baadhi ya maeneo Zanzibar, matarajio ya kijamii bado yanawazuia wanawake kufanya kazi zinazohusisha nguvu au shughuli za baharini. Atuwa anasema baadhi ya watu katika jamii yake hapo awali waliamini uzamiaji si kazi inayowafaa wanawake, hasa wakina mama.
Kadri watu walivyoelewa umuhimu wa urejeshaji wa matumbawe na kumuona Atuwa akiendelea na kazi yake, ukosoaji ulianza kubadilika na wengi sasa wanaelewa faida ya kazi yake.
Atuwa anasema: “Nataka wasichana wajue kuwa wanawake pia wanaweza kulinda bahari. Kama mimi ninaweza kufanya kazi hii, wengine pia wanaweza.”
Hata hivyo, anasema uzamiaji umemfundisha nidhamu, uvumilivu na ujasiri.

Kwa Atuwa, ishara hizo ndogo za kurejea kwa uhai zina maana zaidi ya uhifadhi wa mazingira.
Asifiwa kwa ujasiri wake
Abdul Dunia, mkazi wa Kaskazini Unguja, anasema wanawake wa aina ya Atuwa ni wachache visiwani humo, kwani anaamini kuwa kuzamia si kazi nyepesi hata kwa wanaume kama ilivyo dhana ya wengi.
Bakari Jaha, ambaye amekuwa akifanya kazi kwa muda mrefu na Atuwa, anasema: “Ni mwanamke jasiri, mpambanaji na mwenye kujali mazingira.”
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi, Zanzibar, iliyo na wakazi milioni 1.89, kati ya wakazi hao, 974,281 ni wanawake.
Tano Ame Haji, mzazi wa Atuwa, anasema kuwa mwanaye ni msichana anayejitahidi kufikia malengo yake. Mama huyo anasema: “Alipata fursa ya kuzamia kurejesha matumbawe, akaishikilia na anaifanyia kazi kwa kujituma kwani ina faida kwa vizazi vijavyo.”
Picha ya bango: Atuwa akiwa kazini kurekebisha matumbawe kwenye bahari ya kisiwa cha Mnemba, Zanzibar. Picha kwa hisani ya Atuwa Omari.
