- Wanafunzi hufundishwa kwa vitendo ili kuwaandaa kuwa wahifadhi wa baadaye.
- Wazazi hujengewa uwezo ili wasaidie watoto kutekeleza walichojifunza.
- Miti iliyotoweka imeanza kujerejea na kuleta upepo na hewa safi.
- Mradi umewajengea wanafunzi na wazazi tabia ya kujali na kulinda mazingira.
Wakati Tanzania ikiendelea kupoteza misitu kwa kasi kutokana na sababu mbalimbali, mradi wa kuhifadhi mazingira mashuleni umeanza kuleta mabadiliko kwa kurejesha miti iliyoanza kutoweka na kujenga ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
Takwimu za Global Forest Watch zinaonyesha kuwa Tanzania ilipoteza hekta milioni 3.48 za uoto wa miti kati ya mwaka 2001 na 2024, kwa mwaka 2024 pekee, ikipoteza hekta 271,000.
Sababu zinazotajwa kuchangia upotevu huo ni pamoja na shughuli za binadamu zinazochochewa na hitaji la kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia, kupanuka kwa miji na ukataji wa miti kwa ajili ya kujengea nyumba. Chanzo kikuu ni utegemezi mkubwa wa nishati itokayo na miti ambapo zaidi ya asilimia 85 ya kaya nchini Tanzania hutegemea mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia.
Dk Elikana John, Meneja wa Misitu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), anasema ili kuingilia kati uharibifu huo, TFS ikishirikiana na taasisi na wadau wa mazingira nchini, imekuwa ikitoa miche ya matunda na ya vivuli ili kutekeleza miradi ya kupanda miti sehemu mbalimbali ikiwemo mashuleni, hospitalini na majumbani.

Katika mikoa ya Morogoro, Iringa na Tanga, baadhi ya shule za msingi na sekondari zimeanzisha utaratibu wa kurejesha miti iliyotoweka kupitia programu ya Eco-Schools ambapo wanafunzi ni washiriki wakuu katika uhifadhi wa mazingira. Programu hiyo inafadhiliwa na Shirika la uhifadhi wa misitu la Tanzania Forest Conservation Group (TFCG).
Charles Meshack, Mkurugenzi Mtendaji wa TFCG, anasema walianzisha programu ya Eco-Schools mwaka 2015, na hadi sasa wamezifikia shule 160 zilizoko katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Tanga, Lindi na Mtwara.
Anasema lengo la kuanzishwa kwa programu hizo mashuleni ni kutoa elimu kwa vitendo kwa wanafunzi juu ya umuhimu wa kuitunza rasilimali misitu, ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuandaa wahifadhi misitu mahiri wa baadaye.
Katika programu hiyo, wanafunzi wanafundishwa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na athari zake, na kichocheo chake kikuu ambacho ni ukataji miti ovyo. Pia wanafundishwa kwa vitendo kupanda na kuhifadhi miti na utunzaji wa bustani za mbogamboga kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kuuza.
“Sisi tunatoa elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi na utunzaji mazingira kwa walimu ambao huenda kuwafundisha wanafunzi kupitia klabu za mazingira,” anasema.
Anasema mradi huo pia unashirikisha kamati za wazazi ambazo huelimishwa juu ya masuala mbalimbali kuhusu mazingira ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, upandaji miti pamoja na matumizi ya nishati mbadala katika kupikia kama vile gesi na umeme, ili kupunguza matumizi ya nishati ya kuni.
“Lengo la kuwajengea uwezo wazazi ni kuhakikisha wanawasaidia watoto wao kutekeleza kile tunachowafundisha mashuleni, washirikiane nao kupanda miti na bustani za mboga majumbani, pia kujenga utamaduni wa kutunza mazingira kuanzia ngazi za mitaa,” anasema.
Pamoja na mafunzo, shirika hilo linatoa miche ya miti ya matunda na mbegu za mboga kwa ajili ya kupanda shuleni na nyumbani.
Matokeo chanya
Utekelezaji wa mradi huo umesaidia kurejesha miti iliyokuwa imetoweka.

Amosi Charles Mkane, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Igowole, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa, anasema tangu kuanza kwa mradi wa Eco-Schools shuleni kwake mwaka 2023, wamepanda jumla ya miti ya matunda 220.
Kati ya hiyo miche 200, ambayo ni sawa na asilimia 91, imeota na kukua vizuri na baadhi imeanza kutoa matunda. Kadhalika wamepanda miche 40 ya miti ya kivuli na miche 500 ya miti ya kibiashara aina ya mikaratusi.
Anasema kupitia mradi huo wanafunzi 200 katika klabu ya mazingira wanashiriki kupanda miti na kuihudumia kwa kuweka mbolea na kuimwagilia maji wakati wa kiangazi. Pia wamepanda mboga katika bustani ya shule.
Kwa mujibu wa Amosi, uwepo wa miti katika maeneo hayo umesaidia kuongeza uzalishwaji wa hewa ya oksijeni ambayo inafanya kazi ya kusafisha hewa chafu ya kaboni inayochochea ongezeko la joto na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.
“Kuwepo kwa miti hiyo pia kumebadili hali ya hewa kutoka kuwa joto kali hadi kuwa na upepo wa kutosha, vivuli na hewa safi inayofanya wanafunzi kufurahia mazingira ya nje,” anasema.
Shule hiyo inatumia mbolea ya taka inayotengenezwa na wanafunzi kwa ajili ya kukuzia miti na mbogamboga pamoja na mbolea ya mifugo ambayo wanafunzi pia huifuga shuleni ikiwa ni sehemu ya kujifunza kujitegemea.
Matokeo mengine chanya ya mradi huo ni kwamba kutengeneza mbolea kutokana na taka za kikaboni, kumepunguza kiasi cha taka hizo kinachopelekwa dampo. Taka za aina hiyo huzalisha hewa ya methane inayochochea athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa hiyo kupungua kwake ni hatua nzuri.
Kadhalika, wanafunzi kuhamishia majumbani mwao utamaduni wa kujali na kupenda mazingira, ni matokeo mengine chanya ya mradi huo.
“Kwa miradi ya kuku, ng’ombe, mbuzi, bata na sungura, wanafunzi ndio wanaowaandalia chakula, kuwalisha na kusafishia mabanda kila siku. Pia wamepanda nyasi kwenye maeneo ambayo awali hayakuwa na nyasi, hatua ambayo imesaidia kuzuia mmomonyoko wa ardhi” anasema.
Pia kila mwanafunzi amepewa miche mitatu ya miti ya machungwa, maembe na mastafeli kwa ajili ya kupanda nyumbani ili kupata kivuli na matunda, lengo likiwa ni kupeleka utamaduni wa kupanda na kutunza miti majumbani.

“Tunawapatia pia mbegu za mboga na kuwapa mafunzo ya namna ya kupanda mboga hizo na kuzitunza, pia tunawafundisha ujasiriamali wa kuuza mboga hizo. Haya yote tunayafanya kupitia klabu za mazingira” anasema
Elimu yabadili tabia
Benedikto Fabian, Mwalimu wa Mazingira katika shule ya msingi Makweli, iliyopo kata ya Vugiri, Halmashauri ya Korogwe Mjini, mkoa wa Tanga, anasema walianzisha mradi huo Oktoba mwaka 2023 kama mradi wa majaribio lakini umezaa matunda kwani mpaka sasa wamepanda miche 200, inayotunzwa na wanafunzi 100 wa klabu ya mazingira.
Anasema kupitia mradi huo wanafunzi wamejifunza kuyapenda mazingira ya shule baada ya kuboreshwa, tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya mradi. Hali hiyo imehamasisha wanafunzi hao kupeleka utamaduni huo majumbani mwao.
Anakiri kuwa mradi huo umesaidia kuongeza rutuba kwenye ardhi kwa kutumia mbolea za taka zinazotengenezwa na wanafunzi, pamoja na kinyesi cha wanyama wanaofugwa shuleni kama ng’ombe, mbuzi, sungura, kuku na bata.
Kwa upande mwingine, upandaji wa nyasi, miti na maua umeiweka shule katika hali ya ukijani, umeongeza maeneo ya kupumzika wakati wa jua na kusaidia kuwepo kwa hewa safi kwa binadamu na wanyama.
Katika eneo la shule hiyo lililopandwa miti ya kibiashara karibu na vyanzo vya maji, Mkane anasema kumekuwa na mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji muda wote kwa mwaka tofauti na awali ambapo walikuwa wanapata maji msimu mmoja kwa mwaka.
“Awali kutokana na uhaba wa miti hakukuwa na mvua za kutosha, zilikuwa zikinyesha mara moja au mbili kwa mwaka tena kwa kiasi kidogo, hali iliyosababisha ukame. Hata hivyo uwepo wa miti katika eneo hili umeongeza mvua, kwa sasa inanyenya mara tatu na ni ya kutosha” anasema.
Anasema hata wazazi wameona umuhimu wa program hiyo na wamekuwa wakichangia kupeleka mbegu, miche ya mbogamboga, mbolea ya samadi na vyakula vya mifugo hasa kwa ng’ombe na mbuzi. Serikali ya kijiji nayo imesaidia katika ulinzi wa mali za shule, huku afisa ugani wa kijiji akitoa ushauri na matibabu kwa mifugo.
John Shirima ni mmoja wa wazazi kutoka kijiji cha Igowole, anasema kwa sasa anashirikiana na mtoto wake kutunza miti ya matunda na bustani nyumbani. John ni mmoja wa wazazi walioshiriki mafunzo ya uhifadhi wa mazingira katika shule hiyo kupitia kamati za wazazi.
Pia kwa kushirikiana kamati ya wazazi na wanapita nyumba kwa nyuma katika kijiji hicho kuelimisha jamii kupanda miti na mboga katika maeneo yao pamoja na kuwaelekeza kununua miche katika vitalu vya shule.
“Ingama miti hiyo ni ya biashara lakini uwepo wake umebadilisha hali ya hewa, kwa sasa joto limepungua lakini pia mvua zimeongezeka.Hivyo wamejiwekea utaratibu wa kuipanda kwa kupishana ili wanapouza baadhi mingine iwepo kwa ajili ya kuboresha hali ya hewa,’’ anasema John.
Mafunzo ya uhifadhi
Kwa wanafunzi, mradi huu si somo la darasani pekee. Ni mafunzo yanayogusa maisha yao ya kila siku. Josephina Mandia, mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya Msingi Makweli na mwanachama wa klabu ya mazingira, anasema wanapata mafunzo ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi mara mbili kwa wiki kupitia kablu yao.
Anasema kupitia klabu hiyo, wamepanda miti ya matunda ya machungwa, mapera, mafenesi na maembe nyumbani kwao, pia ameanzisha bustani mboga ikiwemo mchicha, majani ya maboga na sukuma wiki ambayo ikikua anauza na kupata pesa ya matumizi”.
Asha Mustapha, mwanafunzi wa kidato cha tatu wa shule ya sekondari Igowole, anasema alijiunga na klabu ya mazingira mwaka 2024 akiwa kidato cha kwanza na alianzisha bustani nyumbani baada ya kujifunza shuleni.
Changamoto za mradi
Licha ya mafanikio hayo, mradi unakabiliwa na changamoto kadhaa. Mkane anazitaja kuwa ni uhaba wa fedha, hasa kwa ajili ya kununua miche ya miti ya matunda na kivuli, baadhi ya wafugaji kuchungia mifugo yao katika eneo la shule lililopandwa miti, wizi wa miche hasa ya parachichi, na wizi wa mifugo kama kuku.
Changamoto nyingine ni uchomaji wa misitu ovyo unaotokana na shughuli za kilimo katika jamii ya Igowole, kupanda kwa gharama za vyakula vya wanyama, pamoja na magonjwa ya wanyama hasa kuku na mbuzi, ambayo husababisha shule kutumia fedha nyingi kuwatibu.
Hata hivyo, anasema shule imeendelea kupata msaada kutoka TFCG, serikali na jamii inayozunguka shule.
Kama ilivyo kwa Igowole, shule ya Msingi Makweli pia inakabiliwa na changamoto. Mwalimu Fabian anasema muda wa kusimamia mradi hautoshi kwa sababu walimu ni wachache na hutumia muda mwingi kufundisha masomo ya darasani.
Changamoto nyingine ni udogo wa eneo la shule, jambo linalosababisha shule kuwa na miradi michache ya maendeleo. Pia jamii inayozunguka shule bado haina uelewa wa kutosha kuhusu mradi wa Eco-Schools.
Hata hivyo, anasema shule imekuwa ikipata msaada kutoka kwa wafadhili wa mradi kupitia semina mbalimbali kuhusu uendeshaji wa mradi huo.

“Ningependekeza waongeze semina ili kutujengea zaidi uwezo wa kuendesha miradi hii,” anasema
Nini kifanyike
Mwalimu Mkane, wa shule ya Msingi Igowole anashauri kuwa kila shule nchini iwe na mpango wa tathmini ya mazingira kila mwaka unaosimamiwa kikamilifu ili kupanua mpango huu wa uboreshaji mazingira.
Anaiomba pia TFCG kuongeza ufadhili kwa shule nyingi zaidi ili kupanua wigo wa kujifunza kwa shule ambazo hazimo kwenye mradi.
“Kama mwalimu, naona nafasi ya vijana ni kubwa sana, sio tu leo bali leo na kesho. Mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa misitu ni changamoto ya muda mrefu na vijana ndio watakaoishi nayo zaidi,” anasema.
Mkurugenzi wa Shirika la Utu na Mazingira (HUDEFO) , Sarah Pima anashauri program kama hizi zipanuliwe kitaifa kwa kuwekeza zaidi kwa vijana kwa kuwa wana nguvu ya teknolojia na ubunifu.
“Kizazi cha sasa kimezaliwa na simu mkononi. Wanaweza kutumia app za kufuatilia moto misituni, kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha jamii, kubuni na kutengeneza biashara za mkaa mbadala, nishati safi, au kilimo mseto kinachohifadhi miti,” anasema.
Kwa mtazamo wake, njia bora ya kupanua mradi huu ni kuuingiza katika mfumo rasmi wa elimu na kuongeza mafunzo na semina ili kukuza uelewa kwa jamii yote ya Tanzania.
Picha ya Bango: Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Igowole, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa, wakipanda miche ya miti ya matunda katika eneo la shule chini ya mradi wa Eco-Schools. Picha na Jenifer Gilla.