- Matumbawe yako katika hatari ya kutoweka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, shughuli za binadamu.
- Utaratibu wa kupumzisha mwamba, umeokoa matumbawe yaliyokuwa hatarini.
- Upandaji wa mikoko umesaidia kupunguza athari za mmomonyoko wa ardhi na majanga ya asili.
- Uhaba wa vitendea kazi, hasa boti za kufanya doria baharini, hukwamisha vita dhidi ya uvuvi haramu.
Matumbawe ni miongoni mwa mifumo ya ikolojia yenye thamani kubwa duniani. Kwa mujibu wa taasisi ya National Oceanic and Atmospheric Administration (NOAA), rasilimali hiyo ya bahari hutumika kama makazi na chakula kwa takribani asilimia 25 ya viumbe wote wa baharini, wakiwemo pweza, majongoo bahari, kambakochi na changu.
Tofauti na yanavyoonekana, matumbawe si mawe, bali ni viumbe hai wanaopatikana baharini, wanaoishi kwa kutegemeana na viumbe wa bahari kama vile pweza, mwani na nyasi bahari. Upekee huu huifanya miamba ya matumbawe kuwa miongoni mwa mifumo tajiri zaidi ya ikolojia duniani, ikitoa makazi, sehemu za kuzaliana na chakula kwa takribani robo ya viumbe wote wa baharini.
Matumbawe pia hulinda fukwe dhidi ya mawimbi makubwa na mmomonyoko wa udongo, hivyo huzuia mafuriko kwenye nyumba zilizopo karibu na bahari, kuimarisha uvuvi na kuvutia utalii, na hatimaye kusaidia maisha ya mamilioni ya watu wanaotegemea rasilimali za bahari.
Hata hivyo, matumbawe yako hatarini zaidi kutoweka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hasa ongezeko la joto pamoja na shughuli mbalimbali za binadamu.
Kwa mujibu wa Prof. Yunus Daud Mgaya, Mtaalamu wa Biolojia ya Bahari katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mabadiliko ya tabianchi husababisha kuongezeka kwa kiwango cha joto baharini, na joto la maji linapofika zaidi ya nyuzi joto 30, matumbawe hushindwa kuvumilia na kupoteza mwani (algae) wanaowapa chakula kupitia usanisinuru (photosynthesis). Hali hii husababisha matumbawe hupoteza chanzo cha chakula, kudhoofika na yanapopigwa na mawimbi makali hubomoka kwa urahisi.
Ripoti ya International Coral Reef Initiative iliyochapishwa mwaka 2025 inaonyesha ongezeko la joto la bahari duniani kati ya Januari 2023 hadi Machi 2025 limeathiri takribani asilimia 84 ya matumbawe, likiwa ni tukio kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa.
Uharibifu wa matumbawe
Uchunguzi wa Mongabay katika mkoa wa Lindi, ambao uko sehemu ya kusini ya pwani kwenye Bahari ya Hindi, unaonyesha kuwa uharibifu wa matumbawe siyo hadithi za kusimuliwa bali ni uhalisia wa kile kinachoendelea.
Ripoti ya Tathmini ya Hali ya Mifumo ya Ikolojia ya Bahari nchini Tanzania (MEDA 2025) inaonyesha kuwa matumbawe ni miongoni mwa makazi ya baharini yaliyo hatarini zaidi kutoweka kutokana na uvuvi haramu, utalii usiofuata utaratibu, maendeleo yanayofanywa katika maeneo ya pwani, pamoja na uchafuzi wa mazingira.
Mgaya anasema mvuvi anapotumia vilipuzi kulipua miamba ya matumbawe ili kupata samaki, matumbawe yanabomoka na kupoteza uhai, hivyo kupoteza viumbe bahari ambao hupendelea kukaa kwenye miamba hiyo wakifuata chakula pamoja na sehemu za kutaga mayai.
Utalii usiofuata utaratibu, ikiwemo watalii kukanyaga matumbawe, kupiga mbizi bila mwongozo, na boti kutia nanga juu ya miamba pia huharibu miamba. Maendeleo ya pwani kama ujenzi wa hoteli, barabara, na miundombinu huongeza mmomonyoko wa ardhi na kusababisha udongo kuingia baharini na kufunika matumbawe, jambo linalozuia mwanga wa jua kuyafikia matumbawe na kusababisha yapoteze rangi yake.
Aidha, ripoti ya Western Indian Ocean Marine Science Association (WIOMSA) ya mwaka 2024 inaonyesha kuwa mifumo mingi ya matumbawe katika pwani ya Tanzania inakaribia kufikia viwango vya uharibifu visivyorekebishika, (uwezo wake wa kuishi ni chini ya asilimia 10) kutokana na kuongezeka kwa joto la bahari kunakohusishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Katikati ya mashaka hayo, Mgaya anasema matumaini ya kuokoa rasilimali hiyo bado yapo. Anasema iwapo kutakuwa na usimamizi bora wa rasilimali za bahari, ikiwa ni pamoja na utaratibu wa kupumzisha mwamba, matumbawe ambayo yako katika hatari ya kutoweka yanaweza kuokolewa.
Kupumzisha mwamba ni kitendo cha kusimamisha shughuli za uvuvi kwenye eneo la miamba ya matumbawe kwa miezi mitatu ili kuruhusu samaki kuzaliana kwa wingi na mifumo ya ikolojia, ikiwemo ya matumbawe iliyoharibika kutokana na ongezeko la nyuzi joto kwenye maji na uvuvi haramu, kurejea katika hali yake.
Kuharibika kwa miamba
Kwa mujibu wa Mgaya, matumbawe yanapoharibika huathiri ikolojia ya bahari na kusababisha uhaba wa samaki, kwa sababu viumbe bahari huishi kwa kutegemeana. Akifafanua hilo, anasema: “Matumbawe hutegemea kupata chakula kutoka kwa mwani, samaki nao hutegemea matumbawe kama sehemu ya kupata chakula na makazi wakati binadamu hutegemea matumbawe kupata samaki kwa ajili ya chakula”.
Kutokana na hilo anasema: “Ukibomoa matumbawe unaharibu kule kutegemeana na thamani ya hilo eneo inapotea, kwa sababu mwani yanatakiwa yapate pa kushika, wadudu wapate chakula, mimea ipate jua na matumbawe yasifunikwe na mimea na yapate mwanga wa kutosha na hatimaye samaki wapate chakula na binadamu wapate samaki”.
Anasema kuharibika kwa matumbawe pia huathiri shughuli za utalii wa bahari na kuikosesha nchi fedha kwa sababu watalii wanavutiwa kuona mfumo mzima wa ikolojia, yakiwemo matumbawe hai yenye rangi nzuri pamoja na viumbe bahari.
Aidha Mgaya anasema matumbawe yanapoharibika huongeza hatari ya mafuriko katika fukwe za bahari. Hii ni kwa sababu matumbawe hupunguza kasi ya mawimbi makubwa ya bahari kupiga moja kwa moja na kuharibu kingo za bahari.
“Matumbawe yanapokosekana, maji kutoka baharini husababisha makazi yaliyopo karibu kusombwa, mali kuharibiwa, mambo ambayo huathiri uchumi unaotokana na uwekezaji katika fukwe kama hoteli,” anasema.
Anasema kupumzisha mwamba kunaweza kutekelezwa kwa kufuata sera, kanuni na sheria za nchi zinazosimamia uhifadhi wa bahari, ikiwemo Sheria ya Uvuvi Na.22 ya Mwaka 2003, Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009, ambazo zinatoa miongozo mbalimbali inayosisitiza ushirikishwaji wa jamii katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za uvuvi.
Mwendo wa takribani saa tisa, kwa kutumia usafiri wa basi na boti, kilomita 330 kutoka jijini Dar es Salaam, kinapatikana kisiwa cha Songosongo, kilichopo katika Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi. Takribani asilimia 80 ya wakazi 9,000 wa eneo hili wanategemea uvuvi kama njia kuu ya kujipatia kipato.

idha, kwa kipindi cha miaka 20, hali ya kiuchumi haikuwa nzuri kutokana na uhaba wa samaki uliochangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mfumo wa ikolojia ya bahari, ikiwemo matumbawe.
Uvuvi endelevu
Hata hivyo, miaka 10 iliyopita, mambo yalibadilika na matumaini ya kurejesha hali ya kiuchumi kupitia uvuvi yakarejea. Mabadiliko haya yametokana na utekelezaji wa mpango wa uvuvi endelevu ambao lengo kuu ni kurejesha na kuhifadhi ikolojia ya bahari hasa matumbawe kwa kufunga mwamba kwa miezi mitatu.
Utaratibu huo unatekelezwa kupitia mfumo wa usimamizi shirikishi wa uvuvi nchini Tanzania uliowekwa chini ya Sheria ya Uvuvi Na.22 ya mwaka 2003, inayotambua BMUs kama taasisi za kijamii zenye jukumu la kusaidia usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi.
Kwa mujibu wa Mgaya, eneo la bahari linapofungwa kufanyika shughuli za uvuvi kwa muda, huruhusu samaki waliopo kufikia ukubwa wa kuzaliana. Samaki wakubwa huzalisha mayai mengi na yenye ubora zaidi, hivyo kuongeza uzalishaji wa kizazi kipya.
Wakati huo huo, kutokuwepo kwa usumbufu kutoka kwa binadamu kunaruhusu makazi ya samaki kama vile matumbawe na nyasi bahari yaliyokuwa yanaelekea kufa kupona, na hivyo kuboresha upatikanaji wa chakula na maeneo ya kujificha kwa samaki wachanga, jambo linaloongeza kiwango cha kuishi.
Anasema kadri msongamano wa samaki unavyoongezeka ndani ya eneo lililofungwa, samaki huzidi uwezo wa eneo na kuhamia nje kwenye maeneo mengine, hivyo kuongeza mavuno kwa wavuvi wanaozunguka eneo hilo.
Wavuvi takribani 1,000 wa Songosongo kwa sasa wanapofungua mwamba wanavua hadi tani 45 za pweza na mauzo yake huwapatia zaidi ya TSh245.5 milioni ($98,000) ndani ya siku tatu tu za mavuno, fedha ambazo miaka 10 iliyopita kupata kiasi hicho ilikuwa ni ndoto.
Kwa kipindi cha nyuma, mvuvi mmoja alikuwa akivua pweza wasiozidi kilo moja kwa siku akiuza kwa TSh2,000 ($0.8), na hivyo kupata karibu TSh60,000 kwa mwezi ($24), kiasi ambacho hakikukidhi mahitaji ya msingi ya maisha.
Akizungumza na Mongabay, Mwenyekiti wa BMU ya Songosongo anasema safari ya kufunga mwamba ilianza mwaka 2015 baada ya shughuli za uvuvi kuzorota kutokana na kupungua kwa samaki baharini kwa asilimia 90.
Kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji cha Songosongo na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, wavuvi wa Songosongo walifanya utafiti kwa kuzamia baharini na kugundua kuwa uvuvi wa kila siku umechangia kwa kiasi kikubwa kupotea kwa samaki hasa pweza kwa sababu walikuwa wakivua wakiwa wadogo hivyo hawakupata muda wa kukua vizuri na kuzaliana.
Anasema pia waligundua kuwa uvuvi haramu umeharibu sehemu kubwa ya matumbawe katika eneo hilo na iliyobaki imekuwa dhaifu kutokana na joto la maji kuongezeka, hali iliyosababisha uzalishwaji wa samaki hasa pweza kupungua.
“Hapo ndipo tulijifunza kuwa tunahitaji kuwa na utaratibu mzuri wa uvuvi ili kuwapa samaki muda wa kukua na kuzaliana. Kutokana na utafiti wetu, tuligundua kuwa pweza huhitaji takribani miezi mitatu kuzaliana na kukua hadi kukomaa, na tulishirikisha jamii taarifa za matokeo ya utafiti wetu,” anasema

Kwa mujibu wa Hassan, baada ya kugundua tatizo walianza kutafuta njia bora ya uvuvi endelevu ndipo lilipowatembelea na kuwapa mafunzo ya kufunga mwamba na kuwapeleka baadhi ya wavuvi na viongozi wao Zanzibar kwa ajili ya kujifunza mbinu hiyo.
Kufunga mwamba
Kwa mujibu wa Hassan, walianza kufunga mwamba mwaka 2017 bila ya ufadhili wowote. Walichagua mwamba mmoja mkubwa kati ya 24 iliyopo katika eneo hilo, wakaunda kamati ya ulinzi iliyojitolea kulinda mwamba usiku na mchana kwa miezi mitatu walioufunga. Ni wavuvi 300 tu kati ya 800 ndio waliokubali kuingia katika programu hiyo wengine wakihofu kwamba mpango huo hautakuwa na manufaa kwao.
Walipoufungua mwamba baada ya siku 90, kwa mara ya kwanza walivua jumla ya tani tisa, ambapo aliyevua samaki wengi alipata kilo 100 huku aliyevua kidogo akipata kilo 60, jambo ambalo siku za nyuma kabla ya programu hiyo, lisingewezekana.
“Kabla ya kuanza utaratibu wa kufunga mwamba, kwa siku mvuvi alikuwa akipata kilo moja au hapati kabisa, hata pweza au samaki wengine waliowavua walikuwa wadogo. Lakini siku ambayo mwamba unafunguliwa, mvuvi aliyevua sana anapata shilingi milioni mbili ($800) wakati aliyevua kidogo anapata Sh.200,000 ($80).
“Wavuvi wengi walihamasika na matokeo hayo lakini pia Shirika la kimataifa la Blue Ventures walivutiwa na mwaka 2019 wakaingia mkataba wa kutoa fedha kwa ajili ya usimamizi wa rasilimali za bahari. Fedha hiyo ilitumika katika ulinzi wa mwamba, kulipa wafanya doria za kustukiza, kuendesha vikao vya BMU na kutoa elimu kwa wavuvi kuhusu uvuvi endelevu,” anasema Hassan.
Anasema tangu kuwepo kwa ushirikiano na Blue Ventures, usimamizi wa shughuli za kufunga mwamba unakwenda vizuri na samaki wamekuwa wakiongezeka kila mwaka. Anatoa mfano wa Aprili mwaka 2025, ambapo anasema walifunga mwamba na kuufungua mwezi Juni na katika kipindi hicho walipata tani 45 na kilo 300 za pweza. Aliyevua pweza wengi alipata kilo 500 wakati aliyevua kidogo, alipata kilo 60.
Anasema kilo moja ya pweza wanaiuza kwa TSh5,500 ($2.11), kati ya hizo, TSh500 ($0.19) wanalipa kwa BMU, TSh500 ($0.19) zinalipwa kwa wachuuzi na TSh4,000 ($1.53) anabaki nayo mvuvi. Kimahesabu aliyevua kilo 500 atabaki na TSh4 milioni ($1,531.1) wakati aliyevua kilo 60 atabaki na TSh280,000 ($107.1).
Kwa mujibu wa Hassan, pesa wanazochanga kwa BMU zinatumika katika usimamizi wa rasilimali za bahari, ikiwemo ulinzi wa bahari kuhakikisha, wavuvi hawavui samaki kipindi cha maji madogo, kudhibiti uvuvi haramu na pia kusaidia jamii.
“Mfano tulipofungua mwamba mwezi Juni 2025, BMU tulikusanya TSh22.5 milioni. Tulizigawanya katika shughuli za ulinzi wa bahari, lakini pia tumeanzisha utaratibu wa kulipia chakula cha wanafunzi shuleni na tunawanunulia akina mama wanaolima mwani vifaa kama maboya, vijiti na boti za uvuvi,” anasema Hassan.

Ally Tumbwili, mvuvi wa pweza katika BMU ya Songosongo anasema tangu kuingia katika mpango wa kufunga mwamba mwaka 2017, hali yake ya kiuchumi imeboreka kwa kuwa anapata pesa za kutosha kwa mkupuo ambazo hakuwahi kupata siku za nyuma.
Zuhura Kigugila, anasema kupitia mpango wa kufunga mwamba anapata pweza wengi katika maji mafupi kwa sababu wanakuwa wamezaliana na kuzagaa kwa wingi. Anasema awali alikuwa anapata samaki wachache kwa kuwa hakuweza kuchokoa pweza kutoka kwenye kina kirefu cha maji.
Zuhura anatoa ushuhuda kuwa siku ya kufungua mwamba anavua hadi kilo 60 za pweza wakati kwenye miamba ambayo haijafungwa huwa anapapa pweza mmoja au wawili tu ambao hawazidi kilo moja .
Anasema pesa anayoipata kwa mkupuo anaitumia kuboresha kilimo cha mwani na katika mavuno ya mwezi Juni mwaka 2025, alipata TSh300,000 ($114.8) ambazo aliitumia kununua mashine ya kuchakata mwani ambayo anaitumia kutengeneza unga wa mwani.
Mpango wa kufunga mwamba haunufaishi wavuvi tu, bali hata jamii ya ebeo hilo. Mwenyekiti wa Kijiji cha Songosongo, Hamza Saidi, anasema kuwa serikali ya Kijiji hicho inapokea mgawo wa Sh.50 kwa kilo moja ya pweza, na kwamba kwa jumla hukusanya TSh1,000,000 ($382.78) hadi TSh1,500,000 ($574.16) kutengemea na msimu.
Hamasa kutoka Madagaska
Japhet Mwanan’gombe, Mratibu wa Mahusiano kutoka Shirika la Blue Ventures, anasema kuwa wamejifunza kuhusu kufunga mwamba kutoka nchini Madagaska ambao walianza kutekeleza programu hiyo tangu mwaka 2006.
“Madagaska walianza mwaka 2006, walihamasisha wananchi na baada ya muda wakaona matokeo mazuri, na sisi tukaona ni vyema tuulete huku mpango huu na sasa Songosongo imekuwa ni mfano wa kuigwa… hakuna eneo lolote katika ukanda wa bahari ya Hindi waliowahi kuvuna tani 40 kwa siku,” anasema
Anasema miradi hiyo pia inatekekelezwa katika nchi za Kenya, Msumbiji, Indonesia lakini wanajivunia matokeo makubwa wanayopata Songosongo.
Aidha Mwanan’gombe anasema kuwa waliamua kuipatia Songosongo fedha za kuendesha fungamwamba kwa sababu waliona kuwa kile wanachofanya kina umuhimu mkubwa kwa uhifadhi wa bahari, moja ya malengo wanayoyafanyia kazi.
“Tulianza kwa kutoa elimu na kuwasimamia kuhakikisha kwamba wanatumia Sheria ya Uvuvi Na.22 ya Mwaka 2003, Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009, kutengeneza BMU, wakawasimamia kuchagua viongozi wakizingatia usawa wa kijinsia kisha wakatafuta ofisi na kufungua akaunti ya benki, anasema Mwanan’gombe.
Anasema pia waliwapa fedha za usimamizi wa shughuli za bahari kama vile kuimarisha ulinzi wa mwamba unaofungwa, kudhibiti uvuvi haramu na kutoa elimu juu ya mbinu na umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali bahari.
Ili kufanya maamuzi sahihi na kuendelea kuboresha mbinu zao za usimamizi, Mwanan’gombe anasema waliisimamia BMU hiyo kuanzisha kitengo cha ukusanyaji wa takwimu ikiwamo mabadiliko katika ikolojia ya bahari.
“Pamoja na hayo tumewapatia pia boti ya kufanyia doria, tunawalipa walizi pesa kwa ajili ya kufanya ulinzi wa mwamba na kuweka mipaka kwenye mwamba uliofungwa, pia tumekuwa tukiwapa pesa za kuendesha vikao mbalimbali,” anasema.
Anasema mikakati hiyo imeleta matokeo chanya katika upatikanaji wa pweza kwani kwa sasa wanavua pweza mwenye uzito wa kilo moja na zaidi, kinyume na miaka tisa nyuma walipokuwa wakivua hadi pweza mwenye uzito wa gramu 250 kinyume cha sheria ya uvuvi ambayo inaelekeza kuvua pweza mwenye kilo moja.
Ushiriki wa Serikali
Ulimboka Ndile, Ofisa Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, anasema katika kuhakikisha usimamizi wa rasilimali za bahari haurudi nyuma, halmashauri imewapa BMU ruhusa ya kuchukua asilimia 2 ya mapato yake yanayotokana na shughuli za uvuvi.
“Kwa mfano kunapofanyika minada ya pweza, au shughuli za utalii, kodi ya halmashauri itakayokusanywa, asilimia 2 inachukuliwa na BMU husika kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa bahari,
Mradi wa kufunga mwamba Songosongo umeleta hamasa kubwa kwa wavuvi wa wilaya za Kilwa na Lindi na kuwavuta kwenda kujifunza na kuanzisha programu kama hizo katika maeneo yao.
Salehe Juma, Katibu wa BMU ya Magengeni, katika eneo la Kilwa Kivinje, wilayani Kilwa anasema walivutiwa na matokeo ya programu ya funga mwamba katika BMU ya Songosongo na mwaka 2023 wakatuma wajumbe wawili wa bodi kwenda kujifunza, ambapo walirudi na ujuzi na kuwafundisha wengine. Anasema walianza na wavuvi 800.
Ibran Mikidadi, Katibu wa BMU ya Ruvu, Manispaa ya Lindi anasema kwa kipindi cha miaka miwili ya kufunga mwamba maisha ya kiuchumi ya wavuvi yameimarika kiasi cha kumaliza kabisa tatizo la uvuvi haramu.
“Wavuvi wengi wameona faida ya kufunga mwamba na wameona matunda ya uvumilivu wa miezi mitatu. Kabla ya kufunga mwamba tulikuwa tukirekodi matukio mawili hadi matatu ya uvuvi haramu wa kutumia baruti kwa mwezi lakini sasa hatuna matukio hayo” anasema
Ikolojia ya bahari
Licha ya kuboresha maisha ya wavuvi, mradi wa kufunga mwamba unaelezwa kurejesha ikolojia ya bahari iliyokuwa imeharibiwa kutokana na uvuvi bila kupumzika.
Mwenyekiti wa BMU ya Songosongo, Ally Hassan anasema kwa kipindi cha miaka tisa waliotekeleza utaratibu wa kufunga mwamba, wameshuhudia uoto wa asili ukirejea ikiwemo matumbawe na idadi ya samaki ikiongezeka.
Anasema katika eneo la mwamba wanaolifunga, afya ya matumbawe imerejea, yale matumbawe ambayo yalikuwa yameharibiwa na uvuvi haramu yamerejea katika ukubwa wake na yamekuwa na rangi ya kuvutia.
Salehe Juma, Katibu wa BMU wa Magengeni, anasema jinsi ikolojia ya bahari katika mwamba wanaovua inavyoimarika ndivyo upatikanaji wa samaki unavyoongezeka.
Ofisa Uvuvi kutoka Tarafa ya Mchinga, Manispaa ya Lindi, Sharifa Tomela anasema mpango wa upumzishaji wa miamba ya bahari umekuwa na matokeo chanya kwa kuongeza idadi ya viumbe wa baharini, hasa samaki waliokuwa wakivuliwa wakiwa bado wadogo.
Alisema serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuwawezesha wavuvi kiuchumi kwa kuwahamasisha kuunda vikundi vitakavyowawezesha kupata mikopo ya vifaa vya uvuvi kama boti, pamoja na kuhamasisha shughuli mbadala kama ufugaji wa samaki, majongoo bahari na kaa.

Tomela pia alitaja juhudi nyingine za uhifadhi wa mazingira zinazofanywa kuwa ni pamoja na upandaji wa mikoko ili kupunguza athari za mmomonyoko wa ardhi na majanga ya asili kama vimbunga. Aidha, alisema kuwa wavuvi wameanza kujiunga katika makundi yanayorahisisha upatikanaji wa taarifa za mabadiliko ya tabianchi kwa wakati.
Changamoto
Licha ya faida zinazopatikana, ukosefu wa raslimali za kutosha unaelezwa kuwa miongoni mwa mambo yanayorudisha nyuma juhudi za kuhifadhi ikolojia ya bahari hasa matumbawe kupitia mpango huo.
Mwenyekiti wa BMU ya Songosongo, Ally Hassan anataja changamoto nyingine kuwa ni uwepo wa kundi la wavuvi wasio waaminifu wanaoingia na kuvua pweza wakati wa usiku, hali inayochangia uwepo wa mavuno hafifu siku ya kufungua mwamba.
Aidha anasema ukosefu wa fedha za usimamizi wa kufunga mwamba ni changamoto nyingine kwani ulinzi wa mwamba unahitaji takribani TSh 24 milioni ($9186.60) kwa miezi mitatu, pesa ambayo ni ngumu kuipata hasa kwa wanaoanza kutekeleza mpango huo. Hali hiyo anasema imesababisha wafunge mwamba mmoja tu kati ya 24 iliyopo, hali ambayo inarudisha nyuma lengo lao la kuhifadhi ikolojia ya bahari.
Uhaba wa vitendea kazi nao umetajwa kama kikwazo katika mradi huo. Katibu wa Kamati ya Usimamizi wa Uvuvi (BMU) Pwani ya Ruvu, Ibran Mikidadi, anasema uhaba wa vitendea kazi, hasa boti za kufanya doria baharini ni kikwazo, hasa katika kukabiliana na wavuvi wanaoingia katika mwamba uliofungwa na kuvua samaki pamoja na wavuvi haramu.
“Kwa kuwa sisi bado ni wageni katika mpango huu, tunaiomba serikali na wadau wengine wa maendeleo kutusaidia ili tuweze kufanya doria kwa ufanisi zaidi,” alisisitiza.
Akizungumza katika uzinduzi wa Meli ya kwanza ya uvuvi wa Bahari Kuu Aprili 25, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari serikali inaendelea kuimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na mamlaka nyingine za serikali ili kutokomeza uvuvi haramu usifuata sheria na unaoharibu mazingira na uhai wa viumbe bahari.
Alisema Serikali pia inaendelea na mchakato wa kununua meli za uvuvi na kutoa mafunzo ili kujenga uwezo wa taifa kushiriki kikamilifu katika uvuvi wa bahari kuu na kuimarisha mafunzo na tafiti za kitaalam, kuhakikisha rasilimali za bahari na maziwa zinasimamiwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi endelevu.
Aliielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwasaidia wavuvi wadogo kwa mitaji na vifaa vya kisasa ili kuwainua kiuchumi pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa fedha.
Rais pia aliiagiza wizara hiyo kuimarisha mikakati ya kudhibiti uvuvi haramu ili kuwapo na uvuvi endelevu wenye tija na manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Picha ya Bango:Wavuvi kutoka BMU ya Songosongo wakiuza samaki aina ya pweza waliowavuna siku ya kufungua mwamba.Picha kwa hisani ya Blue Venture.