Serikali ya Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na nchi ya Norway katika kuendeleza hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, uhamishaji wa teknolojia, uwekezaji wa kijani pamoja na ulinzi wa mazingira.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Yussuf Masauni wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Katiba ya Norway yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Mei 15, 2026.
Alisema Serikali ya Tanzania inaipongeza Norway kwa kuendelea kuwa kinara duniani katika ufadhili wa masuala ya tabianchi na maendeleo endelevu.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes, alisema maneno machache kuhusu umuhimu wa siku hiyo pamoja na urafiki na mshikamano kati ya nchi hizo mbili.
Uwekezaji zaidi
Masauni alisema kuwa wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza dira yake ya maendeleo ya 2050 na kuendeleza ukuaji wa kijani pamoja na ustawi shirikishi, inakaribisha kwa moyo mkunjufu ushirikiano zaidi, uwekezaji zaidi, na kuimarishwa kwa mahusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Masuala ya uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa vipaumbele katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, iliyozinduliwa Julai 2025 na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
“Kwa zaidi ya miongo sita, nchi zetu zimejenga urafiki uliotokana na kuaminiana, ukaimarishwa na mshikamano, na kuendelea kudumishwa na maadili ya pamoja. Ni urafiki ambao umeendelea kudumu licha ya mabadiliko ya siasa za kimataifa na mageuzi katika uchumi wa dunia,” alisema waziri huyo.
Aliongeza kuwa Tanzania inathamini kwa dhati ushirikiano endelevu wa Norway katika maeneo kama ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, nishati jadidifu, kilimo endelevu, elimu, na utawala bora.
Aliongeza kuwa ushirikiano wa hivi karibuni katika kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi, upanuzi wa nishati jadidifu, na uhifadhi wa mazingira unaonyesha kuwa maendeleo endelevu lazima yaende sambamba.
Ukweli unaounganisha binadamu
Kwa mujibu wa Waziri Masauni, katika miaka ya karibuni, biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Norway vimeongezeka. Kufikia Desemba 2025, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania ilikuwa imesajili jumla ya miradi 46 ya uwekezaji kutoka Norway, yenye thamani inayokadiriwa kufikia dola za Marekani milioni 323.062, na ambayo imezalisha ajira zaidi ya 4,400.
“Kama Waziri mwenye dhamana ya Mazingira na Masuala ya Muungano, niruhusu kusisitiza ukweli mmoja unaounganisha ubinadamu wote: Mabadiliko ya tabianchi hayana mipaka. Mafuriko hayahitaji visa. Ukame hautambui pasipoti. Kuongezeka kwa joto hakihurumii nchi yoyote,” alisema na kuongeza kuwa ndiyo maana ushirikiano kama huu kati ya Tanzania na Norway ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote.
Alisema: “Kwa pamoja, tunapanda zaidi ya miti; tunapanda matumaini. Tunajenga zaidi ya miradi; tunajenga ustahimilivu. Tunaimarisha zaidi ya uchumi; tunaimarisha ushirikiano kwa ajili ya vizazi vijavyo.”
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na maafisa wa kidiplomasia wa nchi mbalimbali walioko Tanzania, wawakilishi wa mashirika ya kiraia, viongozi wa serikali, marafiki wa nchi hiyo pamoja na wawakilishi wa mashirika mbalimbali.
Norway imekuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika kufadhili miradi ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na nishati jadidifu.
Ushirikiano huu umejikita katika maeneo kadhaa muhimu yakiwemo uhifadhi wa misitu, kupunguza hewa ukaa, biashara ya kaboni, na kuimarisha mifumo ya nishati safi.
Picha ya bango: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Yussuf Masauni akiwa na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes.