- Bagamoyo imeendelea kupoteza mikoko kwa kiasi kikubwa kutokana na mahitaji ya kuni na vifaa vya ujenzi.
- Ukataji haramu wa miti bado unaendelea kutokea licha ya kuwepo kwa kanuni.
- Takwimu sahihi ni muhimu ili kupima mafanikio ya muda mrefu ya urejeshaji wa mikoko.
- Mabadiliko ya tabia miongoni ni msingi muhimu wa mafanikio ya muda mrefu ya urejeshaji wa mikoko.
Karibu maeneo yote ya ukanda wa pwani wa Tanzania yanaendelea kukabiliwa na shinikizo linalotokana na maendeleo ya pwani, uvunaji wa kuni na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, Bagamoyo inaonyesha dalili za mafanikio katika juhudi za urejeshaji wa mikoko zinazoungwa mkono na jamii pamoja na mashirika ya uhifadhi.
Tanzania inakadiriwa kuwa na takribani hekta 158,000 za misitu ya mikoko, huku Bagamoyo ikichangia karibu hekta 5,636 zinazoambaa kwenye ukanda wa karibu kilomita 100 za pwani. Ingawa baadhi ya maeneo yanaonekana kuwa na mianya au upungufu wa mikoko wataalamu wanafafanua si maeneo kuwa na mianya au uwazi hakumaanishi kwamba yameharibika kabisa, kwani mikoko inaweza kujirejesha yenyewe endapo mazingira yatakuwa rafiki.
Katika kata za Kisutu, Magomeni, Makurunga, Zinga, Kaole, Dunda na Mapinga, ambazo zina wakazi zaidi ya 205,000, shughuli za urejeshaji zinaendelea kwenye maeneo yaliyokuwa yameharibika hapo awali. Katika maeneo ambayo mikoko mipya imepandwa, wananchi wameanza kushuhudia dalili za urejeshwaji wa ikolojia na kuimarika kwa mazingira ingawa bado kuna changamoto zinazoendelea kuwepo.
Tangu mwaka 2022, inakadiriwa kuwa miche kati ya 42,000 hadi 46,000 ya mikoko imepandwa wilayani Bagamoyo kupitia programu za pamoja za urejeshaji zinazolenga kufufua mifumo ikolojia ya pwani iliyoharibika.

Akizungumza na Mongabay, Meneja wa Mradi wa Sustainable Ocean Alliance (SOA) Tanzania, Yusufu Issa, alisema juhudi hizo zimeelekezwa zaidi katika maeneo yaliyoharibika sana ambayo urejeshaji wa asili hauwezekani tena.
“Tunajikita katika maeneo ya ambayo urejeshaji wa asili hauwezekani tena. Maeneo tunayashughulikia kwa sasa ni kata ya Kisutu, hasa Jangwani, eneo ambalo limeharibika sana, na hatua za kuingilia kati ni muhimu,” alisema.
Mikoko ni mifumo muhimu ya ikolojia ya pwani inayosaidia kupunguza mmomonyoko wa ardhi, kuzuia nguvu za mawimbi makubwa ya bahari, na kutoa mazalia kwa samaki pamoja na viumbe wengine wa baharini. Hata hivyo, Bagamoyo imeendelea kupoteza mikoko kwa kiasi kikubwa kutokana na mahitaji ya kuni na vifaa vya ujenzi.
Mpango wa urejeshaji wa SOA Tanzania ulioanzishwa mwaka 2022 umeendelea kupanuka kuanzia mwaka 2023 hadi 2025, huku shughuli za upandaji zikipangwa kuendelea hadi mwaka 2026. Mpango huo umejengwa katika nguzo tatu kuu: urejeshaji wa mifumo ikolojia, elimu ya mazingira, na uwezeshaji wa jamii.
Programu za elimu ya mazingira zinawalenga wanawake, vijana, na wajasiriamali wadogo kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kiikolojia na kiuchumi wa mikoko pamoja na kuonyesha hatari za ukataji wa misitu.
Kwa mujibu wa Issa, mabadiliko ya tabia miongoni mwa wana jamii ni msingi muhimu wa mafanikio ya muda mrefu ya urejeshaji wa mikoko.
“Jamii zinahitaji kuelewa kwa nini mifumo hii ya ikolojia ni muhimu. Bila uelewa huo, juhudi za urejeshaji pekee haziwezi kuwa endelevu,” alisema.
Asali ya Mikoko
Ili kukabiliana na sababu za kiuchumi zinazochochea uharibifu wa mikoko, SOA pamoja na washirika wake wameanzisha miradi mbadala ya kujipatia kipato chini ya mfumo wa uchumi wa buluu, ikiwemo ufugaji wa nyuki ndani ya misitu ya mikoko
Mradi wa “asali ya mikoko” unatoa mizinga, mafunzo, na vifaa vya kujikinga, hatua inayowezesha jamii kupata kipato bila kukata miti. Programu hiyo inatekelezwa kwa kushirikiana na vikundi vya kijamii kama Mikoko Yetu Bahari Yetu na Bagamoyo Checkrainagu, pamoja na msaada wa kiufundi kutoka sekta binafsi.
Hadi sasa, takribani wanajamii pamoja na vikundi 30 vimeshiriki katika programu hiyo, huku mipango ya kuipanua ikiendelea.
Issa alisema mbinu hiyo inalenga kuwaongezea wananchi motisha ili waone faida ya uhifadhi. Anasema, “Kama watu wanaweza kupata kipato kutokana na misitu bila kuiharibu, mitazamo yao huanza kubadilika”.
Upungufu wa takwimu
Licha ya kuongezeka kwa shughuli za urejeshaji, wahifadhi wa mazingira wanasema ukosefu wa takwimu za kina na mahsusi kwa maeneo fulani unaendelea kukwamisha upangaji madhubuti.
Issa alisema kuwa ingawa makadirio ya kitaifa kuhusu upotevu wa mikoko yapo, bado takwimu za ngazi ya wilaya kwa maeneo kama Bagamoyo ni chache.

“Unaweza kuona wazi uharibifu ukiendelea maeneo mbalimbali, lakini unapohitaji takwimu sahihi, hasa kwa eneo maalumu kama Bagamoyo, inakuwa vigumu sana kuzipata,” alisema.
Aliongeza kuwa takwimu zilizopo mara nyingi ni za jumla mno, hali inayofanya iwe vigumu kupanga hatua mahsusi za uhifadhi.
Kwa sasa SOA inatafuta fursa za ufadhili ili kuzalisha takwimu za kienyeji kuhusu mikoko pamoja na mifumo mingine ya ikolojia ya pwani kama nyasi bahari na miamba ya matumbawe, ambayo nayo bado haijaandikwa kwa kina.
Mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania, Pindi Chana, alizindua Mkakati wa Taifa wa Usimamizi na Uendelezaji wa Mikoko (2025–2035), mpango wa miaka 10 uliotoa wito kwa taasisi zote zinazotekeleza kuhakikisha hatua zinachukuliwa kwa haraka na kuleta matokeo yanayopimika.
Mkakati huo mpya unalenga kurejesha na kuhifadhi asilimia 60 ya misitu ya mikoko iliyoharibika nchini. Pia unaweka mikakati ya utekelezaji inayolenga urejeshaji wa mifumo ya ikolojia, matumizi endelevu, na usimamizi shirikishi.
“Mkakati huu pia unalenga kurejesha na kusimamia kwa njia endelevu mifumo ya mikoko nchini, ambayo ni muhimu kwa bioanuai, ulinzi wa ukanda wa pwani, na ukuaji wa uchumi wa buluu.”
“Mikakati isiachwe kwenye makabati kukusanya vumbi,” alisema. “Taasisi zetu lazima zitenge bajeti, zishirikishe jamii, na kuchukua hatua kwa haraka. Mikoko ni uhai wa jamii za pwani.”
Waziri huyo pia alizitaka taasisi za serikali, hasa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kuanza utekelezaji mara moja kwa kushirikiana na taasisi za utafiti pamoja na washirika wa maendeleo.
Makadirio ya kitaifa yanaonyesha kuwa Tanzania imepoteza zaidi ya hekta hekta 6,000 za mikoko tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990 zaidi ya asilimia 10 ya eneo lote la mikoko nchini. Hata hivyo takwimu hizo zinatokana zaidi na tathmini za jumla.
Shirika la Aga Khan Foundation (AKF) Tanzania, kwa kushirikiana na TFS, pia limechangia juhudi za urejeshaji, ikiwa ni pamoja na mipango ya kuanzisha miradi ya “misitu midogo” katika shule 50 nchini.
Tangu mwaka 2023, AKF na TFS zinaripotiwa kupanda zaidi ya miti ya 150,000 katika maeneo ya pwani yaliyoharibika.
Bagamoyo, ushiriki wa jamii unahusishwa pia na motisha ndogo za kifedha, ambapo kaya hupokea takribani Sh70,000 kwa mwezi kwa kushiriki kwenye shughuli za urejeshaji.
Mkazi wa eneo hilo, Salum Mohamed, alisema kipato hicho kinasaidia mahitaji ya msingi ya familia.

Ingawa motisha za kifedha ni muhimu, wananchi pia wanahamasishwa na manufaa ya muda mrefu ya kimazingira, hasa kuongezeka kwa samaki kadri mifumo ya mikoko inavyoendelea kuimarika.
Sheria ndogo kali
Juhudi za urejeshaji zinaimarishwa na sheria ndogo zilizosasishwa na kuanza kutumika mwaka 2025. Sheria hizi zinahusu uhifadhi wa mazingira, usafi wa mazingira, na usimamizi wa maliasili.
Kanuni hizo zinawataka wakazi wanaoishi karibu na hifadhi za misitu kulinda miti ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa na zinakataza uchomaji au shughuli zinazoweza kusababisha moto wa misitu. Jamii pia zinawajibika kwa pamoja kushiriki katika kuzima moto pale matukio yanapotokea.
Ukataji wa miti ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa unasimamiwa kwa na huhitaji kibali kutoka halmashauri ya wilaya pamoja na uthibitisho wa maafisa misitu ili kuhakikisha miti hiyo imekomaa na uvunaji wake ni endelevu.
Mabaraza ya vijiji pia yana wajibu wa kutenga maeneo ya uhifadhi na kurejesha mifumo ya ikolojia iliyoharibika kupitia upandaji miti na urejeshaji wa makazi ya viumbe hai.
Katika ngazi ya kaya, wakazi wanatakiwa kupanda na kutunza miti, huku taasisi zikitakiwa kuanzisha kanda za miti ya kinga kuzunguka majengo.
Hata hivyo changamoto za utekelezaji bado zinaendelea kuwepo. Afisa mmoja wa misitu alisema kuwa ukataji haramu wa miti mara nyingi hutokea licha ya kuwepo kwa kanuni.
“Wakati mwingine tunapofika, uharibifu unakuwa tayari umefanyika. Wanaofanya vitendo hiyo hutafuta muda mzuri ambao hawawezi kuonekana na kufanya vitendo hivyo,” alisema afisa huyo.
Mabadiliko ya tabianchi
Mikoko inatambuliwa duniani kama mifumo muhimu ya “blue carbon” inayayohifadhi kiwango kikubwa cha hewa ya ukaa huku ikilinda jamii za pwani dhidi ya kupanda kwa kina cha bahari na athari za mawimbi makubwa.
Kwa mujibu wa Costantine Lasway, Afisa Mwandamizi Msaidizi wa Misitu kutoka TFS, ukanda wa mikoko wa Bagamoyo unakadiriwa kuwa na zaidi ya hekta 5,000 na umeenea katika kata karibu 10 kati ya kata 25 za wilaya hiyo. Kata hizo ni pamoja na Kisutu, Mapinga, na Makurunga, maeneo ambayo yamepata uharibifu mkubwa zaidi.
Alisema ushirikiano mzuri kati ya taasisi za serikali, viongozi wa mitaa, na jamii umeongeza uelewa wa uhifadhi pamoja na ulinzi wa maeneo yaliyorejeshwa.
Kwa wakazi wengi, mikoko bado ni chanzo cha maisha na lakini pia ni wajibu wa pamoja wa kutunza mazingira.
Rahima Mohamed, mkazi wa kata ya Makurunga, akikumbuka hali ilivyokuwa siku za nyuma. Anasema: “Zamani tulikuwa tunakata mikoko ovyo kwa ajili ya kuni. Uhifadhi tulikuwa tunausikia tu redioni. Hatukujua kuwa unatakiwa uanzie kwetu sisii”.
Dalili za mafanikio
Katika kata ya Kisutu, maji ya bahari sasa yanapita tena kwenye maeneo mapya ya mikoko iliyopandwa, ishara ya kurejea taratibu kwa mfumo wa ikolojia katika maeneo ambayo hapo awali yaliyokuwa yumeharibiwa sana.
Ingawa maendeleo yanaonekana, wataalamu wanaonya kuwa urejeshaji wa mikoko ni mchakato wa muda mrefu unaotegemea sana ufadhili endelevu, utekelezaji wa sheria, na ubora wa takwimu.
Afisa wa TFS Hamis Ghaji alisema mashirika mbalimbali, yakiwemo AKF, Wetlands International, Tanzania Traditional Energy Development Organization (TaTEDO), na SOA, yanachangia juhudi za urejeshaji katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa pwani.
“Mashirika haya yanafanya kazi katika maeneo tofauti, yakirejesha mikoko na kufuatilia ukuaji wake. Pia kuna watu binafsi wanaochangia kwa hiari kutokana na dhamira zao binafsi,” alisema.
AKF pekee imepanda zaidi ya mikoko 140,000 Bagamoyo, huku Wetlands International ikipanua shughuli za urejeshaji kutoka Mapinga kuelekea Saadani.
Licha ya maendeleo hayo, wataalamu wanasisitiza kuwa takwimu sahihi na za maeneo mahsusi bado ni muhimu katika kupima mafanikio ya muda mrefu ya urejeshaji na pia kujua hatua zaidi za kuchukuliwa.
Picha ya Bango: Mwanakijiji wa kata ya Kisutu, wilaya ya Bagamoyo akionyesha mikoko ilioyorejeshwa kupitia AFK. Picha kwa hisani ya AKF.