- John Maghanga, “John wa Nyoka,” amebadilika kutoka kuwaua nyoka hadi kuwa mhamasishaji wa kuishi nao kwa amani kupitia SCAN, akielimisha jamii kuhusu kujikinga na kuumwa na nyoka.
- Kupitia SCAN, amefikia zaidi ya watu 2,000 na kutoa mafunzo katika shule zaidi ya 20, huku akihamisha nyoka zaidi ya 100 kutoka maeneo ya makazi kwenda hifadhi.
- Jamii za Taita Taveta bado zinakumbwa na changamoto za kuumwa na nyoka, ikiwemo upungufu wa antivenom, huduma duni za afya na ucheleweshaji wa matibabu unaochangia vifo na majeraha.
- Wataalamu wanasisitiza elimu, miundombinu bora ya afya na fidia kwa waathiriwa, wakibainisha kuwa nyoka wana mchango muhimu katika ikolojia na hawapaswi kuuawa kiholela.
Kama wanajamii wengine katika vijiji vya milima ya Taita, John Maghanga, maarufu kama John wa Nyoka, aliwaogopa nyoka akiamini kuwa wanapaswa kuuawa pindi wanapoonekana.
Mwaka 2019, akiwa katika ziara zake msituni katika milima ya Taita, Maghanga alimgusa nyoka kwa mikono yake kimakosa. Alijawa na hofu akijiuliza: “Kama angeniuma ingekuwaje?”
Kabla ya nyoka huyo kuteleza na kupotelea mitini, Maghanga alichukua simu na kupiga picha yake, aliyochapisha kwenye Facebook. Lengo lake lilikuwa kufahamu mengi kuhusu nyoka huyo. Alistaajabu kugundua kuwa nyoka huyo alikuwa mwenye sumu kali.
Mongabay ilimtembelea Maghanga na kumpata akiwa ametoka kuhamasisha wanajamii kuhusu nyoka na jinsi ya kuishi nao kwa amani.
Alielezea jinsi tukio hilo lilibadili mienendo yake: “Baada ya tukio hilo, uoga wangu kwa nyoka ulianza kufifia, na polepole nikataka kufahamu zaidi kuwahusu. Sasa mimi ni mshauri na mtaalamu wa kukamata nyoka na kuwahamisha sehemu salama.”

Katika vijiji vilivyo milimani na tambarare zinazopakana na mbuga za wanyama za Tsavo Mashariki na Tsavo Magharibi, kusini mashariki mwa Kenya, wengi wamepoteza maisha kwa kukosa huduma muhimu kwa upesi na wengine kuachwa na makovu ya ulemavu. Migogoro kati ya binadamu na nyoka mara nyingi hutokea katika msimu wa mvua, wanyama hao wanapotoroka hifadhi zao na kutangamana na binadamu.
Katika maeneo yaliyopakana na mbuga za wanyamapori za Tsavo Mashariki na Tsavo Magharibi, binadamu pia huwaua nyoka kiholela, kutokana na uoga wa kuumwa, japo si nyoka wote ni hatari.
Kupitia shirika la Snake Community Action Now (SCAN) Maghanga sasa anahamasisha umma jinsi ya kuepuka kuumwa na nyoka, hatua za kuchukua mtu anapoumwa, na kwa nini nyoka hafai kuuawa kiholela. Pia amekuwa akihamasisha kuhusu manufaa ya nyoka katika ikolojia.
Tangu mwaka 2021, Maghanga ametoa mafunzo kuhusu nyoka katika zaidi ya shule 20, na kufikia watu zaidi ya 2,000 kupitia mabaraza ya vijiji na makanisa. Pia amewahamisha nyoka zaidi ya 100 kutoka vijijini hadi hifadhi, hatua inayolenga kuchangia katika juhudi za kupunguza visa vya kuumwa na nyoka katika Afrika Mashariki kwa asilimia 50 kufikia mwaka 2030.
“Tulikuwa tukiambiwa nyoka ni hatari, ni adui na ni ishara ya uchawi kwa yeyote anayejihusisha nao. Kila nilipoona nyoka, nilimuua bila kufikiri mara mbili,” anasema Maghanga.
Makovu ya nyoka
Katika kijiji cha Kishushe, Elizabeth Mwakilemba, mama wa watoto wanne, anaelezea jinsi mwanawe Joseph Mwakilemba, akiwa na miaka minane wakati huo, alivyoumwa na nyoka kifutu (puff adder) mwaka 2022, akiwa na wenzake wakiokota kuni karibu na makazi yao.
“Alipelekwa zahanati iliyo karibu, ila hakukuwepo dawa ya kuzuia sumu ya nyoka. Tulielekezwa katika hospitali ya rufaa ya Moi, kilomita zaidi ya 60 kutoka Kishushe. Hapo tulikaa siku chache kabla ya kutumwa tena Hospitali Kuu ya Mkoa wa Pwani, yenye umbali wa kilomita zaidi ya 155. Mwishowe kijana alipata nafuu,” alisema Mwakilemba.
Alisema walimwita Maghanga aje kuwasaidia, ila hakuweza kuwafikia kwa wakati, kutokana na topografia ya maeneo ya Taita, na ukosefu wa usafiri wa haraka. Baadaye Maghanga alifika eneo alikokuwa nyoka huyo na kuwathibitishia kuwa alikuwa nyoka kifutu.
“Wazee wa zamani wangekuwepo wakati huo kijana akiumwa na nyoka, angepewa tiba ya kitamaduni iliyojulikana kama kinonga. Ila kwa sasa hawapo,” Mwakilemba alisema.
Mongabay ilidadisi ili kufahamu iwapo Mwakilemba alimjua yeyote aliyewahi kuumwa na akatibiwa kitamaduni. Kwa tabasamu usoni, alisema hajawahi kuona. Ni hadithi aliyosikia alipokuwa akikua na akasadiki tetesi hizo.
Kilomita chache mwendo wa kama nusu saa kutoka kwa Mwakilemba, tuliwasili nyumbani kwa Erustus Msafiri, na kumpata akiwa amepumzika pamoja na mkewe. Wao pia walipitia masaibu hayo hayo, kwani mtoto wao wa kike, Pili Msafiri, aliumwa na nyoka mkononi, akiwa amelala.

“Tulishangaa sana kugundua kuwa nyoka ambaye Maghanga alimthibitisha kuwa kobra anayemwaga sumu (red spitting cobra) aliingia kitandani na kumuuma mtoto wetu akiwa amelala. Wenzake walidhani ni nge aliyemuuma. Watoto hao walikimbia kwa jirani kuomba dawa ya nge, kisha jirani akawauliza ikiwa walikuwa wamemuua, na wakasema la. Wote waliandamana hadi chumba walicholala, na baba yao aliyekuwa chumba tofauti pia akatoka. Walipomulika kwa tochi, wakaona nyoka huyo amejisokota chini ya kitanda. Majirani walimuua,” alisema Msafiri.
Familia na majirani walifurahi kuwa mtoto wao aliponea. Walikuwa wamekata tamaa wakati walikosa dawa ya sumu ya nyoka katika zahanati iliyo karibu. Baadaye mtoto alitibiwa katika hospitali ya Wesu.
Mongabay ilitafuta kufahamu iwapo wamefuatilia kupata fidia, ila walielezwa na maafisa wa shirika la KWS kuwa halina uwezo wa kufuatilia masuala hayo kwa niaba ya wananchi, baada ya mpango huo wa kutoa fidia kusitishwa.
“Shirika la KWS halina uwezo, ila kuna kamati inayohusika na masuala hayo, ambapo shirika hilo lina mwakilishi mmoja tu. Hivyo ni lazima umma, wajumbe wa wananchi pamoja na kamati hiyo washirikiane kutafuta sera za fidia ya nyoka kwa wanajamii,” aliongezea Maghanga.

Kilomita zaidi ya 80 kutoka nyika zilizokauka za Kishushe, kwenye tambarare ya Voi, katika kijiji cha Kasarani, kaunti ya Taita Taveta, tulikutana na Erick Mwamburi na wanawe. Huzuni ilitanda nyusoni mwao wakitafakari kifo cha mpendwa wao baada ya kuumwa na nyoka mwezi Machi mwaka 2026.
“Tulikuwa shambani mwetu, nyuma ya nyumba yetu ambapo tumeishi kwa zaidi ya miaka 13, wakati nyoka mrefu alipita karibu nasi. Tuliamua kupambana naye. Ghafla alipita karibu nami, kisha akarukia mke wangu na kumuuma pajani kabla ya kuzama shimoni,” alisema Mwamburi.
Mwamburi alielezea kuwa walipata changamoto ya usafiri kutoka nyumbani hadi hospitali. Wakiwa wanatembea, walikutana na jirani aliyewakimbiza hospitalini kwa gari lake. Kwa bahati mbaya, mke wake alifariki akiendelea kupata matibabu.
Maghanga anasema kutembea kwa mama huyo baada ya kuumwa kulichochea sumu ya nyoka kusambaa mwilini kwa kasi. “Wangekuwa na ufahamu, wangemkalisha chini na kutafuta usaidizi wa haraka,” alisema Maghanga.
Maghanga alithibitisha kuwa nyoka huyo alikuwa mamba mweusi (black mamba). Nyoka huyo anaweza kufikia urefu wa zaidi ya futi nne, na ni mwenye sumu kali inayosababisha kifo ndani ya saa chache. Pia ni nyoka mwenye kasi zaidi duniani.
“Black mamba akitishiwa na kuhisi hatari, yeye hujitetea kwa kuuma. Mara nyingi ukijaribu kumdhuru yeye hutafuta namna ya kujilinda. Aidha, kwa sababu ya urefu wake, black mamba huinua nusu ya mwili wake, hivyo kujitetetea kwa upesi zaidi. Kufumba na kufumbua, yeye huwa tayari ameuma. Hivyo tunahimiza wananchi muda wowote wanapoona nyoka, wasijaribu kuua, bali wamwondokee,” alisisitiza Maghanga.
Familia zilizopata majeraha au kupoteza wapendwa wao kwa kuumwa na nyoka zinaendelea kulilia haki, na zinataka fidia. Kwa sasa, Kenya haina mfumo wa serikali wa kutoa fidia kwa waathiriwa wa kuumwa na nyoka. Chini ya Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori ya Kenya ya mwaka 2013, fidia hutolewa tu kwa majeraha au vifo vinavyosababishwa na spishi maalum za wanyamapori zilizoorodheshwa. Fidia za waathiriwa wa kuumwa na nyoka ziliondolewa katika orodha ya zile zinazotokana na migogoro ya wanyamapori na binadamu baada ya marekebisho yaliyofanywa kwa sheria hiyo mwaka 2019.
KWS na wengine wanasemaje?
Naibu Mkurugenzi wa KWS eneo la Tsavo Conservation Wilson K Njue alielezea Mongabay kwamba fidia ya nyoka iliondolewa katika kitengo cha tatu (Third Schedule), Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori ya mwaka 2013, ambayo inaainisha ni wanyamapori gani wanaosababisha uharibifu na aina ya fidia inayofaa kulipwa.
“Fidia ya nyoka iliondolewa kufuatia tuhuma za ufisadi kwa wahusika pamoja na kutolewa kwa maelezo ya uongo kutoka kwa jamii, kuwa wameumwa na nyoka. Kinachoendelea sasa ni mazungumzo kuona iwapo wanaoumwa na nyoka au kufa kutokana na hilo wanapewa fidia, ila ni jambo la kusubiria,” alisema Njue.
Wanyama walioorodheshwa kutolewa fidia iwapo wanasababisha madhara kwa binadamu ni ndovu, simba, chui, fisi, kifaru, kiboko, mamba, ngiri, mbwa mwitu, papa, na nyati, miongoni mwa wengine.
Wakili kutoka shirika la African Wildlife Foundation Benson Kasyoki anasema: “Ni vyema kurudisha fidia hizo za nyoka kwa jamii. Lakini fidia hizo zirudishwe kwa mipangilio maalum ya kuweza kukabili ulaghai na uongo kutoka kwa jamii”.
Kasyoki, hata hivyo, anaitaka serikali na mashirika binafsi kuhakikisha kuna dawa ya kutosha ya sumu ya nyoka wa aina zote, pamoja na kudhibiti migongano kati ya binadamu na nyoka kwa kutoa elimu mahususi ya mnyama huyo.
“Shirika la KWS lina jukumu la kuhakikisha linaandaa kampeni kabambe kote nchini, haswa maeneo yaliyoko na hatari zaidi, kuhusu uhifadhi wa nyoka na kuzuia kuumwa,” aliongeza wakili huyo.
Pia kumekuwa na juhudi za kujaribu kurudisha fidia za kuumwa na nyoka katika orodha hiyo, ikiwemo misukumo na viongozi mbalimbali.

Data ya WHO ya mwaka 2023 inakadiria kuwa watu milioni 5.4 huumwa na nyoka kila mwaka ulimwenguni, huku kati ya milioni 1.8 na milioni 2.7 wakiachwa na makovu ya kudumu. Wengine 100,000 huaga dunia.
Umuhimu wa nyoka
Patrick Malonza, ambaye ni mwanabiolojia wa uhifadhi wa bioanuai, mtaalamu na mtafiti wa viumbe hai, anasema nyoka wanastahili kulindwa kama viumbe wengine, kwa sababu manufaa yao ni mengi katika mazingira.
“Nyoka wanasaidia kukabiliana na panya na wadudu wengine waharibifu katika ikolojia, kwa kudhibiti idadi yao, sababu panya na wadudu wengine wagugunaji huzaana kwa wingi na huguguna vyakula haswa vya mbegu, na kuleta hasara kwa wakulima mashambani, na pia kuathiri usalama wa chakula. Sumu yake hutumiwa kutengezea dawa za kuzuia sumu ya nyoka,” anasema Dkt Malonza.
Malonza anasema nyoka, haswa wale wadogo, pia huwa chakula kwa ndege kama mwewe, tai, na nguchiro. Pia nyoka husaidia kupunguza magonjwa ambukizi kwa kuwala wadudu ambao hubeba virusi vya maradhi mbalimbali. Malonza anasema kuwa nyoka pia husaidia kutambua mazingira iwapo yamechafuliwa na kuharibiwa, ambayo ndiyo makaazi yao.
Takwimu iliyochapishwa mwaka 2021 inaonyesha nyoka wana manufaa mengi katika ikolojia, ikiwemo kupunguza idadi ya panya na wadudu waharibifu kwa ukulima. Inathibitisha aliyoyasema Malonza.
Changamoto za kukabiliana na kuumwa na nyoka
Maghanga alieleza uwepo wa changamoto nyingi zinazoweza kuangaziwa na kudhibitiwa. “Miundombinu duni, ukosefu wa huduma ya kwanza karibu na jamii, ukosefu wa wataalamu walio na ujuzi wa nyoka, uhamasishaji mdogo kwa jamii kuhusu hatua za kuchukua mtu anapoumwa na nyoka; ni baadhi ya changamoto zinazochochea vifo na ulemavu unaotokana na kuumwa na nyoka,” alielezea Maghanga.
Anasema changamoto hizi zinaweka wazi mianya iliyopo katika sekta za afya, licha ya serikali na washirika mbalimbali ulimwenguni kuweka mikakati ya kukabiliana na vifo vinavyotokana na kuumwa na nyoka.
Vile vile, anataja mbinu kadha wa kadha na rahisi, zinazoweza kutumiwa ili kuepuka madhara ya nyoka. “Kwanza ni kusafisha miji, na kutoacha mazingira yanayoweza kuwafanya nyoka kujificha, kuziba mianya ya nyumba vizuri, kutupilia mbali tiba za kitamaduni, kutumia tochi usiku na kutolala chini usiku. Huku kutazuia, kwa asilimia kubwa, kuumwa na nyoka,” anasema Maghanga.
Mongabay ilitaka kufahamu hatua za kuchukua mtu anapoumwa na nyoka. “Kitu cha kwanza, ukiona nyoka, kaa mbali naye. Ikiwa nyoka amekutemea mate machoni, osha kila jicho peke yake kutumia maji mengi kwa dakika 15-30. Funika macho kwa kitambara kutokana na kuwasha. Fika hospitali kwa uangalizi zaidi.
“Ukiumwa na nyoka usitembee; tulia ulipo ili kupunguza kasi ya kusambaa kwa sumu mwilini. Itisha usaidizi wa matibabu. Toa mapambo mwilini, kama vile saa, ushanga, na pete. Ukiweza, nakili saa uliyoumwa na nyoka. Kunywa maji mengi kuzuia kiu, na usitumie mbinu zozote za kiasili kutibu sumu ya nyoka kama vile chumvi, makaa, kuweka barafu au kuchanja au kunyonya damu ulipoumwa,” Maghanga aliiambia Mongabay.
Akizungumza na Mongabay, Zablon Mbogori, mkurugenzi mkuu wa shirika la SCAN, Kenya, alieleza kuwa ukosefu wa dawa sahihi ya sumu ya nyoka, wauguzi wasio na ufahamu wa nyoka, miundombinu duni, na ukosefu wa hamasa kwa umma, ni baadhi ya changamoto zinazoongeza vifo vinavyotokana na kuumwa na nyoka.

“Dawa zinazotumika sasa nchini Kenya zinaagizwa kutoka India na Ulaya. Hakuna dawa zinazopatikana hapa nchini, hivyo kulazimu taifa kuagiza kutoka nchi zingine. Kwa kuwa kila sehemu zina nyoka wa kipekee, dawa hizo si sahihi. Kuna uhaba wa wahudumu wanaofahamu sumu za nyoka na kutoa huduma za kwanza,” aliongeza Mbogori.
Mongabay ilipata mashirika mengine ambayo yanatoa dawa hizi kutoka Afrika Kusini, Mexico na India.
Mbogori alisisitiza kuwa hamasa kama inayotolewa na Maghanga kwa jamii vitasaidia kukabiliana na ugonjwa huu uliotelekezwa, jinsi inavyoorodheshwa na shirika la afya duniani WHO, kwa bara la Afrika, katika maelekezo yaliyochapishwa mwaka 2019.
Kenya ina aina zaidi ya 140 za nyoka. Zinazoorodheshwa katika vitengo vya walio na sumu kali (elapids na vipers), walio na sumu ya kiwango cha kati, na wasio hatari kama vile boas na house snakes. Nyoka wenye sumu kali ni pamoja na wanaojulikana kwa Kiingereza kama mambas, cobras, vipers, adders na pythons.
Utafiti wa National Library of Medicine unaonyesha kuwa nchini Kenya, maeneo ya Baringo, Kitui, Tiaty, Kilifi, Kwale, Taita Taveta, Kakamega na Kajiado yanashuhudia visa zaidi vya kuumwa na nyoka.
Changamoto zikabiliwe
Mbogori anapendekeza kulindwa kwa umma pamoja na kupewa fidia kwa wale walioathiriwa na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, jinsi ilivyo ratibishwa katika Katiba ya Kenya, kipengee cha 43, sehemu ya (1),(a), iliyo na jukumu la kulinda maisha ya wanajamii. Ila jukumu la kulipa fidia walioumizwa au kuuawa na wanyamapori ni jukumu la Wildlife Conservation and Management Act.
“Serikali ijaribu iweke dawa ya sumu ya nyoka kwa hospitali za Daraja la Tatu na Nne mashinani katika maeneo yenye visa vingi vya nyoka. Walioumwa na nyoka watibiwe bure, kwa sababu dawa moja ya kutibu sumu ya nyoka ni ghali mno. Katika hospitali za serikali, dawa hiyo hufikia KSh6,500 ($50), na katika hospitali za kibinafsi dawa hiyo hufikia KSh14,000 ($108),” anasema Mbogori.
Data iliyotolewa na Wizara ya Afya katika Kaunti ya Taita Taveta kutoka Kenya Health Information System (KHIS) kuhusu visa vya nyoka nchini Kenya na katika kaunti hiyo kuanzia mwaka 2021 inaonyesha kupungua kufikia mwaka 2026, vingi vikiwa havijanakiliwa.
Data hiyo, ambayo pia imesisitiza kuwa kuumwa na nyoka na sumu yake ni ugonjwa uliopuuzwa wa kitropiki (NTD), unaoleta wasiwasi wa afya ya umma nchini Kenya umeonyesha kuwa mwaka 2021 kulirekodiwa visa 20,987, visa 17,706 mwaka 2022, visa 17,953 mwaka 2023, na mwaka 2024 visa hivyo vikashuka na kufikia 17,184. Mwaka 2025 kulirekodiwa visa 16,924 na mwaka 2026, kukiwa kumenakiliwa visa 3,553 kote nchini kufikia mwisho wa robo mwaka ya kwanza.
Charo Mwambire, mshirikishi mtendaji, kitengo cha magonjwa yasiyoambukiza, Taita Taveta, aliiambia Mongabay kuwa visa vingi vya nyoka vinaweza kuzuiliwa ikiwa jamii itafunzwa mbinu rahisi na sahihi.
Vile vile, anasema: “Mbali na changamoto kama uhaba wa dawa za nyoka, wizara hutayarisha bajeti ya magonjwa yasiyoambukiza, huchukua data za visa vya nyoka kwa maeneo yote kila mwezi na kuituma kila mwanzoni mwa mwezi, kwa halmashauri ya afya, KHIS. Na pia tunatoa mafunzo kwa jamii na wahudumu kama njia za kukabili ugonjwa huu uliotelekezwa”.
Utafiti mwingine, uliochapishwa Disemba 2025, uliopima matukio ya kuumwa na nyoka nchini Kenya, umebaini tofauti kubwa za kijiografia katika visa vinavyoripotiwa kote nchini, huku baadhi ya kaunti zikirekodi kiwango cha matukio kuanzia takriban 3.7 hadi zaidi ya visa 400 kwa kila watu 100,000.
Utafiti huo pia ulikadiria kuwa maelfu ya visa haviripotiwi katika kumbukumbu rasmi za afya, hali inayoonyesha mapengo makubwa katika ufuatiliaji na upatikanaji wa huduma katika ngazi ya jamii. Utafiti huo pia ulionyesha kuwa kuumwa na nyoka hakusambai kwa usawa, huku maeneo ya vijijini na ya kilimo yakibeba mzigo mkubwa zaidi.
Wanaume walibainika kuathirika zaidi kuliko wanawake, hali inayoakisi hatari za kazi zinazohusiana na shughuli za nje kama vile kilimo na ufugaji.
Kwa ujumla, matokeo hayo yalithibitisha kuwa kuumwa na nyoka bado ni changamoto kubwa ya afya ya umma nchini Kenya, lakini iliyopuuzwa, ikiwa na makadirio ya makumi ya maelfu ya visa na zaidi ya vifo elfu moja kila mwaka.
Utafiti huo unatoa wito wa hatua lengwa, upatikanaji bora wa dawa ya kupambana na sumu ya nyoka (antivenom), na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na majibu ya jamii katika maeneo yaliyo hatarini.

Migogoro kati ya binadamu na nyoka
Malonza, ambaye pia ni mtaalamu wa herpetolojia (herpetologist) katika Makumbusho ya Kitaifa ya Nairobi, anasema migogoro kati ya binadamu na nyoka hushuhudiwa zaidi wakati rasilimali kama vile maji na chakula zinapungua.
“Wakati nyoka wanakosa maji na wadudu kama panya msituni, huwafuata ambapo mara nyingi wanapatikana karibu na binadamu kuliko na chakula, na hapo mara nyingi unashuhudia migogoro, hivyo kuweka hatarini maisha ya binadamu na ya nyoka pia,” asema Malonza.
Anaongezea kusema kuwa, msimu wa mvua, mizozo ya binadamu na nyoka huwa kidogo au kukosekana kabisa, sababu rasilimali za maji na chakula hupatikana kwa wingi kwa urahisi, na kila mmoja husalia maeneo yake.
Mtaalamu huyo anahimiza umma kuhifadhi vyema mazingira na vyakula wakati wa kiangazi na kuhakikisha wanaziba mianya, na kukabiliana na wadudu au panya wanaoingia majumbani, kwa sababu nyoka huwafuata kunapokuwa na ukame, hivyo kugongana na binadamu.
Suluhu za kudumu
WHO inasema katika bara la Afrika pekee, kati ya watu 435,000 na 580,000 huumwa na nyoka kila mwaka, huku jamii maskini zilizoko nchi zenye kipato cha chini na cha kati zikiachwa na makovu ya kuumwa na nyoka. Shirika la Conservation Biology limetaja kuuawa kwa nyoka kiholela kuwa sababu kuu ya kupungua kwa idadi yao.
Hata hivyo, si wanajamii wote wanafurahishwa na kazi anayoifanya Maghanga. “Wanafamilia wa karibu nami wanadhani kwa kuhakikisha nyoka hawauawi, ninatumia ushirikina. Katika jamii kumekuwa na dhana potofu ya kuwahusisha nyoka na ushirikina,” Maghanga alisema.
Waliozungumza na Mongabay, kama vile Eliza Walowe, wanasema wanaowashika nyoka lazima wawe wanatumia aina fulani ya ushirikina au uchawi. “Mimi siamini jambo hilo. Wewe fikiria binadamu wa kawaida; unawezaje kumshika nyoka hata kama unatumia fimbo, na atulie hadi ahamishwe? Huoni hicho ni kitu kisichowezekana kwa uhalisia wa maisha? Sitaamini kamwe kuwa anafanya hivyo bure,” alisisitiza Walowe.
Lakini Maghanga hafi moyo wala kupoteza mwelekeo. Anasisitiza: “Suluhu za kudhibiti nyoka hazitoki kwa hospitali au serikalini; suluhu huanza na jamii kubadili fikra na tabia kuhusu mazingira na viumbe hai ili kuweza kuhifadhi binadamu na wanyama pori. Hivyo lazima tufunze jamii mengi zaidi kuhusu nyoka ili tuwe salama na nyoka awe salama”.

Akiwa kielelzo chema, anasema hamasa ya kutosha kuhusu nyoka kwa jamii kuanzia mashinani, ina manufaa kwa jamii binafsi ili kuepukamadhara ya nyoka, kuacha kuua nyoka kiholela na kulinda mazingira na wanyama.
“Tunahitaji wengi wapewe mafunzo ya kuwashika nyoka, tupate vifaa muhimu kama vile gumboots, tochi, miwani maalum, fimbo maalum za kushika nyoka pamoja na pikipiki zitakazowezesha kuwafikia haraka watakaokuwa katika hatari. Dawa pia ziwe kila sehemu. Naamini kuwa kati ya watu 10 watakaopata hamasa hiyo, watatu au watano watabadili mawazo yao kuhusu nyoka na jinsi ya kuishi nao kwa usalama,” alisema Maghanga.
Picha ya bango: Nyoka aliyeuawa katika kijiji cha Kishushe, Taita Taveta. Picha na Linah Mwamachi, Mongabay.