- Asilimia 60 hadi 75 ya taka hazikusanywi ipasavyo na husababisha uchafuzi wa mazingira.
- Taka zisizosimamiwa vizuri huathiri mifumo ya ikolojia na vyanzo vya maji.
- Magonjwa sita kati ya kumi yanayoathiri jamii yanahusishwa na uchafuzi wa mazingira.
- Usafi wa mazingira unapaswa kuwa ajenda ya kudumu katika ngazi zote za maamuzi.
Serikali ya Tanzania imeandaa Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Taka (2025-2030) ambao unalenga kupunguza uzalishaji wa taka kwa kutumia dhana ya uchumi wa mzunguko ili kutunza mazingira, kuimarisha afya ya jamii na kukuza maendeleo endelevu ya miji.
Mkakati huo umekuja kipindi ambacho uzalishaji wa taka ngumu unazidi kuongezeka nchini huku usimamizi wake ukiwa wa kiwango cha chini. Kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Tanzania huzalisha kati ya tani milioni 14.4 hadi milioni 20.7 za taka ngumu kila mwaka.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Riziki Shemdoe, jijini Dodoma katika Mkutano wa Mwaka wa Tathmini ya Utekelezaji wa Afua za Usimamizi wa Taka Ngumu na Usafi wa Mazingira mijini.
Mkutano huo uliwakutanisha viongozi waandamizi wa serikali, washirika wa maendeleo, na wataalamu wa mazingira kwa lengo la kutathmini maendeleo yaliyofikiwa na kuweka mikakati ya kuboresha mifumo ya usimamizi wa taka.

Taka na fursa za kiuchumi
Waziri Riziki alisema kuwa usimamizi wa taka unapaswa kuingizwa katika mikakati mipana ya uwezeshaji wa kiuchumi kwa kuwa taka zinapaswa kuonekana kama rasilimali ya kiuchumi inayoweza kuzalisha ajira na kipato ikiwa zitasimamiwa ipasavyo.
Aliziagiza mamlaka za serikali za mitaa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa taka, na kuwahamasisha vijana na wanawake kutumia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kuwekeza katika shughuli za ukusanyaji, urejelezaji na uchakataji wa taka.
Kuimarika kwa usafi nchini kumepunguza milipuko ya magonjwa kama kipindupindu katika baadhi ya maeneo nchini, na pia kumesaidia serikali kuokoa rasilimali ambazo sasa zinaelekezwa kwenye vipaumbele vingine vya maendeleo.
Alisisitiza kuwa usafi wa mazingira unapaswa kuwa ajenda ya kudumu katika ngazi zote za maamuzi ya serikali, kuanzia ngazi za mikoa hadi vijiji.
Mkakati huo unaendana na Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) ya mwaka 2004, pamoja na Hati ya Tanzania ya Michango ya Taifa Iliyoainishwa chini ya Mkataba wa Paris (NDCs).
Mkurugenzi Msaidizi wa Mabadiliko ya Tabianchi na Tathmini kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Kanizio Manyika, alisema Tanzania huzalisha zaidi ya tani milioni 17 za taka ngumu kila mwaka. Kwa mujibi wa Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, miaka ya nyuma kwa mfano 2021-2023, ilizalisha kati ya tani milioni 12 hadi 14 kwa mwaka. Asilimia 60 hadi 75 ya taka hizo hazikusanywi ipasavyo, hali inayosababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira.
Alionya kuwa taka zisizosimamiwa vizuri zinaweka hatari kubwa kwa mifumo ya ikolojia, vyanzo vya maji na afya ya binadamu, akisisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo ya kisasa na jumuishi ya usimamizi wa taka.
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) anayeshughulikia afya, Profesa Tumaini Nagu, alisisitiza kuwa mifumo bora ya usimamizi wa taka ni muhimu katika kulinda afya ya jamii na kuzuia uharibifu wa mazingira katika miji inayokuwa kwa kasi.
Elimu kwa umma
Aidha alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya madhara ya kuzagaa kwa taka mitaani ili kupunguza milipuko ya magonjwa na gharama za huduma za afya.
“Kuboreshwa kwa usafi wa mazingira kutapunguza kwa kiasi kikubwa mzigo kwa mfumo wa afya na kuruhusu rasilimali zaidi kuelekezwa katika huduma nyingine za afya zilizopewa kipaumbele,” alisema.
Picha ya Bango: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, akizungumza katika katika Mkutano wa Mwaka wa Tathmini ya Utekelezaji wa Afua za Usimamizi wa Taka Ngumu na Usafi wa Mazingira mijini uliofanyika mjini Dodoma. Picha: Maktaba ya Wizara.