- Miongoni mwa athari kubwa za mimea vamizi ni kuua mimea asilia.
- Mimea vamizi pia huathiri wanyama walao nyasi kwa kuzuia uotaji wa nyasi zinazopendwa.
- Wafugaji hukutana mara mbili kwa wiki kung’oa mimea vamizi ili kuponya mazingira yao.
- Serikali iandae sera na mkakati wa pamoja wa kitaifa wa kudhibiti mimea vamizi.
Isaack James amesimama kimya katikati ya hifadhi ya wanyama huku akitazama nyasi ndefu zenye mchanganyiko wa rangi ya kijani kibichi na ya njano zilizonyauka kiasi. Kwa mtu wa kawaida kama Isaack, mandhari hii inavutia, lakini kwa wataalamu wa mazingira na watafiti, badala ya kuwafurahisha, mandhari hiyo inawaogopesha. Kwa nini? Hizo nyasi zilizokauka tayari zimeshambuliwa na mimea vamizi ambayo ni hatari, si tu kwa ustawi wake bali hata kwa ikolojia ya eneo hilo.
Mimea vamizi ni spishi za kigeni zinazoingia katika maeneo mapya na kuanza kukua kwa kasi na kuizidi mimea ya asili huku ikihatarisha uhai wa mimea ya asili.
Kwa mujibu wa Kituo cha Taifa cha Taarifa za Spishi Vamizi, mimea ya aina hiyo huingizwa eneo jipya kupitia njia mbalimbali; ikiwa ni pamoja na mbegu zake kushika kwenye nguo za watu wanaotembelea sehemu yenye mimea hiyo, kusafirishwa kwenye magari bila wahusika kujua, au kuingizwa katika maeneo jirani kwa matumizi mengine kama maua au malisho ya mifugo na baadaye mbegu hizo kupeperushwa na upepo hadi eneo jingine.
Watafiti kutoka Taasisi ya Tathmini ya Rasilimali (IRA) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika andiko lao “Status, Impact and Management of Invasive Alien Species in Tanzania,” wanasema mimea vamizi iligundulika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mwaka 1945 kwenye mashamba ya mkonge na baadaye kuenea kwenye karanga na migomba katika maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa andiko hilo, kutokana na ongezeko la wageni wanaotembelea maeneo yaliyoathirika, mimea vamizi iliendelea kusambaa katika maeneo mbalimbali na kuendelea kuathiri mimea asilia.

Revocatus Meney, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti Wanyamapori (TAWIRI), na Mratibu wa Mradi wa Tembo Tarangire na Ziwa Manyara, aliiambia Mongabay kuwa baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na mimea vamizi ni mifumo ya ikolojia ya hifadhi maarufu nchini, zikiwemo Ngorongoro (NCAA), hifadhi iliyopigiwa kura kuwa Kivutio Bora cha Utalii Afrika mwaka 2023 na 2025, Hifadhi za Taifa za Tarangire, Ziwa Manyara, na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Victoria Shayo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayeshughulikia Utafiti wa Wanyamapori na Ikolojia katika Mamlaka ya Eneo la Hifadhi Ngorongoro (NCAA), anasema eneo la mfumo wa ikolojia lililoathiriwa na mimea vamizi ni asilimia 47, ambapo takriban asilimia 17 ni eneo lililo ndani ya hifadhi na asilimia 30, nje ya hifadhi. Mimea mingi iliyovamia hifadhi hizo kitaalam inajulikana kama Parthenium Hysterophorus, Lantana Camara, Tagetes Minuta, Bidens Schimperri, Gutenbergia Cordifolia na Datura Stramonium.
Athari za mimea vamizi
Victoria Shayo aliiambia Mongabay kuwa miongoni mwa athari kubwa za mimea vamizi ni kuua mimea asilia. Akifafanua namna uharibifu huo unavyotokea, anasema: “Hizi spishi vamizi hushindana na mimea asilia ya eneo husika kwa kugombea maji, mwanga na hata rutuba na matokeo yake, mimea asilia inayoshindwa kupambana na mimea vamizi, hufa”.
Revocatus Meney, Mtafiti kutoka TAWIRI na Mratibu wa Mradi wa Tembo Tarangire na Ziwa Manyara, naye anasisitiza namna mimea vamizi ilivyo na athari kubwa kwa mfumo wa ikolojia wa maeneo yanayovamiwa.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Mongabay, Meney anasema tatizo kubwa katika maeneo ya Tarangire na Ziwa Manyara ni mimea inayojulikana kama “Kongwa weed” na Bidens pilosa. “Kongwa weed ina tabia ya kutambaa na hivyo kuzuia mimea mingine kuota na kumea vizuri wakati Bidens pilosa una tabia ya kutoa sumu inayozuia mimea mingine kuota na hivyo kuharibu kabisa malisho ya wanyama wanaokula nyasi.
“Mmea wa Bidens pilosa unaweza kukua hadi sentimita 150 na kwenye kivuli chake hakuna mmea mwingine unaweza kuota kwa kuwa zaidi ya kutoa sumu, pia huinyima mwanga mimea mingine. Matokeo yake, wanyama wanaokula nyasi za chini kama vile nyati, hukosa malisho kwenye maeneo hayo,” anasema.
Meney anafafanua kuwa utafiti wao unaonyesha kuwa kila kwenye Bidens pilosa 10, mimea mingine haiwezi kuzidi minne; na kwamba mmea huo una uwezo mkubwa wa kutoa mbegu kati ya 3,000 hadi 6,000, na huweza kuishi kwa miaka mitano hadi sita.
Anasema mmea huo pia hutoa kemikali za allelopathy, ambayo huathiri mimea kwa namna mbili: Kwa kuzuia mbegu za mimea mingine kuota; na kupunguza ukuaji wa mizizi ya mimea jirani.
Aidha, Meney anasema mimea vamizi pia huathiri wanyama walao nyasi kwa kuwa huzuia uotaji wa nyasi zinazopendwa na wanyama kama vile pundamilia na nyumbu. Anasema: “Nyasi laini na zenye lishe nyingi hushambuliwa na mimea vamizi na kushindwa kumea, hivyo kusababisha wanyama kukosa chakula”.
Anasema eneo kubwa la mfumo wa ikolojia ya Maasai Steppe limeathirika na mimea vamizi yenye tabia ya kuzuia mingine isiote kama vile mikungugu (acacia) na ndulele (Sodom Apple).
Kwa mujibu wa Meney, maeneo yaliyo nje ya hifadhi yameathiriwa zaidi, kwani hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa kuyalinda na mashambulizi ya mimea vamizi. Akitoa mifano halisi, Meney anasema katika eneo la mfumo wa ikolojia ya Hifadhi za Tarangire na Ziwa Manyara ni asilimia 10 tu ya eneo linaloangukia katika maeneo yaliyohifadhiwa, ambayo ni Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, Pori Tengefu la Lokisale, maeneo ya usimamizi wa wanyamapori ya Randilen na Burunge, na Pori la Akiba la Mkungunero, ambayo kwa pamoja yaunda mfumo wa ikolojia ya Maasai Steppe.
Hii inamaanisha kuwa asilimia 90 iliyobaki ni maeneo yasiyohifadhiwa na hivyo hayana uangalizi maalum wala hakuna hatua kubwa zinazochukuliwa kupambana na mimea vamizi humo.
Uvamizi wa mimea hiyo korofi katika maeneo yaliyo nje ya hifadhi una athari kubwa kwa sababu kipindi cha ukame wanyama kutoka hifadhini hutoka nje kwenda kutafuta malisho, kwa hiyo malisho yanapokuwa yameathiriwa na mimea vamizi, inaleta athari kwa wanyama pia.
“Januari hadi Mei, hifadhini huwa na upungufu wa malisho. Wanyama hutoka nje kutafuta chakula na hurejea kati ya Juni na Novemba kufuata maji hifadhini,” anasema.
Athari kwa ufugaji
Theophil Robert Mwangi ni mfugaji katika kijiji cha Vilima Vitatu kinachopakana na hifadhi ya Taifa ya Tarangire. Kwa Mwangi, adui wa mifugo yake si tu wanyama wakali kama vile simba, chui au fisi; kuna adui mpya – mimea vamizi.

Mwangi aliiambia Mongabay kuwa pamoja na maeneo ya malisho kupungua kutokana na eneo la hifadhi kupanuliwa, kuna tatizo la mimea vamizi inayozuia nyasi kuota na kukua kwa ajili ya chakula cha mifugo.
“Tatizo kubwa tulilonalo ni kuingia kwa masida, yaani mimea inayotengeneza kichaka kinachozuia nyasi kuota chini yake, ambayo mara nyingi huwa tunayang’oa na kuyakusanya ili kuyachoma,” anasema.
Mwangi anasema kuwa suala hilo limeathiri, kwa kiasi kikubwa, ustawi wa mifugo yake pamoja na ya wafugaji wengine.
Jacob Amos, Mwenyekiti wa wafugaji katika kijiji cha Vilima Vitatu, kilichopo ndani ya Mfumo wa Ikolojia ya Tarangire, aliiambia Mongabay kuwa kutokana na mimea vamizi kuongezeka katika eneo la malisho na eneo jingine karibu na Ziwa Manyara kujaa maji, tatizo kwa wafugaji limekuwa kubwa zaidi.
“Tunajitahidi kutoa elimu na kukusanyana ili kung’oa mimea hii, jambo tunalofanya mara mbili kwa wiki,” anasema.
Juhudi za Udhibiti
Akieleza juhudi zinazofanyika kukabiliana na hali hiyo, Meney anataja mbinu ya kuchoma moto na kung’oa mimea hatari kama baadhi ya njia zinazotumika.
Naye Victoria Shayo wa NCAA alisema katika kipindi cha mwaka 2025 na 2026, jumla ya hekta 652.9 za eneo lililovamiwa zilisafishwa kwa kung’oa mimea vamizi kwa mikono, kazi ambazo lengo lake lilikuwa ni kulinda udongo huku mimea vamizi ikiondolewa moja kwa moja bila kudhuru mimea asilia.
Kamishina Victoria anasema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2026/2027, NCAA imepanga kutumia TSh1 bilioni ($382,775) katika shughuli za kuondoa mimea vamizi huku ikilenga kusafisha hekta 8,000 kwa kuchoma moto na hekta 1,200 kwa kufyeka.
Aidha Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia Mazingira, ina Mkakati na Mpango Kazi wa Kitaifa wa Usimamizi wa Viumbe Vamizi (2019–2029. Mkakati huo umeweka njia kadhaa za kupambana na mimea vamizi, ukilenga kuzuia, kudhibiti na kurejesha mazingira. Njia hizo ni pamoja na kuhakikisha mimea vamizi haipati nafasi ya kuingia nchini au kuenea katika maeneo mapya; utambuzi wa mapema na majibu ya haraka, ambapo maeneo hufuatiliwa mara kwa mara ili kugundua uwepo wa mimea vamizi mapema, pamoja na udhibiti na uondoaji wa mimea vamizi katika maeneo ambayo tayari yameathirika.
Katika hali hii, mimea inaweza kudhibitiwa kwa kupunguza kasi ya kuenea kwake au kuondolewa kabisa, hasa pale inapokuwa bado imejikita kwenye eneo dogo.
Njia nyingine, kwa mujibu wa mkakati huo, ni kurejesha maeneo yaliyoharibiwa baada ya kuondoa mimea vamizi. Katika hatua hii, mimea ya asili hupandwa tena ili kurejesha uoto wa asili na kulinda udongo dhidi ya mmomonyoko, huku pia ikisaidia kuzuia kurudi kwa mimea vamizi katika eneo hilo.
Utoaji wa elimu na uhamasishaji wa jamii ambapo wananchi, hasa wakulima na wafugaji, hupewa elimu kuhusu madhara ya mimea vamizi na namna ya kuzuia kuenea kwake, ni njia nyingine iliyoainishwa katika mkakati huo. Ushiriki wa jamii katika ufuatiliaji na udhibiti unasisitizwa kama sehemu muhimu ya mafanikio ya mkakati.
Njia nyingine ni utafiti na matumizi ya teknolojia ambapo wataalamu hufanya tafiti kubaini aina mpya za mimea vamizi, mbinu bora za kudhibiti, pamoja na matumizi ya data na mifumo ya ufuatiliaji wa maeneo yaliyoathirika ili kusaidia maamuzi ya kisayansi.
Kuimarisha sera, sheria na uratibu wa taasisi mbalimbali za Serikali na wadau binafsi ili kuhakikisha kuwa kuna mfumo mmoja wa kitaifa wa kushughulikia tatizo hili kwa ufanisi, ni njia nyingine.
Kwa mujibu wa Meney, mbinu hizi za kisera zinaungana na juhudi zinazofanywa na asasi zisizokuwa za kiserikali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kupambana na mimea vamizi na kuajiri vibarua kwa ajili ya kung’oa mimea hiyo katika maeneo mbalimbali.

Jacob Amos, Mwenyekiti wa Wafugaji katika Kijiji cha Vilima Vitatu, anasema wafugaji hukutana mara mbili kwa wiki kung’oa mimea vamizi na kuichoma kwa lengo la kuiangamiza moja kwa moja na hivyo kuponya mazingira yao.
Angalizo la CAG
Juhudi za kudhibiti mimea vamizi, zimeibua maswali kuhusu gharama ambazo zingeweza kuepukwa iwapo udhibiti wa mimea vamizi ungefanywa ipasavyo.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya kipindi cha 2024/2025, inabainisha kuwa juhudi zinazofanywa kwa kung’oa, kufyeka na kuchoma hazijawa za kiwango cha kutosha na hufanywa kwa mtindo wa ‘zimamoto’ badala ya kuwa na mkakati wa muda mrefu ambao utaweza kuzuia kurejea na kuenea zaidi kwa mimea vamizi.
Ripoti hiyo inapendekeza ushirikiano zaidi kwa taasisi zinazohusika na uhifadhi kama vile Mamlaka ya Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA) na NCAA. Aidha inaishauri Serikali kuandaa sera na mkakati wa pamoja wa kitaifa wa kudhibiti mimea vamizi utakaokuwa na malengo ya muda mfupi, wa kati na mrefu, badala ya hatua za dharura zisizo endelevu.
Aidha ripoti hiyo inapendekeza kuimarishwa kwa mfumo wa kitaasisi ambapo NCAA na TANAPA zitafanya kazi kwa mfumo mmoja ulioratibiwa na pia kuwepo kwa chombo au kitengo kinachosimamia juhudi zote za kudhibiti mimea vamizi nchini.
Mbinu za kisasa zitumike kung’oa na kuchoma mimea vamizi ili kukomesha tatizo kwa kuwa mimea hii huweza kurejea kwa kasi kutokana na uwezo wake wa kutoa mbegu nyingi, imeshauri ripoti hiyo.
Picha ya Bango: Vibarua na watumishi wa Mamlaka ya Eneo la Hifadhi Ngorongoro wakiondoa mimea vamizi hifadhini. Picha kwa hisani ya NCAA.