- Wakazi wa Sakwa, Kaunti ya Siaya, waliandamana kupinga mpango wa Serikali ya Kenya kujenga kinu cha nyuklia chenye uwezo wa megawati 2,000 karibu na Ziwa Victoria, wakihofia athari za mazingira na usalama wao.
- Wananchi wameeleza wasiwasi kuhusu usimamizi wa taka za mionzi, uwezekano wa kuhamishwa kutoka ardhi za mababu zao, pamoja na migogoro ya fidia na makazi mapya.
- Jamii za wavuvi zina hofu kuwa ajali au uchafuzi wa mionzi unaweza kuharibu bioanuwai ya Ziwa Victoria, kuathiri mazalia ya samaki na kuhatarisha chakula na uchumi wa eneo hilo.
Mnamo Mei 21, wakazi wa Sakwa Kusini Mashariki mwa Kenya, walikusanyika kupinga mpango wa Serikali wa kujenga kinu cha kuzalisha umeme wa nyuklia karibu na makazi yao, kandokando ya Ziwa Victoria.
Sakwa, iliyopo katika kaunti ya Siaya, ni makazi ya jamii ya Waluo na iko kwenye mwambao wa ziwa hilo kubwa zaidi lenye maji safi barani Afrika, ambalo linapatikana Kenya, Uganda na Tanzania.
Mwisho wa Machi 2026, wakati wa kongamano la kimataifa kuhusu nishati ya nyuklia, Rais wa Kenya William Ruto alitangaza ujenzi wa kinu cha nyuklia chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,000 katika eneo hilo.
Kwa sasa hakuna taarifa rasmi kuhusu mpango huo kwenye tovuti ya Nuclear Power and Energy Agency (NuPEA). Hata hivyo, Ruto alisema ujenzi utaanza mwaka ujao na kinu hicho kinatarajiwa kuanza kuzalisha umeme mwaka 2034. “Hakuna nchi yoyote duniani iliyowahi kufanikisha malengo yake ya maendeleo bila kuwa na nishati ya kutosha na ya kuaminika,” alisema Ruto.
Pia alisisitiza kuwa nishati ya nyuklia inatambuliwa na Umoja wa Mataifa kama chanzo cha nishati chenye kiwango kidogo cha uzalishaji wa hewa ukaa na muhimu katika kufanikisha Agenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030. “Kuunganisha nishati ya nyuklia katika gridi ya taifa ni hatua ya kimkakati ya kupata suluhisho la muda mrefu litakalokidhi ongezeko la mahitaji ya umeme nchini Kenya,” alisema.
Katika hotuba yake, Ruto alifafanua kuwa tayari alikuwa ameshauriana na wakazi wa Siaya na kujiridhisha kuwa jamii za eneo hilo zinaunga mkono mradi huo. Hata hivyo, maandamano ya hivi karibuni yanaonyesha hali halisi ni tofauti.
Aidha, ombi la kupinga mradi huo uliozinduliwa mwezi Aprili, lilipata zaidi ya saini 400 kabla ya kuwasilishwa kwa NuPEA na kwa gavana wa kaunti hiyo.
Mongabay ilipitia ombi hilo na kubaini kuwa wananchi walionyesha wasiwasi kuhusu usimamizi wa taka za mionzi, kupoteza ardhi za mababu zao, na uwezekano wa kuhamishwa kwa lazima.
“Uhamishaji wa aina hiyo hautatokea kwa mtu mmoja mmoja pekee; utavunja umiliki wa ardhi za kifamilia, kuvuruga mifumo ya urithi, na kusababisha migogoro kuhusu fidia na makazi mapya, changamoto ambazo Kenya imekuwa na historia ya kushindwa kuzisimamia kwa usawa,” ilisema sehemu ya ombi hilo.
Hofu kwa wavuvi
Uwepo wa kinu cha nyuklia karibu na mazingira nyeti kiikolojia ya Ziwa Victoria pia umeibua hofu kwa jamii za wavuvi wanaotegemea ziwa hilo kwa chakula na kipato chao.
“Uvujaji wa mionzi, utoaji wa maji yenye joto kali, au ajali kutoka kwenye shughuli za nyuklia unaweza kubadilisha mfumo wa viumbe wa majini, kuvuruga mazalia ya samaki, na kuingiza uchafuzi wa mionzi katika mlolongo wa chakula kwa muda mrefu,” ombi hilo lilieleza.
Ziwa hilo pamoja na bioanuwai yake ya kipekee tayari limeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi pamoja na viumbe vamizi. Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya Worldwide Fund for Nature, Maziwa Makuu ya Afrika yana idadi kubwa zaidi ya aina za samaki wa maji safi duniani.
Hata hivyo, viumbe vamizi vimesababisha Ziwa Victoria kushuhudia mojawapo ya matukio makubwa zaidi ya kutoweka kwa viumbe wenye uti wa mgongo.
Pamoja na hayo, ziwa hilo ni muhimu sana kwa mifumo ya chakula na uchumi wa eneo hilo, likizalisha zaidi ya tani za metriki 800,000 za samaki kila mwaka. Wananchi wana hofu kuwa samaki hao wanaweza kuathiriwa na uchafuzi wa mionzi iwapo taka za nyuklia hazitasimamiwa vizuri au endapo ajali itatokea.
Picha ya Bango: Ziwa Victoria upande wa Kenya. Picha: Jozef020 kupitia Wikimedia Commons (CC BY-SA 4.0).
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 22/05/2026