- NuPEA ya Kenya imetangaza kampeni mpya za uelimishaji wa umma kuhusu mradi wa nyuklia wa Sh500 bilioni unaopangwa Siaya, ili kushughulikia wasiwasi wa usalama, haki za ardhi na maisha ya wananchi kabla ya ujenzi kuanza.
- Shirika hilo limesema halitaanza ujenzi wa mradi huo hadi jamii ya Siaya ielimishwe kikamilifu na ikubaliane nao, likiahidi kubadilisha mkakati kutoka kampeni za kitaasisi kwenda uhamasishaji wa wananchi wa vijijini.
- Wakazi wa Sakwa, Bondo wameandamana kupinga mradi huo, wakihofia athari kwa ikolojia ya Ziwa Victoria, riziki zao na upatikanaji wa chakula endapo mazingira yatachafuliwa.
- Wakosoaji na baadhi ya wataalamu wa nishati wameonya kuhusu mradi huo, wakisema nishati jadidifu ni salama na ya haraka zaidi, huku nyuklia ikihitaji muda mrefu na inaweza kuathiri mazingira na bioanuwai ya eneo la Ziwa Victoria.
Nuclear Power and Energy Agency (NuPEA) ya Kenya imetangaza mipango ya kufanya kampeni mpya za wazi, madhubuti na za ngazi mbalimbali za uelimishaji wa umma ili kutafuta muafaka juu ya wasiwasi uliopo kuhusu usalama wa nishati ya nyuklia, haki za ardhi, na maisha ya wananchi kabla ya kuanza kwa ujenzi wa mradi wa nishati ya nyuklia wenye thamani ya shilingi bilioni 500 za Kenya katika kaunti ya Siaya.
“Kama wakala wa nishati ya nyuklia, tunasikia na kuheshimu sauti za wakazi wa Siaya. Ushiriki wa umma si jambo la kufuata taratibu tu. Ni haki ya kikatiba,” shirika hilo lilisema katika taarifa yake.
Taarifa hiyo ilitolewa siku mbili baada ya wakazi wa Sakwa, Bondo katika Kaunti ya Siaya inayopakana na Ziwa Victoria, kuandamana kupinga mradi huo. Wakazi hao walieleza hofu kuhusu hatari za kimazingira iwapo ziwa hilo kubwa zaidi lenye maji safi barani Afrika na lenye utajiri mkubwa wa ikolojia litachafuliwa. Pia walitaja hofu ya kupoteza riziki, chakula na mahitaji mengine muhimu.
Katika taarifa yake ya kujibu maandamano hayo, iliyotiwa saini na Afisa Mkuu Mtendaji wa NuPEA, Justus Wabuyabom, shirika hilo lilisema kuwa ujenzi wa mradi huo hautaanza hadi wakazi wa Siaya waelimishwe kikamilifu na wakubaliane na mradi huo.
NuPEA kubadili mkakati
NuPEA iliongeza kuwa itabadilisha mkakati wake “kutoka mipango ya kitaasisi ya ngazi za juu kwenda katika uhamasishaji wa kina kwa wananchi wa vijijini” kuhusu mradi huo unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,000.
Wakati huohuo, Power Shift Africa (PSA) imekosoa msisitizo wa kutumia nishati ya nyuklia kama chanzo cha umeme, ikisema kuwa hatua hiyo inaweza kuondoa umakini na rasilimali kutoka kwa suluhisho za nishati jadidifu ambazo ni safi zaidi, salama zaidi, na rahisi kutekelezwa kwa haraka, ambazo Kenya tayari inazo kwa wingi.
Katika taarifa iliyotumwa kwa Mongabay, Mkurugenzi wa PSA, Mohamed Adow, alisema: “Pia kuna suala la muda mrefu unaohitajika kujenga na kuanza kuendesha mtambo wa nyuklia. Hili linaweza kuchukua kati ya miaka 10 hadi 15. Kwa kulinganisha, mtambo wa nishati ya jua wa megawati 55 huko Garissa ulikamilika ndani ya mwaka mmoja tu. Ikiwa kweli tunahitaji kuwafikishia watu umeme kwa kasi kubwa, basi hatupaswi kutazama mbali zaidi ya nishati jadidifu.”
Awali, Rais wa Kenya, William Ruto, aliwahakikishia wananchi juu ya usalama wa mradi huo mkubwa wa nishati.
Mwanzoni, mradi huo ulipangwa kujengwa Kilifi, eneo la pwani, lakini baadaye ukahamishiwa kaunti ya Siaya. Timu ya NuPEA pia imewahi kufanya mashauriano na wadau pamoja na jamii za Siaya ili kuwashawishi kukubali wazo la mradi wa nishati ya nyuklia.
Ziara kwa Spika
Mnamo Februari, ujumbe kutoka NuPEA na Shirika la Kuzalisha Umeme Kenya (KenGen) ulifanya ziara ya heshima kwa Spika wa Bunge la Kitaifa la Kenya kwa lengo la kujadili Sheria ya Udhibiti wa Nishati ya Nyuklia, kuimarisha “ushirikiano wa kitaasisi na msaada wa sera kwa programu ya nishati ya nyuklia,” pamoja na “kumjulisha Spika kuhusu hatua muhimu zilizofikiwa katika utekelezaji wa ramani ya maendeleo ya nishati ya nyuklia ya Kenya na uratibu wa taasisi unaohitajika ili kufanikisha ujenzi wa mtambo wa kwanza wa nyuklia nchini.”

Hata hivyo, Mohamed Adow anaonya kuwa: “Ripoti ya mwaka 2024 ya Taasisi ya Council on Strategic Risks, ilibaini kwamba kupungua kwa bioanuwai katika bonde la Ziwa Victoria kunaweza kusababisha migogoro, kuyumba kwa uchumi, uhamaji wa watu na ukosefu wa usalama kote Afrika Mashariki. Tayari, kupungua kwa idadi ya samaki, uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa ikolojia vinatishia maisha ya watu, mshikamano wa kijamii na utulivu wa kikanda. Mamilioni ya watu wanaoishi kandokando ya ziwa hili wanahitaji ulinzi wa mazingira, si alama ya fahari ya nishati.”
Alhamisi, wakazi wa Sakwa, eneo la Bondo katika Kaunti ya Siaya, kwa usaidizi wa mashirika ya kiraia, baadhi ya viongozi wa eneo hilo pamoja na wanamazingira, waliandamana mitaani kupinga mradi huo.
Wakosoaji wa mradi huo wameeleza hofu kuhusu hatari ya mionzi ya nyuklia ambayo inaweza kuhatarisha mazingira na jamii zinazoishi karibu na mradi huo, pamoja na madhara ya muda mrefu kwa ikolojia ya Ziwa Victoria linalopatikana Kenya, Uganda na Tanzania, na ni eneo muhimu la kuzaliana kwa samaki na viumbe wengine wa majini. Hivyo, ni chanzo muhimu cha chakula, maji na riziki kwa jamii nyingi za wavuvi wanaolizunguka.
“Hatupingi maendeleo, lakini sote tunajua madhara yanayoweza kutokea kufuatia uwepo wa mtambo wa nyuklia. Ukaribu wa Siaya na ziwa hauwezi kupuuzwa. Tunajua yaliyotokea wakati wa milipuko ya mabomu ya atomiki ya Hiroshima na Nagasaki. Huwezi kusema tunachochewa. Tunaukataa mradi huu,” alisema mwanamume aliyejitambulisha kama Davis Omanga.
Wanaounga mkono mradi huo wa nishati wanakiri kuwa mfumo wa sasa wa mchanganyiko wa nishati nchini Kenya ni imara na endelevu, lakini wanasema unakabiliwa na changamoto za kimuundo ambazo haziwezi kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme yanayoongezeka kwa asilimia 5 hadi 7 kila mwaka.
Changamoto ya umeme wa maji
“Umeme wa maji bado uko hatarini kutokana na mabadiliko ya tabianchi, huku nishati ya upepo na jua hutegemea mabadiliko ya hali ya hewa. Aidha, upanuzi wa nishati ya jotoardhi unakwamishwa na gharama kubwa za uwekezaji pamoja na vikwazo vya kijiografia,” alisema Kefa Seda, Mkurugenzi Mkuu wa PPP wakati wa mkutano wa kimataifa kuhusu nishati ya nyuklia uliofanyika Nairobi mwezi Machi.
Mradi huo wa nishati kwa sasa uko katika hatua ya upangaji na ushirikishwaji wa wadau, huku Rais wa Kenya, William Ruto, akidokeza kuwa ujenzi wake unaweza kuanza mwaka 2027.
Mbali na kuongeza uzalishaji wa nishati, serikali imeahidi kupunguza gharama za umeme pamoja na kuongeza nafasi za ajira. Mwezi uliopita, Gavana wa kaunti ya Siaya, James Orengo aliunga mkono mradi huo kwa masharti, akisisitiza kuwa jamii ya eneo hilo lazima iridhie ujenzi wake.
Awali, serikali ilitaka mradi huo utekelezwe katika ukanda wa pwani ya Kenya, lakini upinzani uliochochewa na masuala ambayo hayakuwa yametatuliwa, ulisababisha kuhamishwa kwake. Baadhi ya waandamanaji walihoji hatua hiyo.

“Kwa nini Siaya? Kwa nini? Mradi huu ulipaswa kujengwa pwani,” alisema Donnah Akuku, aliyejitambulisha kama muuzaji wa samaki.
Kwa sasa, mradi huo ambao serikali inasema utatekelezwa “kwa awamu kulingana na viwango bora vya kimataifa”, bado uko katika hatua ya upangaji na ushirikishwaji wa wadau. Hata hivyo, maandamano hayo yanaashiria kwamba kukubalika kwa mradi huo kwa wananchi kutakuwa muhimu sawa na uwezekano wa kiufundi katika kuamua hatima yake.
Mpango wa Kenya Energy Transition and Investment Plan unaonyesha dhamira ya Kenya kuendelea kutegemea kwa kiasi kikubwa nishati jadidifu.
Mohamed Adow ana maoni kwamba: “Kenya haina upungufu wa nishati jadidifu, bali changamoto ya upatikanaji wa nishati, gharama zake na usambazaji wake. Suluhisho lipo katika kupanua nishati jadidifu zinazozalishwa karibu na wananchi, kuimarisha miundombinu ya gridi ya taifa, na kuwekeza katika mifumo ya nishati inayozingatia jamii’’.
Akitumia mfano wa mradi mdogo wa nishati wa Elan katika kaunti ya Garissa, anasema: “Tunachokataa ni kuhatarisha mustakabali kwa kutegemea nishati ya nyuklia yenye hatari kubwa karibu na moja ya mifumo muhimu zaidi ya ikolojia ya maji safi barani Afrika.”
Picha ya bango: Ufukwe wenye shughuli nyingi wa Ziwa Victoria katika Ufukwe wa Usenge, Bondo, Kaunti ya Siaya mnamo Mei 2, 2026. Wanaopinga mradi uliopendekezwa wa nishati ya nyuklia unaotarajiwa kujengwa katika Kaunti ya Siaya karibu na ziwa hili wametaja hatari kwa ikolojia ya ziwa hilo, chanzo chao cha riziki na chakula. Picha na Lynet Otieno, Mongabay.