- Sheikh Ibrahim Lethome anaeleza jinsi mafundisho ya Kiislamu yanavyoweza kutumika kuhamasisha utunzaji wa mazingira, akisisitiza kuwa kulinda mazingira ni sehemu ya ibada na sadaka.
- Lethome alikuwa sehemu ya juhudi za kupinga mradi wa mtambo wa umeme wa makaa ya mawe wa Lamu, akisaidia kuhamasisha jamii kuhusu athari zake za kimazingira na kijamii hadi mradi huo kusitishwa mwaka 2025.
- Anasema changamoto kubwa katika uhifadhi wa mazingira ni umaskini, rushwa na tamaa, ambazo husababisha ukataji miti, uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa rasilimali kwa manufaa ya wachache.
- Kupitia GreenFaith Afrika na Msikiti wa Jamiah, Lethome anaendeleza kampeni za kupanda miti, usafi wa mazingira, mafunzo kwa maimamu na matumizi ya majukwaa ya kidini kuhamasisha hatua za vitendo za kulinda mazingira.
Mwezi Machi mwaka huu wa 2026 ulikuwa na shughuli nyingi, hasa kwa upande wa dini. Waislamu pamoja na baadhi ya waumini wa Kikristo walikuwa katika vipindi vya mfungo wa Ramadhani na Kwaresima, ambavyo vilihitimishwa kwa sikukuu za Iddi el-Fitri na Pasaka, mtawalia. Mwezi huohuo, Kenya ilikumbwa na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko na vifo vya watu zaidi ya 82.
Mongabay ilimtembelea Sheikh Ibrahim Lethome alipokuwa kwenye mfungo wa Ramadhani ili kupata maoni yake kuhusu juhudi zake katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
Lethome amejitaja kuwa aliyetekeleza kile ambacho huenda kilionekana kama jukumu dogo katika juhudi za kupinga mradi wa umeme wa makaa ya mawe huko Lamu, Kenya. Juhudi hizo ziliongozwa na viongozi wa Save Lamu pamoja na wawakilishi wa jamii, mawakili wa masuala ya mazingira, wanaharakati na taasisi za serikali pamoja na mamlaka za udhibiti kama NEMA na mahakama za mazingira. Hatimaye, mradi huo ulisitishwa Desemba mwaka 2025.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano yake na Lynet Otieno wa Mongabay, yaliyofanyika katika ofisi za Msikiti wa Jamiah jijini Nairobi.
Mongabay: Tafadhali tueleze kwa ufupi wewe ni nani, kama msomi, kiongozi wa kidini na mwanaharakati wa mazingira.
Lethome: Mimi kitaaluma ni mwanasheria na msomi wa elimu ya Kiislamu. Ninafanya kazi katika fani zote mbili. Nimekuwa mwanachama wa Msikiti wa Jamiah kwa miaka 32 sasa. Ninaongoza Idara ya Dini. Pia ni mwanachama wa bodi ya kimataifa ya GreenFaith, na mwenyekiti wa bodi ya GreenFaith-Afrika, taasisi inayotumia mafundisho ya dini kuhamasisha uhifadhi wa mazingira.
Mwelekeo wangu ni kuangalia jinsi mafundisho ya dini yanavyoweza kutumika kushughulikia changamoto nyingi ambazo binadamu wanakabiliana nazo. Ninaamini kwamba Mungu hakutupa dini kwa ajili ya kwenda mbinguni tu, bali kwanza tufanye dunia hii kuwa mahali bora zaidi.
Mongabay: Unaizungumziaje safari yako kama msomi na kiongozi wa kidini anayejikita katika masuala ya mazingira?
Lethome: Nimekuwa nikiona watu kutoka makundi mbalimbali wakikusanyika kujadili changamoto kama mabadiliko ya tabianchi, na nikajiuliza kama inawezekana kupata suluhisho la tatizo hili kupitia dini. Nilikuwa nikitafuta nafasi ya kueleza hilo. Fursa ya kwanza ilikuja nilipojiunga na Baraza la Maimamu na Mashirika ya Dini Kenya (Inter-Religious Council of Kenya – IRCK). Walikuwa na idara ya mazingira.
Huo pia ndio wakati ambapo mradi tata wa mtambo wa umeme wa makaa ya mawe huko Lamu ulipendekezwa. IRCK, kupitia Kamati ya Mazingira iliyoongozwa na Sujatha Kotamraju wakati huo, ilikuwa kinara wa kampeni ya kupinga mradi huo wa makaa ya mawe.

Tulizunguka sehemu mbalimbali za nchi kuhamasisha watu kuyafanya mazingira yao yawe ya kijani, kama sehemu ya ibada. Nilivutiwa sana na mafundisho mengi ya dini yetu yanayohimiza uhifadhi wa mazingira. Uislamu unafundisha kwamba ukiona jambo linalodhuru, una wajibu wa kulibadilisha, ama kwa kutumia mikono yako au kwa kutumia kauli yako. Kama huwezi kufanya moja kati ya hayo mawili, basi chukia uovu huo. Hicho ndicho kitu ambacho muumini anatarajiwa kukifanya.
Angalia utofauti wa kidini; Wakristo, Waislamu, Wahindu na dini nyingine zote, wote wanaishi kwenye mazingira yale yale. Mimi huyaita mazingira kuwa ni kiunganishi cha wanadamu wote. Hivyo, kuzungumzia mazingira ni fursa ya kuleta dunia pamoja, bila kujali dini zetu.
Katika mikutano ninayohudhuria, huwa nawauliza kama miti tunayopanda ina dini. Miti ni miti tu! Haina tofauti ya kidini. Oksijeni tunayovuta inatuunganisha sote! Hakuna oksijeni ya Kiislamu, Kihindu au Kikristo. Vivyo hivyo, athari za mabadiliko ya tabianchi hazichagui kama wewe ni Mkristo au Mwislamu.
Mongabay: Unasema ulishiriki kikamilifu katika kampeni dhidi ya mradi wa mtambo wa umeme wa makaa ya mawe wa Lamu. Ni mchango gani unaujivunia zaidi?
Lethome: Nafurahi kwamba sisi (timu ya IRCK) hatukuishia tu kuzungumza, bali pia tulichukua hatua. Tulikwenda Mui Basin, Kitui, kwa sababu huko ndiko watu waliokuwa wakihamishwa ili kupisha mradi wa Lamu walitarajiwa kupelekwa na kulipwa fidia ya ardhi iliyopotea. Tulihamasisha jamii kutokubali watu wapya kuhamia eneo hilo. Kisha tulikwenda Lamu na kuzungumza na jamii ya huko, baadhi yao wakiwa maskini sana na wasio na uelewa wa kina. Katika moja ya kaya tulizotembelea, tuliuliza kama wanajua kuwa mtambo wa makaa ya mawe ungetengenezwa hapo. Mmoja wao alisema: “Ndiyo, ninafurahi kwa sababu nitapata fidia ya ardhi yangu na nitaweza kuishi katika mji mkubwa ambako nitaona magari.” Walikuwa na uelewa mdogo kiasi kwamba kuona magari ilikuwa jambo kubwa sana kwao. Tulieleza athari ambazo mradi wa makaa ya mawe ungeleta kwao. Walikubali ushauri wetu. Ninajivunia kwamba tulichukua hatua hiyo.
Mongabay: Ni tukio gani baya au uzoefu upi mbaya uliopitia katika harakati zako za utunzaji wa mazingira?
Lethome: Kesi ya Lamu ndiyo ilikuwa mbaya zaidi kwangu, kwa sababu ilihusisha vitisho. Siku moja tulipokuwa tukirudi kutoka Lamu, tulikumbana na askari wa kikosi cha wanamaji (Navy). Walifikia hatua ya kumpiga kofi nahodha wa boti yetu. Kulikuwa pia na majaribio ya kutushawishi na kutuhonga. Tulipewa safari za kwenda Uturuki ili tuone mtambo wa umeme wa makaa ya mawe unaodaiwa kuwa rafiki wa mazingira.
Huu ulikuwa uzoefu wangu mbaya zaidi kwa sababu ulikuwa wa moja kwa moja. Lakini ninafurahi kwamba tuliweza kuwaokoa watu wa Lamu, Bonde la Mui, na Wakenya, na pia tulitekeleza kitendo cha ubinadamu kwa ujumla. Ninaamini kwamba ni jambo linalompendeza Mungu kwamba tulifanya tulichokifanya. Katika Uislamu, dini si tu uhusiano kati ya mtu na Mungu au wanadamu wenzake, bali pia na viumbe vingine. Kupitia matendo yetu, wanyama, wakiwemo viumbe wa baharini ambao wangeathirika, waliokolewa. Nahisi kwamba Mungu ameridhika nasi.

Mongabay: Uislamu unafundisha nini hasa kuhusu utunzaji wa mazingira na binadamu kama makhalifa?
Lethome: Kwanza kabisa tunajua, kwamba Mungu alituumba sisi na viumbe wengine wote. Alitupa mamlaka juu ya viumbe hivi vyote. Mungu anasema katika Qur’ani: “Hakika nimeumba mwanadamu kuwa khalifa wangu katika ardhi hii”. Tuna wajibu kama wasimamizi wa viumbe vyote. Pia tunajua kwamba dini ina malengo mawili; kuleta yale yaliyo mema duniani. Tunaita Maslaha. Pia inapaswa kuzuia yale yaliyo mabaya. Hivyo, kati ya mambo haya mawili, ninaamini kwamba pamoja na mafundisho mengine, Uislamu unatutaka kuhakikisha tunafanya dunia hii kuwa mahali bora, kama sehemu ya ibada.
Zaidi ya viumbe wengine wote, Mungu alitupa akili. Nguvu yetu haipo katika nguvu za mwili au ukubwa wetu, bali katika akili tuliyopewa na Mungu ya kutofautisha mema na mabaya. Katika Uislamu, lengo la uumbaji ni kumwabudu Mungu. Dhana ya ibada ni pana sana; chochote unachofanya kinachompendeza Mungu ni ibada. Hivyo basi, je, kulinda mazingira kunampendeza Mungu? Jibu ni ndiyo. Hivyo ni aina ya ibada. Tuna wajibu wa kuacha kile kisichompendeza Mungu.
Pia katika Uislamu, unapopanda kitu, huhesabiwa kama sadaka, kwa sababu kiumbe chochote cha Mungu kinaweza kunufaika nacho, iwe ni kivuli kwa mnyama au makazi kwa ndege. Hivyo, kulinda mazingira ni sadaka. Kuondoa kitu kinachodhuru mazingira pia ni sadaka. Katika Uislamu, watu watatu hulaaniwa na Mungu: anayejisaidia karibu na chanzo cha maji (kwa sababu mnyama, mmea au binadamu anaweza kutaka kunywa maji hayo), anayejisaidia chini ya kivuli, na yule anayeweka kitu chenye madhara njiani kwa wengine. Kwa kifupi, tunafundishwa kulinda mazingira. Pia tunaamini kwamba Mungu aliumba dunia kwa ukamilifu. Ilikuwa na uwiano kati ya wanyama, mimea na binadamu. Tukidumisha uwiano huo, kila mmoja atakuwa na furaha.
Mafundisho mengine niliyokuwa nikitoa msikitini leo ni kuhusu ubadhirifu. Sehemu ya matatizo tunayokumbana nayo leo ni ubadhirifu. Aya moja ya Qur’ani inasema kwamba watu wabadhirifu ni ndugu na washirika wa shetani. Shetani hamshukuru Mungu kwa neema yoyote. Ukifanya ubadhirifu, wewe si mtu mwenye shukrani. Unapofanya ubadhirifu, kumbuka kuna watu wanaohitaji kile unachopoteza.
Mafundisho haya ya Uislamu yanaweza pia kufundishwa kwa wengine.
Tunakumbana na matatizo mengi leo kutokana na ubadhirifu na tamaa. Wakati mwingine tunataka kukusanya mali kwa kuumiza wengine na mazingira. Qur’ani inasema: “Hakuna hata mmoja wenu atakayehesabiwa kuwa muumini mkamilifu mpaka awe na uwezo wa kumtakia mwenzake apate kile anachokipenda yeye mwenyewe”. Kwa mfano, kama una kiwanda kitakachokupa faida, jiulize kitawaathiri wengine namna gani, si walio hai tu leo bali hata vizazi vijavyo. Huwa ninatumia neno hili kujenga hoja kwamba hatuhitaji kuwa na au kutumia zaidi ya mahitaji yetu.
Pia kuna mafundisho ya Qur’ani yanayosema: “Kwa Mungu, si muumini! Kwa Mungu, si muumini! Kwa Mungu, si muumini! Yule ambaye jirani yake hahisi usalama kutoka kwake”. Ikiwa ninafanya kitu kinachotishia watu wengine, basi mimi si muumini wa kweli.
Ninaamini dini siyo tu kuhusu kwenda mbinguni. Mbingu itakuja yenyewe, lakini inategemea jinsi unavyoishi duniani, katika uhusiano wako na Muumba wako, binadamu wenzako na viumbe wengine wote. Hatimaye, unaishi vipi na mazingira? Mungu aliviumba kwa makusudi. Jinsi unavyohusiana na dunia huamua uhusiano wako na Mungu, na hatimaye huamua hatima yako.
Mongabay: Ni hatua zipi mashirika ya kidini yanaweza kufanya kwa vitendo ili kuhakikisha ulinzi wa mazingira unakuwa endelevu?
Lethome: Tunahitaji kuangalia upya madhumuni ya dini. Mafundisho yapo kwenye vitabu vitakatifu, lakini tunayapuuza. Tunapaswa kutumia majukwaa yenye nguvu ya kidini tuliyonayo. Tunapohubiri kuhusu mbingu, lazima pia tuweke msisitizo sawa kuhusu umuhimu wa kuishi kwa namna inayolinda mazingira. Tuitumie mifumo ya kidini kuwafundisha waumini kwamba kutunza mazingira ni sehemu ya ibada. Pia tunahitaji kuhamasisha wafuasi wetu kuchukua hatua za vitendo kulinda kile ambacho Mungu ametupatia katika mazingira, kurejesha tulichoharibu na kuepuka uharibifu zaidi. Tunaweza pia kutumia fursa za matukio ya kidini.
Kwa mfano, kama sehemu ya kuadhimisha Ramadhani, tunaweza kuchagua kutenga siku kwa ajili ya kupanda miti, kusafisha taka au kusafisha Mto Nairobi. Hivi ndivyo tunavyofanya. Tunahimiza watu kupunguza tamaa na tabia ya ubadhirifu pamoja na kuendeleza ushirikiano. Katika mwezi huu wa Ramadhani, tumetambua familia 2,000 ambazo tutazipelekea vyakula vilivyotolewa na familia zenye uwezo. Tunahamasisha kugawana rasilimali. Ili kuwafikia wengi, kila Ijumaa huwa ninaandika makala kwenye magazeti kuhusu mazingira.
Mongabay: Ni juhudi gani nyingine za uhifadhi ambazo umewahi kushiriki?
Lethome: Elimu ya upandaji miti mashuleni, kuwafundisha wanafunzi kwamba usafi ni sehemu ya imani na ibada. Sasa hivi tunawahamasisha maimamu watenge baadhi ya hotuba zao za Ijumaa kwa ajili ya mazingira. Mwezi mmoja uliopita tulikuwa na warsha kwa maimamu kuhusu namna ya kuandaa hotuba zao za Ijumaa. Tumefanya hivyo Nairobi, na sasa tunaendeleza hili kwenye maeneo mengine. Tunachukua idadi ya maimamu kutoka misikiti muhimu katika kila kaunti, kisha tunawafundisha kupitia warsha.
Mongabay: Je, mnaona matokeo gani?
Lethome: Tunakumbana na changamoto. Baadhi ya watu hawataki kuliona hili kama wajibu. Kuwafikia walengwa wetu si rahisi; tunahitaji kujenga kundi kubwa zaidi la wasomi watakaojitolea kwa masuala ya mazingira. Katika jamii, hasa zile za maeneo kame na ukame wa wastani, ni vigumu kuwashawishi watu kutunza miti wakati kwao mti huo ni chanzo cha haraka cha kipato, wakiukata na kuutumia kutengeneza mkaa. Huo unaweza kuwa ndiyo chanzo chao pekee cha mapato. Hivyo, umaskini ni adui. Wakati watu wanakosa mahitaji ya msingi, hugeukia mazingira kwa ajili ya kuishi. Hapo unakuta mti wa miaka 50 ukikatwa ili kutengeneza mifuko michache ya mkaa, ambayo kila mfuko huuzwa kwa takribani $25 (KSh3,000).
Rushwa pia ni kikwazo. Ninatoka Kajiado. Ni eneo la ukame wa wastani. Lakini sehemu kubwa ya mkaa unaotumika Nairobi unatoka Kajiado. Je, hii ni halali? Hapana! Lakini mkaa huo unaingizwaje Nairobi? Biashara hiyo inaendeshwaje? Watu walio na mamlaka hutoa vibali vya kuharibu mazingira kwa maslahi yao binafsi. Siku nyingine niliona kwenye televisheni jinsi mtandao wa mafisadi (cartel) ulivyokamatwa. Walikuwa wanakata miti ya asili kutengeneza mkaa. Baadhi ya majengo yaliyo katika maeneo ya mito na mabonde, vibali vya ujenzi wake vinapitishwa na watu wenye mamlaka kupitia rushwa. Ni nani anaamua mahali pa kutupa taka?
Haki ya mazingira na usawa wa kijamii
Mongabay: Una maoni gani kuhusu uharibifu wa mazingira na haki za kijamii?
Lethome: Angalia, kwa mfano, uchafuzi unaotokana na viwanda. Viwanda hivyo si vya watu maskini. Matajiri ndio wanaonufaika kwa kuharibu mazingira. Maskini ndio wanaoathirika. Kajiado, kwa mfano, vumbi kutoka viwanda vya saruji linaathiri maskini, na kesi za magonjwa ya pumu zinaongezeka. Lakini wamiliki wa viwanda hivyo hawaishi karibu na maeneo hayo.
Uchafuzi unaoingia Mto Nairobi hauwaathiri matajiri kwa sababu si watoto wao wanaoogelea kwenye mto huo uliochafuliwa. Wakati mwingine maji ya Mto Nairobi, licha ya uchafu wake, hutumika kumwagilia mazao kama nduma chini ya mto. Nduma hizo huuzwa sokoni, na watu maskini hununua. Wanaochafua zaidi mazingira duniani na ndani ya nchi mara nyingi ndio wanaoathirika kidogo zaidi. Huo ndio ukosefu wa haki.

Mongabay: Ni ujumbe gani ungependa kuwapa watunga sera kuhusu usimamizi wa mazingira unaoongozwa na dini?
Lethome: Imani ni mshirika wa kimkakati katika kulinda mazingira. Kumbuka dini ina nguvu sana. Mara mtu anaposhawishika kwamba jambo fulani linatakiwa na dini yake, huwa halipingwi kirahisi. Pia lina hisia kali. Hivyo, dini, taasisi za kidini na viongozi wa dini wanapaswa kutambuliwa kama rasilimali muhimu katika juhudi za kulinda mazingira. Watunga sera pia wanaamini katika dini mbalimbali zinazowataka kulinda mazingira na kuepuka rushwa. Mamlaka ya kupambana na rushwa isingekuwa na umuhimu mkubwa kama watu wangeishi kwa kumcha Mungu. Uharibifu wa mazingira pia ungekuwa mdogo. Kama tunamcha Mungu, tutahakikisha tuna sera sahihi na tunazitekeleza bila kuathiriwa na rushwa.
Mongabay: Je, kazi yako ya uhifadhi imebadilisha mtindo wako wa maisha au tabia zako kwa namna yoyote?
Lethome: Bila shaka! Familia yangu inajua hilo. Hakuna kuharibu. Ukila, pakua kile unachoweza kumaliza. Kama huwezi kumaliza, kwa sababu yoyote ile, weka kwenye friji kwa matumizi ya baadaye. Ondoa chochote unachokiona kina madhara. Familia yangu mwanzoni ilifikiri ninaleta tu usumbufu, lakini sasa haya yamekuwa sehemu ya maisha yao. Wanahakikisha mazingira yao ni safi. Hatukati miti, hasa ile ya asili. Popote ninapokwenda na kuona mti mzuri, hujitahidi kuupanda. Mahali ninapoishi, nimebadilisha mazingira kabisa. Niliponunua kiwanja hicho, kilikuwa kama jangwa dogo. Leo, nyumba yangu haionekani kwa sababu ya idadi ya miti niliyoipanda ndani ya eneo hilo. Wakati wangu bora zaidi ni ninapokaa chini ya mti na kusikiliza ndege wakiimba juu yangu.
Mongabay: Ni nini maono yako ya muda mrefu kuhusu mazingira?
Lethome: Ni dunia ambapo viongozi wa dini wataona ulinzi wa mazingira kama sehemu ya ibada. Dunia ambapo kila mtu atatekeleza wajibu wake, hata kama mchango wake utakuwa ni mdogo kiasi gani, katika kufanikisha maono haya. Mungu aliiumba dunia hii ikiwa nzuri, na alikusudia ibaki hivyo. Tunapaswa kuilinda kama Mungu alivyoikusudia.
Picha ya bango: Sheikh Ibrahim Lethome wakati wa mahojiano na Mongabay yaliyofanyika kwenye ofisi zake za Msikiti wa Jamia jijini Nairobi. Picha na Lynet Otieno, Mongabay.