- Upande wa mashtaka wadai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
- Hakimu aamuru hati ya kumfikisha mshtakiwa mahakamani itolewe.
- Mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili.
Raia wa Korea Kaskazini Un Hyok Ra (37), anayekabiliwa na mashtaka ya kukutwa akimiliki nyara za serikali ambazo ni vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya TSh6.4 bilioni anaendelea kusota rumande kufuatia upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Kesi hiyo imetajwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Hata hivyo mshtakiwa hakuwepo mahakamani.
Un Hyok Ra anakabiliwa na mashtaka mawili: kukutwa akimiliki nyara za serikali na kujihusisha na biashara hiyo.
Akiwakilisha upande wa Mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Florida Wancelaus amemwambia Hakimu Mkazi Mkuu Salome Mshasha anayesikiliza kesi hiyo kuwa upelelezi bado haujakamilika na akaomba shauri lipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mshasha baada ya kusikiliza hoja za upande wa Mashtaka, aliamuru hati ya kumfikisha mshtakiwa mahakamani itolewe ili kesi itakapotajwa Juni 9, 2026, mshtakiwa aletwe kortini.
Awali, ilidaiwa katika hati ya mashtaka kuwa Ra, ambaye ni mkazi wa Mikocheni, Dar es Salaam, Aprili 19, 2026, katika eneo la Hoteli ya Golden Tulip, Masaki, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, alikutwa akimiliki nyara za serikali ambazo ni vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya TSh6,476,534,750 ($2,481,433) mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali wala leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika shtaka la pili, Ra anatuhumiwa kuwa tarehe hiyo na mahali hapo, alijihusisha na biashara haramu ya nyara za serikali kwa kuuza vipande 504 vya meno ya tembo vyenye thamani ya TSh6,476,534,750 ($2,481,433) mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali au leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza mapema mwezi Mei na mshtakiwa alikana mashtaka hayo na kurudishwa rumande.
Mshtakiwa huyo hakuwa na wakili. Nchini Tanzania, kumiliki meno ya tembo bila kibali ni kosa la uhujumu uchumi. Kisheria, tembo ametambuliwa kama mnyama wa kuwindwa na nyara zake ni mali ya serikali.
Hivyo, kisheria, kumiliki, kununua, kuuza au kusafirisha nyara hizo bila kibali ni kosa linaloweza kusababisha adhabu ya kifungo cha muda mrefu na/au faini kubwa, pamoja na makosa mengine ya jinai chini ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori (Wildlife Conservation Act, No. 5 of 2009).
Picha ya bango: Craig, tembo maarufu wa Amboseli mwenye pembe kubwa za kipekee (‘Super Tusker’), aliyefariki Januari 2026. Nchini Tanzania, kumiliki meno ya tembo bila kibali ni kosa la uhujumu uchumi. Kisheria, tembo ametambuliwa kama mnyama wa kuwindwa na nyara zake ni mali ya serikali. Picha na Elodie Toto, Mongabay.