- Mwongozo utaelekeza namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
- Elimu itatolewa kuhusuuvuvi na ufugaji unaostahimili mabadiliko ya tabianchi.
- Mradi wa Bandari ya Uvuvi ya Bagamoyo bado unafanyiwa tathmini ya mazingira.
Ili kuhakikisha shughuli zinazofanywa na sekta ya mifugo na uvuvi zinazingatia uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali, serikali ya Tanzania imepanga kuandaa mwongozo utakaoweka mikakati ya uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Bashiru Ally, amesema mpango huo wa kwanza wa usimamizi wa mazingira utakaotekelezwa kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2027/2028 hadi 2032/2033, pia utatoa miongozo kuhusu matumizi endelevu ya rasilimali na namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2026/2027 ya wizara yake, akiwa katika kikao cha bajeti kinachoendelea katika makao makuu ya nchi, Dodoma, Bashiru alisema katika kipindi cha mwaka 2026/2027, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pia imepanga kufanya tathmini ya athari za mazingira katika miradi ya ujenzi wa minada ya mifugo, mialo na masoko ya samaki.
Kwa mujibu wa Bashiru, mpango mwingine utakaofanywa na wizara yake katika kipindi cha mwaka wa fedha 2026/2027 ni kutoa elimu kwa wafugaji na wavuvi 1,000 katika ukanda wa pwani, kaskazini na nyanda za juu kusini kuhusu utunzaji wa mazingira kwa uvuvi na ufugaji unaostahimili mabadiliko ya tabianchi.
“Vilevile, Wizara itaendelea kufanya tathmini ya athari za mabadiliko ya tabianchi na kuandaa mpango wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa ukanda wa pwani,” alisema Bashiru.
Alisema katika mwaka 2026/2027, wizara yake itafanya ukaguzi wa mazingira kwa miradi 10 ya uwekezaji katika sekta za mifugo na uvuvi ili kuhakikisha uzingatiaji wa sheria, kanuni na miongozo ya usimamizi wa mazingira.
Pia, wizara hiyo itaendelea na utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, pamoja na kuanzisha Mtandao wa Blue Carbon Tanzania kwa jamii katika ukanda wa pwani, alisema Waziri.
Viashiria vya hatari za mabadiliko ya tabianchi
Waziri aliongeza kuwa katika kipindi hicho cha mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara pia itafanya tathmini ya viashiria vya hatari za mabadiliko ya tabianchi katika shughuli za uvuvi katika Ukanda wa Pwani kwa lengo la kuandaa mpango wa kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi utakaoimarisha ustahimilivu wa Sekta ya Uvuvi na jamii zinazotegemea rasilimali za bahari
“Wizara, katika kutekeleza matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake, inaendelea na tathmini ya athari kwa mazingira na jamii zinazoweza kusababishwa na mradi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Bagamoyo. Mradi huo unalenga kubaini na kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza. Tathmini hiyo imefikia asilimia 25.”
Wakitoa maoni kuhusu hotuba ya Waziri, baadhi ya wadau wamesema hotuba hiyo imefanikiwa kuainisha vipaumbele na kugusa maeneo mengi muhimu katika sekta hiyo.
Ernest Masunga, msambazaji wa madawa ya mifugo katika mkoa wa Kigoma amesema bajeti hiyo ikiwa itatekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele mbalimbali vilivyoainishwa, itasaidia kuongeza tija katika sekta hiyo.
“Vipaumbele kama kuongeza uzalishaji, kuimarisha masoko na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi, pamoja na kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za sekta hizo, ni maeneo muhimu ambayo yakitekelezwa kikamilifu, yatabadilisha maisha ya wafugaji na wavuvi,” amesema Masunga.
Marco Sekivundi, ambaye kitaaluma ni mtaalamu wa mifugo, amesema ili mipango na mikakati mizuri iliyoainishwa na wizara, ifanikiwe na kuleta tija kwa wafugaji na wavuvi nchini, ni muhimu maeneo ya utafiti na mafunzo yazingatiwe na kutekelezwa kwa vitendo.
Picha ya bango: Katika jitihada za kuimarisha uzalishaji wa malisho ya mifugo na kuongeza uwezo wa wafugaji kukabiliana na athari za ukame, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Kaskazini imefanikiwa kujenga bwawa lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 1.2 za maji kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji katika eneo la shamba darasa la uzalishaji wa malisho ya mifugo. Picha kutoka Maktaba ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.