- Wizara inaboresha miongozo ya usanifu namatumizi ya malighafi za ujenzi kwa kuzingatia uhimilivu.
- Maandalizi ya mpango wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi wa Sekta ya Ujenzi kuanza.
- Miundombinu iliyoathirika itajengwa kwa viwango vinavyoweza kuhimili majanga.
DODOMA, Tanzania – Mabadiliko ya tabianchi yametajwa kama changamoto kubwa iliyoathiri utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ujenzi katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi Tanzania, Abdallah Ulega, wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2026/2027, mnamo Mei 20, katika kikao cha bajeti kinachoendelea katika Makao Makuu ya Nchi, Dodoma.
Amesema majanga yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, kama vile mafuriko, yalisababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo mbalimbali nchini.
Ili kukabiliana na hali kama hiyo, Waziri alisema wizara yake inaboresha miongozo ya usanifu na matumizi ya malighafi za ujenzi kwa kuzingatia uhimilivu wa miundombinu.

“Vilevile, wizara imepanga kupanda miti 40,000 katika barabara kuu na barabara za mikoa, na kuanza maandalizi ya mpango wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi wa Sekta ya Ujenzi,” amesema waziri.
Aidha, amesema wizara itaendelea kuchukua hatua za haraka kurejesha na kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko pamoja na athari nyingine za mabadiliko ya tabianchi.
Gharama za uharibifu
“Barabara na madaraja yaliyoathirika yatajengwa kwa viwango vinavyoweza kuhimili majanga hayo, ili kuepuka kuongeza mzigo kwa serikali kugharamia uharibifu unaojitokeza kila msimu wa mvua kubwa na kuhakikisha barabara zetu zinapitika majira yote ya mwaka hata wakati wa changamoto za hali ya hewa,” amesema Waziri.
Kauli hiyo ya Waziri imekuja kipindi ambacho taifa bado linaugulia maumivu ya hasara kubwa zilizosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na mafuriko na maporomoko.
Mwishoni mwa mwaka 2025, vyombo vya habari nchini viliripoti kuwa mvua kubwa ziliharibu miundombinu ya barabara, madaraja na mifumo ya umeme.Madaraja yaliyoathirika kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua hizo ni pamoja na Kidete lililoko katika wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro na Gulwe lililoko katika wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Uharibifu wa miundombinu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, eneo maarufu zaidi la utalii wa wanyamapori nchini, zilizoharibiwa wakati wa mvua zilizonyesha mwanzoni mwa mwaka 2026, inatarajiwa kugharimu takribani TSh8.1 bilioni.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa fedha hizo zitatumika katika kukarabati barabara na madaraja yaliyoharibiwa na mvua kubwa, ambazo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ilihusisha na mabadiliko ya tabianchi.
Vyombo vya habari vinasema mvua hizo zilisomba sehemu za barabara na kuharibu madaraja kadhaa ndani ya hifadhi hiyo, hali iliyosababisha baadhi ya magari ya watalii kukwama kwa muda na kuvuruga safari za utalii.
Waziri Kijaji, aliyekuwa kwenye ziara ya ukaguzi ndani ya hifadhi hiyo alisema fedha hizo zitaruhusu ukarabati wa haraka wa madaraja na barabara zilizoharibiwa ili shughuli za utalii ziweze kuendelea kwa usalama.
Alisema ukarabati huo utahusisha ujenzi upya wa madaraja muhimu kama Orangi Upper, Orangi Lower, Banagi na Bona, pamoja na makaravati na maeneo ya kuvukia maji katika barabara ya Naabi–Seronera.

Aliongeza kuwa sehemu ya fedha hizo pia itatumika kufanya tafiti za kihandisi zitakazolenga kuimarisha miundombinu dhidi ya matukio makubwa ya hali mbaya ya hewa siku zijazo.
Naye Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara wa TANAPA, Massana Mwishawa, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa miundombinu bora itasaidia kuhakikisha hifadhi hiyo itafikika mwaka mzima, hata wakati wa mvua na kiangazi.
Picha ya bango: Njia za reli zilikuwa miongoni mwa miundombinu iliyoharibiwa na mvua kubwa nchini Tanzania. Picha kwa hisani ya Wizara ya Ujenzi Tanzania.