- Mkutano wa Africa Forward Summit uliofanyika Nairobi ulisisitiza kuwa Afrika inapaswa kutambuliwa kama mshirika muhimu katika uzalishaji, ubunifu na uongozi wa uchumi wa dunia, badala ya kuwa soko au chanzo cha malighafi pekee.
- Viongozi wa Afrika na washirika wa kimataifa walijadili haki ya tabianchi, mpito wa nishati ya kijani na umuhimu wa kuhakikisha Afrika inanufaika zaidi na rasilimali zake huku ikipata ufadhili na teknolojia kwa usawa.
- Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema Afrika ina asilimia 60 ya maeneo bora kwa nishati ya jua duniani lakini inapokea asilimia 2 pekee ya uwekezaji wa kimataifa katika nishati safi.
- Tamko la mwisho la mkutano liliahidi kuimarisha uwekezaji katika viwanda vya kijani, nishati jadidifu, uchakataji wa madini ndani ya Afrika na ushirikiano wa kikanda ili kuchochea maendeleo endelevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano wa Africa Forward Summit ulifungwa jijini Nairobi Mei 12 kwa tamko la pamoja la kisiasa lililosisitiza kuwa Afrika inapaswa kutambuliwa “siyo tu kama soko la baadaye, bali kama mshirika katika uzalishaji, ubunifu na uongozi wa uchumi wa dunia.”
Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano wa Kenya na Ufaransa. Ulihudhuriwa na wakuu wa nchi takribani 30, wafanyabiashara wakubwa, watunga sera, taasisi za kimataifa, na wadau wa masuala ya tabianchi, mijadala iligusa mpito wa nishati ya kijani na umuhimu wa kuhakikisha makosa ya zamani ya uchimbaji na unyonyaji wa rasilimali hayarudiwi. Badala yake, mjadala ulisisitiza haki ya tabianchi, upatikanaji sawa wa fedha na teknolojia, pamoja na ulinzi wa mazingira.
Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alipohutubia kikao cha ngazi ya juu katika mkutano huo, alisisitiza suala la haki ya tabianchi. Alieleza mchango mdogo wa Afrika katika ongezeko la joto duniani, na akibainisha kuwa licha ya hali hiyo, bara hilo bado linaendelea kuathirika zaidi na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Hali hiyo iliakisiwa katika tamko la mwisho la mkutano huo, ambalo liliahidi “kuendeleza mifumo ya haki na usawa katika ufadhili wa miradi ya tabianchi na maendeleo endelevu, wakati Afrika ikipewa sauti kubwa zaidi katika maamuzi ya kimataifa, utawala, uwekaji wa viwango na utungaji wa sheria.”
Guterres pia alizungumzia uwezo mkubwa wa Afrika katika nishati jadidifu, akisema kuwa kuna pengo kubwa la uwekezaji katika sekta ya nishati safi duniani.
“Afrika ina asilimia 60 ya maeneo bora zaidi duniani kwa uzalishaji wa nishati ya jua lakini inapokea asilimia 2 pekee ya uwekezaji wa kimataifa katika nishati safi. Kwa ufadhili sahihi, bara hili linaweza kuzalisha umeme mara 10 zaidi ya mahitaji yake ifikapo mwaka 2040, yote yakitokana na nishati jadidifu. Afrika lazima iwe sehemu kuu ya mjadala wa haki ya tabianchi,” alisema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.
Wakati tafiti zikionyesha kuongezeka kwa uwekezaji wa kimataifa katika nishati jadidifu kati ya mwaka 2015 hadi 2024, tafiti nyingine zimeonyesha kuwa bado kuna pengo kubwa la uwekezaji, huku nchi zinazoibuka kiuchumi na zinazoendelea nje ya matumizi ya kimataifa katika nishati safi.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa matumizi ya Afrika katika nishati jadidifu yaliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 9 mwaka 2019 hadi dola bilioni 22 mwaka 2024, ikilinganishwa na China ambayo matumizi yake yaliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 164 hadi dola bilioni 359 katika kipindi hicho.
Kwa mujibu wa World Resources Institute, “Kuongeza matumizi ya nishati jadidifu sasa kunaweza kusaidia kuepuka utegemezi wa muda mrefu wa mafuta ya kisukuku huku rasilimali nyingi za asili zilizopo katika ukanda huu zikitumika ipasavyo.”
Kwa mfano, Afrika ina takribani asilimia 60 ya maeneo bora zaidi duniani kwa uzalishaji wa nishati ya jua, lakini inachangia asilimia moja tu ya uwezo wa dunia wa nishati ya jua uliowekwa rasmi.
Kauli za Guterres zilisisitiza changamoto za kifedha ambazo zimekuwa zikikwamisha Afrika kuhamia kwenye nishati hiyo, licha ya bara hilo kuwa na rasilimali nyingi za upepo, jua, maji na jotoardhi. “Hili si bara linalosubiri suluhisho. Hili ni bara linalozalisha suluhisho,” alisema. “Lakini tuwe wakweli kuhusu kinachokwamisha Afrika,” aliongeza.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahamoud Ali Youssouf, akihutubia wajumbe wa mkutano huo alisema: “Afrika pia lazima ichangie katika maamuzi kuhusu uchumi wa dunia… Mustakabali wa mambo mazuri yajayo ni kwa ajili ya bara la Afrika. Bara la Afrika litakuwa kitovu cha ukuaji wa uchumi duniani.”
Majadiliano hayo yalipelekea kuundwa kwa kipengele cha nne kati ya vipengele 11 vya Tamko la Nairobi, kilichopewa jina la “Powering Growth Through Green Industrialization and Energy Transition (Kuchochea Ukuaji Kupitia Uendelezaji wa Viwanda vya Kijani na Mpito wa Nishati)”.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Rais wa Kenya William Ruto waliongoza mkutano huo kwa pamoja. Tamko la mwisho lilisisitiza nafasi ya Afrika katika teknolojia na uzalishaji viwandani, kwa lengo la kuondoka katika nafasi yake ya jadi ya kuwa msambazaji wa malighafi pekee, na badala yake kushiriki kikamilifu kama mdau mkubwa mwenye manufaa zaidi kwa bara na wananchi wake. Pia liliahidi kuhakikisha maendeleo endelevu yanafungamanishwa na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Tunakiri kuwa upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na endelevu ni muhimu kwa maendeleo na utekelezaji wa ajenda ya muda mrefu ya maendeleo ya Afrika kupitia ukuaji shirikishi, uundaji wa ajira na utajiri,” lilisema tamko la mwisho lililotolewa mwishoni mwa mkutano huo wa siku mbili.

Ili kufanikisha tamko hilo, bara hilo litapaswa kuendeleza viwanda vya kijani kupitia uwekezaji katika nishati jadidifu, mifumo ya uzalishaji yenye hewa ukaa kidogo, hidrojeni ya kijani na miradi mikubwa ya nishati safi kama umeme wa maji, jotoardhi, uzalishaji wa nishati kutoka taka, pamoja na nishati ya nyuklia.
Viongozi hao walisema watashirikiana kuimarisha usalama na uhuru wa nishati, hasa kwa kutumia uwezo mkubwa wa Afrika katika nishati jadidifu, pamoja na kuunga mkono maendeleo ya minyororo ya thamani ya bidhaa za nishati safi zinazozalishwa ndani ya bara hilo. Pia walisisitiza kuongeza upatikanaji wa nishati safi, ikiwemo nishati safi ya kupikia, na kuanzisha masoko ya nishati yaliyounganishwa.
Jambo muhimu katika mkutano huo lilikuwa kuhakikisha ya kwamba mamlaka ya kitaifa yanaheshimiwa juu ya rasilimali za asili, “ikiwemo madini muhimu ya kimkakati, kukuza uchakataji wa ndani, kuongeza thamani, na usindikaji endelevu wa madini muhimu ya Afrika ili kusaidia maendeleo ya viwanda, utofauti wa uchumi, na minyororo imara ya thamani ya kikanda.”
Hatimaye, viongozi hao walikubaliana kuendelea kuunga mkono Mkataba wa Paris na sera zinazotegemea ushahidi wa kisayansi, “na kufanya kazi pamoja kutekeleza matokeo ya tathmini ya kwanza ya kimataifa ili kuharakisha mpito wa haki wa nishati, wakati tukizingatia kanuni na malengo ya pamoja yaliyomo katika Mkakati na Mpango Kazi wa Umoja wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo Himilivu (2022–2032).”
Haya ndiyo yaliyokuwa hitimisho kuu la mijadala ya mazingira iliyotawala mazungumzo ya siku hizo mbili. “Kwa muda mrefu sana, rasilimali za Afrika zimekuwa zikichimbwa, thamani yake ikinufaisha mataifa mengine, huku uharibifu wa mazingira ukibaki Afrika. Wananchi wa Afrika lazima wanufaike kwanza na zaidi kutokana na rasilimali za Afrika,” António Guterres aliandika baadaye kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.
Picha ya bango: Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Rais wa Kenya William Ruto wakati wa Mkutano wa Africa Forward Summit 2026 katika Ukumbi wa Taifa jijini Nairobi, ambapo Kenya na Ufaransa zilitia saini makubaliano 11 yanayohusiana na miundombinu, ubunifu na maendeleo ya uchumi. Picha kwa hisani ya TechTrendsKe.