- GLF 2026 Nairobi imehitimishwa kwa wito wa kutambua wafugaji wa kuhamahama kama washirika wa maendeleo, si kikwazo.
- Mijadala ilisisitiza umuhimu wa nyanda za malisho kwa bioanuwai, chakula na kaboni, na ushiriki wa jamii katika maamuzi ya ardhi.
- Wataalamu walionya kuhusu pengo la maarifa, haki za ardhi na matumizi ya teknolojia bila kuhusisha jamii za wenyeji.
- Serikali na wadau walihimiza sera bora, ufadhili na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na urejeshaji wa rangelands.
Baada ya mkutano wa siku mbili wa kujadili huduma za mifumo ya ikolojia ya nyanda za malisho na jamii za wafugaji wa kuhamahama, Mkutano wa nane wa jukwaa la Global Landscapes Forum umehitimishwa jijini Nairobi kwa tamko lililosisitiza umuhimu wa jamii ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikionekana kama kikwazo kwa maendeleo.
Katika mkutano huo uliofanyika katika kituo cha CIFOR-ICRAF na kuhudhuriwa na maafisa wa serikali, wanasayansi pamoja na wawakilishi wa jamii za asili kutoka nchi 135, mjadala ulijikita katika mifumo ya ikolojia inayosaidia bioanuwai, usalama wa chakula, maisha ya watu, utamaduni, uhifadhi wa kaboni na huduma nyingine za kiikolojia bila kuvuruga maisha endelevu na tamaduni za jamii za wafugaji, badala ya kuweka msisitizo kwenye uwekezaji unaoshinikizwa na serikali kwa lengo la kupata faida.
“Tunapaswa kujiuliza: Maendeleo haya yanafanywa kwa ajili ya nani? Je, jamii zinahusishwa katika maamuzi kuhusu uwekezaji unaofanywa kwenye ardhi yao? Na ni kwa manufaa ya nani miradi hii ya kibiashara inayowasilishwa kana kwamba ni juhudi za kutoa ajira na fursa nyingine kwa wakazi? Sauti zao zina umuhimu,” alisema Tahira Mohamed Shariff kutoka Jameel Observatory for Food Security Early Action siku ya kwanza ya mkutano huo.

Monicah Yator, Wakili na Mwanzilishi wa Indigenous Women and Girls Initiative, alisema kuwa ufugaji wa kuhamahama si shughuli ya mifugo pekee. “Ni mfumo wa maisha, chakula na utamaduni. Kuna sera zinazowalinda wafugaji. Sasa wafugaji wanafahamu kwamba ardhi yao inaweza kubadilishiwa matumizi,” alisema, akiongeza kuwa maarifa ya asili bado ni muhimu na yenye mchango mkubwa katika uhifadhi wa mfumo wa ikolojia.
“Jamii zetu za wafugaji lazima zitambue thamani ya mifugo na ardhi. Ukweli kwamba mifugo inauzwa nje ya nchi unaonyesha kuwa ina thamani kubwa. Tunahitaji kulinda ardhi na mifugo. Ardhi ya jamii ni rasilimali muhimu kwa wanajamii wote. Lazima tuisajili ardhi hiyo.”
Kauli yake iliungwa mkono na Vivian Silole, Meneja wa Programu wa IMPACT Kenya. Alisema: “Kuona maeneo ya pamoja ya wafugaji wa kuhamahama kama janga kunatokana na dhana kwamba maeneo hayo yako wazi kwa kila mtu kuyatumia bila utaratibu, si sawa. Inachukuliwa kwamba hakuna mifumo, sheria, uratibu wala uwajibikaji uliowekwa. Ukweli ni kwamba mifumo ya asili ya wafugaji inaongozwa na sheria za kimila zilizo wazi, maarifa ya jadi na maamuzi ya pamoja yanayosimamia rasilimali hizi na kuhakikisha uendelevu.”
Yator aliiambia Mongabay kwamba kila mtu anaangalia ardhi za wafugaji ambazo mara nyingi huonekana kana kwamba hazina matumizi ya maendeleo. “Hatupaswi kuruhusu serikali kuamua kubadilisha matumizi ya ardhi ya wafugaji, maeneo tunakolisha mifugo. Hapa ndipo tulipo, hapa ndipo tunapoishi, na hatuwezi kuondoka,” alisema.

Majadiliano mengine kadhaa yalijikita katika kujadili pengo kati ya maarifa waliyonayo wanasayansi na yale ya jamii za wenyeji, nafasi ya jinsia katika uhifadhi wa maeneo ya malisho, ufadhili wa kuhakikisha maeneo hayo yanabaki salama na endelevu, pamoja na sera ambazo ama zimekuwa kichocheo cha kuweka kipaumbele kwa uhifadhi kwa gharama ya ufugaji wa kuhamahama, au zimekuwa zikilinda maslahi ya jamii hizo.
Wasilisho kutoka kwa watu waliotoka katika jamii za wafugaji au waliowahi kufanya utafiti kuhusu jamii hizo, lililenga kuonyesha picha ya jamii zinazojitosheleza na ardhi zao, lakini ambazo mara nyingi huaminishwa kimakosa kwamba hazijakamilika, zinahitaji kubadilishiwa mfumo wao wa maisha, na kwamba uwekezaji unaofanyika kwenye ardhi zao ni neema kwao, hata kama mara nyingi hauongezi thamani halisi.
“Mfumo wa maisha ya wafugaji umejengwa juu ya wingi. Kama mtu anamiliki ngamia 1,000 nchini Somalia, unadhani mtu huyo ana wasiwasi wa kupata chakula? Hana, kwa sababu ngamia wanampa maziwa, na akihitaji chakula kingine anaweza kupata nyama. Hii ni mifumo inayojitegemea na pia imejengwa juu ya jamii na uwezo wa kujitawala,” alisema Fozia Noor, Mkurugenzi wa Organization for Pastoralist Peace Development na Mwanzilishi Mwenza wa Somali Women Pastoralist Network.

Teknolojia na nafasi yake katika uendelevu wa maeneo ya malisho, pamoja na viashiria vya ustawi wa maeneo hayo, vilikuwa miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa kwa mitazamo chanya na hasi. Hoja iliyojirudia mara kwa mara ilikuwa umuhimu wa kuzishirikisha jamii za wenyeji katika kubuni na kutumia teknolojia yoyote inayolenga kuwawezesha wafugaji au kupunguza changamoto zao, hasa inapohusu uchoraji wa ramani za maeneo ya malisho wakati wa ukame.
Éliane Ubalijoro, Mkurugenzi Mkuu wa CIFOR-ICRAF, alihitimisha mjadala huo kwa kusema: “Afrika haiwezi kuwa mpokeaji wa kawaida wa zana za akili bandia (AI) zilizobuniwa kwingine kwa mazingira tofauti. Afrika lazima iwe sehemu ya kuunda miundombinu ya data, mifumo ya usimamizi na mifumo ya maadili inayozingatia mazingira ya Afrika, maarifa ya Kiafrika na umiliki wa Kiafrika. Hii inamaanisha mamlaka ya data, ridhaa, mgawanyo wa manufaa na uwajibikaji. Zaidi ya yote, inamaanisha kuhakikisha kwamba jamii ambazo zimekuwa zikisimamia maeneo haya kwa muda mrefu ndizo ziwe za kwanza kunufaika na maarifa haya mapya yanayohusu jamii hizo.”
Katika kukabiliana na vitisho vinavyoongezeka kutoka kwa wawekezaji wasio waaminifu, mabadiliko ya tabianchi, na ulinzi wa njia za kupita za wanyamapori, wataalamu waliendelea kuhoji huku serikali zikiwekwa katika hali ngumu ya kutoa majibu.
Kendi Borana, kiongozi wa Afrika wa Nia Tero, alihoji kwa nini katika miongo ya hivi karibuni kumekuwa na msisitizo mkubwa juu ya ustawi wa wanyamapori bila kuzingatia jamii za wenyeji na mifugo yao. “Kwa nini tunasherehekea uhamaji wa wanyamapori lakini tunaukosoa mfumo wa maisha wa kuhamahama wa wafugaji, ilhali vyote ni harakati za kutafuta mahitaji ya msingi? Serikali zinaonekana kujali sana usalama na ustawi wa njia za wanyamapori, lakini wafugaji wanapohama, hilo linaonekana kama tatizo. Vyote ni harakati za kutafuta maisha,” alisema.
Siku ya kwanza ya mkutano, serikali mbalimbali, ikiwemo Kenya, nchi mwenyeji, zilitangaza kuunga mkono maeneo ya malisho yenye afya na endelevu, zikieleza miradi iliyotekelezwa na ile iliyopo kwenye mipango, huku zikiahidi kuendelea kusaidia kupitia sera na kanuni mbalimbali.
Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu wa Kenya, Deborah Barasa, alitoa hotuba mbili siku ya kwanza ya mkutano huo, akizihimiza serikali nyingine kuungana katika kuimarisha sera zinazounga mkono usimamizi endelevu wa nyanda za malisho. “Washirika, tuongeze ufadhili wa urejeshaji wa mazingira na ustahimilivu. Sekta binafsi, tuwekeze katika mifumo endelevu ya uzalishaji na kuunga mkono fursa za ukuaji wa kijani. Taasisi za utafiti, tuendelee kutoa suluhisho yanayotegemea ushahidi. Jamii zetu, endeleeni kuwa walinzi wa maeneo haya,” alisema.
Akizungumzia zaidi suala la sera, Johann Saathoff, Katibu wa Serikali katika Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani, alisema: “Mabadiliko katika sera yanahitajika ili kuimarisha huduma zinazohusiana na wafugaji huku tukitambua kikamilifu thamani yao ya kimazingira, kiuchumi na kitamaduni.”
Alizungumzia pia juhudi zilizofanywa na nchi yake kupitia ushirikiano wa maendeleo wa Ujerumani, miongoni mwa juhudi hizo ukiwemo ufadhili wa “ripoti ya kimataifa kuhusu uchumi wa urejeshaji wa maeneo ya malisho, ambayo itazinduliwa katika mkutano ujao wa UNCCD COP17 nchini Mongolia.”
Serikali nyingine iliyowakilishwa katika mkutano huo ilikuwa Luxembourg. Waziri wake wa Mazingira, Tabianchi na Bioanuwai, Serge Wilmes, alisema: “Kuna mlolongo mkubwa wa fursa kwenye miradi ya kaboni ya udongo, ufugaji unaochangia urejeshaji wa mazingira, urejeshaji wa maeneo ya malisho, mifumo ya thamani ya bidhaa za wafugaji yenye kuongeza thamani, lakini kikwazo kikubwa kwa wawekezaji ni kutambua, kutathmini na kulinganisha miradi halisi inayoongozwa na jamii za wenyeji.”

Vitisho vya mabadiliko ya tabianchi havikukosekana katika mijadala ya vikao mbalimbali vya mkutano huo. “Masuala kuhusu maeneo ya malisho lazima yapewe kipaumbele kwenye hatua za kimataifa za mazingira. Yanagusa moja kwa moja masuala ya mabadiliko ya tabianchi, bioanuwai na ardhi. Maeneo hayo ni muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kupunguza madhara yake na pia katika uhifadhi wa bioanuwai. Aidha, yanasaidia katika kupambana na uharibifu wa ardhi na ukame,” alisema Yasmine Fouad, Katibu Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na kupambana na jangwa (UNCCD).
Umiliki wa ardhi na usalama unaotokana na umiliki huo, pamoja na namna hali hiyo inavyoathiri mabadiliko ya matumizi ya ardhi, vilikuwa miongoni mwa mada zilizovutia washiriki wengi katika kumbi za mikutano.
Akisoma taarifa ya kufunga mkutano huo wa siku mbili uliowahusisha washiriki 800 waliokuwepo na wengine 6,000 walioshiriki mtandaoni, Amos Amanubo alisema kuna haja ya kuthamini na kutambua nafasi ya maeneo ya malisho na jamii zinazoishi humo kwa kuwashirikisha kuanzia hatua za utafiti hadi utekelezaji wa miradi, ikiwemo ya huduma za msingi kama maji na afya.
“Kisichoonekana mara nyingi hakipewi thamani. Na kisichopewa thamani hakifadhiliwi, hakilindwi wala hakipewi kipaumbele katika maamuzi. Changamoto iliyopo mbele yetu si kuendelea tu na mazungumzo, bali kubadilisha mwonekano kuwa utambuzi, utambuzi kuwa haki, na haki kuwa msaada wa kudumu kwa jamii zinazolinda maeneo haya kila siku,” alisema katika muhtasari wake wa vikao 67 vilivyofanyika ndani ya siku hizo mbili.
Umoja wa Mataifa umetangaza 2026 kuwa mwaka wa kimataifa wa nyanda za malisho na wafugaji.
Jarida la Global Change Biology linaeleza kuwa nyanda za malisho zinachukua zaidi ya asilimia 54 ya uso wa ardhi duniani. Angalau asilimia 50 ya maeneo hayo yameharibiwa, hali inayodhuru usalama wa chakula na hifadhi ya kaboni ya dunia. Sehemu kubwa ya maeneo hayo ya malisho ipo katika maeneo kame. Jarida hilo linaongeza kuwa maeneo ya malisho “yanasaidia maisha ya takribani watu bilioni mbili” pamoja na “mifumo ya uzalishaji wa mifugo na ufugaji wa kuhamahama.”
“Nikizungumza kama mfugaji, ardhi si rasilimali tu. Ng’ombe si mtaji tu. Wala sisi si nguvu kazi tu. Sisi ni mfumo mmoja uliounganishwa na tunategemeana. Teknolojia haipo ili kuondoa mamlaka ya kufanya maamuzi kutoka kwa jamii. Inaweza kutoa utabiri na kurahisisha michakato na mipango, lakini si kufanya maamuzi. Hayo lazima yabaki mikononi mwa wafugaji,” alisema Joshua Daniel Laizer, Mwanzilishi Mwenza wa TACCEI na Mratibu wa GLFx Maasai Steppe.
Picha ya bango: Mshiriki akitoa mchango wake katika moja ya vikao wakati wa kongamano la siku mbili la Global Landscapes Forum 2026 jijini Nairobi. Picha kwa hisani ya GLF.